KIKWETE AKIRI RUSHWA INAIPELEKA CCM 'KUZIMU'...

Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya  Kikwete amesema vitendo vya rushwa na ununuaji kura vinavyoendelea katika kutafuta uongozi ndani ya chama hicho visipodhibitiwa vitakipeleka pabaya.
Akifunga Mkutano wa Jumuiya ya Wanawake (UWT) juzi mjini hapa, Rais Kikwete alifafanua kuwa vitendo hivyo vitaendelea kuleta makundi ndani ya CCM ambayo yatakifikisha pabaya.
Huku akionesha kusikitishwa na vitendo vya rushwa kwa wanawake ambao wamekuwa wakitumia fedha kununua uongozi ndani ya CCM na hata jumuiya zake, Rais Kikwete alitaka viongozi waliochaguliwa kufanya jitihada za kupunguza mgawanyiko uliotokea baada ya uchaguzi huo.
“Ninasikitika sana kusikia hata wanawake sasa wanajihusisha na utoaji rushwa ili kununua nafasi za uongozi, kitu ambacho ni hatari sana,” alisema Rais Kiwete na kusisitiza kuwa chama kinakoelekea si kuzuri na ni lazima zifanyike jitihada za mabadiliko. 
Katika kupunguza mgawanyiko uliotokea baada ya uchaguzi, Rais Kikwete alitaka wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi UWT walioshindwa wasiweke visasi na walioshinda kutowapiga vijembe walioshindwa na kuwakumbusha kuwa kazi iliyo mbele yao ni kubwa, kwa kuwa CCM hivi sasa inakabiliwa na hali ngumu ya ushindani wa kisiasa.
Alisema demokrasia ya uchaguzi ina athari zake, kwani baada ya uchaguzi kumalizika kuna kazi kubwa ya kujenga umoja na mshikamano ambao kazi ya kwanza ni kuziba nyufa na mipasuko iliyotokea wakati wa uchaguzi
“Ukomavu wa kisiasa na ustahmilivu unahitajika sana. Jambo la kufahamu ni kwamba kugombea ni haki ya mwanachama na pia kila mwanachama ambaye ni mjumbe ana haki ya kumuunga mkono mjumbe anayemwona anafaa.
“Mnaweza kuchukiana kwa mtu kugombea, kwa nini kagombea nafasi yangu, Katiba inasema utakuwa kiongozi miaka mitano nafasi yako ilishakwisha, sasa unaomba upya,” alisema.
Alisema mwanachama hapaswi kumchukia mwenzake kwa vile ameomba nafasi anayoitaka wakati nafasi hiyo ni haki ya kila mwanachama. Pia alitaka walioshinda au kushindwa  wasichukie ambao hawakuwaunga mkono. 
“Ukimchukia mtu aliyetumia haki ya demokrasia kugombea au asiyekuunga mkono utakuwa umeonesha udhaifu wa hali ya juu sana, utakuwa hujiamini, utakuwa kiongozi ambaye daima utaongoza kwa makundi … hawa wangu, hawa si wangu, hakuna mtu wa binafsi, wote ni wa chama”,
“… lazima wote wapewe fursa ya kutumikia jumuiya kwa uwezo wao, sifa yao isiwe hakuniunga mkono, mkifanya hivyo mtaua jumuiya,” alionya.
Alisema uchaguzi una mifarakano lakini kiongozi akipatikana ni lazima aungwe mkono na wa kuonesha mfano ni wale walioshinda, hawapaswi kuwabeza walioshindwa kwa kuwaambia kiko wapi.
Rais Kikwete alisema madhumuni ya CCM yaliyotamkwa katika Katiba ya Chama hicho ni kushinda uchaguzi wa Serikali Kuu na serikali za mitaa, Tanzania Bara na Zanzibar ili kuunda Serikali Kuu na  za mitaa.
“Madhumuni ya msingi ya kuundwa kwa CCM ni kushinda uchaguzi, sisi si chama cha mpira, riadha,  ama utamaduni sisi ni chama cha siasa kazi yetu ni kukamata Dola, tunataka Serikali ya Mtaa na Kijiji iwe CCM na halmashauri iwe mikononi mwa CCM, wabunge na serikali zote mbili ziwe za
CCM,” alisema.
Rais Kikwete alisema Tanzania ni nchi ya kidemokrasia ya vyama vingi, inapozungumziwa kushinda Dola ni kushinda uchaguzi na maana yake ni kupigiwa kura nyingi kuliko wenzao.
Alisema ushindi wa CCM unapatikana kwa kukubaliwa na kuungwa mkono na wananchi wengi zaidi watakaojitokeza kupiga kura na jumuiya za chama zimeundwa kwa ajili ya kusaidia CCM na kila jumuiya ina kazi zake.
“Kwa vile mmemaliza uchaguzi, jipangeni sawa sawa ili mtimize wajibu wenu na kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa viongozi na wanachama,” alisema.
Aliwapongeza kwa kukamilisha uchaguzi wa viongozi watakaoongoza Jumuiya hiyo kwa miaka mitano na hata waliojitokeza kugombea, kwani kuvunjika kwa koleo si mwisho wa uhunzi … uchaguzi si kazi ndogo kuna mambo mengi husemwa.
Aliwataka kushughulikia masuala ya uchumi ya kinamama na si kuhuburi tu maneno ya CCM bila kuwa na msaada wowote.
Awali Mwenyekiti wa UWT, Sofia Simba alisema  wamefanya mengi ikiwamo kuongeza wanachama na wamejipanga kuhakikisha wanaleta ushindi katika uchaguzi mkuu 2015.
Alisema UWT imepiga hatua kubwa na kufanikiwa kupata hatimiliki ya viwanja na mashamba ambayo ni mali ya jumuiya. Alimshukuru Rais Kikwete kwa kutambua uwezo wa wanawake tangu alipoingia madarakani ambapo viongozi wanawake wamekuwa wakiongezeka mwaka hadi mwaka.
Simba alisema hata katika CCM hivyo hivyo idadi ya wanawake katika uongozi imekuwa ikiongezeka na ameendelea kulea Jumuiya hiyo na sasa wamefanikiwa kupata magari matano makao makuu na pikipiki kwa kila wilaya.
Licha ya kuwapa vitendea kazi kwa nyakati tofauti, Simba alisema Rais Kikwete pia amekuwa akitoa msaada wa hali na mali jambo linalochangia mafanikio yao.
Katika uchaguzi uliomalizika juzi UWT, Simba alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa UWT kwa mara nyingine baada ya kupata kura 715 na kumshinda Anne Kilango-Malecela  aliyepata kura 310 na May Rose Majinge aliyepata kura saba.
Akitangaza matokeo hayo Jumamosi saa 7 usiku, Msimamizi wa Uchaguzi huo, Abdul-rahman Kinana, alitaja walioshinda kuwa wajumbe wa Baraza Kuu la UWT na kura zao kwenye mabano kuwa ni  Naibu Waziri wa Fedha, Janeth Mbene (610), Pindi Chana (734), Diana Chilolo (555), Zainab Kawawa (580) na  Betty Machangu (516).
Wengine ni Mbunge wa Ukonga, Eugen Mwaiposa (600) Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Mary Mwanjelwa (517), Shamsa Mwangunga (606) na Subira Mgalu (603).
Aliyechaguliwa Makamu Mwenyekiti wa umoja huo ni Asha Bakari Makame (559) na kumshinda mshindani wake  Asha Abdalah  Juma (403).
Kwa upande wa viti sita vya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM ni Panya Alli  Abdallah (472), Fatma Said Ally (580), Maulide Castico (614), Mbunge wa Koani, Amina Andrew Clement (456), Waride Bakari Jabu (416), na Tauhida Cassian Nyimbo (620).
Wajumbe wa Baraza Kuu la UWT ni  Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mjini, Halima Dendegu (585),
Juliana Manyerere (548), Amina Masenza ( 441), Mbungwa wa Nkenge, Assumpter Mshama (442) na Shamsa Mwangunga (488).
Wengine kutoka Zanzibar ni Mwanajuma Majid Abdallah (433), Khadija Hassan Aboud (442),  Elizabeth Lazaro Mayala (419),  Catherine Peter Nao (666) na Zainab Hamis Shomari (486).
Uwakilishi UVCCM Taifa ni Esther Mambali (682) uwakilishi Wazazi ni Namelok Sokoine (740) aliyemwangusha Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata.

No comments: