KANISA LENYE MIAKA 100 LAGUNDULIWA TANZANIA...

Katika tukio linalotajwa kuwa ni la kihistoria, lakini ambalo halifahamiki kwa watu wengi nchini, kitongoji cha Kitika tarafa ya Kasanga, wilayani Kalambo, mkoani Rukwa katika mwambao wa Ziwa Tanganyika kina hadhi ya kuwa makao makuu ya Kanisa la Watch Tower duniani.
Kanisa hilo lililoanzishwa miaka 98 iliyopita, ndipo yalipo makazi ya kudumu ya Baba Mtakatifu au Papa wa Kanisa hilo lenye waumini zaidi ya 70,000 duniani, wengi wakitoka Tanzania, Zambia, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Uchunguzi umebaini katika makao makuu ya Kanisa hilo lililoanzishwa na Baba Mtakatifu wa Kwanza, Enock Sindani akitoka Marekani alikokuwa anaishi na kufanya kazi, umebaini kuwa kwa sasa limegawanyika, na kusababisha kuwapo Baba Watakatifu watatu, kila mmoja akiwa na waumini wake, lakini wote wakibakiza makao makuu kijijini hapo.
Mwandishi wa habari hizi aliyesafiri kwa zaidi ya kilometa 80 kutoka hapa kwa lengo la kuyafikia makao makuu ya Kanisa hilo maarufu kama ‘Vatican City’, alifanya mahojiano na Baba Watakatifu hao kwa nyakati tofauti ili kupata undani wa Kanisa hilo maarufu katika mwambao wa Ziwa Tanganyika.
Baba Mtakatifu Wilson Sikazwe (73), alisema ndiye mrithi halali wa upapa, akisema tangu kuanzishwa kwa Kanisa hilo, limeshakuwa na Baba Watakatifu watano.
Aliwataja kuwa ni muasisi Sindani, Samwel Mwimanzi, John Chamboko, Edwin Simugala na sasa Sikazwe; na wote mbali ya kuwa viongozi wa juu wa kiroho wa Kanisa hilo pia wanajishughulisha na kilimo ili kujikimu kimaisha na hadi sasa hakuna Baba Mtakatifu wa Kanisa hilo anayetoka nje ya nchi hii.
Alifafanua, kuwa mgawanyiko kanisani humo uliibuka mwaka 1982 na baadhi kutangaza kujitenga, ingawa viongozi wao bado wanaendelea kushika sheria, kanuni na miiko ya Kanisa hilo.
Baada ya mpasuko, Baba Watakatifu waliopo na wanaotambuliwa, kila mmoja akiwa na waumini wake, lakini wote wakiwa na makao makuu 'Vatican City’ ni Sikazwe, Jonas Simulunga (65) wanaoishi makao makuu, wakati Joseph Simgomba (50), akiwa wa Turiani, Morogoro.
Akizungumzia mgawanyiko huo Sikazwe alisema ulisababishwa na Baba Mtakatifu wa wakati huo, Chamboko, baada ya kuhukumiwa na Mahakama kifungo cha miezi sita au kulipa faini kwa kukutwa na hatia ya kuiba kuku wanne. Alilipa faini na kumrejeshea kuku wanne mtu aliyedai kuibiwa.
Tukio hilo linatajwa kuchafua hali ya hewa na ndipo Simulunga, licha ya kukiri mbele ya mwandishi wa habari hizi kuwa alikuwa mfuasi wa karibu wa Chamboko, hakukubaliana na tuhuma hizo akidai ni njama za baadhi ya viongozi wa juu wa Kanisa hilo hivyo alijitenga na kuanzisha Kanisa lake na kuteuliwa Papa.
Alitamba kuwa kwa sasa ana waumini zaidi ya 50,000 ndani na nje ya nchi zikiwamo nchi jirani ya Zambia, Malawi na DRC.
Lakini mapapa wengine Sikazwe na Simgomba wanasisitiza kuwa ni kweli Chomboko ambaye ni marehemu, `alikwapua’ kuku hao na alistahili adhabu ya kifungo. Kutokana na tuhuma hizo, Kanisa lilimtawaza Edwin Simgala kuwa Papa mpya.
Lakini muda mfupi tangu alipoteuliwa kuwa Baba Mtakatifu, Simgala alikumbwa na tuhuma za uzinifu akitajwa kuwa na uhusiano wa siri kimapenzi na shemeji yake ambaye alikuwa mjane wa nduguye. Simgala naye kwa sasa ni marehemu.
Aidha, kutokana na kashfa hiyo kwa Kanisa, Simgomba alijiengua kutoka Kanisa hilo na kuanzisha lake na baadaye kutawazwa kushika wadhifa wa Baba Mtakatifu.
Mapapa hao wote watatu wanadai kuwa makanisa yao hayo hayana mfadhili yeyote na kwamba yamejengwa kwa nguvu za waumini wao pia wao hawalipwi mshahara wowote.
Kwa mujibu wa Baba Watakatifu hao, Kanisa hilo ambalo lina misimamo mikali linaongozwa na Amri 10 za Mungu ambapo waumini na viongozi wake wanalazimika kuzishika kwa uaminifu na uadilifu mkubwa, kinyume cha hivyo wanatengwa au kuvuliwa madaraka.
Kanisa hilo lina sherehe moja kubwa kwa mwaka, nayo ni ya Mwaka Mpya. Kwa sasa, kutokana na mpasuko, kila Papa husherehekea na waumini wake katika maeneo tofauti, lakini ndani ya Kitika.
Walidai kuwa Baba Mtakatifu ni chaguo la Mungu hata akiwa hajui kusoma na kuandika, kwa kuwa Mwenyezi Mungu huwajaza hekima, busara na uwezo wa kutawala kupitia Roho Mtakatifu.
Kauli hiyo imejidhihirisha kwani uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwa kati yao, mwenye kiwango cha juu ana elimu ya darasa la saba.
"Si lazima uwe na elimu ya Chuo Kikuu ili uwe Baba Mtakatifu, mie nimehitimu darasa la saba tu, hebu nikuulize, Yesu ulisikia wapi kuwa alisoma darasa lolote?" Alihoji Simulinga.
Hata hivyo kwa mujibu wao waumini na viongozi wao wanazuiwa kujiunga na chama chochote cha siasa au kushika nyadhifa za juu serikalini na hawajawahi kupiga kura katika uchaguzi wowote ukiwamo Uchaguzi Mkuu tangu nchi hii ijipatie Uhuru miaka 50 iliyopita.
Wakifafanua, walidai kuwa wanawafananisha wanasiasa na watu waongo kwamba kusema uongo ni dhambi kwa mujibu wa Amri za Mungu, pia hawapigi kura kwa kuwa inasababisha chuki, ugomvi na mgawanyiko miongoni mwa wagombea na wafuasi wao, hivyo kwa mujibu wa amri hizo mojawapo inaamuru kuwa ugomvi, chuki ni dhambi.
Aidha, waumini wa Kanisa hilo ambalo licha ya kuwapo kwa miaka 98 sasa halijasajiliwa kokote kutokana na agizo la muasisi wake, hawaruhusiwi kushiriki michezo ya aina yoyote ikiwamo soka, ngumi na mingine kwa kuwa wakati wa kucheza watu wanaumizana, wanazozana na mtafaruku wa aina yote yakiwamo kumsababishia mtu maumivu mwilini, kwao ni dhambi.
Hata hivyo, wote wamekiri kuwa hawako tayari waumini na viongozi wao kujitokeza kujiandikisha katika Sensa ya Watu na Makazi Agosti 26, kwa kuwa wao wanachodai wanataka wahesabiwe tu bila kuulizwa maswali tena yasiwe ya siri kwa kuwa hawako mahakamani.
Pia hawaruhusiwi kuoa zaidi ya mke mmoja, kunywa pombe na kuvuta sigara au aina yoyote ya dawa za kulevya, ingawa gazeti hili lilibaini kuwa viongozi hao wa Kanisa wanawagwaya wafanyabiashara wakubwa, kwa kuwa baadhi yao wameoa zaidi ya mke mmoja, lakini hawajachukuliwa hatua zozote za kinidhamu.
Walidai kuwa wanajihusisha na kujitolea katika shughuli za maendeleo zikiwamo kujenga shule, zahanati na pia wanaruhusu watoto wao kwenda shule na hata wao wenyewe wanatibiwa hospitalini, lakini ni marufuku kumsaidia mtu damu au kuongezwa damu kwa madai kuwa ni mali ya mtu. Hawana miiko katika suala la chakula. Kwao, chakula cha aina yoyote, wanakula.
Hata hivyo, wanaruhusiwa kufanya au kuhudhuria sherehe za harusi, ubatizo ambao unafanyika mtoni; pia mapapa wote waliopita wamezikwa katika kaburi moja. Waumini wametengewa eneo la makaburi katika eneo hilo ambapo pia wasio waumini wa Kanisa hilo nao wanaruhusiwa kuzikwa.
Imebainika kuwa Kanisa hilo lina waumini wa fani mbalimbali wakiwamo walimu wa viwango vyote, madaktari, wakulima, wavuvi, wafanyabiashara, lakini wengi wa wanaofikia kilele cha mafanikio katika masomo yao, ikiwamo kufika vyuo vikuu, hulazimika kujitenga na madhehebu hayo, kwa kuwa watakuwa wanashikilia madaraka na nyadhifa za juu.
Baadhi ya waumini wa madhehebu mbalimbali wakiwamo wa makanisa ya Moravian, Pentekoste na Katoliki, walidai kuwa wanaishi nao vizuri, kwani hawaingilii imani zao na wanavumiliana.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiji cha Kasanga chenye vitongoji vitatu vikiwemo vya Lusambo, Kitika ‘Vatican City’ na Songambele, Edward Msikiti (Chadema) alikiri kutengwa na Kanisa hilo, kwa kuwa mwanachama na kiongozi wa chama cha siasa.
Mganga wa Kituo cha Afya Matai wilayani Kalambo, Boniface Chapanga alikiri kuwa waumini wa Kanisa hilo wako tayari kupoteza maisha, kuliko kuongezwa damu ya mtu mwingine hata kama ni mwumini mwenzao, pia wanazuiwa watoto wao kupewa chanjo au kinga ya ugonjwa wowote.
Ni kitongoji chenye heshima ya kipekee, ndiyo maana kila mwaka kitongoji hicho hupokea maelfu ya waumini kwa sherehe za Mwaka Mpya unaoadhimishwa kila Aprili 14, huku kipindi hicho kikitumika maalumu kwa ajili ya ‘Hija’. Na katika kipindi hicho, waumini hupokea chakula cha Bwana ‘Sakramenti Takatifu’ ambacho hutolewa mara moja kwa mwaka.

No comments: