JAJI MIHAYO AHOJI UHALALI WA POLISI KUUA RAIA HADHARANI...

Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Baraza la Habari Tanzania, Jaji mstaafu Thomas Mihayo amesema taifa ambalo maisha ya wananchi wake wanapotea bila sababu, lina matatizo kwani hata Katiba ya nchi lengo lake kuu ni kulinda uhai wa watu na sio kuua.
Akizungumza kwenye kipindi cha Jenerali on Monday kinachorushwa na televisheni ya Channel Ten, kila Jumatatu usiku, Jaji Mihayo alisema yapo matukio mengi ya mauaji ya raia wasio na hatia yanayoihusisha Polisi na kushangaa hakuna hatua za kisheria zilizochukuliwa dhidi yao.
"Kuna haja ya kubadilisha jina la Jeshi la Polisi, kutoka neno jeshi na kuwa chombo cha Usalama wa Raia, kwani neno hili halijakaa kirafiki, na ndio maana hata wanapokwenda kukamata raia wanawapiga bila hata sababu, kwa nini? alihoji Jaji Mihayo.
Akifafanua kauli yake kuhusu taifa ambalo maisha ya raia wake yanapotea bila sababu halina haja ya kuwepo, Jaji Mihayo alisema, uhai ni haki ya msingi ya raia yeyote na kwamba hata Katiba ya nchi msingi wake mkubwa ni kujali utu na kwamba kukatiza uhai wa mtu ni kosa na linahitaji adhabu.
"Nilipoanza kazi mahakamani miaka mingi iliyopita, polisi hawakuwa wakipiga watu ovyo tena hadharani, hata kama walifanya hivyo walifanya kwa siri na walijitahidi wasionekane wakipiga, lakini sasa kipigo kwa raia kinafanywa wazi na polisi," alisema Jaji Mihayo.
Alisema matukio mengi ya kunyanyasa raia bila sababu yamekuwa yakifanywa na Polisi na hakuna aliyewawajibisha, jambo ambalo amewashangaa hata wanasheria nchini kwa kutochukua hatua ya kuwafungulia mashtaka polisi hao, kwani mwanasheria mzuri ni yule anayezungumzia jambo mahakamani na sio kutoa matamko.
Jaji Mihayo aliongeza, kutochukuliwa hatua kwa polisi hao kumewapa kiburi kujiona wako juu ya sheria na kwamba pamoja na hayo upo umuhimu wa polisi hao kufundishwa sheria ili wazifahamu na kutofanya maamuzi ya kinyama.
"Haiwezekani kutoka maeneo mbalimbali kama vile Singida, Arusha, Morogoro na Iringa polisi kote iseme hawajakosea, kwenye mauaji ya raia wasio na hatia, hii sio sahihi hata kidogo, kwani polisi wanahusika," alisema Jaji Mihayo.

No comments: