Rubani mwanafunzi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kapteni Deo Mangushi amekufa huku mwenzake Kapteni F. Kwidika akijeruhiwa wakati wakijiokoa katika ajali ya ndege waliyokuwa wakiitumia kufanya mazoezi ya mafunzo.
Marubani hao wanafunzi walikuwa katika mafunzo na ndege hiyo na walipoona hatari, walitumia mfumo wa kujiokoa wa ndege hiyo wa kurushwa angani wakiwa na viti umbali wa meta 100 kwa kasi ya risasi kutoka ndege hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe alisema ajali hiyo ilitokea saa 4.25 asubuhi katika Kikosi cha Anga cha Airwing, Ukonga ndege hiyo ikiwa imeruka meta 100 kutoka ardhini.
Alifafanua kuwa waliporushwa angani, wakati wa kutua, Kapteni Kwidika parachuti lake lilifunguka na kujaa upepo akashuka ardhini salama, lakini Kapteni Mangushi la kwake halikufunguka vizuri ndipo alipojibamiza kwenye paa la hanga (karakana ya ndege) na kufa papo hapo.
Hata hivyo, pamoja na Kapteni Kwidika kutua na parachuti, alijeruhiwa na amelazwa katika hospitali ya Jeshi ya Lugalo, Dar es Salaam ambako hali yake ya afya inaendelea vizuri.
Mgawe alisema ndege iliyopata ajali imeharibika kiasi kwenye bawa na eneo linaloonesha kasi ya ndege, lakini inaweza kutengenezeka na taarifa zaidi wanatarajia kuzipata kutoka kwa Kapteni Kwidika mara akipata nafuu.
No comments:
Post a Comment