RAIS KIKWETE AWACHARUKIA WANAOFAGILIA UDINI, UKABILA...

Rais Jakaya Kikwete akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge wa mwaka huu, Kapteni Honest Mwanossa wakati wa sherehe za kuzima Mwenge zilizofanyika kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga jana. Wa pili kushoto ni Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara.
Rais Jakaya Kikwete amewataka Watanzania kukataa kugawanywa kwa misingi ya dini na ukabila ikiwamo kutumiwa kutoa maoni katika mchakato unaoendelea wa kukusanya maoni kwa ajili ya Katiba mpya.
Akizungumza katika sherehe za kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru mjini Shinyanga jana, alisema sherehe hizo zimeambatana na Kumbukumbu ya miaka 13 ya kifo cha Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye alipiga vita mgawanyo wowote wa rangi, udini na ukabila.
Rais Kikwete alisema ingawa ni miaka 13 sasa tangu kifo cha kiongozi huyo mashuhuri nchini, lakini hawezi kusahaulika kutokana na mema aliyowafanyia Watanzania ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha na kuhamasisha umoja na mshikamano na kuwapatia uhuru.
“Ameacha nchi yenye upendo, umoja na amani licha ya watu wake kuwa na tofauti ya rangi, dini na kabila, haya yote yanatosha kujenga mshikamano, tusikubali kugawanywa, ndio maana Waswahili wanasema msione vinaelea vimeundwa amani na mshikamano umeundwa na Nyerere,” alisema.
Alisema kiongozi huyo alitengeneza sera nzuri zenye lengo la kuwainua wananchi na sasa katika kumbukumbu ya kifo chake njia bora ni kutekeleza sera hizo bila kuwapa nafasi wanaotaka kuvunja sera hizo wawe watu binafsi, wanasiasa au vyama vya siasa.
“Nawaombeni watu wa aina hii tusiwape kipaumbele kwa kuwa hawatutakii mema, tukiwaendekeza watatupeleka pabaya, majuto ni mjukuu, tuendelee kukataa kugawanywa kwa misingi ya kidini na ukabila, tuwe wamoja licha ya tofauti zetu za ukabila na dini,” alisisitiza.
Kuhusu mchakato unaoendelea wa kukusanya maoni ya Katiba mpya, Rais Kikwete aliwataka Watanzania katika maeneo ambayo bado Tume ya Kukusanya Maoni inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba wajitokeze kwa wingi kutoa maoni yao.
Hata hivyo, aliwatahadharisha kuepuka kutumiwa katika kutoa maoni hayo na kuhakikisha kuwa wanachangia maoni yao na mabadiliko wanayotaka yaingizwe kwenye Katiba hiyo mpya.
“Nawaombeni Watanzania mjitokeze kwa wingi kutoa maoni yenu, epukeni kutumiwa wala kulishwa maneno na mtu yeyote, msikubali kugeuzwa redio kaseti au santuri ya mtu,” alisisitiza.
Alisema mpaka sasa Tume ya Kukusanya Maoni katika awamu yake kwanza na ya pili imefanya mikutano 842 katika mikoa 15 Zanzibar miwili na Tanzania Bara 13 na watu 517,427 walihudhuria ambao kati yao zaidi ya 29,414 walitoa maoni yao kwa mdomo na 120,000 walitoa kwa njia ya maandishi.
Alisema awamu ya tatu inaendelea sasa ambapo Tume hiyo itatembelea mikoa tisa Zanzibar miwili na Tanzania bara saba. “Natarajia awamu ya nne na ya mwisho ya ukusanyaji huu wa maoni inaweza ikakamilika kabla ya mwaka huu,” alisema.
Akizungumzia tatizo la ugonjwa wa Ukimwi, Rais Kikwete alisema kwa sasa Tanzania imepiga hatua na ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa upimaji wa virusi vya ugonjwa huo duniani ambapo hadi sasa watu milioni 12.2 wamepima kwa hiari.
Alisema elimu kupitia kwenye jamii, shuleni imesaidia kwa asilimia 80 kupunguza kasi ya maambukizo ya ugonjwa huo ambao kwa sasa umepungua kwa asilimia 5.7 ingawa bado idadi ya wanaoambukizwa ni wengi kwa kuwa takwimu zinaonesha kati ya watu 100, watu sita wameathirika.
Alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha kasi ya maambukizo ya ugonjwa huo inapungua kutoka asilimia 25 ya sasa na kufikia asilimia 50 hadi 90 ambapo pia alibainisha kwa sasa asilimia 57 ya walioathirika wameanza kutumia dawa za kuongeza maisha ARVs huku asilimia 43 wakisubiri ushauri wa daktari.
Kuhusu dawa za kulevya Rais Kikwete, alisema kwa sasa bado tatizo hilo ni kubwa nchini ambapo pamoja na kupunguza nguvu kazi ya Taifa, kuongeza kasi ya maambukizi ya Ukimwi pia limesababisha vijana wengi nchini kuwa mazezeta.
Alisema Serikali kupitia Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya na Kikosikazi alichokiunda mwaka huu imekamata kilo 250 za heroin, tani 150 za kokeini, tani 45 za bangi na mirungi tani sita huku watuhumiwa 44 wakikamatwa kwa tuhuma za kukutwa na dawa hizo za kulevya.
“Ninawaambia kamwe Serikali haitokubali kushindwa katika hili wala kuacha Taifa liangamie kwa kuwa na vijana wengi mazezeta, naombeni wananchi tushirikiane kuwafichua wanaouza na wanaonunua kwani watu hawa ni wauaji, jamani ajizi nyumba ya njaa,” alisema.
Kwa upande wa rushwa, Rais alisema pamoja na Serikali kujitahidi kupambana na tatizo hilo bado ni kubwa na kuwataka wananchi wasiiachie Serikali na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kukabiliana na tatizo hilo pekee.
“Vita hii dhidi ya rushwa ni ya kila mtu awe raia, mgeni, mtumishi wa umma, mfanyabiashara, mtu binafsi wote tunahusika katika kupambana nayo,” alisisitiza.
Kwa upande wa vijana, Rais Kikwete aliwataka waache uvivu na uzembe wa kukimbilia vijiweni kucheza pool na badala yake wajitume.

No comments: