BASIL MRAMBA AWASUKUMIA 'JUMBA BOVU' YONA NA MGONJA...

KUTOKA KUSHOTO: Gray Mgonja, Daniel Yona na Basil Mramba.
Aliyekuwa Waziri wa Fedha katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Basil Mramba amedai mahakamani kwamba aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Gray Mgonja alimshauri asaini taarifa ya Serikali ya kuisamehe kodi kampuni ya Alex Stewart Government Business Assayers.
Mramba alitoa madai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati akijitetea katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi na kusamehe kodi kulikoisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7.
Akiongozwa na Wakili Peter Swai, Mramba alidai kuwa alisaini taarifa ya kusamehe kodi kampuni hiyo, kwa kuwa katika mkataba kati ya Serikali na kampuni hiyo, kuna kipengele kinachoeleza kuwa vifaa vyote vitakavyoingizwa nchini katika utelezaji wa mradi wa ukaguzi wa dhahabu, vitasamehewa kodi.
Alidai kuwa alishauriwa kusaini taarifa hiyo na waliokuwa makatibu wake ambao ni Gray Mgonja na Peniel Lyimo na walifanya hivyo, kwa kuwa Waziri hushauriwa na Katibu katika mambo ya kiutawala na katika mambo ya kisheria hushauriwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mramba alidai, hakuhusika kumtafuta mwekezaji huyo bali kazi yake ilikuwa ni kuhakikisha Benki Kuu inatoa fedha za kuanzia na kuweka mradi katika mfumo wa bajeti.
Pia alidai kupata kibali kutoka Baraza la Mawaziri, cha kuwasilisha bungeni bajeti ya nyongeza ambayo ilipitishwa na wabunge.
Kwa mujibu wa madai ya Mramba, hakuna hasara yoyote aliyosababisha na hata mashahidi wawili wa upande wa mashitaka, walielea wazi kuwa mkataba huo ulifuata sheria, utaratibu na kanuni zote kwa kuwa kodi ikishasamehewa, hakuna mtu anayepaswa kusema amepata hasara.
Aidha, alidai kampuni hiyo ilileta mafanikio makubwa nchini, ikiwamo kuandaa wataalamu wengi wa masuala ya ukaguzi wa migodi ambao walitumika kuanzisha Wakala wa Ukaguzi wa Migodi nchini.
Mramba aliendelea kudai kuwa mwekezaji huyo, alitoa mafunzo ya jinsi ya kukagua migodi kitaalamu na kifedha kwa Watanzania zaidi ya 30 na Serikali ilipata mitambo mikubwa na ya kisasa ambayo baada ya mkataba kwisha, mwekezaji huyo aliiacha nchini.
Jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji John Utamwa akisaidiwa na Jaji Sam Rumanyika na Msajili Sauli Kinemela, waliahirisha kesi hiyo hadi leo Mramba atakapohojiwa na mawakili wa upande wa mashitaka.
Mbali na Mramba, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Mgonja.
Inadaiwa kuwa kati ya Agosti, 2002 na Juni 14, 2004, Dar es Salaam, washitakiwa wakiwa watumishi wa umma, walitumia vibaya madaraka yao na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7. Washitakiwa hao wanadaiwa kutoa msamaha wa kodi isivyo halali kwa Kampuni ya Alex Stewart ya Uingereza hatua iliyosababisha hasara hiyo.

No comments: