WAFA BAADA YA GARI LAO KUTUMBUKIA KORONGONI MLIMA KITONGA...

Watu wanne wamekufa papo hapo na mmoja kujeruhiwa vibaya baada ya malori mawili kugongana na kutumbukia bondeni katika mteremko wa mlima Kitonga wilayani Kilolo katika Barabara Kuu ya Iringa - Dar es Salaam.
Malori hayo, moja lenye shehena kubwa ya madini aina ya shaba na lingine lenye bidhaa mbalimbali za dukani, yanalindwa na askari Polisi wa wilaya hiyo ili kunusuru mali hizo zisiibwe.
Akizungumza katika eneo la ajali Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Taifa, Mohamed Mpinga alisema kwamba ajali nyingi zinazoendelea kutokea nchini zimekuwa zikisababishwa na uzembe wa madereva.
Taarifa kutoka kwa mashuhuda waliokuwapo katika eneo la tukio, zimedai ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia jana na kuwa chanzo cha ajali hiyo ni lori lenye namba za usajili T587 BGP aina la Scania.
Mashaka Abdala alisema lori lenye mali mbalimbali za dukani lilikuwa limeharibika na kuegeshwa kando ya barabara hiyo na liligongwa na lori lingine lenye namba za usajili T319 BDG aina ya Scania pia, ambalo breki zake zilikataa wakati likiteremka katika mlima huo.
Akithibitisha vifo vya watu waliokuwamo kwenye malori hayo, Mpinga alisema taarifa za Polisi zimethibitisha watu wanne kati ya sita kufa papo hapo huku mmoja akijeruhiwa vibaya na kukimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa.
Mbali na majina yao kutofahamika mara moja, mpaka tunakwenda mitamboni maiti mmoja alikuwa hajatolewa kutoka kwenye ‘kibini’ ya moja ya malori hayo iliyopondwa na kufunikwa na kontena za malori hayo, katika bonde la mlima huo.
Taarifa za kipolisi zimedai kwamba katika ajali hiyo, ‘kibini’ ya lori lililokuwa limepakia shaba, lilifunikwa na kontena za malori hayo baada ya malori hayo kutumbukia katika korongo la mlima huo.
Ajali hiyo ni moja kati ya ajali nyingi zinazoendelea kutokea mkoani Iringa huku ukiwa katika maandalizi ya kitaifa ya kuadhimisha Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani.
Kamanda Mpinga aliwakumbusha madereva kuzingatia sheria za barabarani na akaahidi kwamba msako mkali wa wale wanaokiuka sheria hizo utaanza kufanywa.
Mpinga alisema Kikosi cha Usalama Barabarani kitaweka utaratibu wa ukaguzi maalumu wa magari katika maeneo ambayo ajali zimekuwa zikitokea mara kwa mara ikiwa ni pamoja na katika mlima huo.

No comments: