WALIMU WAKATWA MISHAHARA KUTOKA NA MGOMO...

Walimu wa shule za sekondari na msingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Lindi, wanadaiwa kukatwa mshahara wa Agosti kutokana na mgomo walioufanya Julai mwaka huu.
Kitendo hicho kimelalamikiwa na walimu hao wapatao 111 waliojiandikisha baada ya fedha zao kukatwa.
Mweka Hazina wa Chama cha Walimu (CWT), Lindi Vijijini, Mwalimu Hassani Murtaza alidai jana kuwa makato hayo yamefanyika kulingana na mshahara wa kila mmoja na kutoa mfano kwamba yeye amekatwa Sh 99,733.
Mwalimu Murtaza alidai kuwa walimu wengine waliogoma kwa siku nne, walikatwa hadi Sh 150,000 na kuongeza kuwa fedha hizo zilizokatwa hazikutolewa risiti na mamlaka husika.
Kwa mujibu wa madai ya Mwalimu Murtaza, mbali na kukatwa fedha hizo kwa kugoma, pia walimu hao wamekatwa pia Sh 5,000 za mbio za Mwenge na hakuna risiti waliyopewa.
Alilalamika kuwa wapo pia walimu wasioona wanaofundisha shule za wenye ulemavu ambao pia wamekatwa mishahara yao.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alipoulizwa alisema kuwa yuko katika jimbo analoliwakilisha la Songwe na kwamba hajajua yanayotokea.
Alifafanua kuwa malipo ya walimu wa sekondari na shule za msingi hufanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Alipotafutwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia alishauri suala hilo iulizwe halmashauri ambao ndio waajiri wa walimu hao.
"Mimi sio mwajiri wa walimu hao na wala sijawakata mishahara, wamekatwa na mamlaka zao, hivyo waulizeni waliowakata wametumia sheria gani," alisema Ghasia.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lindi, Selemani Ngaweje alipoulizwa alithibitisha kuwepo malalamiko hayo yanayoelekezwa kwa Mkuu wa Idara ya Elimu wa Shule ya Msingi na kuwataka walimu hao wapeleke taarifa hiyo kwake.

No comments: