HANDAKI LA AJABU LA WAKOLONI LAGUNDULIKA MKOANI IRINGA...



Mamia ya wakazi wa mjini Iringa wakiwa wamekusanyika eneo la Kitanzini kushuhudia handaki hilo (kulia).
Habari zilizotufikia hivi punde zinasema kwamba handaki linaloaminika kutumiwa na Wakoloni wa Kijerumani limegunduliwa jana katika eneo la Kitanzini, mkoani Iringa kwenye Mtaa wa Sokoni na kuibua gumzo kubwa na hofu miongoni mwa wakazi wa mkoa huo.
Kugundulika kwa handaki hilo linalokadiriwa kufikia ukubwa wa futi 6 kwa 6, kumekuja wakati wafanyakazi wa Kampuni ya JR wanaoshugulika na uboreshaji wa miundombinu ya maji mjini humo wakiendelea na kazi ya uchimbaji mitaro kwa ajili ya kusimika mabomba mapya ya maji safi.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, mmoja wa wananchi aliyeingia katika handaki hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Abdukareem, amesema kuwa yeye ni mkazi wa eneo hilo na alipopata taarifa hizo alifika akiwa na mwenzake aliyemtaja kwa jina moja la Salehe na kukubaliana kuingia ndani ili kujionea wenyewe kwa macho.
Amesema kutokana na shimo hilo kuwa refu walitafuta ngazi lakini hawakufanikiwa kwani ngazi hiyo ilikuwa pana na kuamua kutafuta fimbo kubwa ya muanzi na kamba na ndipo walipofanikiwa kuingia ndani.
Aliendelea kusema kwamba walipofika ndani walikuta chumba ambacho ni kama futi tatu na kuona vidirisha vidogo kwa mbele huku bado kukiwa kumejengewa kwa zege na kubainisha kulikuwa na vyumba vingine zaidi ambavyo hawakuweza kuingia kutokana na kuwa vimezibwa.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Dk Leticia Warioba alifika katika eneo la tukio huku akiwa ameongozana na wafanyakazi wa  Kampuni ya JR pamoja na Ofisa wa Usalama ambao waliishia kuangalia njia hiyo kwa nje bila kuingia ndani ya handaki hilo.
Inadhaniwa kwamba mahandaki hayo yalikuwa yakitumiwa enzi za ukoloni wa Wajerumani, na kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kuendelea kugundulika mahandaki zaidi katika siku za usoni kwenye maeneo mbalimbali mkoani humo.

No comments: