DK EDWARD HOSEAH AWAITA WANASIASA NI WANAFIKI...

Dk Edward Hoseah.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imesema utashi wa ushiriki wa baadhi ya viongozi wa kisiasa katika mapambano dhidi ya rushwa, umekuwa wa kinadharia zaidi kuliko vitendo.
Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa viongozi wa Takukuru jana Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Dk Edward Hoseah alifafanua kuwa wanasiasa wamekuwa kinadharia zaidi kwa kuwa wameshindwa kuwa mfano katika mapambano hayo.
Huku akitaja changamoto zinazokabili mapambano hayo mbali na ya wanasiasa kukosa kuwa mfano, Dk Hoseah alisema taasisi hiyo imekuwa ikikosa ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji wa mapendekezo yanayotolewa na utafiti wanaoufanya wa kuziba mianya ya rushwa.
Mbali na kukosa ushirikiano na wanasiasa kuzungumza kinadharia, Dk Hoseah alisema  pia kesi wanazopeleka mahakamani zimekuwa zikikaa muda mrefu  bila kutolewa uamuzi na kutoa mfano kuwa kesi nyingi huchelewa mahakamani kwa zaidi ya miaka minne hadi sita.
Kutokana na changamoto hizo, Dk Hoseah alipendekeza kuundwa divisheni ya kesi za rushwa katika mahakama ili kuongeza ufanisi na uhamasishaji wa kusikiliza kesi hizo.
“Tunajitahidi kukaa na Mahakama ili kuangalia uwezekano wa kusikiliza kwa mfululizo kesi zetu na hivyo kutumia muda mfupi,” alisema Dk Hoseah akielezea juhudi za sasa za kuharakisha kesi hizo.
Alitaja changamoto zingine kuwa ni baadhi ya mashahidi kutopenda kutoa ushahidi mahakamani kwa kuogopa kulipiziwa kisasi.
Ukiacha woga huo, Dk Hoseah alisema pia wamekuwa wakilazimika kuchukua muda mrefu kupata ushahidi wa nyaraka kutoka nje ya nchi kwa ajili ya uchunguzi wa kesi kubwa.
Kutokana na changamoto hiyo, uchunguzi wa kesi hizo umekuwa ukichukua muda mrefu na gharama kubwa za kufuatilia ushahidi ikiwamo ya kusafiri nje ya nchi wakati bajeti ya kufanya kazi hiyo, haitoshi.
Alitaja nyingine kuwa ni mahitaji makubwa ya majengo ya kujitegemea hasa wilayani kwani uwezo wa taasisi hiyo ni kujenga jengo kila mkoa. Pia wananchi na wadau wametajwa kuikwaza Takukuru kwa kutotambua mapambano dhidi ya rushwa na mafanikio ya taasisi hiyo.
Dk Hoseah alisema katika mwaka huu wa fedha, Takukuru imechunguza tuhuma 2,784 ambapo tuhuma 983 uchunguzi ulikamilika na majalada 355 yalifungwa kwa kuwa ushahidi wa kuthibitisha haukupatikana.
Alisema kati ya tuhuma zilizokamilika majalada 181 yalifikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwa ajili ya kuomba kibali cha kuwafikisha watuhumiwa mahakamani.
Aidha, alisema katika mwaka huo wa fedha, kesi 612 ziliendeshwa mahakamani na kati yao, 478 zinaendelea na 149 zilitolewa uamuzi huku kesi 50 watuhumiwa walipatikana na hatia na kesi 32 ziliondolewa mahakamani kutokana na sababu mbalimbali. Kesi 67 watuhumiwa waliachiwa huru na saba zimekatiwa rufaa.
Vilevile alisema hadi sasa kesi za rushwa kubwa 54 zipo mahakamani katika hatua mbalimbali na majalada matano yanayohusu kesi kubwa za rushwa yalifikishwa kwa DPP na kupata kibali na watuhumiwa wamefikishwa mahakamani.

No comments: