WABUNGE WAVUTANA MUSWADA MIFUKO YA HIFADHI ZA JAMII...

Moja ya vikao vya Bunge mjini Dodoma.
Suala la kuwasilisha muswada binafsi bungeni wa marekebisho ya Sheria ya Hifadhi za Jamii ili kurejesha fao la kujitoa, limeingia sura mpya baada ya kuibuka mvutano wa kunyang’anyana hoja baina ya wabunge wawili.
Wabunge hao; Seleman Jafo wa Kisarawe (CCM) na John Mnyika wa Ubungo (Chadema), wote wana lengo la kumtetea mfanyakazi apate mafao yake mara anapoachishwa kazi hata kabla ya kustaafu, lakini kila mmoja anataka kuonekana hoja ni yake.  
Juzi, Mnyika alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa amewasilisha hati ya dharura kwa Katibu wa Bunge ya kusudio la kuwasilisha muswada binafsi kuhusu marekebisho ya sheria  hiyo.
Wakati Mnyika akieleza hayo, jana  Jafo ambaye ndiye alitoa hoja hiyo kwa mara ya kwanza katika Bunge la Bajeti lililopita, aliwaambia waandishi wa habari kuwa, amekamilisha mchakato wa kuwasilisha muswada binafsi katika Bunge lijalo kuhusu marekebisho ya sheria hiyo.
“Napenda kuwaeleza, kwamba lile kusudio langu la kuwasilisha Muswada binafsi wa marekebisho ya Sheria za Hifadhi ya Jamii limekamilika, Bunge lililopita liliiagiza Serikali iwasilishe muswada huo lakini nimebaini haina kusudio hilo mpaka sasa,” alisema Jafo.
Akizungumza jana katika ofisi ndogo za Bunge, Dar es Salaam, Jafo alidai amepita katika kamati za Bunge zinazohusika na masuala ya jamii na kugundua Serikali haijatekeleza agizo hilo, hivyo atawasilisha muswada huo bungeni.
“Baada ya kubaini hilo, nitawasilisha mimi muswada huo na tayari nimefanya mikutano na wafanyakazi wa sekta za madini, barabara, hoteli, watumishi wa Serikali na asasi za kiraia katika mikoa ya Mwanza, Geita, Mara na Dar es Salaam kupata maoni,” alisema Jafo.
Alisema tayari amewasilisha kusudio hilo kwa hati ya dharura kwa Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah ili suala hilo lijadiliwe na kumalizika katika Bunge lijalo la tisa.
Dk Kashililah alipoulizwa jana kuhusu mvutano huo, aliliambia gazeti hili kuwa Jafo alizungumza naye na kumweleza kufikisha suala hilo kwake, lakini hajaona hati hiyo mezani kwake wala ya Mnyika.
“Mimi hizo hati sijazipokea mezani kwangu, nilizungumza na Jafo, alisema amewasilisha ila hazijanifikia mezani kwangu hivyo siwezi kusema zaidi, hata ya Mnyika sijaiona,” alisema Dk Kashililah.
Jafo alisema katika Bunge la Nane alitoa maelezo binafsi akiitaka Serikali ilete bungeni muswada wa fao la kujitoa na kwa kuwa dalili hazipo, tayari amekamilisha mchakato ikiwamo kupata saini za wabunge 10 wa kuunga mkono hoja kwa mujibu wa kanuni ya 80 kipengele cha kwanza na cha tano.
Wabunge waliosaini kuunga mkono hoja hiyo ni pamoja na Dunstan Kitandula (Mbunge wa Mkinga-CCM), Neema Mgaya (Viti Maalumu-CCM), Abdulsalaam Amer (Mikumi-CCM), Seleman Bungara (Kilwa Kusini-CUF)  na Esther Bulaya (Viti Maalumu-CCM).
Wengine ni Hussein Mussa Mzee (Jang’ombe-CCM), Mendrad Kigola (Mufindi Kusini-CCM), Juma Othman Ali (Tumbatu-CCM), Waride Bakari Jabu (Kiembe Samaki-CCM) na Jafo.
Kuhusu hoja ya Mnyika kudai kuwasilisha hoja hiyo pia kwa hati ya dharura, Jafo alisema Mnyika amedandia hoja hiyo kwa mbele kwa kuwa haikuwa yake. 
Kwa mujibu wa taarifa ya juzi ya Mnyika, tayari naye amewasilisha hati ya dharura ya kusudio la kuwasilisha muswada binafsi wa Hifadhi ya Jamii kwa Dk Kashililah.
Jafo alisema kabla ya marekebisho ya Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kupita mwaka 2012, kulikuwa na utaratibu wa mwanachama wa mifuko hiyo nchini kufaidika na fao la kujitoa.
Alisema baada ya marekebisho hayo, ni vigumu kwa mfanyakazi aliyeachishwa kazi kabla ya umri wa kustaafu ambao ni miaka 55 kwa hiari au 60 kwa lazima, kunufaika na mafao yake ya uzeeni hasa kutokana na uhakika mdogo wa watu wengi kufikia umri huo.

No comments: