UCHAGUZI WA CCM WAINGIA DOSARI MKOANI MWANZA...

Uchaguzi wa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza umeingia dosari baada ya basi walilokuwa wakisafiria wajumbe 70 kutoka wilayani Kwimba, kupata ajali na dereva kufa huku wengine 10 wakijeruhiwa vibaya.
Ajali hiyo ilitokea jana saa 3.30 asubuhi katika eneo la Buhongwa nje kidogo ya Jiji la Mwanza wakati wajumbe hao wakienda jijini Mwanza kwa ajili ya kuwachagua viongozi wa chama hicho ngazi ya mkoa.
Mmoja wa majeruhi hao, Shija Malando ambaye ni Diwani wa Kata ya Hungumalwa, alisema ajali hiyo ilitokea baada ya gari la kubeba mchanga kukatiza ghafla wakiwa katika mwendokasi, hali ambayo ilisababisha kugongana na basi hilo kisha basi hilo kutumbukia katika mtaro.
Malando alisema katika ajali hiyo wanaCCM wengi walijeruhiwa vibaya na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
“Kama unavyoniona nimeumia sehemu ya sikio langu la kulia pamoja na mbavu, lakini wajumbe wenzetu wameumia vibaya akiwemo Mwenyekiti wa zamani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, Antony Swagi  ambaye amevunjika mkono na mmoja wa maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa aliyekuwa akiisindikiza gari yetu amevinjka mkono,” alisema Malando.
Alisema kati ya watu 10 waliopata ajali hiyo, saba kati yao ni madiwani wa wilaya hiyo akiwamo yeye mwenyewe na wengine ambao mpaka sasa wapo Bugando wakiendelea na matibabu ni Abel Mayenga, Feissa Yassin, Elias Nonitale, Shija Lutena, Martin Malecha pamoja na Anthon Swangisi.
Akizungumza katika mkutano wa uchaguzi, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza anayemaliza muda wake, Clement Mabina alitoa taarifa kwa wajumbe wa mkutano huo kuwa kuna wajumbe wamepata ajali, lakini kwa bahati mbaya dereva wa gari hilo aliyefahamika kwa jina moja la Makoye, amefariki dunia.
“Ndugu wajumbe tumepata taarifa mbaya kuhusiana na ajali ya basi lililosababisha dereva wa basi lililokuwa limewabeba wajumbe wa Kwimba kufariki, tunawaomba msimame dakika moja kwa ajili ya kuwaombea wenzetu walioumia pamoja na dereva aliyefariki,” alisema Mabina.
Mabina ambaye alikuwa anashindana na Anthony Diallo pamoja na wagombea wengine wawili, matokeo ya awali yalionesha kuwa alikuwa anakabwa koo na mbunge huyo wa zamani wa Ilemela.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Lily Matola alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kudai kuwa taarifa kamili zitatolewa baada ya askari waliofika eneo la tukio kukamilisha uchunguzi.

No comments: