Serikali imesema inatarajia kuunda upya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB) ili ijiendeshe yenyewe na kupunguza utegemezi wa Serikali na kuwezesha kurejesha Sh trilioni 1.1 zilizokopwa na wanafunzi.
Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, hivi sasa Bodi hiyo inapata asilimia 75.5 ya bajeti yote ya wizara hiyo huku asilimia 25.5 pekee ikibaki wizarani.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Celestine Gesimba aliyasema hayo jana alipo kuwa akijibu hoja za wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyotaka ufafanuzi kuhusu utegemezi wa Bodi hiyo kwa Serikali utakwisha lini.
Hoja ya wajumbe wa kamati hiyo, iliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, John Cheyo, Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP) ilitokana na utegemezi wa asilimia 75.5 kwa bajeti ya Serikali na namna ya kulipa madeni kwa wanafunzi waliokopa.
Akifafanua kuhusu hoja hizo na kiasi cha deni lililopo mpaka sasa na kilicholipwa baada ya ripoti ya CAG kuonesha upungufu, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Bodi hiyo, Onesmas Laizer alisema mpaka Juni Bodi imekopesha Sh trilioni 1.087.
“Hata hivyo, Bodi ina miaka saba sasa tangu ianzishwe na kabla haijaanza bodi, serikali ilishakopesha wanafunzi Sh bilioni 51.1, jumla ni Sh trilioni 1.138 zilizokopwa. Mikopo iliyoiva tayari kurejeshwa ni Sh bilioni 160.7,” alieleza Laizer.
Hata hivyo, alisema kati ya hizo Sh bilioni 160.7 ambazo marejesho hufanywa kwa awamu, fedha zilizopaswa kuwa zimerejeshwa ni Sh bilioni 39.54 lakini mpaka Juni wameshakusanya Sh bilioni 20.15 pekee huku Sh bilioni 19 zikiwa mikononi mwa wakopaji.
Cheyo alihoji kwa nini Bodi iendelee kiutendaji wa namna hiyo na kueleza kuwa tatizo la wizara na Bodi ni mfumo wa kumbukumbu (Data Base) na upungufu wa vyanzo mbadala vya mapato, unaorudisha nyuma ubora wa elimu nchini.
Akifafanua hilo, Kaimu Katibu Gesimba alikiri kuwepo kwa tatizo kubwa katika utegemezi wa Bodi na kueleza kamati kuwa tayari Waziri mwenye dhamana aliliona hilo na aliunda timu kutoa mapendekezo ya namna ya kuboresha vyanzo vya mapato vya Bodi.
“Ni kweli tatizo lipo, asilimia 75.5 ya bajeti inakwenda Bodi lakini siku zinavyokwenda na mahitaji ya mikopo kwa wanafunzi yanaongezeka, ila tayari mapendekezo ya awali yanaonesha kuwa Bodi itaundwa upya ili kupata vyanzo vya mapato, utendaji na kuongeza ufanisi,” alisema Gesimba.
Ingawa hakusema timu itafanya kazi lini, Gesimba aliwambia waandishi wa habari nje ya kikao kuwa, tayari mapendekezo ya awali ya timu yamemfikia Waziri na yanachambuliwa ili kufikisha serikalini, na Serikali ikibariki, maboresho yatafanyika.
No comments:
Post a Comment