POLISI WAUA MAJAMBAZI WATANO MOSHI...

Kamanda Robert Boaz
Polisi mkoani Kilimanjaro imeua watu watano wakituhumiwa kufanya ujambazi katika duka la mfanyabiashara Moshi Vijijini ambapo walimjeruhi mlinzi wa duka hilo kwa sime.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Robert Boaz jana alimtaja mfanyabiashara aliyeibiwa kuwa ni Gaudence Temu (39) na mlinzi aliyejeruhiwa ni Hamisi Juma (25).
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda Boaz alisema watuhumiwa hao walivamia duka hilo saa saba usiku wa kuamkia jana katika kijiji cha Kyala, Marangu Kitowo.
Kwa mujibu wa Kamanda Boaz, watuhumiwa hao walivamia duka hilo na kuiba sinki la choo na chokaa; walinzi wa sungusungu waliposikia kelele za kuomba msaada kutoka kwa mmiliki wa duka hilo, walijitokeza kusaidia.
Alisema majambazi hao waliwashambuliwa kwa mapanga baadhi ya sungusungu na kuwajeruhi Richard Temu (33) na Eric Yuda (30) ambao wamelazwa katika hospitali ya Kilema kwa matibabu.
Baada ya shambulio hilo, Kamanda Boaz alisema taarifa za uvamizi huo zilifika Polisi na kwa haraka askari wa doria walifika kutoa msaada na kukuta watuhumiwa wametoweka.
Kutokana na hali hiyo, Kamanda Boaz alidai polisi walifanya ufuatiliaji wa kina na kubaini maficho ya watuhumiwa hao katika nyumba ya mmoja wao kijijini Kyala.
Kamanda alisema askari walifika kwenye nyumba hiyo na walipojaribu kufungua mlango huku wakiwataka majambazi hao wajisalimishe walikataa.
Kutokana na ukaidi huo, polisi walitupa bomu la machozi ndani ya nyumba hiyo na kusababisha watuhumiwa hao kutoka nje huku wakifyatua risasi ambazo zilimjeruhi  mguu wa kushoto askari namba G 406 Konstebo Lameck.
"Kutokana na hali hiyo askari nao walijibu mapigo na kuua majambazi watano waliojaribu kutoroka kutoka nyumba hiyo na kati yao, wanne wametambuliwa na mmoja bado," alisema Kamanda Boaz.
Kwa mujibu wa Kamanda katika eneo la tukio vilikutwa vitu vilivyoonesha kuwa vya wizi ikiwamo bunduki aina ya shotgun Greener namba 858356, risasi nne na maganda ya risasi.
Kamanda Boaz alisema kuwa bunduki hiyo iliibwa Septemba 15 katika kijiji cha Chemchem wilaya ya Moshi kwa Karibia Mmari.
Mbali na bunduki hiyo, Kamanda alisema walikuta pia bastola aina ya Browning namba zake zikiwa zimefutwa, risasi zake mbili, risasi 10 za bunduki aina ya SMG, mapanga na sime zenye damu, mkoba wenye mabomba ya sindano na uzi wa kushonea na zana mbalimbali za kuvunjia.
Alivitaja vitu vingine kuwa ni pamoja na godoro, televisheni, redio aina ya Sea, piano, masufuria, vitambaa vya mapambo, chokaa, masinki ya choo na ya kunawia, vitambaa vipya vya suruali, viatu, DVD, nyama za mbuzi na kondoo waliochinjwa zikiwa kwenye ndoo.
Kamanda alisema baadhi ya mali zimetambuliwa na wananchi walioporwa katika matukio tofauti na miili ya majambazi hao imehifadhiwa katika mochari ya Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi.
Polisi ilitoa mwito kwa wananchi kuimarisha vikundi vya ulinzi katika maeneo yao na kuwa wepesi wa kutoa taarifa za wahalifu Polisi ili hatua zichukuliwe pia haraka.

No comments: