WAWAKILISHI WAIKATAA RIPOTI YA UBADHIRIFU SERIKALINI...

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakiwa katika moja ya vikao vyao, mjini Unguja.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamekataa taarifa iliyotolewa na Serikali kuhusu Kamati teule ya Baraza hilo ya kuchunguza matukio mbalimbali ukiwamo ubadhirifu wa mali za Serikali.
Wakichangia ripoti hiyo iliyowasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud jana, wawakilishi walisema ripoti hiyo imeshindwa kugusa na kuwatia hatiani watendaji waliohusika na ubadhirifu na ufujaji wa mali za umma.
Mwakilishi wa Wawi, Saleh Nassor Juma (CUF) akichangia alisema anaikataa ripoti hiyo kwa sababu imekwepa watendaji waliotajwa na ripoti wakihusika na ubadhirifu wa mali za umma wakiwamo wengine kujigeuza madalali wa mali za Serikali.
“Sikubaliani na taarifa ya Serikali kuhusu ripoti ya ubadhirifu wa mali za umma ... ripoti hii haikutia hatiani wahusika wakiwamo watendaji wa Serikali kama mawaziri na makatibu wakuu,” alisema Juma.
Mwakilishi wa Chaani, Jecha Ussi Simai (CCM), alisema anapinga taarifa ya Serikali ambayo haikutia hatiani watendaji wa Serikali wanaojishughulisha na ubadhirifu.
“Mimi nikiwa Mwakilishi pamoja na wananchi wa Chaani tunaikataa ripoti hii kwa sababu inalinda watendaji wa Serikali waliohusika moja kwa moja na ubadhirifu,” alisema Simai ambaye kitaaluma ni mwanasheria.
Mwakilishi wa Viti Maalumu Wanawake, Mwanajuma Faki Mdachi (CUF), alisema Serikali imeidharau ripoti ya Kamati Teule na kusema hakuna makosa yaliyofanywa kwa watendaji wake, kitendo ambacho kinalidhalilisha Baraza la Wawakilishi na kuonekana kuwa waongo.
“Mimi napinga taarifa ya Serikali kuhusu Kamati Teule ambayo inaonesha kwamba hakuna ubadhirifu uliofanywa na watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ),” alisema.
Mwakilishi wa Konde, Suleiman Hemed Khamis (CUF), alisema hivi karibuni Serikali iliunda Tume ya kupambana na rushwa ikiwa na lengo la kudhibiti tatizo hilo, lakini haoni kama kutakuwa na mafanikio katika mapambano hayo kutokana na tabia ya kuoneana chuki katika utekelezaji wa vita dhidi ya vitendo vya ubadhirifu.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi 24 walichangia taarifa ya Serikali kuhusu ripoti ya Kamati Teule ya kuhusu ubadhirifu na tuhuma za watendaji wa Serikali na wote kuikataa ripoti hiyo.
Agosti 9 mwaka jana, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho alikubaliana na uamuzi wa wajumbe wa Baraza kuunda Kamati kuchunguza vitendo vya ubadhirifu serikalini katika taasisi mbalimbali kwa watendaji wake, baada ya wajumbe kuonesha wasiwasi mkubwa.
Ripoti iliyosomwa na Waziri Aboud iliwasafisha kwa kutowahusisha na makosa yoyote aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi katika awamu iliyopita, Machano Othman Said na tuhuma mbalimbali ikiwamo kuuza viwanja vya Serikali.
Machano ambaye kwa sasa ni Waziri wa Nchi asiye na Wizara Maalumu na pia Mwakilishi wa Chumbuni, alihusishwa na tuhuma katika wizara hiyo pamoja na Katibu Mkuu.
Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa ya Serikali inayotokana na ripoti ya Baraza la Wawakilishi, Aboud alikiri kuwapo ukiukwaji wa taratibu za kazi na utumishi ambapo baadhi ya wakurugenzi wamekuwa wakiunda kampuni zao binafsi katika sehemu za kazi na kufanya biashara.
“Taarifa ya Serikali imegundua kuwapo wakurugenzi wanaofanya biashara katika sehemu za kazi na kutaka wachague moja.,” alisema Aboud na kuongeza:
“Mkurugenzi wa Mamlaka ya Anga, Said Iddi Ndobugani anayemiliki kampuni ya Aero Tech, Serikali inamtaka ajiondoe kama anataka kubaki kuendelea na wadhifa wa ukurugenzi serikalini.”

No comments: