Dk Willibrod Slaaa na aliyekuwa mkewe, Rose Kamili. |
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia
mbali pingamizi lililowekwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa,
katika kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa mkewe, Rose Kamili akipinga ndoa kati ya
mumewe huyo na mchumba wake wa siku nyingi, Josephine Mushumbusi.
Jaji Lawrence Kaduri anayesikiliza kesi hiyo akisoma uamuzi jana,
alisema Kamili alikuwa sahihi kuwasilisha kesi hiyo mahakamani na hivyo
anatupilia mbali pingamizi la Dk Slaa na kupanga kesi hiyo itajwe tena Desemba
6.
Dk Slaa katika pingamizi lake alikuwa akidai kuwa Kamili hakuwa mkewe
halali na hivyo hakupaswa kufungua kesi mahakamani.
Aidha, alidai pia kuwa suala la ndoa halikupaswa kuwasilishwa mahakamani
kama la madai, bali kwa kutumia hati ya kuitwa mahakamani ikiambatanishwa na
kiapo cha mdai.
Kiongozi huyo wa Chadema na Josephine walipanga kufunga ndoa Julai 21
mwaka huu wilayani Karatu mkoani Arusha, lakini Kamili aliwasilisha pingamizi
mahakamani kupinga ndoa hiyo.
Kamili katika kesi hiyo anadai fidia ya Sh milioni 550 za gharama ya
malezi ya familia na usumbufu aliopata kwa kutelekezwa na mumewe. Kesi hiyo
ilifunguliwa na kusajiliwa kwa namba 5 mwaka huu.
Kwa mujibu wa hati ya madai, Kamili anadai yeye na Dk Slaa ni wanandoa
na Josephine ndiye alisababisha Dk Slaa atelekeze familia, akidai walifunga
ndoa mwaka 1985 na Juni 18, 1987 wakajaliwa mtoto wa kwanza wa kike Emiliana na
wa pili Septemba 23, 1988 Linus, na maisha yao awali yalikuwa ya upendo.
Anadai kuwa kabla ya hapo, Dk Slaa alikuwa padri, lakini kwa ridhaa yake
aliacha kazi hiyo ili aishi na familia yake na kutimiza majukumu yake katika
ndoa hiyo.
Aidha, alidai kuwa kuanzia hapo yeye na mdaiwa waliishi nyumba moja
baada ya Dk Slaa kuacha utumishi wa
Mungu kama mke na mume na walitambuliwa kuwa wanandoa, kwa sababu taratibu zote
za ndoa zilifuatwa na familia zote mbili ambazo zinatambua hilo.
No comments:
Post a Comment