KAMANDA BARLOW KUAGWA RASMI LEO...

Mwili wa aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow ukiingizwa kwenye Uwanja wa Nyamagana kwa ajili ya kuagwa na wakazi wa Jiji hilo jana.
Baada ya kuagwa na maelfu ya watu katika uwanja wa Nyamagana jijini hapa jana, leo aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, marehemu Liberatus Barlow ataagwa Dar es Salaam.
Jana saa 4.15 asubuhi msafara wa magari kutoka Pasiansi, nyumbani kwa marehemu uliingia katika uwanja huo uliokuwa tayari umefurika watu kuanzia saa 2 asubuhi huku wengine wakiendelea kuingia.
Kuagwa kwa Barlow kulitanguliwa na Misa iliyoongoza na Padri Raymond Mayanga na baadaye watu mbalimbali walipata nafasi ya kutoa salamu zao. Na baada ya shughuli hiyo mwili huo ulisafirishwa kwenda Dar es Salaam iliko familia yake.
Leo mwili wa Kamanda Barlow unatarajiwa kuagwa kuanzia saa tano asubuhi katika Kanisa Katoliki Ukonga.
Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, baada ya kuagwa, mwili utasafirishwa kwenda nyumbani kwao Kilema, Moshi Vijijini, Kilimanjaro kwa maziko yatakayofanyika  kesho mchana  kwa kufuata taratibu za kidini na kuhitimishwa na taratibu za kijeshi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Polisi nchini (IGP) Said Mwema, Mkurugenzi wa Upelelezi wa  Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Manumba alisema Polisi itahakikisha inakamata wote waliohusika na mauaji ya Kamanda Barlow sambamba na mauaji ya vikongwe, wenye ulemavu wa ngozi na wanaochukua sheria mkononi.
“Huu ni wakati wa kutafakari, tukio hili linatufundisha nini katika kuwekeza kwenye mapambano dhidi ya uhalifu wa kijambazi, migogoro ya kidini, koo, viongozi wa siasa kuhamasisha wafuasi kufanya vurugu, kuelekeza mashambulizi kwa vikongwe, albino na utamaduni wa kuchukua sheria mkononi bila kujali kama kuna mahakama.
“Tujiulize, tunapowekeza kwenye vurugu tunalipeleka wapi Taifa, kwani kinachodumu kwenye jamii ni usalama na amani ambavyo vitatuwezesha kufanya shughuli zetu,”  alisema Manumba.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi
na Usalama ya Mkoa alisema mkoa umepata pigo kwa RPC kuuawa.
Alisema saa chache kabla ya kifo chake, alikuwa ofisini kwake na viongozi wengine wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wakizungumzia masuala ya kikazi huku akitoa michango mizuri ya uboreshaji.
Alisema Jamii ya Watanzania imechukizwa na tukio hilo ovu kwa mtu ambaye alikuwa akiongoza Jeshi la Polisi kwa ufanisi mkubwa na kufanikiwa kupunguza uhalifu wa kutumia silaha,  katika Ziwa Victoria, dawa ya kulevya na mauaji ya albino kwa kiasi kikubwa.
Akiongoza Misa, Padri Mayanga alisema Kamanda Barlow alijitahidi kutumikia Watanzania wenzake kuhakikisha haki inatendeka na kama alikuwa na upungufu basi ni wa kibinadamu ambao kila mtu anao.
Alisema kifo cha Barlow kinatoa fursa ya kujifunza kwa kujiuliza kwa nini kimetokea katika hali hii na kila mmoja ajichunguze moyoni mchango wake ni nini katika hilo kwani watu wanashindwa hata kumwogopa Mungu.
“Maisha ya binadamu ni zawadi kutoka kwa Mungu na hakuna mwenye haki ya kuyatoa, Watanzania tumwogope Mungu, ndiyo maana maandiko yanasema heri walio wapatanishi wataitwa wana wa Mungu,” alisema.
Akiwasilisha salamu za Serikali kwa Niaba ya Waziri Mkuu, Waziri  wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu, William  Lukuvi alisema Serikali imeshitushwa na kifo hicho.
“Natoa pole kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Mwema kwa msiba huu mkubwa, lakini pia niwape pole Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na wananchi wote wa mkoa huu kwa kuondokewa na mtumishi wenu namba moja, najua wote tutakufa, lakini RPC wenu kwa mazingira haya ndivyo alivyoandikiwa kifo chake,” alisema.
Alitaka wakazi wa hapa kuondoa hofu ya kuondokewa na kiongozi wao kwa kuwa Serikali iko kamili katika kulinda mali na maisha yao na kuwataka waendelee na shughuli za uzalishaji mali kama kawaida.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Chalres Tizeba alisema  ameguswa na msiba wa Kamanda Barlow ambaye aliwahi kufanya kazi naye akiwa Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, yeye akiwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora.
Naibu Waziri wa Maji, Dk Binilithi Mahenge, alisema kifo cha Kamanda Barlow ni pigo kwa Taifa na alitoa salamu za pole kwa Mkuu wa Mkoa, Polisi nchini na wakazi wa Mwanza.
Rais Jakaya Kikwete alieleza kushitushwa na kuhuzunishwa na mauaji ya Kamanda Barlow ambapo katika salamu zake za rambirambi kwa IGP Mwema, Rais aliagiza Jeshi hilo kuhakikisha linachukua hatua za lazima kukamata na kuwafikisha mbele ya sheria watuhumiwa wa kupanga na kutekeleza mauaji hayo.
“Nimepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi taarifa za kifo cha ACP Barlow kilichotokea usiku     Mwanza ambako watu wasiojulikana walimpiga risasi na kumwua ofisa huyo mwandamizi wa Jeshi letu la Polisi.
“Historia ya ACP Barlow ni ya mfano katika utumishi wa umma na hususan katika Polisi. Kwa hakika, Polisi imepoteza kamanda hodari na wananchi wa Tanzania, hususani wa Mwanza, wamepoteza mlinzi shupavu wa usalama wao na mali zao,”  alisema Rais Kikwete katika salamu hizo.
Alimwomba IGP amfikishie salamu kwa familia ya marehemu akiwajulisha kuwa yuko nao katika wakati huo mgumu.  Pia alilitia moyo Jeshi la Polisi akiltaka mauaji hayo yasikikatishe tamaa  katika kutimiza wajibu wake. 
Akisoma wasifu wa marehemu, Ofisa Upelelezi wa Mkoa wa Mwanza, Joseph Konyo alisema alizaliwa katika kijiji cha Kou, Moshi Vijijini Desemba 26 mwaka 1959 akiwa mtoto wa tatu katika familia yao.
Alipata elimu ya msingi katika shule ya msingi Lombetha na kuhitimu mwaka 1974. Alijiunga na   Seminari ya Maua Moshi Vijijini na mwaka 1979 alijiunga na kidato cha tano Sekondari Milambo, Tabora alikohitimu mwaka 1981. 
Baada ya sekondari, Barlow alilitumikia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Operesheni Imarisha   Mafinga, Iringa.
Mwaka 1982, alijiunga na Chuo cha Mafunzo cha Polisi (CCP) Moshi alikopata mafunzo ya awali ya Sheria ya Uhamiaji na baadaye kupangiwa kazi mpakani mkoani Mtwara akiwa Mkuu wa Kituo cha Uhamiaji.
Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1984 kusomea Shahada ya Kwanza ya Utawala na kuhitimu mwaka 1987. Mwaka huo huo alijiunga rasmi na Polisi kupitia Chuo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam alikopata mafunzo ya uongozi ngazi ya Mkaguzi Msaidizi wa Polisi. Amekuwa Kamanda wa Polisi katika mikoa ya Mara, Tabora na Mwanza.
Kamanda Barlow aliuawa usiku wa manane kuamkia Jumamosi na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi katika eneo la Kitangiri, Mwanza.

No comments: