MWAKYEMBE ASHUGHULIKIA RIPOTI YA BANDARI 'NENO KWA NENO'...

Dk. Harrison Mwakyembe.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amesema anaipitia kwa umakini ripoti ya chanzo cha kutofanya vizuri kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na atakuwa akitoa msimamo wake kuhusu maagizo ya ripoti hiyo kila wiki.
Dk Mwakyembe alikabidhiwa matokeo ya uchunguzi huo na Mwenyekiti wa Kamati maalumu aliyoiunda mwishoni mwa Agosti, Bernard Mbakileki juzi.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kupokea ripoti hiyo juzi, alisema kwa kushirikiana na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba, wataisoma mstari kwa mstari na kuyafanyia kazi mapendekezo ya kamati hiyo kuhusu utendaji wa bandari.
“Kama mnavyoiona ripoti hii ni kubwa hii inaonesha kuwa kazi iliyofanyika pia ni kubwa, sasa sisi tunachowaahidi ni kuipitia mstari kwa mstari hakuna kitu tutakachokiacha na tutawataarifu wananchi kila wiki hatua tulizochukua kuhusu maagizo ya ripoti hii,” alisema Dk Mwakyembe.
Kuhusu waliokwepa kuhojiwa na kamati hiyo kwa visingizio mbalimbali, Waziri huyo alisema kamwe hawawezi kuepuka kwa kuwa sasa watahojiwa mbele yake na kama polisi itahusika watahojiwa pia Polisi.
Awali Mbakileki wakati akiwasilisha ripoti, pamoja na kukamilisha kazi ya uchunguzi, alisema walikabiliwa na matatizo ya hujuma kutoka kwa baadhi ya watu waliostahili kuhojiwa, lakini walikwepa kwa visingizio mbalimbali bila kuwataja majina watu hao.
Hata hivyo, Dk Mwakyembe hakutaka kuwataja pia majina watu hao wanaotajwa kukwepa kuhojiwa wakisingizia misiba, kuugua na wengine kuzima simu zao zaidi ya kuihakikishia kamati hiyo lazima watahojiwa mbele yake na mbele ya polisi pale itakapowezekana.

No comments: