TIMU YA AZAM YAMTIMUA TENA KOCHA WAKE...

Kikosi cha timu ya soka ya Azam.
Uongozi wa timu ya soka ya Azam umemtimua tena kocha wake Mserbia Boris Bujak ‘Buka’ kwa madai ya kutoridhishwa naye.
Mserbia huyo amefukuzwa ikiwa ni miezi mitatu tu tangu achukue jukumu la kuinoa timu hiyo kutoka kwa Muingereza Stewart Hall, ambaye naye alitimuliwa kwa tuhuma kama hizo baada ya kuifanya timu hiyo kushika nafasi ya pili katika michuano ya Kombe la Kagame ambapo ilifungwa na Yanga mabao 2-0 Julai mwaka huu.
Habari za uhakika kutoka kwa baadhi ya wachezaji wa Azam zilizopatikana Dar es Salaam jana, zilisema, uongozi wa timu hiyo umeamua kumrudisha kocha wake Hall ambaye kwa sasa anaifundisha Sofapaka ya Kenya.
“Kocha Buka amefukuzwa hivi ninavyokwambia ameshalipwa haki zake zote na ameshakatiwa tiketi yake Ijumaa anaondoka, mechi zijazo timu itakuwa chini ya kocha msaidizi Kally Ongala mpaka Hall atakapokuja… na hatachelewa kuja kwa maana Sofapaka hana mkataba,” alisema mtoa habari wetu.
Habari zaidi zinasema kuwa sababu ya Azam kumtimua kocha huyo ni kutoridhika na kiwango kinachooneshwa na timu tangu kupewa jukumua la kuinoa.
Timu hiyo mwishoni mwa wiki ilifungwa mabao 3-1 na Simba, katika mechi ya Ligi Kuu Bara na ushindi wa juzi wa Coastal Union umeishusha hadi nafasi ya nne kwenye msimamo ikiwa na pointi 18.
“Lakini pia hata sisi wachezaji hatukumbali, hivyo wengine walikuwa na kamgomo baridi, hata katika mechi na Simba, kulikuwa na mzozo kwenye benchi, baadhi ya wachezaji wakilaumiana kufanya hujuma ili kocha aondolewe, wale ambao hawamkubali walicheza chini ya kiwango kwa makusudi,” alisema mtoa habari wetu.
Msemaji wa Azam, Jaffar Iddi hakuwa tayari kulizungumzia hilo kwa madai alikuwa hajafika ofisini mpaka saa tisa alasiri jana.
Mbali na kuiongoza Azam kushika nafasi ya pili kwenye michuano ya Kombe la Kagame, Hall ambaye awali alikuwa kocha wa timu ya taifa ya Zanzibar, aliiongoza timu hiyo kushiriki michuano ya kimataifa mwaka huu baada ya kushika nafasi ya pili msimu uliopita nyuma ya Simba.

No comments: