MAMIA WAMUAGA KAMANDA BARLOW DAR...

Askari wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa Kamanda Liberatus Barlow, Ukonga, Dar es Salaam jana.
Mamia ya wakazi wa Dar es Salaam waliohudhuria katika ibada ya kumuaga aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow jana walibaki na manung’uniko baada ya kushindwa kuaga mwili wa marehemu huyo aliyeuawa Oktoba 13, mwaka huu.
Mwili wa marehemu ulifikishwa nyumbani kwake Ukonga Dar es Salaam jana saa 6:30 mchana ukitoka Mwanza ambako aliuawa usiku wa kuamkia Jumamosi baada ya kupigwa risasi na watu wanaodhaniwa kuwa majambazi, kisha kufuatiwa na ibada katika Kanisa la Katoliki Ukonga.
Hata hivyo, kutokana na umati wa watu waliofurika katika msiba huo, ilibidi viongozi wa Serikali na Jeshi la Polisi waliohudhuria waruhusiwe kuaga mwili ili usafirishwe kwenda Kilimanjaro, kijiji cha Kilema, Moshi Vijijini kwa ajili ya maziko yatakayofanyika leo, na kuacha watu wengine wakilalamika.
Awali, akitoa salamu za rambirambi, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Saidi Mwema alisema jeshi hilo litahakikisha watuhumiwa wote waliohusika na mauaji hayo wanakamatwa na kuchukuliwa hatua.
“Raia ni wengi na wahalifu ni wachache hivyo tunaamini kwa kushirikiana na wananchi tutawapata wahalifu hao na Jeshi la Polisi litahakikisha usalama, amani na utulivu vinadumu nchini kwa kuwa lipo imara,” alisema IGP Mwema.
Alisema Kamanda Barlow alikuwa kiongozi mwadilifu na muaminifu katika utendaji wake wa kazi na ameacha pengo kubwa kwa kuwa kuondokewa na askari mmoja ni sawa na kuondoa ulinzi kwa wananchi zaidi ya 1,300.
Aidha, aliwaomba viongozi wa dini kuwahamasisha Watanzania kutii sheria bila shuruti akisema wao ni viongozi wa kiroho na kimwili, lakini polisi ni viongozi wa kimwili pekee hivyo ni vyema washirikiane katika kutokomeza uhalifu nchini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima alisema wamepokea kifo hicho kwa masikitiko na wamepoteza nguzo imara ambayo Serikali na Polisi ilikuwa ikiegemea na kuwa hawawezi kurudisha uhai wake, lakini watahakikisha waliohusika wanakamatwa na kuchukuliwa hatua.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile alisema alimfahamu Barlow kwa muda mrefu na Jeshi la Polisi limepoteza kiongozi ambaye alimwita jembe kwa kuwa alikuwa mkakamavu, mwenye uwezo wa kufanya uamuzi na alisaidia kupunguza uhalifu mkoani Mwanza.

No comments: