MGAWO, KUKATIKA-KATIKA UMEME SASA KWAZIKWA RASMI...

Wizara ya Nishati na Madini imeondoa kabisa mgawo wa umeme nchini, ikiwa ni pamoja na kero ya kukatikakatika kwa umeme katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Hatua hiyo imewezekana baada ya kutumia zaidi ya Sh bilioni 20.2 kukarabati miundombinu ya umeme jijini Dar es Salaam, ikiwamo kununua transfoma mpya katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliakim Maswi aliwaeleza wabunge na madiwani wa Jiji la Dar es Salaam jana wakati akiwaeleza mipango ya kuboresha miundombinu ya umeme katika jiji hilo lililokuwa likiongoza kwa kuwa na umeme wenye nguvu ndogo na kukatika mara kwa mara.
Alisema wamenunua na kuweka transfoma mpya kwenye vituo vya kupozea umeme na kukarabati laini za kusafirisha umeme ikiwamo kubadilisha waya na nguzo na kukarabati maungio na kubadilisha vikombe.
Alisema katika kipindi cha Juni mwaka 2011 hadi Septemba mwaka huu, Serikali imeondoa mgawo wa umeme uliotesa nchi kwa muda mrefu na kuwahakikishia wananchi kuwa wamefanya mikakati ya kuhakikisha hakuna mgawo.
“Nimekuwa kimya katika kuhakikishia kuwa hakutakuwa na mgawo, lakini kawa sasa nina uhakika na hilo kutokana na kuwa hata jana nimepata fedha ambazo zimenihakikishia kutokuwa na mgawo hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi,” alisisitiza Maswi.
Alisema kwa kuanzia mkoani Dar es Salaam, wametumia fedha hizo katika kufunga transfoma sehemu mbalimbali katika maeneo ya Kariakoo, katikati ya Jiji, Mbezi, Mbagala, Buguruni, Gongo la Mboto, New Kunduchi, Kigamboni, Oysterbay, Ubungo, Kipawa, Tegeta na Mikocheni ambapo nyingine zimekamilika na nyingine ndiyo zinafungwa.
“Wizara inadhamiria kuendelea kujiimarisha zaidi kiutendaji kwa lengo la kuondoa kabisa mgawo wa umeme na kukatika katikati kwa umeme katika jiji na nchi nzima ili sekta iweze kutoa mchango stahiki kwa maendeleo ya nchi,” alisisitiza Maswi.
Alisema licha ya mafanikio hayo, wamekuwa na changamoto ya ukosefu wa viwanja kwa ajili ya kujenga na kupanua vituo vya kupozea umeme, kwa wananchi kukataa kupisha maeneo yanayotakiwa kujengwa au kupanuliwa laini za umeme kwa ajili yao.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadik aliwataka watendaji kuwajibika katika kulinda miundombinu ya umeme ili kuepuka gharama zinazotokana na kulipuka kwa transfoma hivyo kuwataka kujipanga kila mmoja katika maeneo yake kulinda na kuacha kuwaachia Tanesco pekee.

No comments: