Askari wa usalama waliovalia kiraia wakimdhibiti mmoja wa waandamanaji katika moja ya mitaa ya Kariakoo jana. |
Mabomu ya kutoa machozi, milio ya risasi za
moto, ukamataji waandamanaji, kutanda kwa mgambo, polisi na wanajeshi, ndiyo
ilikuwa mandhari ya baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam jana.
Jiji hilo liligeuka ‘uwanja wa vita’ baada ya vikosi vya ulinzi na
usalama kukabiliana na mamia ya waandamanaji waumini wa dini ya Kiislamu
waliokuwa wakitaka kuandamana kwenda Ikulu.
Hata hivyo, haikueleweka mara moja dhamira ya waumini hao kutaka kwenda
Ikulu ilikuwa nini, lakini hali
isiyokuwa ya kawaida ilijitokeza Kariakoo, jambo lililofanya pia biashara
kusimama baada ya maduka mengi kufungwa.
Katika vurugu hizo, polisi kutoka vikosi vya Kutuliza Ghasia (FFU),
askari wa kawaida na mgambo wa Jiji, walilazimika kutumia nguvu za ziada kuzima
maandamano yaliyokuwa yakijitokeza katika Msikiti wa Idrissa, Kariakoo.
Ilikuwa kama mchezo wa kuigiza katika eneo hilo, kwani kila baada ya
dakika zisizopungua tano askari walilazimika kufyatua risasi angani ili
kutawanya waumini hao waliokuwa kwenye vikundi wakipanga kutimiza azma yao.
Baadhi ya polisi wakiwa katika mavazi ya kiraia, walifanya kazi ya ziada
kukamata waandamanaji hao waliokuwa wakikimbilia katika majengo mara askari
walipowakimbiza na kutokana na mazingira ya msongamano wa majengo Kariakoo,
kazi hiyo ilikuwa ngumu.
Bila kuogopa askari hao, waandamanaji walikusanyika hadharani mbele ya
polisi na kupanga mikakati yao ambayo hata hivyo ilikuwa ikivunjika kwa polisi
kuwakimbiza na kuwakamata.
Hata hivyo, idadi kamili ya waliokamatwa haikuweza kujulikana mara moja
kutokana na viongozi wote wa Polisi eneo hilo kuwa na majukumu ya kuhakikisha
usalama unakuwapo eneo hilo.
Katika hali isiyo ya kawaida, waandamanaji walishangilia kila risasi au
bomu yalipofyatuliwa huku wakikimbia na baadhi ya waliokuwa wakipita katika
mitaa hiyo hususani wanawake, waliangua vilio kwa hofu ya milio hiyo.
Vurugu hizo pia zilijitokeza eneo la Msikiti wa Kichangani, Magomeni
ambazo hata hivyo zilizimwa baada ya polisi kuweka ulinzi wa kutosha eneo hilo.
Mashuhuda katika eneo la Kinondoni walisema mchana yalionekana malori
yaliyojaa askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ) wenye silaha yakipita
jirani na Msikiti wa Mtambani kuelekea Magomeni.
Pamoja na malori hayo ya JWTZ mashuhuda pia walielezea kuonekana kwa
helikopta katika maeneo ya Jiji la Dar es Salaam ya Kariakoo, Magomeni na
Kinondoni iliyoruka kuangalia hali ya
usalama.
“Hali ni mbaya sana hapa Kariakoo polisi wanapambana na waumini wa dini
ya Kiislamu. Kwa ujumla hali ni tete sana, kila mmoja anakimbia kuokoa maisha
yake ... maduka yamefungwa. Kariakoo yote iko kimya kwa mara ya kwanza tangu
niifahamu, hali ni mbaya sana … ndugu na jamaa wanakimbia huku na kule.
“Kuna polisi wengi sana wamesheheni silaha za kila aina, magari ya maji
ya kuwasha na silaha zingine, mbele
yangu naona kundi la watu wanakimbia. Kwa ujumla Kariakoo yote si shwari. Niko
mbele ya kituo cha Polisi Msimbazi nikiongozana na askari kwa ajili ya usalama
wangu,” alisema shuhuda aliyejitambulisha kwa jina la Mohamed Ismail wa
Kariakoo kwa njia ya simu.
Habari zaidi kuhusu vurugu hizo zilisema waandamanaji walipambana na
askari Polisi kwa kuwarushia mawe, Kariakoo na Magomeni huku polisi wakitumia
mabomu ya kutoa machozi.
Kabla ya vurugu hizo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck
Sadiki alikutana na waandishi wa
habari ofisini kwake asubuhi kutoa tamko
kuhusu hali ilivyo jijini.
Katika tamko lake, Mkuu wa Mkoa alisema kumeibuka vitisho vya hapa na
pale Dar es Salaam baada ya kukamatwa kwa Shekhe Ponda Issa Ponda ambaye anajulikana
kama Katibu wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu, hatua aliyosema Serikali
inakabiliana nayo.
“Mpaka sasa wametoa taarifa kuwa kutakuwa na maandamano kuelekea Ikulu
ili kushinikiza kuachiwa huru kwa Shekhe Ponda na wafuasi wake.
“Maandamano hayo hayana kibali chochote ila ni kutaka kuibua vurugu na
uvunjifu wa amani Dar es Salaam, hivyo naomba wananchi kutokushiriki maandamano
hayo, kwani kufanya hivyo hatua kali
zitachukuliwa dhidi yao.
“Ni lazima tufike mahali tuishi kwa kufuata misingi ya taratibu na
sheria kwani Shekhe Ponda hakukamatwa kama Shekhe, bali kama mchochezi wa
vurugu na kushawishi wafuasi wake kuidharau Serikali na vyombo vya usalama.
Hivyo amekamatwa kama mtuhumiwa mwingine yeyote.
“Hivyo yatupasa tuwe na subira na kufuata taratibu kwani kama Shekhe
Ponda hana hatia ataachiwa na kama anayo, atahukumiwa kama ilivyo kawaida kwa
mtuhumiwa apatikanaye na hatia. Lazima tujue kuwa nchi inaongozwa kwa misingi
ya taratibu na sheria na hakuna aliye juu ya sheria,” alionya Mkuu wa Mkoa.
Katika hatua nyingine, alipiga marufuku
mihadhara ya kidini kwa sasa hadi hali itakapokuwa shwari. Shekhe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa aliwataka waumini wa dini
ya Kiislamu kuvuta subira katika kutatua suala hili na wasijipange kufanya
vurugu ya aina yoyote, kwani suala hilo limeshafika katika vyombo vya sheria,
hivyo waviachie vyombo hivyo vifanye
kazi na haki itajulikana baadaye.
Shekhe huyo alieleza kuridhishwa kwake na maneno ya maaskofu katika
kuwataka waumini wao kuwa watulivu na si kulipiza kisasi. Lakini pia alitaka
Waislamu nao watulie katika hilo.
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Padri Anthony Makunde
alisema anaungana na viongozi wengine wa makanisa kusisitiza viongozi wa dini
ya Kikristo kuendelea na subira katika kipindi hiki, kwani njia pekee na sahihi
ya kutafuta suluhu na amani ni mazungumzo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema Jeshi
la Polisi linaungana na Mkuu wa Mkoa kukabiliana na vurugu jijini. Alisema mtu yeyote akifanya kosa atakuwa mhalifu kwa sababu sheria
haibagui wala kuchagua, inakata kotekote haiangalii kama ni Padri au Shekhe.
Kuhusu maandamano Kamanda Kova alisema: “Jeshi la Polisi limejipanga
vema kukabiliana na mtu yeyote hivyo ajitahidi kutafakari mara mbili itakuwaje baada
ya hapo kwake na familia yake.
Aliwataka Mukadam Salehe, Kondo Juma, Saaban Mapeo, Jaffary Mneke,
Rajabu Katimba na Amani Moshi kujisalimisha Polisi vinginevyo sheria itafuata
mkondo wake.
Hali ya ukosefu wa amani imeendelea kuikumba Zanzibar baada ya jana
vurugu kubwa kutanda katikati ya mji wa Unguja, huku milio ya mabomu na vilio
vya wananchi vikisikika wakati wa mapambano baina ya vikundi vya wana Uamsho na
Polisi.
Katika vurugu hizo, majengo yalishambuliwa na vijana Mji Mkongwe,
likiwamo Kanisa Kuu la Anglikana Zanzibar lililopo Mkunazini ambalo
lilinusurika kulipuliwa kwa moto, huku baadhi ya vifaa vyake vikiwamo viyoyozi
vikiharibiwa.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Kanisa hilo ambaye hakuwa tayari kutaja jina
lake gazetini kwa sababu za kiusalama, alisema kundi la vijana likiwa na
petroli lilivamia Kanisa saa sita usiku wa kuamkia jana kwa lengo la kulilipua.
Hata hivyo, mmoja wa wamiliki wa nyumba jirani, Mohammed Ally, baada ya
kuona hatari hiyo aliwasihi kutofanya hivyo kwa kuhofia hasara kwa nyumba za
jirani ikiwamo yake.
Barabara inayokwenda katika Kanisa hilo hadi Benki ya CRDB iliharibiwa
kwa vizuizi vya magogo yaliyotiwa moto.
Ofisa Mwandamizi wa Kanisa hilo, John Mwakanjuki aliiomba Serikali
kuyapa ulinzi makanisa ambayo yanaonekana kulengwa na vijana wanaofanya fujo.Katika fujo za juzi, Salum Hassan Muhoja (30) inadaiwa aliuawa kwa
kupigwa risasi akiwa katika jaribio la
kufanya uporaji kwenye baa iliyopo Amani inayomilikiwa na mfanyabiashara
maarufu Mbawala.Baa hiyo ilivunjwa juzi na watu wanaoaminika kuwa wafuasi wa Uamsho siku
ya kwanza ya vurugu hizo huku ikichomwa moto na bidhaa kadhaa kuporwa.Kijana huyo inadaiwa alipigwa risasi na walinzi wa vikosi vya Serikali
ya Mapinduzi akiwa katika jaribio la
kuiba vifaa wakiwa na gari.Hata hivyo, akizungumza na mwandishi wa habari hizi Kaimu Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Said Juma Hamis alisema hadi jana Polisi
haikuwa imepata taarifa za kuuawa kwa kijana huyo zaidi ya kifo cha polisi.
Kamanda Hamis alisema hadi jana jumla ya watuhumiwa waliokamatwa ni 50
huku watuhumiwa wanane wakifikishwa mahakamani na wengine wanaendelea kuhojiwa
Polisi.
Alisema pia Polisi inaendelea na juhudi za kumtafuta kiongozi wa Jumuiya
ya Uamsho, Shekhe Farid Hadi Ahmed ambaye inadaiwa ametekwa.
No comments:
Post a Comment