RAIS KIKWETE AKERWA NA WAISLAMU WALIOSHAMBULIA MAKANISA MBAGALA...

Rais Jakaya Kikwete akioneshwa moja ya uharibifu uliofanywa na kundi la watu wanoaminika kuwa ni waumini wa dini ya Kiislamu kupinga kitendo cha kijana mmoja aliyekojolea kitabu kitakatifu cha Qur'an, wakati alipofanya ziara ya ghafla huko Mbagala, Dar es Salaam jana.
“Jamani poleni sana…Nimekuja kuwapeni pole kwa tukio lililotokea. Ni mambo  yanayosikitisha, yanayotia fedheha na yanayoleta aibu kwa Taifa la Tanzania.
“Ni tukio linalotia doa undugu na urafiki baina ya Waislamu na Wakristo uliodumu nchini kwa miaka mingi sana nyuma. Ni kweli kwamba kijana aliyekojolea kitabu ya Kurani alifanya kosa, lakini kosa hilo lilikuwa tayari limedhibitiwa na vyombo vya kisheria.
“Kitendo cha kushambulia makanisa ambayo pengine hata hayakumtuma na pengine hayamfahamu kabisa kijana yule ni cha fedheha, aibu na kinaleta masikitiko makubwa sana. Nimeambiwa tayari watu 122 wamekamatwa na 36 kati yao ni wale waliokuwa wamelizunguka kanisa, nataka niwahakikishie kwamba hatua kali zitachukuliwa kwa wote waliohusika.”
Hiyo ni kauli ya Rais Jakaya Kikwete ambaye jana alifanya ziara ya ghafla ya kuyatembelea makanisa yaliyoshambuliwa na kuharibiwa vibaya na watu wanaodaiwa kuwa ni waumini wa dini ya Kiislamu wanaodaiwa kukasirishwa na kitendo cha kijana mkazi wa Chamazi, Mbagala Dar es Salaam kukojolea na kutemea mate Kurani, Jumatatu wiki hii.
Tofauti na alivyozoeleka, Rais Kikwete aliyewasili katika Kanisa la Kiinjili la Kirutheri (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Jimbo la Kusini, Usharika wa Mbagala saa 12.30 jioni jana, alikuwa mwenye nyuso ya huzuni huku sauti yake ikidhihirisha kusikitishwa na tukio hilo.
Alipowasili Rais Kikwete alilakiwa kwa kilio na baadhi ya waumini waliokuwa wamekusanyika kanisani hapo kumlaki kiongozi wao wa nchi, kilio ambacho kilikoma baada ya Rais kuanza kuwahutubia kwa kuwapa pole huku akiwataka kuwa watulivu na wenye moyo wa kutokukubali kulipiza kisasi.
“Ombi langu ni kwa viongozi kukabili changamoto ya kufanya kazi katika mazingira magumu. Uamuzi wa watu kuvamia makanisa na kufanya uharibifu kama huu ni uamuzi wa makosa.
“Sitarajii kama Kanisa linaweza kuwa na moyo wa kulipiza kisasi kwa tukio kama hili maana kisasi hakisaidii sana na badala yake tutazidi kuivuruga nchi yetu. Kitendo hiki kinaweza kujenga picha kwamba kuna ugomvi mkubwa sana baina ya Waislamu na Wakristo katika nchi yetu ya Tanzania, jambo ambalo si sahihi.
“Nawahakikishia hakuna yoyote aliyehusika na tukio hili ambaye ataachwa. Hata wale watakaobainika walihusika kwa kutoa maelekezo au kwa kushinikiza wakiwa mahala popote watakamatwa na kushughulikiwa. Naomba tuviache vyombo vya sheria vifanye kazi yake. Ni jambo baya ni jambo la aibu na fedheha sana kwa nchi ya Tanzania,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete katika ziara yake hiyo alishuhudia kuchomwa moto na kuteketea kwa madhabahu ya kanisa hilo, kuvunjwa na kuibwa kwa fedha katika ofisi ya Chama cha Akiba na Mikopo (Saccos) kanisani hapo, kuharibiwa kwa madirisha, milango, vinanda na mali nyingine za kanisa hilo. Alipata nafasi pia ya kuyatembelea makanisa ya TAG na Anglikana ambayo pia yalishambuliwa na kuharibiwa katika tukio hilo.
Awali akimkaribisha Rais kuzungumza na waumini, Askofu Msaidizi wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Jimbo la Kusini, George Fupe, aliwataka waumini kuwa watulivu hasa baada ya Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Askofu Alex Malasusa kuwataka kuvaa nyoyo za uvumilivu na subira kutokana na tukio hilo.

2 comments:

Anonymous said...

Heya i'm for the first time here. I found this board and I find It truly useful & it helped me out a lot. I hope to give something back and aid others like you helped me.
Stop by my web blog ... keyword

Anonymous said...

“Kitendo cha kushambulia makanisa ambayo pengine hata hayakumtuma na pengine hayamfahamu kabisa kijana yule ni cha fedheha, aibu na kinaleta masikitiko makubwa sana".
Hayo ni maneno ya Mhe. Rais ............ pengine hata hayakumtuma na pengine na pengine hayamfahamu .......... ni maneno gani yanayoongelewa na Mhe. Rais. Hii ni kuleta chuki, mhe. Rais tuseme ana wasiwasi labda hayo makanisa yamemtuma na yanamfahamu huyo kijana. Nina wasiwasi na yeye alikuwepo kwenye hizo vurugu tena ni mmojawapo wa viongozi wa hizo vurugu.