Kamanda wa Polisi, Evarist Mangala. |
Mkazi wa mjini
Kahama ameuawa kwa kupigwa na wahudumu na walinzi wa baa ya Renny iliyoko
Shunu, Nyahanga, baada kuagiza na kunywa bia mbili zenye thamani ya Sh 4,000 na
kushindwa kuzilipia kwa wakati.
Hayo
yalithibitishwa jana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Evarist Mangara ambaye
alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 2.30 usiku, baada ya mteja Yusuph Andrew
(27) kuagiza kinywaji hicho na alipotakiwa kukilipia alishindwa.
“Kutokana na hali hiyo wahudumu na walinzi wa baa hiyo walimpiga
kumshinikiza alipe bia alizokunywa na kusababisha hali yake kuwa mbaya na
kukimbizwa katika hospitali ya wilaya alikoanza kupatiwa matibabu,” alisema
Kamanda Mangala.
Hata hivyo, alisema jitihada za madaktari wa hospitali hiyo kutaka
kunusuru maisha ya mgonjwa huyo zilishindikana na saa sita usiku alipoteza
maisha.
Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi linashikilia watu wanne kwa
tuhuma za kuhusika na mauaji hayo na baada ya uchunguzi kukamilika,
watafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayowakabili.
Aidha, Kamanda Mangara alisema katika tukio lingine, mwanamke mkazi wa
kijiji cha Mpilimo, Ngogwa, Kahama alibakwa kwa zamu na watu wawili na kumpora
Sh 10,000.
Alisema mwanamke huyo (jina tunalo) alifikwa na tukio hilo saa 1.45
usiku wakati akitoka sokoni.
Kwa tukio hilo, watu wawili, Paulo Mathias (19) na Masumbuko Lufungulo
(19) wa kijiji hicho, wanashikiliwa na Polisi na uchunguzi utakapokamilika
watafikishwa kortini.
No comments:
Post a Comment