ZITTO KABWE ASEMA ANA UWEZO WA KUIONGOZA TANZANIA...

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema) amesema uwezo, uadilifu na uzalendo wa kuwa Rais wa Tanzania anao.
Zitto alitoa kauli hiyo bungeni jana alipokuwa akichangia Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2012/2013 ya Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu Prof. Makame Mbarawa.
Alisema baada ya kumalizika tamasha la vijana na wasanii mkoani Kigoma, maneno mengi yamekuwa yakizungumzwa yakimhusisha yeye na suala la kuwania urais wa Tanzania  na kuongeza kuwa anachoamini yeye kama urais upo utakuja na kama haupo hautakuja hata kifanyike nini.
"Sina mashaka hata kidogo kwamba uwezo, uadilifu na uzalendo wa kuwa Amiri Jeshi Mkuu ninao… kama urais upo utakuja tu, lakini kwa hilo sina mashaka hata kidogo," alisema.
Akichangia hotuba hiyo, Zitto alisema kampuni ya Onmobile imeingia mkataba na kampuni za simu za mkononi za Airtel na Vodacom kwa ajili ya suala la miito ya milio ya simu, lakini kampuni hiyo haina leseni.
Alisema kampuni za simu za mkononi kwa mwaka zinapata faida ya sh. Bilioni 43 kutokana na biashara ya miito ya simu, lakini fedha hizo zinazinufaisha kampuni zenyewe bila kuwahusisha wasanii.
Alisema kati ya fedha zinazopatikana kutokana na malipo ya nyimbo za wasanii, asilimia 80 zinaenda kwa kampuni za simu, asilimia 13 kampuni ya Onmobile na asilimia saba zinaenda kwa msanii husika jambo alilosema ni unyonyaji mkubwa.
Alisema tayari suala hilo amemjulisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara na Naibu Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, Januari Makamba.
"Kampuni hii haina leseni, waliomba hawakupewa… hawajaajiri watu wengi ina watu wawili tu, ila ndiyo wenye mikataba yote. Inauma sana kampuni ya simu inakula asilimia 80 ukiwauliza wanasema wao hawana mikataba na wasanii ila kampuni ya Onmobile, " alisema Zitto.

No comments: