MGOGORO KANISA LA MORAVIAN WACHUKUA SURA MPYA...


Mgogoro Kanisa la Moravian, Jimbo la Misheni Mashariki (Dar es Salaam) umeingia sura mpya baada ya uongozi wa Kanisa hilo nchini kupiga marufuku uongozi wowote wa Jimbo hilo kuzungumza na waandishi wa habari.
Mkutano uliopiga marufuku ulifanyika Jumatatu iliyopita asubuhi, Dar es Salaam ukihusisha uongozi wa Umoja wa Mabaraza ya Wazee na Maaskofu wa Kanisa la Moravian Tanzania (KMT). Mbali na hilo, pia ulisitisha ziara zote za Makamu Mwenyekiti wa Jimbo, Mchungaji Saul Kajula jimboni humo ili kuruhusu uchunguzi.
Kajula na baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Jimbo hilo wanatajwa kuhusika na mgogoro huo. Wanadaiwa kumwandikia barua Mwenyekiti (Fumbo) Julai 31 kumvua nafasi yake kwa madai ya kukiuka Katiba, kutokuwa na uhusiano mzuri na viongozi wenzake na kushindwa kusimamia vyema mali za kanisa.
Mwenyewe alipoulizwa alikana kuandikiwa barua yoyote kama inavyodaiwa na kusema kwamba yeye yupo ofisini akiendelea na kazi kama kawaida. Hata hivyo alikiri kuwepo mgogoro ila alidai hajui sababu na yeye ataendeela kuwatumikia waumini bila kuchoka wala kukata tamaa.
Taarifa zilizopatikana kutoka katika Mkutano wa Mabaraza ya Wazee na waumini wa Sharika za jimbo hilo uliofanyika Jumatatu hiyo mchana baada ya ule wa Maaskofu wa Umoja wa Wazee, zimethibitisha kuwa uongozi wa KMT umezuia mawasiliano yoyote na vyombo vya habari.
“Sijawahi ona Askofu akilia, lakini leo (Jumatatu iliyopita) nimejionea, mengi tuliowaeleza walikuwa hawayajui, baada ya mjadala mrefu, walituomba tusitishe kuongea na waandishi wa habari, tuwape muda wa kushughulikia taarifa zetu,” alisema kiongozi mmoja.
Hilo lilidhihirika pia baada ya mwandishi wa habari hizi kumpigia simu Katibu wa Umoja wa Wazee, Nelson Ngajilo kupata majumuisho kama alivyokubali atayatoa bila jibu na alipotumiwa ujumbe wa simu yake ya mkononi, hakujibu. Hata viongozi wengine hawakupokea wala kupatikana ofisini kwao. 
Viongozi wa Umoja huo wakitoa taarifa kwa mkutano wa wazee wote walisema, wameridhia agizo la Maaskofu na kuwataka wazee wote kutii kwa kuwa Maaskofu hao walipokea taarifa zao kuhusu mgogoro huo na wameomba wapewe muda kushughulikia ili kuchukua hatua.
“Maaskofu wametupokea vizuri na kushangazwa na mambo yanayoendelea jimboni kuhusu mgogoro huo, tumewapa taarifa ya vikao vyetu vya mabaraza vya Julai 29 na Agosti 5. Tulipata nafasi ya kuongea mmoja mmoja na kueleza yote ya moyoni,” alisema mmoja wa viongozi.
Aliwaambia wazee kwamba katika mkutano wao na Maaskofu uliokuwa chini ya Uenyekiti wa Askofu Kiongozi wa KMT kutoka Jimbo la Kusini (Jimbo Mama), Alinikisa Cheyo, wamewaeleza pia vyanzo vya migogoro kuwa ni uchu wa madaraka na fedha kwa baadhi ya wachungaji.
Kiongozi huyo ambaye hakupatikana jina mara moja, aliwaambia wazee kuwa mkutano wao na Maaskofu ulikuwa na ajenda 10 na miongoni mwa mambo waliokubaliana ni pamoja na kusitisha ziara zote za Makamu Mwenyekiti jimboni humo.
“Pia tumekubaliana tuwape muda, na Mwenyekiti (Fumbo) arudishwe madarakani na hatua za ukaguzi wa fedha kwa mujibu wa taratibu zifanyike. Hapo hapo Maaskofu waliitisha Halmashauri ya Jimbo ili ianze kazi hiyo mara moja, mrejesho wa maazimio tutawaletea wakitufikishia siku chache zijazo,” alisema kiongozi huyo.
Baadhi ya wajumbe walionekana kutokuwa na imani na hatua hizo na kuwataka viongozi wa mabaraza wawe tayari kuchukua uamuzi mgumu ikionekana wenye nguvu za fedha, wanaendelea kunyenyekewa ndani ya kanisa hilo. Hata hivyo baada ya ufafanuzi, waliridhika.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa, mgogoro huo uliibuka baada ya Mchungaji Fumbo kwenda likizo ya masomo ya Shahada ya Uzamivu (Phd), inadaiwa aliandikiwa barua ya kusimamishwa na nafasi yake akakaimu Kajula ambaye anadaiwa kung’ang’ania nafasi hiyo.
Aidha pia baadhi ya taarifa zinaeleza kuwa, baadhi ya wajumbe wa halmashauri wanachochea vurugu wakitaka kumuondoa Fumbo ili waweke mtu wao waweze kufanya baishara zao kwa mgongo wa kanisa kutokana na nguvu za fedha. Mabaraza ya wazee wanawapinga wajumbe hao. 
Miongoni mwa mjumbe anayetajwa ni Yona Sonelo lakini alipoulizwa alidai ni uzushi na kwamba wapo baadhi ya watu wahuni wanaomzushia hayo na huku wakijua wazi kwamba taratibu zote za kanisa zinafanywa kwa vikao si vinginevyo. 
Kwa mujibu wa Katiba ya Kanisa, Mkutano Mkuu wa Kanisa unaofanyika mara moja baada ya miaka minne (ujao mwaka 2014) ndio pekee wenye mamlaka ya kumvua nafasi Mwenyekiti.

No comments: