ALHAJI SHAABAN MINTANGA AACHIWA HURU...

Alhaji Shaaban Mintanga (kulia) afuatilia hukumu yake Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imemuachia huru aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Ngumi nchini  (BFT), Alhaji Shaban Mintanga baada ya upande wa Mashitaka kushindwa kuthibitisha mashitaka na hivyo Mahakama hiyo kumkuta mshitakiwa hana kesi ya kujibu.
Uamuzi huo ulitolewa leo na Jaji aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, Jaji Dk Fauz Twaib baada ya kusikiliza mashahidi wanne wa upande wa Jamhuri na mwisho kuamua kufunga ushahidi wao baada ya upande huo kukwama kuleta mahakamani mashahidi wengine katika kipindi kirefu huku wakidai kuwa mashahidi hao ambao ni muhimu wako  Mauritius.
Kesi hiyo leo ilikuja mahakamani kwa ajili ya uamuzi wa kama mshitakiwa ana kesi ya kujibu au la, ndipo Mahakama hiyo ilifikia uamuzi wa kumuachia huru kwasababu kwa mujibu wa mashahidi wote wanne waliotoa ushahidi hakuna ushahidi wa moja kwa moja kwamba mshitakiwa alitenda makosa hayo.
Katika kesi hiyo ambayo Mintanga alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Julai 2008 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na upelelezi ulipokamilika alifikishwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa, Mintanga alikuwa akituhumiwa kula njama na kusafirisha dawa za kulevya zenye uzito wa kilo 4.8, kutoka Tanzania kwenda Mauritius kwa kuwatumia wachezaji wa timu ya Taifa ya Ngumi za Ridhaa. 
Jaji huyo katika uamuzi wake alisema swali la kujiuliza ilikuwa ni je upande wa Mashitaka umeweza kuonesha mshitakiwa kuhusika katika mashitaka hayo? Hata hivyo alisema kwa mujibu wa ushahidi imethibitika kuwa ushahidi uliotolewa ni dhaifu hakuna ushahidi unaoonesha Mintanga alikula njama na alisafirisha dawa za kulevya kama inavyodaiwa katika mashitaka.
“Ushahidi pekee uliotolewa na kumgusa ni wa shahidi Christopher Mutarukwa kuwa namba ya simu ya mshitakiwa ndiyo iliyofanya mawasiliano kukata tiketi zilizowasafirisha washitakiwa waliokamatwa Mauritius wakiwa na dawa za kulevya hata hivyo barua mbalimbali za BFT zilikuwa zikitumia namba hiyo ya simu,” alisema Jaji Twaib. 
Aidha ushahidi wa shahidi Nassoro Irenge umeonesha kwamba Mintanga aliwatambulisha kwake washitakiwa hao katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere lakini hata hivyo hajui dawa hizo zilisafirishwaje lakini watu hao walikamatwa  Mauritius. 
Jaji huyo alisema anaungana na hoja ya Wakili wa mshitakiwa, Jerome Msemwa kwamba hakuna ushahidi wa dawa zilizokamatwa ulioletwa mahakamani hata picha zilizopigwa dawa hizo, hata hivyo hakuna ushahidi pia kuwa zilikuwa dawa za kulevya kwasababu hazikuletwa mahakamani.
Pia kulikuwa na utata wa uzito wa dawa hizo za kulevya, ushahidi wa upande wa Mashitaka ulidai Kamishna wa Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya Christopher Shekiondo alikadiria uzito na thamani za dawa hizo bila kuziona. Vilevile kwasababu dawa hizo zilikamatwa Mauritius hakuna ushahidi wa dawa hizo na kesi hiyo ambayo inamkabili mshitakiwa Mintanga.
Ni wazi udhaifu wa upande wa Mashitaka umejionesha kwasababu umeshindwa kuwasilisha mahakamani cheti bali Kamishna alikusanya ushahidi wake kwa kupiga simu tu Mauritius, kwa mujibu wa ushahidi wa Charles Ulaya ambaye ni mpelelezi wa shauri alidai uzito wa dawa hizo ulikuwa kg 4.8 na ushahidi mwingine unaonesha ni kg 6.
Jaji huyo alisema pia kuwa kuna utata kwa mujibu wa Ulaya mtu aliyetajwa kwa jina la Mika ambaye bado anatafutwa ambaye ndiye anayedhaniwa kuhusika na usafirishaji wa dawa hizo kwasababu ndiye aliyetajwa na washitakiwa walioshikiliwa Mauritius kuwa walipewa dawa hizo na Mika katika Hoteli iliyoko Manzese. Katika maelezo waliyoandikisha huko walieleza kuwa Mika ndiye walikuwa wakiwasiliana naye.
Katika uamuzi huo, Jaji huyo alisema kuwa kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashitaka Mika ndiye aliyetakiwa kuhusishwa na mashitaka hayo kwasababu ndiye aliyekuwa akiwasiliana na mwanamke waliyekutana naye Kenya na pia ndiye aliyewapa fedha  na sio mshitakiwa Mintanga.
Upande wa Mashitaka, Jaji Twaib alisema kuwa umeshindwa hata kuthibitisha ni wapi na lini mshitakiwa alikula njama ya kusafirisha dawa hizo za kulevya na hivyo kumuachia huru mshitakiwa kwa kifungu cha sheria namba 293 (1) ya mwenendo wa makosa ya jinai.
Nchini Mauritius, mabondia  Petro Mtagwa, Elia Nathaniel, Ally Msengwa na Emilian Patrick waliokamatwa na dawa hizo wakiwa wamemeza tumboni walipohojiwa  walieleza kuwa dawa hizo walipatiwa na mtu anayeitwa Mika na aliwamezesha dawa hizo katika hoteli moja iliyoko Manzese na aliwapatia dola 1,000 za Marekani kwa kila mmoja  Agosti 10, 2008.

No comments: