ZITTO KABWE ASEMA: IKITHIBITIKA NIMEPOKEA RUSHWA NAJIUZULU...

Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Kabwe Zitto, ameapa kujiuzulu nafasi yake ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), iwapo itathibitika pasipo shaka kwamba amehongwa.
Aidha, ameonya kuwa Watanzania wanaodhani hiyo ni vita dhidi yake, wamepotea njia kwa kuwa itakiumiza chama chake, Chadema.
Akizungumza na waandishi wa habari bungeni jana, Zitto alidai tuhuma hizo ni mkakati wa CCM kusambaratisha Chadema na kuwataka wabunge wenzake wanaoshabikia, wajinasue katika mtego huo.
Mbali na kuwataka wabunge wenzake wajinasue katika mtego aliodai umetengenezwa na CCM wa kumtuhumu kwa rushwa, lakini aliwatuhumu hata wabunge wenzake wa upinzani kwa kunyemelea cheo chake cha Mwenyekiti wa POAC.
"Nafahamu pia kuwa kuna wanasiasa hasa wa upinzani ambao wanautaka sana Uenyekiti wa POAC na wanafanya kila njia kutaka kunidhoofisha, lakini hawajui kuwa anayepanga wajumbe wa Kamati ni Spika wa Bunge," alisema Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini na kuongeza:
"Msishangae pia kuja kubaini baadaye kuwa baadhi ya wanasiasa wenye midomo mikubwa ya kutuhumu wenzao wao, ndio vinara wa kupokea rushwa."
Hata hivyo, hakuzungumzia kauli ya Serikali ya kuokoa Sh bilioni 6 kwa mwezi kwa uamuzi wa kuzinyima kampuni za Oryx na Camel Oil fedha za kununua mafuta mazito na kuipa Puma Oil fedha hizo.
Zitto aliyejinasibu kuwa taswira yake ya uongozi inaakisi njozi na matumaini ya wananchi si wa Kigoma Kaskazini tu, bali pia wanyonge na vijana kote nchini bila kujali itikadi, alidai tuhuma za kuhongwa kwake zilianza kutolewa na watendaji wa Serikali.
Tuhuma hizo alisema zimeandikwa na vyombo vya habari tena kurasa za mbele ambapo zimeonesha kuwa waandishi na jamii, imeaminishwa kuwa yeye ni mla rushwa kiasi cha wengine kuhoji kwa nini hakutajwa katika orodha iliyotolewa na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu.
Alidai kuwa moja ni kutaka kuvunjwa kwa POAC, kutokana na kiu ya wasioitakia nchi mema kwa kuwa kamati hiyo imekuwa mwiba kwa mikakati yao ya kifisadi.
Kutokana na shauku hiyo ya mafisadi kwa mujibu wa madai ya Zitto, ameomba ahukumiwe yeye kama Zitto na si POAC kwa kuwa hakuna mjumbe mwingine yeyote anayetajwa kwa rushwa.
Pia aliwatuhumu Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliakim Maswi kwa kushiriki kueneza tuhuma hizo.
"Najaribu sana kujizuia kutokua na mashaka na ushiriki wao huo ikizingatiwa uzito wa taswira ya nafasi zao katika jamii, lakini wameshindwa kunidhihirishia hilo," alisema Zitto ambaye katika mkutano huo alifuatana na wabunge 11 wa Chadema.
Alidai kuwa yeye hatasita kusimamia utaratibu wala hatafunga mdomo kwa wanaokiuka taratibu kwa madai alihusika kuitetea Tanesco na Mkurugenzi Mtendaji wake, William Mhando.
Hata hivyo, alibainisha kuwa alitaka kujua kama utaratibu haukuvunjwa kwa kuwa kulikuwa na taarifa kuwa kusimamishwa kwa Mhando kulikuwa na lengo baya.
"Zilikuwepo tetesi kuwa kusimamishwa kwa Mhando siku chache kabla ya kusomwa Bajeti ya Nishati na Madini, kulikuwa na lengo la kufunika madudu makubwa zaidi kwa kulichagiza Bunge na tukio hilo dogo (kusimamishwa kwa Mhando)," alisema.
Kwa mujibu wa Zitto, lengo hilo la Wizara, ameona limefanikiwa sana.

No comments: