WAZIRI KAGASHEKI AWAKALIA KOONI WALIOGEUZA MALIASILI 'SHAMBA LA BIBI'...

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki amebaini uwapo wa mianya ya ufisadi katika umiliki wa vitalu vya uwindaji na kuwaonya watumishi wa wizara hiyo waliojigawia vitalu hivyo, kuwa wakibainika watakuwa wamejifukuzisha kazi.
Hayo alisema jana Dar es Salaam alipokutana na wadau wa uwindaji wa kitalii kujadiliana jinsi ya kuleta mabadiliko katika sekta hiyo nchini pamoja na kuzibaini changamoto zilizomo.
Balozi Kagasheki alisema wizara yake iko katika uchunguzi ili kubaini watumishi wake wenye vitalu na wakibainika, watakuwa wamejifukuza kwani utaratibu huo ni kinyume cha utaratibu wa sheria za utumishi wa umma.
Akizungumzia suala la vitalu, alisema wawindaji wengi wanaopewa vitalu, hawafuati sheria na wengine huwauzia wawekezaji kinyume cha utaratibu wa umiliki wa kitalu.
“Nina ushahidi wa majina kuwa kuna watu wamepewa kitalu wamekwenda kwa mwekezaji wanataka kuuza kwa dola laki sita (zaidi ya Sh milioni 700)...huo ni ulanguzi,” alisema Balozi Kagasheki na kuongeza kuwa tatizo kubwa ni sheria ambayo inamtaka aliyepewa kitalu akishindwa kukiendesha akirudishe.
Kuhusu hisa za kampuni zinazomiliki vitalu, alisema kwa sasa Watanzania wanamiliki asilimia 25 ya hisa ambazo ni ndogo na kutaka sheria irekebishwe angalau kufikia asilimia 50 kwa 50 ili wengi zaidi wanufaike.
“Sijui kwa nini sheria hiyo ilifanywa hivyo, wabunge wenyewe waliifikisha hapo na sijui walitumia vigezo gani na kwa nini isiwe asilimia 50, sioni mantiki ya kuweka hilo katika sheria kwamba iwe na hisa asilimia 25 kwani kuna Watanzania wanaojiweza,” alisema Balozi Kagasheki.
Aidha, alisema sheria ya uwindaji wa kitalii ni mbaya, inahitaji kufanyiwa marekebisho ili ifanye kazi kwa kulinufaisha taifa.
Kuhusu bei ya uuzaji wa wanyama, Waziri Kagasheki alisema wapo wanaoamini kuwa bei ya sasa ni kubwa jambo ambalo si la kweli.
Alisema kwa mfano bei ya mamba mmoja ni Dola za Marekani 1,700 (Sh milioni 2.55) wakati mkanda mmoja wa kuvaa uliotengenezwa kwa rasilimali hiyo unauzwa Dola za Marekani 1,200 (Sh milioni 1.8).
Mbali na mkanda unaotokana na mamba kuuzwa bei hiyo, Kagasheki alisema pia mkoba mmoja unaotokana na mamba unauzwa dola 1,500.
Alitoa mfano mwingine wa bei ya tembo mmoja ambayo alisema hata Tanzania anauzwa dola 12 wakati Namibia anauzwa dola 20 na kusema ipo haja ya kuwatendea haki watanzania.
“Wawindaji lazima mfanye kazi kwa utaalamu, ibadilisheni Wizara ya Maliasili na Utalii kutoka huko mlikoifikisha… sina raha kabisa jinsi mambo yanavyokwenda, ninahitaji kuijenga wizara hii na kuitoa katika hali ya kulalamikiwa kila mara,” alisema Balozi Kagasheki.
Alisema kukutana na wadau hao ni fursa nzuri ya kukaa pamoja ili kufungua ukurasa mpya wa kuondosha matatizo yanayowakabili na kuongeza kuwa wanaweza kuona kuwa Serikali haiwatendei haki wakati shabaha kubwa ni kulinda maslahi ya taifa.

No comments: