WAPINGA UMRI WA RAIS KUWA CHINI YA MIAKA 40...

Jengo la Ikulu ya Dar es Salaam.
Umri wa anayepaswa kushika kiti cha urais nchini umetajwa katika mchakato wa kuchangia maoni ya Katiba mpya ikielezwa kuwa haupaswi kuwa chini ya miaka 40 kwani kufanya hivyo, atapatikana ‘rais wa watoto’.
Mwakilishi wa Viti Maalumu, Asha Bakari Makame (CCM) amesema umri wa rais unapaswa uwe zaidi ya miaka hiyo ambao unamwezesha kiongozi kutumia busara katika kuongoza nchi.
Asha alisema hayo juzi katika mkutano ambao Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilikutana na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ili kutoa maoni yao binafsi.
Maoni hayo ambayo yamekuja huku kukiwa na maoni mengine ambayo yamekuwa yakitolewa hususan na vijana wakitaka umri wa urais uanzie miaka 35 badala ya miaka 40 ya sasa.
Miongoni mwa waliopata kukaririwa wakitaka umri wa urais upunguzwe, ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema).
Alisema umefika wakati Taifa kupunguza umri kwa alichosema hakuna sababu za kisayansi zinazomfanya mtu mwenye chini ya umri wa miaka 40 kukosa sifa za urais.
Katika hatua nyingine, Asha alipendekeza ibara ya 22  ya Katiba inayoeleza juu ya haki za kufanya kazi, iongezwe kifungu kinachopiga marufuku mwanandoa kuzuia mwenzake kufanya kazi.  
Alisema licha ya kuwapo sheria za kidini juu ya umiliki wa mali kwa mwanamke, Katiba iweke wazi kwamba mwanamke ana haki ya kumiliki mali inayohamishika na isiyohamishika.
Alitaka katika ibara ya 33 ambayo Katiba inaainisha uwiano katika ngazi za juu, iongeze ibara itakayotoa masharti ya kuwapo uwiano wa kijinsia katika ngazi za juu na kuhakikisha kwamba rais hatakuwa mdhalilishaji wa kijinsia wala mnyanyasaji.
Mwakilishi huyo pia alipendekeza Katiba itamke wabunge wanawake idadi yao isipungue asilimia 50 na utaratibu wa kupatawabunge wa viti maalumu uwe sawa kwa vyama vyote.
Alipendekeza pia idadi ya wabunge wanawake kwa kila chama iendane na viti vya majimbo ambavyo chama cha siasa kitakuwa kimeshinda.
Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho alisema Muungano unapaswa uwepo, kwa kuwa kila upande una watu wanaoishi upande mwingine hususan Wazanzibari waliofanya uwekezaji mkubwa Bara ambao wanaweza kuathirika iwapo utavunjika.  
Alisisitiza kwamba Muungano hautavunjika na kutaka suala la mafuta ya Zanzibar lipatiwe ufumbuzi mapema, kwani ni miongoni mwa mambo yanayoleta malalamiko makubwa juu ya Muungano.  
Akichangia maoni yake, Kificho alisema: “Ukienda Dar es Salaam, Tanga, Arusha … yapo mambo makubwa ambayo tumefanya.
“Leo hii ukisema Muungano uvunjike, katika hali ya ubinadamu, wenzetu wanaweza kujenga chuki. Kwa hiyo Muungano uwepo,  Muungano huu tulionao unafaa,” alisema.
Kificho ambaye alisisitiza kwamba ni vizuri yakaainishwa mambo yote ya Muungano, alisema kwa muda mrefu moja kati ya matatizo makubwa ni suala la mafuta, ikizingatiwa kwamba Zanzibar haiwezi kuendesha Serikali bila uchumi.
Alisema  mbali na karafuu na utalii wakati huu, Zanzibar hakuna mambo mengine  yanayohusu madini ya kuwajenga kiuchumi. Alisema ipo haja ya kuangalia uchumi, kwa sababu suala hilo halimo katika mambo ya Muungano kwa maana kwamba  kila  upande unakwenda kwa utashi wake.
Alitoa mfano wa masuala ya ushirikiano na nchi nyingine ambayo ni ya Muungano, akisema Zanzibar haiwezi kuingia moja kwa moja katika ushirikiano na nchi nyingine.
Alisema ilikuwa ni vizuri kwa kuwa uchumi ni suala ambalo halimo kwenye Muungano, uwepo uhuru wa upande wowote wa Muungano kwenda nchi yoyote kuanzisha ushirikiano kwa ajili ya kuinua uchumi. “Nchi yetu ni kisiwa, bila shaka mfumo sahihi wa kuinua uchumi unakuwa ni mdogo,” alisisitiza.
Kuhusu mafuta ambayo hata hivyo alisema hayajawa na uhakika wa kuwapo, ni eneo litakaloinua uchumi na ambalo uamuzi wake unatakiwa ufanywe mapema ili kuondoa shutuma zinazotolewa juu ya Muungano.
Mwakilishi wa Mtambwe, Salimu Abdallah Ahmad  (CUF) alisema Wazanzibari walio Bara wamewekeza na kuinufaisha Bara wakati wanaokuja hapa wanawekeza kwenye sumu za mbu na kunguni pekee.
Akizungumzia malalamiko juu ya Muungano wakiwamo wanaotaka uwe wa mkataba, Mbunge wa Dole, Shawana Buhati Hassan (CCM) alisema katika suala lolote la kibinadamu upungufu hauwezi kukosekana.
Alisema Muungano umefanya mambo mengi mazuri hadi sasa, huku akisifu kwamba hata hatua ya kutoa nafasi ya kurekebisha Katiba, ni matunda ya Muungano.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Zanzibar, Dk Mwinyi Haji Makame aliilalamikia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, akidai kwamba viongozi wake wanaidharau Zanzibar na hawaitendei haki.
Akizungumzia kasoro za Muungano, Dk Makame alisema Wizara hiyo, chini ya Waziri Bernard Membe haifanyi mkakati wowote wa kuitangaza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kiasi kwamba haitambuliki.
Alitupia lawama Ofisa wa Kitengo cha Diaspora ambaye hakumtaja jina, akisema ni dada, kwamba ilipotokea safari ya Rais Marekani ambayo alitaka uwepo ujumbe kutoka SMZ, ofisa huyo alizuia mwaliko huo.
Alisema amepata kumsemea ofisa huyo kwa Waziri Membe, lakini hadi sasa hakuna hatua alizochukua dhidi yake.
Aidha alidai Waziri Membe alipata kuhujumu nafasi yake wakiwa ziarani China akidai kwamba kulikuwa na mkataba ambao ulihitaji kusainiwa naye kama Waziri wa Zanzibar,  lakini Membe akaenda kuusaini peke yake.
“Mkataba wangu mimi kauchukua yeye sijui ni kwa kutojua? Mimi naona ni makusudi, kwa sababu ulikuwa umetayarishwa kwa ajili ya Zanzibar, akaenda akausaini. Nilipomwuliza, akasema mimi sina instrument (chombo).
“Hii ni dharau … wewe kitu si chako … yeye kajiona ni Waziri mkubwa wa SMT (Serikali ya Muungano Tanzania) mimi kaniona ni Waziri mdogo wa SMZ,” alilalamika.
Mwakilishi wa Kwamtipura, Hamza Hassan Juma (CCM) alitaka wizara zote za Muungano ziongozwe kwa pamoja na Wazanzibari na Wabara.
Alitaka iwapo Waziri anatoka Bara, Naibu atoke Zanzibar; vivyo hivyo Naibu akitojka Bara, basi Waziri awe wa Zanzibar. Pia kwa upande wa makatibu wakuu na manaibu wao, mgawanyo uwe kama huo.

No comments: