ZOEZI LA BOMOABOMOA MADALE LAIBUA MAPYA...


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki.
Sakata la bomoa bomoa katika eneo la Madale linalodaiwa kuvamiwa na watu wasiomiliki maeneo hayo, limechukua sura mpya baada ya kubainika kwamba waliokuwa vinara wa uporaji wa maeneo hayo ni raia wa nchi jirani waliogeuza maficho na kuanzisha 'serikali yao’ katika eneo hilo.
Katika hatua nyingine, Serikali imesema operesheni hiyo haikufanywa kwa kukurupuka bali ilikuwa na baraka ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam, huku wananchi wakionywa kuacha mara moja kuvamia maeneo ya watu na kuheshimu maagizo yanayotolewa na Mahakama na mamlaka za serikali.
Kubainika kuwa vinara wa uvamizi huo ni raia wa kigeni kulielezwa Dar es Salaam jana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,  Said Meck Sadiki alipozungumza na waandishi wa habari.
“Tumewakamata vijana hawa ambao ni wa nchi jirani na tayari tumewakabidhi katika Ofisi za Uhamiaji ambao wanaangalia ni jinsi gani ya kuwarejesha nchini kwao,” alisema Mkuu wa Mkoa.
Alisema uchunguzi huo pia umebaini kwamba vinara hao ambao inadaiwa walikuwa wameanzisha utawala na serikali yao tofauti na ile ya Tanzania katika eneo hilo, walikuwa wanalindwa na baadhi ya viongozi wa serikali wasiokuwa na uadilifu.
“Watu hawa leo wanaodai wameonewa walivamia maeneo hayo na kuwaondoa watu halali wa maeneo hayo kwa kutumia vijana waliokuwa na silaha za jadi kama mishale na mikuki na tumegundua vijana hao si raia wa hapa nchini ila ni wa nchi jirani na walikuwa wameunda serikali yao kabisa na walikuwa wakijeruhi watu.
 “Sisi tunawaondosha watu hawa baada ya kupata hati kutoka mahakamani, sasa wao wanadai wameonewa wakati walivamia maeneo hayo na kuwaondoa watu halali wa maeneo hayo kwa kutumia vijana waliokuwa na silaha za jadi kama mishale na mikuki, ambao kama nilivyosema tumegundua  si raia wa hapa nchini ila ni wa nchi jirani ambao walikuwa wameunda serikali yao kabisa na walikuwa wakijeruhi watu.
“Wavamizi hawa wamewachelewesha wamiliki halali kufanya shughuli zao za maendeleo kwa miaka 10… napenda watu wote wafahamu kwamba zoezi hili si la Kinondoni peke yake, bali tutalifanya katika wilaya zote,” alisema.
Akizungumzia madai kwamba operesheni hiyo imeendeshwa kwa kukurupuka, Sadik alipuuza madai hayo, akisema ilifanywa chini ya baraka zote za Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Alisema katika operesheni hiyo vijana zaidi ya 68 walikamatwa wakiwemo wahamiaji hao haramu, baadhi wakifikishwa polisi ili kufikishwa mahakamani na wageni wakikabidhiwa Uhamiaji.
 “Watu hao wanaodai wameonewa tumewadai hati halali, lakini wameshindwa kutupatia matokeo yake wamepanga maandamano ya kwenda kwa Rais na kuwatanguliza wanawake na watoto wadogo mbele jambo ambalo si sahihi kwa kuwa serikali yetu haidhulumu mtu.”
Aliwataka wananchi wote wanaotaka kununua viwanja wafuate utaratibu halali kwa kuwa wakiendelea kununua kinyemela watavunjiwa nyumba zao na wataendelea kupata hasara.
“Kama mtu una fedha yako fuata utaratibu kujipatia ardhi ili baadaye usipate hasara, kwa kuwa serikali haipo tayari kuona haki ya mtu inapotea… nawashauri pia wanaowatetea wavamizi hawa ambao ni wahalifu watambue kwamba haki haipo upande mmoja,” alisema.

No comments: