WALIMU WAKUU 10 WAVULIWA MADARAKA KUTOKANA NA MGOMO...

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa.
Walimu wakuu 10 wa shule za msingi wilayani Tarime mkoani Mara, wamevuliwa madaraka yao hayo baada ya kubainika kufunga ofisi, kushindwa kulinda mali za shule na wanafunzi na kuhamasisha mgomo kwa walimu wenzao.
Ofisa Elimu wilayani humo, Emanuel Johnson alikiri walimu hao kuvuliwa madaraka yao tangu Agosti mosi, mwaka huu na kwamba bado mchakato unaendelea wa kuwabaini walimu wengine waliohusika na mgomo huo.
“Ni kweli tumewavua madaraka walimu wakuu wa shule za msingi 10 tangu Agosti mosi na tunaendelea na mchakato wa kuwabaini wengine waliohusika katika kushindwa kulinda mali za shule na wanafunzi na kufunga ofisi za umma na kuwezesha walimu kugoma kufundisha na kuathiri sekta ya elimu,” alisema.
Alimtaja mmoja wa walimu wakuu waliovuliwa madaraka kuwa ni Esther Magesa wa Shule ya Msingi Mturo ambaye alikamatwa na Polisi na kuhojiwa kwa zaidi ya saa mbili na kuachiwa baada ya kudhaminiwa.
Walimu wengine waliovuliwa madaraka wanatoka shule za msingi za Kwihanche, Reamagwe, Nkerege, Gibaso, Kitagutiti na Nyamwino na walimu wakuu wa shule mbili za Nyankoni na Itiryo walipewa onyo ambapo ikibainika kuhusika, na wao watavuliwa madaraka.
Johnson alisema Polisi wilayani humo inamsaka Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wilaya ya Tarime, Matinde Magabe kwa tuhuma za kuchochea mgomo wa walimu, kutoa vitisho kwa walimu waliokataa kugoma na kusababisha uvunjivu wa amani katika baadhi ya shule.
Walimu waligoma kwa siku kadhaa mapema wiki iliyopita nchini kote wakishinikiza kulipwa baadhi ya madai yao na kutaka nyongeza ya mishahara ya asilimia 100; madai ambayo Serikali ilisema haiwezi kuwalipa hasa nyongeza ya mishahara kwa asilimia hiyo.
Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi iliamuru walimu hao warejea kazini baada ya kueleza kuwa mgomo wao ulikuwa batili kwa sababu haukufuata sheria na kuwataka walipe fidia kwa kutokwenda shuleni.

No comments: