BIMA YAILIPA ATCL SHILINGI BILIONI 12.2/-...YAPANGA KUNUNUA NDEGE MBILI MPYA...

Ndege ya ATCL ambayo ilihusika kwenye ajali iliyotokea mkoani Kigoma hivi karibuni ambapo sasa Shirika la Bima limelipa fidia ya Shilingi bilioni 12.2.
Serikali imesema itatumia Sh bilioni 10.6 kama malipo ya awali kwa ajili ya kununua ndege mbili mpya na kwamba fedha hizo ni kiasi cha Sh bilioni 12.2 ambazo Kampuni ya Ndege (ATC) imelipwa kutokana na bima ya ajali ya ndege iliyotokea Aprili mwaka huu.
Pia imesema katika jitihada za kuboresha usalama barabarani, Wizara ya Uchukuzi inafanya mazungumzo na Wizara ya Viwanda na Biashara ili jukumu la kukagua magari yaliyotumika yanayoingia nchini lifanywe na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alitoa kauli hiyo bungeni jana alipowasilisha makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Wizara hiyo mwaka 2012/2013, ambapo imeomba Bunge liidhinishe kiasi cha Sh 317, 710, 481,000 kwa matumizi mbalimbali.
Alisema katika mwaka 2012/13 ATCL itaendelea kutoa huduma kwa kutumia ndege ya kukodi aina ya Boeing 737-500 na ndege aina ya Dash 8-Q300 ambayo kwa sasa inafanyiwa matengenezo makubwa nchini itakamilika mwezi huu.
"Aidha, kwa kutumia fedha ambazo kampuni imelipwa shilingi bilioni 12.2 kutokana na bima ya ajali ya ndege iliyotokea mwezi Aprili 2012 kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 10.6 zitatumika kama malipo ya awali kwa ajili ya kununua ndege mpya," alisema.
Pia Dk Mwakyembe alisema katika jitihada za kuboresha usalama barabarani, Wizara ya Uchukuzi inafanya mazungumzo na Wizara ya Viwanda na Biashara ili jukumu la kukagua magari yaliyotumika yanayoingia nchini lifanywe na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji.
Alisema chuo hicho tayari kimepokea msaada wa seti nne za vifaa vya kisasa vya ukaguzi wa magari kutoka Benki ya Dunia na kwamba vifaa hivyo vina uwezo wa kukagua magari 800 kwa siku.
Kuhusiana na suala la udhibiti wa usalama wa vyombo vya majini, Waziri Mwakyembe alisema hadi Juni mwaka huu, Masjala ya Tanzania Bara inayosimamiwa na Sumatra ilikuwa na jumla ya meli 100 na kuwa usajili huo ulizingatia sheria ya meli ya mwaka 2003.
Alisema masharti ya usajili yanahusisha umri wa meli ambao hauzidi miaka 15 kwa usajili wa kwanza, ubora wa meli kwa ujumla wake, vifaa vya usalama na umiliki meli ambapo inatakiwa imilikiwe na Watanzania kwa hisa ya zaidi ya asilimia 50.
Alisema Sumatra imekuwa ikikagua mara kwa mara vyombo vya usafiri wa majini na kuwa vile vilivyoonekana havikidhi ubora wahusika hutakiwa kuvifanyia marekebisho kabla ya kupewa vyeti vya ubora.
Alisema kati ya Julai mwaka jana hadi Juni mwaka huu, Sumatra ilikagua vyombo vidogo vya usafiri wa majini 2, 949 ikilinganishwa na vyombo 2,076 katika kipindi kama hicho mwaka 2010/2011.
Alieleza kuwa kati ya vyombo hivyo 1,740 au asilimia 59 vilikidhi viwango vya usalama na kupewa vyeti wakati vyombo 1,209 sawa na asilimia 49 vilishindwa kukidhi vigezo na kuzuiliwa kufanya kazi baharini na kuongeza kuwa kwa vyombo vikubwa kwa mwaka uliopita meli nne zilikutwa na kasoro na kuzuiliwa kufanya kazi.

No comments: