OMBAOMBA MAARUFU MATONYA AFARIKI DUNIA...


Ombaomba maarufu nchini  kwa jina la Matonya  amefariki  dunia usiku wa kuamkia jana na kuzikwa katika Kijiji cha Mpamantwa wilayani Bahi mkoani Dodoma.
Licha ya uvumi kuwa mzee huyo alikuwa ni tajiri wa ng’ombe, lakini ukweli wenyewe umedhihirika baada ya kifo chake baada ya kufa katika hali ya ufukara, jambo ambalo pia limesababisha kuzikwa bila ya sanduku.
Mkongwe huyo alizikwa mita tatu kutoka usawa wa nyumba yake ambapo taarifa zinaeleza kuwa alizikwa na nguo nyeusi moja huku mwili wake ukibebwa na ngozi kuu kuu ya ng’ombe kuelekea katika nyumba yake ya milele.
Matonya, ambaye aliingia jijini Dar es Salaam kwa mara ya kwanza Desemba 7 mwaka 1961, katika siku za hivi karibuni alikuwa ni gumzo kwa serikali na viongozi huku akipachikwa jina la Kiboko ya Makamba.
Idadi ndogo ya watu nyumbani kwa Matonya walikuwa wakiomboleza huku watoto watatu ambao walikuwepo kati ya watano aliowaacha hai, wakisema kuwa baba yao amefariki kutokana na umasikini na ufukara mkubwa walio nao.
“Hatukuweza kumpeleka hata hospitali kupata vipimo kwani hatukuwa na uwezo wa kwenda mjini Dodoma kutokana na kukosa hata nauli ya kufanya hivyo ndiyo maana tumekuwa kimya hadi Mungu alipomchukua,’’ hiyo ni kauli ya mtoto wa nne wa Matonya David Paulo.
Kijana huyo ambaye alionekana kuwa na huzuni zaidi, alisema kuwa baba yake aliianza kuugua kikohozi Mei mwaka huu na kwa wakati wote hawakuwa na msaada wa aina yoyote wa kumfikisha hospitali kutokana na ukata.
Taarifa za kifo cha Matonya zilisambaa jana majira ya asubuhi ambapo ilielezwa kuwa alifia nyumbani kwake Kijiji cha Mpamantwa mahali yalipofanyikia maziko yake.
Umaarufu wa Matonya ulitokana na kupingana na serikali kwa nyakati tofauti ambapo alipinga kurudishwa kwao Bahi na mara kadhaa alimweleza aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuf Makamba kuwa yeye ni mtoto wa mjini hivyo asingemuweza.
Mkoani Morogoro Matonya aliweka kambi katika eneo la Darajani mahali aliposema kuwa ilikuwa ni makazi yake mapya katika utafutaji kwenye maisha na hapo ndipo alipobadili staili ya kuomba akiwa amelala chali na kuinua kopo juu kwa muda mrefu bila ya kuchoka.
Mtoto mkubwa wa marehemu, Elizabeth Paulo alisema kuwa baba yake hakuacha chochote na kukanusha uvumi kutoka kwa watu kuwa Mzee Matonya alikuwa na mali nyingi.
Mke wa marehemu ambaye alikuwa na Matonya  hadi kifo chake, Paulina Matonya alisema kuwa walitengana  zaidi ya miaka 37 iliyopita na wakati huo alikuwa na ng'ombe wengi.
“Tulipotengana tu, mimi nilirudi kwetu na watoto wangu walikuwa bado wadogo na bahati mbaya mdogo wake aliyekuwa akiwatunza ng’ombe wa Matonya alifariki dunia na huo ukawa ndio mwanzo wa kumaliza mifugo yote kwani watu waliwaiba wote,’’ alisema Paulina.
Kwa mara ya mwisho, Matonya alirudi kijijini kwake Novemba 2010 akitokea mkoani Morogoro  kwa ajili ya mapumziko ya mwishoni mwa mwaka na Sikukuu ya Krismasi na hiyo ilikuwa ni kawaida yake.
Matonya ambaye hadi jana umri wake ulikuwa ni wa kukisiwa kuwa ni miaka 90, ameacha mjane na watoto watano wakiwemo wajukuu 9 huku nyumba yake ndogo ya tembe ikikosa hata kuku wa kufugwa.

No comments: