PPRA YAANZA KUCHUNGUZA MANUNUZI TANESCO, WIZARA YA NISHATI...

Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), imeanza kuchunguza mchakato wa zabuni ya ununuzi wa mafuta mazito uliosababisha kuwapo na mvutano baina ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Wizara ya Nishati na Madini.
Habari kutoka ndani ya mamlaka hiyo ilifafanua kuwa kitakachochunguzwa ni mchakato uliotumiwa na Wizara ya Nishati na Madini kuipatia zabuni ya kusambaza mafuta mazito kampuni ya Puma wakati mchakato wa zabuni hiyo ulishakamilika.
Lakini pia PPRA pia itachunguza taratibu zilizotumiwa na Tanesco katika mchakato wote wa kutoa zabuni ya usambazaji wa mafuta mazito ya kuendesha mitambo ya umeme ya IPTL kwa kampuni ya Oryx.
PPRA ambayo ndio wenye sheria ambayo hivi karibuni ilizusha maneno bungeni, imejinasibu kuwa ni lazima ichunguze suala hilo na kujiridhisha kama kulikuwa na ukiukwaji wowote wakati wa kutoa zabuni hiyo kwa taasisi zote mbili.
“Tanesco lazima wachunguzwe kuangalia mchakato mzima wa kutoa zabuni hiyo kwa kampuni ya Orxy,” alisema afisa mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini na kuongeza kuwa wizara nayo lazima ichunguzwe kwa nini ikubali kutoa zabuni kwa Puma nje ya taratibu zilizoanishwa kwenye sheria.
“Unajua katika masuala ya zabuni kuna utaratibu, sasa kinachotufanya sisi tuichunguze wizara ni kutaka kuona huyu mzabuni aliyekuja nyuma kuwashawishi wampe zabuni ni taratibu gani zilitumika,” aliongeza ofisa huyo.
Maelezo ya ofisa huyo yanabainisha kuwa ni lazima kulikuwa na ushawishi uliofanywa na Puma na ili kupata kazi hiyo kwa kuungwa mkono na umma walilazimika wapunguze bei “Kama wangeenda na bei ya juu ingekuwa nia ajabu, lakini sisi tunaangalia kama taratibu zilifuatwa.”
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya mamlaka hiyo vinaeleza kuwa vinatia shaka uadilifu wa kampuni ya Puma inayodaiwa kumilikiwa kwa ubia na Serikali na wawekezaji binafsi kutokana na hatua yake ya awali kugoma kuuza mafuta kwa bei ambayo iliwekwa na Serikali.
Chanzo hicho pia kilibanisha kuwa wanafahamu ndani ya sekta ya mafuta kuna michezo michafu ya ushawishi inayofanya kukiukwa kwa baadhi ya taratibu ikiwamo hiyo ya manunuzi ya umma na ndio maana PPRA imeamua kujiridhisha.
Chanzo hicho kilibanisha kuwa watafanya uchunguzi na wataishauri Serikali kutokana na matokeo watakayoyapata ili hali ya migongano isijitokeze tena siku za usoni kati ya taasisi na wizara inayoisimamia taasisi husika.
Suala la utoaji wa zabuni ya ununuzi wa mafuta mazito umezua mtafaruku bungeni huku baadhi ya wabunge wanaodaiwa kuitetea Tanesco wakihusishwa na rushwa. Wabunge wengine walitetea uamuzi wa wizara wa kuipa zabuni Puma kuwa ni kitendo cha uzalendo kwa vile kimeokoa fedha za umma.
Mtafaruku huo umesababisha Spika wa Bunge, Anne Makinda kuunda Kamati Ndogo ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa ajili ya kuchunguza kama kweli baadhi ya wabunge walishiriki katika mchezo mchafu kwa ajili ya kuitetea Tanesco.

No comments: