ABIRIA 36,000 KUTUMIA 'DALADALA' ZA TRENI KILA SIKU DAR...

Serikali imesema abiria 36,000 wanatarajiwa kutumia usafiri wa treni kwa siku jijini Dar es Salaam katika mradi utakaoanza Oktoba mwaka huu.
Aidha, imepiga marufuku kuanzia sasa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kuwatoza nauli watoto wa umri chini ya miaka saba.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana mjini hapa na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alipokuwa akiwasilisha makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Wizara hiyo mwaka 2012/13.
Dk Mwakyembe alisema kutokana na tatizo la msongamano wa magari jijini Dar es Salaam, Wizara yake kwa kipindi cha muda mfupi ujao, inakusudia kuanza kutoa huduma za usafiri wa abiria kwa njia ya reli.
Alisema mwaka uliopita wa fedha, Wizara kupitia Kampuni ya Usimamizi wa Reli (RAHACO), TRL na Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) ilifanya tathimini ya gharama za huduma za reli.
"Kwa kuanzia huduma hii itatolewa kutoka Stesheni ya Reli Dar es Salaam hadi Ubungo Maziwa (kilometa 12) na kutoka Mwakanga hadi Kurasini kupitia Stesheni Dar es Salaam (kilometa 34.5)…Kwa njia ya reli kati ya Stesheni ya Dar es Salaam hadi Ubungo kiasi cha shilingi bilioni 4.75 zitatumika kwa ajili ya ukarabati wa injini tatu za treni na mabehewa 14 ya abiria.
"Fedha hizi zimepatikana, na kazi ya ukarabati wa njia ya reli, injini na mabehewa imeanza na inatarajiwa kukamilika Oktoba 2012," alisema Dk Mwakyembe na kuongeza kuwa huduma hiyo itaanza kwa kuwa na treni mbili asubuhi na mbili jioni kuanzia Jumatatu hadi Jumamosi.
Alisema treni moja itaanzia Stesheni ya Dar es Salaam na nyingine Ubungo Maziwa na zitapishana Buguruni na kuwa zitasimama kwenye vituo sita na kuvitaja kuwa ni Kamata, Buguruni kwa Mnyamani, Tabata Matumbi, Mabibo na Ubungo Maziwa.
"Kila treni itakuwa na mabehewa sita yenye uwezo wa kubeba abiria waliokaa na wale waliosimama takribani 1,000 kila safari, mpango huu utawezesha kuwa na jumla ya safari nane za treni asubuhi na nane jioni hususani wakati wa mahitaji makubwa ya huduma," alisema.
Alieleza kuwa muda wa usafiri kutoka eneo la Stesheni ya Dar es Salaam hadi Ubungo Maziwa itakuwa dakika 35 na inakisiwa kwa siku, treni hizo mbili za njia ya Ubungo zitasafirisha abiria 16,000.
Alisema eneo la Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimetoa ekari nne kwa ajili ya maegesho ya magari ili kuwawezesha watu wenye magari wanaotokea maeneo mbalimbali waegeshe magari yao Ubungo na kupanda treni kwenda Stesheni ya Dar es Salaam.
Kuhusu upande wa reli ya Tazara, alisema Sh milioni 838 zinahitajika kwa ajili ya ukarabati wa injini tatu ya treni na mabehewa 14 na kuwa kazi hiyo sasa inaendelea na zinatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba mwaka huu.
Alisema huduma hiyo ya treni inatarajwa kutolewa kati ya vituo vya Kwa Fundi Umeme, Yombo, Kwa Limboa, Lumo, Kigilagila, Barabara ya Kitunda, Kipunguni B, Moshi Bar, Majohe, Shule ya Sekondari Magnus, Mwakanga, Chimwaga, Maputo, Mtoni Relini, Kwa Azizi Ali Relini hadi Kurasini.
Dk Mwakyembe katika hotuba yake hakueleza kwa njia hiyo ya Tazara abiria wangapi wanatarajiwa kutumia, lakini akizungumza na gazeti hili nje ya Bunge, alisema wastani wa abiria 20,000 watachukuliwa kwa siku hivyo kwa njia zote mbili pamoja na ile ya Ubungo kuwa abiria 36,000.
"Unajua njia ya Ubungo Maziwa ni rahisi kufanya utafiti kwa sababu ni moja tu, ile ya Mwakanga hadi Kurasini inatawanyika sana ndiyo maana wataalamu bado hawajanipa taarifa rasmi, lakini ile ya awali roughly (makisio) ni kama abiria 20,000 kwa siku," alisema Dk Mwakyembe.
Akizungumzia kuhusu TRL kwenye hotuba yake, Dk Mwakyembe alisema ili kuimarisha na kuboresha utendaji wa kampuni hiyo, Wizara yake imetenga Sh bilioni 104 kwa mwaka huu wa fedha ambazo zitatumika kutekeleza miradi mbalimbali.
Alitaja miradi hiyo kuwa ni kuzijenga upya injini za treni nane aina ya 88xx, kufanya malipo ya awali ya ununuzi wa injini za treni mpya 13, kufanya malipo ya awali ya ununuzi wa mabehewa mapya ya abiria 22 na kukarabati mabehewa mabovu ya mizigo 125 na kufanya malipo ya awali ya ununuzi wa mabehewa mapya ya mizigo 274.
"Kufanya malipo ya wali ya ununuzi wa mabehewa mapya ya breki 34 na ukarabati wa karakana za Tabora na Dar es Salaam," alisema na kuongeza kuwa kati ya fedha hizo, Sh bilioni 18.9 zimetengwa kwa ajili ya kulipa madeni ya kimkataba na IFC, RITES na RVR.
"Ni matumaini ya Wizara kuwa uwezeshaji huu wa kifedha utaongeza idadi ya treni za abiria kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma kufikia treni tatu kwa wiki ifikapo mwishoni mwa mwaka huu na kurejesha huduma ya treni za abiria kwenda Mwanza mara tatu kwa wiki kabla ya mwisho wa mwaka huu," alisema.
Alisema Serikali imepiga marufuku utozaji tiketi kwa watoto wadogo chini ya umri wa miaka saba na kuiagiza TRL kubuni utaratibu mpya utakaoondoa walanguzi wa tiketi kwenye stesheni za reli na wizi unofanyika kwa tiketi zinaazokatwa ndani ya treni.
Pia alisema Serikali imeagiza TRL kuachana na mtindo wa kuwatoza abiria mizigo yao kwa kutumia vigezo vya uzito wa mizigo unaotumiwa kwenye usafiri wa ndege ambapo abiria anaruhusiwa kubeba kilo 20 tu.
Alisema kiwango cha uzito anaoruhusiwa msafiri bila kutozwa gharama kiongezwe kulingana na hali halisi ya watumia usafiri wa reli na uwezo mkubwa wa treni kubeba mizigo na kuwa mabadiliko hayo yaanze Oktoba mosi mwaka huu.
Kwa upande wake, Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwa Wizara hiyo, Said Amour Arfi alisema inashangaza kwa Serikali kutumia kiasi cha Sh bilioni 1.7 kwa ajili ya ukarabati mabehewa na injini za usafiri wa Dar es Salaam kwa eneo ambalo halizidi kilometa 10 kutoka Stesheni hadi Ubungo.
Alisema eneo hilo, usafiri upo isipokuwa tatizo ni foleni na kuongeza kuwa bado pia kuna mradi mkubwa wa mabasi yaendayo kasi (DART), unaendelea kutekelezwa eneo hilo na kuacha kutatua matatizo mengi ya Reli ya Kati.
Alitolea mfano wa malipo ya kununulia vipuri vya kukarabati mabehewa ya abiria 31 kwa ajili ya safari ya Kigoma- Dar es Salaam zinahitajika Sh bilioni 1.488 ila hazikutolewa na Serikali inasema haina fedga.
Wizara hiyo imeomba Bunge liidhinishe kiasi cha Sh 317, 710, 481,000 kwa matumizi mbalimbali, ambapo mjadala wa wizara hiyo unatarajiwa kuendelea leo.

No comments: