BAJETI YA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA KWA MWAKA 2012 - 2013...


HOTUBA YA WAZIRI WA VIWANDA
NA BIASHARA MHESHIMIWA
DKT. ABDALLAH O. KIGODA (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO
YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA
KWA MWAKA 2012/2013

1.0 UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, kutokana na taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara ambayo ilichambua Bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara tarehe 5 – 7 Juni, 2012, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu sasa likubali kupokea, kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka 2012/2013.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee, nachukua fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani yake aliyonayo kwangu kunipa dhamana ya kuongoza na kusimamia majukumu ya Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Mheshimiwa Gregory George Teu, Mbunge wa Mpwapwa, akiwa Naibu Waziri wa Wizara hii. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Rais kuwa nitayatekeleza majukumu hayo kwa moyo, uwezo na ujuzi wangu wote kwa kushirikiana na Baraza la Mawaziri na Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii pia, kuwashukuru Mheshimiwa Dkt. Cyril A. Chami, Mbunge wa Moshi Vijijini ambaye alikuwa Waziri wa Viwanda na Biashara; Mheshimiwa Lazaro S. Nyalandu, Mbunge wa Singida Kaskazini na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii kwa misingi imara waliyoiweka ya kutekeleza majukumu ya Wizara hii ambayo inanibidi niiendeleze. 
Mheshimiwa Spika, napenda kuwapongeza Wabunge wapya: Mheshimiwa Prof. Sospeter Muhongo (Mb), Waziri wa Nishati na Madini; na Mheshimiwa Janet Mbene (Mb), Naibu Waziri wa Fedha. Aidha, nawapongeza, Mheshimiwa Mohammed Said Mohammed, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi; Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Jimbo la Igunga; Mheshimiwa Joshua Samwel Nassari, Mbunge wa Arumeru Mashariki; Mheshimiwa James Mbatia, Mbunge wa Kuteuliwa; na Mhe. Saada Mkuya Salum, Mbunge wa Kuteuliwa. Nawatakia mafanikio katika majukumu yao mapya.
Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mheshimiwa Mahmoud Hassan Mgimwa, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini (CCM) na Makamu wake Mheshimiwa Gaudence Cassian Kayombo, Mbunge wa Mbinga Mashariki (CCM), na Wajumbe wote wa Kamati, kwa kuendelea bila kuchoka kutoa ushauri na maelekezo yao makini wakati wa kujadili muhtasari wa makadirio ya matumizi ya Wizara hii. Ushauri na maelekezo yao yametumika ipasavyo kuboresha Hotuba hii ninayoiwasilisha leo. 
Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kukushukuru wewe mwenyewe, Naibu Spika, Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge, Katibu wa Bunge na Watendaji wote wa Ofisi ya Bunge pamoja na Bunge lako Tukufu kwa ushirikiano wenu mnaotupa katika kuwasilisha masuala mbalimbali ya Wizara yangu, ikiwemo miswada ya sheria na mapendekezo ya Bajeti ya Wizara hii. Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, napenda kuwahakikishia kwamba Wizara yangu itaendelea kutoa ushirikiano unaohitajika ili kutekeleza malengo ya kisekta.
Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru Mawaziri walionitangulia kuwasilisha hoja zao. Namshukuru Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda, Mbunge wa Jimbo la Katavi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hotuba yake fasaha na inayobainisha mafanikio na mwelekeo wa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne. Aidha, napenda kumpongeza Mheshimiwa Steven Wassira, Mbunge wa Jimbo la Bunda (CCM) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Uratibu na Mahusiano kwa hotuba yake ambayo imetoa mwelekeo wa uchumi. Nampongeza pia, Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. William A. Mgimwa, Mbunge wa Jimbo la Kalenga (CCM), kwa hotuba yake makini inayobainisha malengo ya Bajeti ya Serikali. 
Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru wananchi wa Jimbo langu la Handeni kwa dhamana kubwa waliyonipa kuwawakilisha katika Bunge lako Tukufu. Pia, kwa namna ya kipekee naishukuru familia yangu hususan mke wangu, watoto na ndugu zangu wote kwa ushirikiano na upendo ambao wamenipa na hivyo kuniwezesha kutekeleza majukumu yangu ipasavyo.
Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kuzishukuru Wizara na Taasisi za Serikali  na wadau wote, hususan Asasi za Sekta Binafsi zikiwemo Chama cha Wadau  wa Ngozi na Mazao yake; Baraza la Kilimo Tanzania; Baraza la Taifa la Biashara; Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania; Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo Tanzania; Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania; Chama cha Wafanyabiashara Wanawake na Vikundi vya Biashara Ndogo kwa michango yao katika kuendeleza Sekta ya Viwanda, Biashara, Masoko na Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo ambazo Wizara yangu inazisimamia. Aidha, ninawashukuru wananchi wote kwa ushirikiano wao kwa njia ya kutoa maoni na mapendekezo yao kupitia vyombo vya habari na wengine kutoa malalamiko yao moja kwa moja kuhusiana na utendaji wa Wizara. Maoni yao yamesaidia kuboresha utendaji wa Wizara. Ni mategemeo yangu kuwa katika mwaka unaofuata wataendeleza ushirikiano waliouonesha ili kuchangia maendeleo ya sekta na uchumi wa nchi yetu kwa ujumla. 
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee napenda kuwashukuru viongozi wenzangu wa Wizara ya Viwanda na Biashara nikianzia na Naibu Waziri, Mheshimiwa Gregory George Teu (Mb); Katibu Mkuu, Bi. Joyce K. G. Mapunjo, Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Shaaban R. Mwinjaka; na Wakuu wa Idara na Taasisi zilizo chini ya Wizara, kwa ushirikiano wanaonipa kutekeleza majukumu ya Wizara hii. Aidha, nawashukuru wataalam na wafanyakazi wote wa Wizara na Taasisi zake kwa kujituma katika kutekeleza majukumu yao. Vilevile, napenda kuwashukuru wale wote ambao kwa njia moja au nyingine, tulishirikiana nao katika maandalizi ya hotuba hii ninayoiwasilisha leo. Sina budi kumshukuru Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali na wachapishaji wengine kwa kuchapisha machapisho mbalimbali ya Wizara yangu kwa wakati na kwa ubora. 
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kuungana na Waheshimiwa Mawaziri wenzangu waliotangulia kutoa hotuba zao na kutoa msisitizo na kuwahamasisha watanzania washiriki kikamilifu katika zoezi la sensa tarehe 26 Agosti, 2012. Kwa namna ya kipekee, napenda kuwahimiza wadau wote wa Sekta ya Viwanda, Biashara, Masoko na Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo, kushiriki kikamilifu katika siku hiyo ili kuweza kuhesabiwa. Taarifa za sensa ni muhimu kwa kila mfanyabiashara, mjasiriamali, wenye viwanda na wafanyakazi na kwa maendeleo ya sekta. Kwa hiyo, Wizara ya Viwanda na Biashara inatarajia kutumia taarifa za wadau katika kupanga na kuboresha mipango ya sekta na inawatakia kila la kheri Watanzania wote siku hiyo ya kuhesabiwa.

2.0 MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI KWA MWAKA 2011/2012

2.1 HALI YA SEKTA YA VIWANDA, BIASHARA, MASOKO NA VIWANDA VIDOGO NA BIASHARA NDOGO 
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Viwanda na Biashara ni mojawapo ya sekta za kipaumbele katika utekelezaji wa MKUKUTA II, KILIMO KWANZA, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12-2015/16), Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Mpango Elekezi wa Mwaka 2011 - 2025 na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya 2010, ili kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati unaoongozwa na maendeleo ya viwanda ifikapo mwaka 2025. Ili kufanikisha azma hiyo, suala la kuongeza thamani ya mazao na bidhaa zake limepewa kipaumbele, hususan katika Mkakati Unganishi wa Kuendeleza Sekta ya Viwanda (Intergrated Industrial Development Strategy) ulioandaliwa na Wizara yangu.

SEKTA YA VIWANDA
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2011/2012, ukuaji wa Sekta ya Viwanda ulikua kwa asilimia 7.8 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 7.9 mwaka 2010/2011. Pamoja na ukuaji wa sekta kuwa chini ya matarajio ya sera, mikakati na maazimio mbalimbali ya kitaifa, mchango wake katika Pato la Taifa uliongezeka kutoka asilimia 9.6 mwaka 2010/2011 na kufikia asilimia 9.7 mwaka 2011/2012 (Jedwali Na. 1). Ongezeko dogo la mchango wa sekta ni pamoja na matokeo ya mdororo wa uchumi duniani na mgao wa umeme nchini uliosababisha ukuaji wa sekta kupungua. Hata hivyo, kutokana na jitihada zinazoendelea za Serikali za kuimarisha uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano uliobainisha maeneo ya kimkakati ikiwa ni pamoja na Sekta ya Viwanda inategemea kufanya vizuri zaidi.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2011, uzalishaji katika baadhi ya viwanda kama vile vya konyagi, sigara, pombe ya kibuku, bia na chuma uliongezeka. Ongezeko hilo lilitokana na kuongezeka kwa mahitaji ya bidhaa hizo katika soko la ndani. Uzalishaji wa konyagi uliongezeka kwa asilimia 38.0 kutoka lita 11,186,000 mwaka 2010 hadi lita 15,432,000 mwaka 2011. Aidha uzalishaji wa pombe ya kibuku uliongezeka kwa asilimia 11.6 kutoka lita 21,037,000 mwaka 2010 hadi  lita 23,474,000 mwaka 2011. Uzalishaji wa mabati uliongezeka kwa asilimia 7.9 kutoka tani 71,276 mwaka 2010 hadi tani 76,912 mwaka 2011. Uzalishaji wa bia uliongezeka kutoka lita 242,689,000 mwaka 2010 hadi lita 323,393,000 mwaka 2011, sawa na ongezeko la asilimia 33.3. Uzalishaji wa sigara uliongezeka kutoka sigara milioni 6,181 mwaka 2010 hadi kufikia sigara milioni 6,630 sawa na ngezeko la asilimia 7.3. Uzalishaji wa chuma uliongezeka kwa asilimia 19.7 kutoka tani 33,384 mwaka 2010 hadi tani 39,955 mwaka 2011 (Jedwali Na. 2).
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Wizara imeshirikiana na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Duniani (UNIDO) katika nyanja mbalimbali zinazolenga kuongeza ufanisi wa Sekta ya Viwanda. Kufuatia ushiriki wa Wizara katika mikutano ya Nchi Maskini Duniani (LDC) na Mkutano Mkuu wa UNIDO (UNIDO General Conference) iliyoandaliwa na UNIDO ili kujadili maendeleo na changamoto za Sekta ya Viwanda, Wizara iliweza kujadiliana na viongozi wa UNIDO na kukubaliana juu ya miradi ya kutekelezwa kwa ushirikiano. Miradi hiyo ambayo tayari imeanza ni Mradi wa Kujenga Uwezo wa Wizara na Wadau Wake wa kufanya uchambuzi wa Sera za Viwanda na zinazoendana na sera hiyo; Mradi wa Industrial Upgrading and Modernisation unaolenga kusaidia kuboresha ufanisi wa viwanda hasa vidogo na vya kati ambavyo vinahitaji msaada kidogo ili kuweza kuuza bidhaa zake katika masoko ya nje. Miradi mingine ni wa Kujenga uwezo wa wanaviwanda katika uzalishaji wa bidhaa bora na kuwaunganisha na masoko makubwa ya nje (Subcontracting and Partnership Exchange - SPX) unaotekelezwa chini ya TCCIA. Vilevile, Mradi wa Africa Agro-processing and Agri-business Development Initiative (3ADI) ambao kwa Tanzania unalenga uongezaji thamani mazao ya korosho, nyama na ngozi ili kuchochea utekelezaji wa KILIMO KWANZA. Pia, mradi wa Kutathmini Maendeleo ya Viwanda nchini unaotekelezwa kwa kushirikiana na National Bureau of Statistics (NBS) na Shirikisho la Wanaviwanda Tanzania (CTI) kwa lengo la kuwezesha kupata takwimu sahihi za Sekta ya Viwanda kwa matumizi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa mwongozo katika kupanga mipango ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, Wizara iliendelea kushirikiana na Sekta Binafsi kwa kuandaa vikao vya kisekta kujadili maendeleo na changamoto za sekta husika. Vikao hivyo vilitoa  mapendekezo Serikalini ya kisera na mfumo wa kodi. Sekta hizo ni pamoja na nguo na mavazi; ngozi na bidhaa za ngozi; chuma na uhandisi; kemikali; chakula na vinywaji; karatasi na vifungashio; mafuta ya kula na sabuni. Aidha, Wizara ilishiriki katika mikutano ya EAC , SADC na UNIDO/CAMI ya kuandaa sera na mikakati ya kuendeleza Sekta ya Viwanda katika Jumuiya hizo.

SEKTA YA VIWANDA VIDOGO NA BIASHARA NDOGO
Mheshimiwa Spika, Sekta ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo imeendelea kutoa mchango mkubwa katika ajira na hadi kufikia Aprili, 2012 imechangia asilimia 23.4 na imetoa ajira zipatazo 5,000,000. Aidha, mchango wa sekta katika Pato la Taifa kwa sasa umefikia asilimia 27.9. 
SEKTA YA BIASHARA
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2011, mchango wa Sekta ya Biashara kwa ujumla ulikua kwa asilimia 8.1 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 8.2 mwaka 2010. Aidha, mchango wa sekta katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 12.2 mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 12.1 mwaka 2010. 
Mheshimiwa Spika, ukuaji huo umechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuongezeka kwa fursa za masoko kwa bidhaa na uboreshaji wa mazingira ya biashara. Fursa hizo ni pamoja na zile zitokanazo na masoko ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika, Jumuiya ya Ulaya, Asia, Marekani na Mashariki ya Kati. Thamani ya mauzo ya bidhaa zetu kupitia fursa hizo kwa ujumla yaliongezeka. Kwa mfano, mauzo ya bidhaa katika Soko la Ulaya yaliongezeka kutoka Dola ya Marekani milioni 1,151.1 mwaka 2010, na kufikia Dola ya Marekani milioni 1,382.0 mwaka 2011 sawa na ongezeko la asilimia 20.1. Aidha, thamani ya mauzo ya bidhaa kwenye Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika iliongezeka kutoka Dola ya Marekani milioni 625.1 mwaka 2010 na kufikia Dola ya Marekani milioni 1,158.9 mwaka 2011 sawa na ongezeko la asilimia 85.4.
Mheshimiwa Spika, mauzo ya Tanzania kwenda nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki yalikuwa Dola ya Marekani milioni 352.4 mwaka 2011 ikilinganishwa na Dola ya Marekani milioni 450.0 mwaka 2010 sawa na pungufu ya asilimia 21.7. Kushuka kwa mauzo yetu kwenye soko la EAC kulichangiwa na baadhi ya changamoto ikiwemo tatizo la ukosefu wa umeme kwa kipindi husika ambapo viwanda vingi vilizalisha chini ya uwezo na vilevile, kuzuiwa uuzaji nafaka nje ya nchi kwani nafaka ni mojawapo ya bidhaa inayouzwa kwa wingi soko la Jumuiya na hasa nchi ya Kenya. Mauzo katika Bara la Amerika nayo yaliongezeka na kufikia Dola ya Marekani milioni 59.9 mwaka 2011 ikilinganishwa na Dola ya Marekani milioni 51.0 mwaka 2010 sawa na ongezeko la asilimia 17.8. Kwa upande wa Bara la Asia, mauzo yalifikia kiasi cha Dola ya Marekani milioni 1,414.6 mwaka 2011 ikilinganishwa na Dola ya Marekani milioni 1,200.2 mwaka 2010 sawa na ongezeko la asilimia 17.9. Bidhaa husika ni pamoja na kahawa, korosho, nguo na mavazi, pamba, vinyago, madini, samaki, na bidhaa zake, pareto na tumbaku. Bidhaa hizo huuzwa kwa masharti nafuu ya soko yaani bila kulipa ushuru na bila ukomo.
Mheshimiwa Spika, thamani ya bidhaa zilizonunuliwa kutoka nje ziliongezeka kutoka Dola ya Marekani milioni 7,165.5 mwaka 2010 hadi kufikia Dola ya Marekani milioni 9,827.5 mwaka 2011, ikiwa ni ongezeko la asilimia 37.2. Ongezeko hilo lilitokana na kuongezeka kwa mahitaji ya mafuta na ununuzi wa mitambo ya kufua umeme, ili kukabiliana na tatizo la umeme lililojitokeza mwaka 2011. Mchanganuo unaonyesha kuwa kulikuwa na ongezeko katika uagizaji wa bidhaa za uwekezaji na usafiri, bidhaa za kati na bidhaa za kawaida ikiwa ni pamoja na nafaka. Vilevile, kwa wastani, bei za bidhaa katika soko la dunia nazo zilipanda.
Mheshimiwa Spika, bidhaa za kukuza mitaji zilizoagizwa kutoka nje kwa mwaka 2011, zilikuwa na thamani ya Dola ya Marekani milioni 3,560.5 ikilinganishwa na Dola ya Marekani milioni 2,715.2 mwaka 2010, sawa na ongezeko la asilimia 31.1. Ongezeko hilo lilichangiwa na kuongezeka kwa uagizaji wa mitambo kwa ajili ya shughuli za uwekezaji katika sekta ya gesi asilia na mafuta ya petroli. Uagizaji wa mitambo uliongezeka kwa asilimia 49.1 hadi Dola ya Marekani milioni 1,794.3 mwaka 2011 ikilinganishwa na Dola ya Marekani milioni 1,203.4 mwaka 2010. Thamani ya uagizaji wa vifaa vya usafirishaji iliongezeka kwa asilimia 11.9 kufikia Dola ya Marekani milioni 1,008.5 mwaka 2011 kutoka Dola ya Marekani milioni 901.1 mwaka 2010. Kwa upande wa uagizaji wa vifaa vya ujenzi, kulikuwa na ongezeko la asilimia 24.1 kufikia Dola ya Marekani milioni 757.7 mwaka 2011 ikilinganishwa na Dola ya Marekani milioni 610.6 mwaka 2010. Hii inaashiria mwelekeo mzuri katika kuwezesha uchumi kuimarika na kukua. Thamani ya uagizaji wa bidhaa za kati za viwandani nao uliongezeka kwa asilimia 21.9 kwa mwaka 2011 ikilinganishwa na Dola ya Marekani milioni 609 kwa mwaka 2010. Ni dhahiri kuwa bidhaa zinazotumika kuzalisha bidhaa zaidi viwandani na pembejeo za kilimo navyo vina mwelekeo mzuri wa kukua hivyo kuliwezesha Taifa kuuza bidhaa zilizoongezewa thamani.
SEKTA YA MASOKO
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, kwa jumla kumekuwa na ongezeko la bei kwa mazao makuu ya chakula ya mahindi, mchele, maharage, ngano, sukari, ulezi, na mtama (Jedwali Na.7 ). Wastani wa bei ya jumla kwa gunia la mahindi la kilo 100 ilipanda kutoka Shilingi 34,247 mwaka 2010/2011 na kufikia Shilingi 43,309 mwaka 2011/2012 ikiwa ni ongezeko la asilimia 26. Aidha, bei ya gunia la maharage la kilo 100 ilipanda kutoka Shilingi 109,537 hadi Shilingi 123,606 sawa na ongezeko la asilimia 13. Kupanda kwa bei ya mazao makuu ya chakula kulichangiwa na kuongezeka kwa bei ya mafuta ya petroli kulikosababisha ongezeko la gharama za uzalishaji na usafirishaji, na ongezeko la mahitaji ya mazao hayo ikilinganishwa na ugavi.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2011/12, bei ya mkulima kwa mazao ya biashara ya chai, kahawa, mkonge, pamba, korosho ghafi na miwa iliongezeka. Bei iliyolipwa kwa mkulima kwa zao la chai katika mwaka 2011/2012 ilikuwa wastani wa Shilingi 196 kwa kilo ikilinganishwa na wastani wa Shilingi 126 kwa mwaka 2010/2011. Aidha, kwa mwaka 2011/2012, bei ya mkulima kwa zao la kahawa ya mild Arabica, ilipanda kutoka wastani wa Shilingi 3,350 hadi Shilingi 3,903 ikiwa ni ongezeko la asilimia 17. Bei ya kahawa aina ya Robusta iliongezeka kutoka Shilingi 900 hadi Shilingi 941 ikiwa ni ongezeko la asilimia tano. Vilevile, bei ya mkonge kwa wakulima ilipanda kutoka wastani wa Shilingi 921.40 mwaka 2010/2011 hadi Shilingi 1,114 kwa kilo mwaka 2011/2012, sawa na ongezeko la asilimia 21. Bei ya pamba mbegu ilipanda kutoka wastani wa Shilingi 650 mwaka 2010/2011 mpaka Shilingi 1,000 kwa kilo mwaka 2011/2012, sawa na ongezeko la asilimia 53.8, wakati bei ya korosho ghafi daraja la kwanza ilipanda kutoka wastani wa Shilingi 800 mwaka 2010/2011 mpaka Shilingi 1,200 mwaka 2011/2012 kwa kilo, sawa na ongezeko la asilimia 50. Aidha, bei ya miwa kutoka kwa wakulima wadogo imepanda kutoka Shilingi 54,103 hadi Shilingi 56,240 kwa tani sawa na ongezeko la asilimia 4, kwa Kiwanda cha Kilombero, na kwa Kiwanda cha Mtibwa bei iliongezeka kutoka Shilingi 38,000. hadi Shilingi 38,337.kwa tani sawa na ongezeko la asilimia 1 ambapo kwa Kiwanda cha Kagera bei iliongezeka kutoka Shilingi 33,600 hadi Shilingi 35,000 kwa tani sawa na ongezeko la asilimia 4
Mheshimiwa Spika, mwenendo wa bei za rejareja kwa bidhaa nyingi za viwandani umeonesha kupanda. Bei ya rejareja ya sukari ilipanda kutoka wastani wa Shilingi 1,700 hapo 2010/2011 hadi kufikia Shilingi 2,200 mwaka 2011/2012 kwa kilo. Bei hiyo ilipanda zaidi katika robo ya kwanza ya mwaka 2012 hadi kufikia Shilingi 2,500 katika maeneo mengi nchini. Kufuatia jitihada za Serikali za kuruhusu uingizaji wa sukari kutoka nje, ilisaidia bei ya sukari kushuka hadi kufikia wastani wa Shilingi 2,200 kwa kilo. Serikali ina mkakati wa makusudi wa kuhamasisha ujenzi wa viwanda vipya na kuongeza uzalishaji wa sukari. Bei ya rejareja ya saruji ya mfuko wa kilo 50 katika masoko nchini ilikuwa wastani wa Shilingi 16,940 mwezi Desemba 2011 na kushuka hadi Shilingi 16,265 mwezi Machi 2012. Vilevile, bei ya bati la geji 30 ilipanda kutoka wastani wa Shilingi 16,000 mwaka 2010/2011 hadi kufikia wastani wa Shilingi 19,000 mwezi Machi 2012.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, kumekuwa na ongezeko la bei ya mifugo kwa ng’ombe, mbuzi na kondoo. Wastani wa bei ya jumla ya ng’ombe daraja la pili iliongezeka kutoka Shilingi 393,853 mwaka 2010/2011 hadi Shilingi 427,438 mwaka 2011/2012, sawa na ongezeko la asilimia 9. Aidha, bei ya ng’ombe daraja la tatu ilipanda kutoka Shilingi 285,359 mwaka 2010/11 hadi Shilingi 328,151 mwaka 2011/12, sawa na ongezeko la asilimia 15. Bei ya mbuzi ilipanda kutoka Shilingi 38,805 mwaka 2010/11 hadi Shilingi 42,323 mwaka 2011/12 sawa na ongezeko la asilimia 9,  wakati bei ya kondoo ilipanda kutoka Shilingi 32,677 hadi Shilingi 37,078 katika kipindi hicho sawa na ongezeko la asilimia 13. (Jedwali Na. 9). Kupanda kwa bei hizo kumechangiwa na ongezeko la ubora wa mifugo, gharama za usafirishaji na ongezeko la mahitaji.

2.2 FURSA ZILIZOPO ZA SEKTA NA UTEKELEZAJI WA MAELEKEZO YA ILANI YA UCHAGUZI YA CCM YA MWAKA 2010 
Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Taasisi zilizo chini yake, imeendelea kutekeleza malengo endelevu ya Sekta ya Viwanda, Biashara, Masoko na Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo kwa kipindi cha mwaka 2010 – 2015. Aidha, Wizara imeendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Wizara (Strategic Plan 2011/2012 – 2016/17) ambao kwa sehemu kubwa umezingatia utekelezaji wa maelekezo ya Ilani. Pamoja na changamoto zilizojitokeza, mafanikio yaliyopatikana hadi sasa kwa kutumia fursa zilizopo katika kutekeleza maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 ni kama yafuatayo:

SEKTA YA VIWANDA

Kuimarisha Ushiriki wa Sekta Binafsi (PPP) Katika Uwekezaji na Biashara Katika Soko la Ushindani
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa Mauzo Nje (EPZA) imeandaa utaratibu wa kuanzisha Kituo Kimoja cha Huduma za Uwekezaji (One Stop Services Centre) katika eneo Maalum la Uwekezaji la Benjamin William Mkapa, kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa huduma zote muhimu zinazohusika na uwekezaji wa viwanda. Aidha, baada ya utaratibu huo kukamilika, Mamlaka sasa inawasiliana na Wizara husika kupata maafisa wa kutoa huduma katika Kituo hicho. Pia, Wizara inaendelea kushirikiana na taasisi zinazohusika na utoaji wa mikopo hususan Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) ili kurahisisha upatikanaji wa mitaji ya kuwekeza katika Sekta ya Viwanda, Biashara, Masoko na Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo. Vilevile, Wizara kupitia SIDO na TanTrade imeendelea kutoa mafunzo kwa wajasiriamali mbalimbali kuhusu uzalishaji wa bidhaa zenye ubora ili kuweza kuhimili ushindani katika soko la ndani na nje.
Mheshimiwa Spika, mikoa 20 imekwishatenga maeneo maalum ya uwekezaji ili yawekewe miundombinu ya msingi itakayovutia Sekta Binafsi kujenga viwanda na kufanya biashara katika maeneo hayo. Hatua hiyo itapunguza changamoto ya upatikanaji wa ardhi kwa wawekezaji wanaotaka kuanzisha viwanda nchini. Aidha, kupitia Sheria za Maeneo Maalumu ya Uzalishaji kwa Mauzo Nje (EPZ) na Maeneo Maalumu ya Uchumi (SEZ), Serikali imebainisha vivutio mbalimbali ikiwa ni pamoja na nafuu za kodi ili kuhamasisha ushiriki wa Sekta Binafsi katika uwekezaji. Mikoa ambayo bado haijatenga maeneo hayo ni ile mipya ambayo ni  Katavi, Simiyu, Geita na Njombe. Mamlaka ya EPZ inawasiliana na mikoa hiyo ili nayo iweze kutenga maeneo.

Kujenga na Kuimarisha Ujuzi Katika Biashara na Kuweka Msukumo Zaidi Katika Kutumia Fursa za Masoko
Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea na utekelezaji wa Programu ya Kaizen itakayotoa mafunzo ya kuongeza tija, ufanisi, usimamizi wa shughuli za viwanda na kuongeza ubora wa bidhaa. Hii ni baada ya kukamilika kwenye hatua ya majaribio kwa Sekta Ndogo ya Nguo ambapo wajasiriamali 113 waliopata mafunzo wameweza kuboresha uzalishaji wa bidhaa na kumudu ushindani. Maandalizi yanaendelea kwa ajili ya Programu hiyo kutekelezwa kwa ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na Japan kwenye Sekta ya Viwanda vya Usindikaji Mazao ya Kilimo kwa mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma kuanzia mwezi Septemba, 2012. 
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Sekta ya Viwanda vya Ngozi, Chuo cha DIT Kampasi ya Mwanza kimeanza kutoa mafunzo ya muda mfupi na kinaendelea kukamilisha maandalizi ya kutoa mafunzo ya muda mrefu katika fani ya leather technologists. Aidha, Wizara kupitia SIDO imeanzisha Kituo cha Mafunzo na Uzalishaji wa bidhaa za ngozi Dodoma. Wizara imeendelea kuwezesha na kuimarisha vituo kama hivyo ambavyo viko chini ya Chama cha Wadau wa Ngozi Tanzania (LAT) vilivyoko mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro. 

Kujenga Mifumo Imara ya Viwanda, Biashara na Masoko Yenye Kuendeleza na Kukuza Mauzo Nje
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji (SEZ) ya mwaka 2006 ilipitishwa na Bunge na kwa sasa Wizara kupitia Mamlaka ya EPZ imekamilisha uandaaji wa rasimu ya Kanuni za Sheria hiyo. Kukamilika kwa Kanuni hizo kutaufanya mfumo wa SEZ uanze kutumika rasmi hivyo kupanua wigo wa uwekezaji katika maeneo maalum.

Kuimarisha Kifedha Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) ili kiwe Chombo Madhubuti cha Kuchochea Mapinduzi ya Viwanda Nchini kwa Kutoa Mikopo ya Muda Mrefu na Riba Nafuu kwa Wawekezaji Wakubwa, wa Kati na Wadogo Nchini Kote
Mheshimiwa Spika, Serikali imelenga kuiongezea TIB mtaji wa Shilingi bilioni 500 katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2010 ili kuimarisha uwezo wa utoaji mikopo ya muda mrefu kwa wawekezaji hususan kwenye kilimo na viwanda. Hadi sasa, Serikali imetoa jumla ya Shilingi bilioni 60 kwenda TIB, kati ya hizo, Shilingi bilioni 10 zimetolewa katika mwaka 2011/2012. 
Kuwekeza katika Mradi wa Makaa ya Mawe ya Mchuchuma, Chuma cha Liganga na Viwanda vya Kemikali na Mbolea katika Kanda za Maendeleo Kikiwemo Kiwanda cha Mbolea Aina ya Urea Mkoani Mtwara na Kuwezesha Kiwanda cha Minjingu Kuzalisha Mbolea Bora ya NPK na MPR ili Kufikia Lengo Lililowekwa 

Mheshimiwa Spika, kama Bunge lako tukufu lilivyoelezwa katika Hotuba ya mwaka 2011/12, mwezi Januari 2011 Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) lilifanikiwa kumpata mwekezaji katika Mradi wa Makaa ya Mawe wa Mchuchuma na wa Chuma cha Liganga, Kampuni ya Sichuan Hongda Group (SHG) ya China. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa tarehe 21 Septemba, 2011 NDC na Kampuni ya Sichuan Hongda Group walisaini Mkataba wa Ubia ambapo kampuni ya ubia iitwayo Tanzania China International Mineral Resources Limited (TCIMRL) imeanzishwa kwa ajili ya kutekeleza miradi husika kwa mfumo unganishi.
Mheshimiwa Spika, asilimia 20 ya hisa za kampuni ya ubia zinamilikiwa na Serikali kupitia NDC na asilimia 80 inamilikiwa na Kampuni ya SHG. Miliki ya hisa za Serikali inatokana na mashapo ya madini ya mawe na chuma (free carried interest). Hivyo, Serikali haiwajibiki kuwekeza ili kumiliki hisa hizo wala kulipa fedha taslimu. Mkataba unatoa fursa kwa Serikali kuongeza hisa zake hadi kufikia asilimia 49 baada ya Kampuni ya SHG kulipa deni litakalokuwa limekopwa. Aidha, kulingana na mkataba huo, SHG itawekeza Dola ya Marekanibilioni 3.0 kwenye miradi hiyo. Kampuni ya ubia itaanza utekelezaji wa miradi hiyo kwa kufanya uhakiki wa mashapo ya makaa ya mawe na upembuzi yakinifu wa mashapo ya chuma cha Liganga.  Zoezi la uhakiki wa makaa ya mawe limeanza mwezi Julai, 2012 na linatarajiwa kumalizika mwezi Machi, 2013. Kwa upande wa chuma cha Liganga, uchorongaji wa kutafiti wingi na ubora wa madini ya chuma unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 12-18 kuanzia Agosti, 2012. Inategemewa kuwa, uzalishaji wa umeme MW 300 kutokana na makaa ya mawe ya Mchuchuma utaanza mwaka 2015 na kufikia MW 600 mwaka 2017/2018 na uzalishaji wa chuma kutokana na madini ya chuma ya Liganga unatarajiwa kuanza mwaka 2015/2016.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa kushirikisha wananchi ili kunufaika na fursa za miradi mikubwa kama Mchuchuma na Liganga, Wizara kupitia NDC imeandaa utaratibu wa jinsi ya kuwahudumia wananchi watakaopisha utekelezaji wa miradi katika Wilaya ya Ludewa tangu mwaka 2009 kwa kushirikiana na Halmashauri husika ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata maeneo mengine. Tayari maeneo mapya yamekwishatengwa na elimu kuhusu utaratibu wa kuthaminisha mali zilizopo ndani ya maeneo ya mradi na ulipaji fidia imeishatolewa. Aidha, mwezi Desemba, 2011 NDC iliendesha warsha kwa Halmashauri ikieleza fursa zitokanazo na miradi hiyo. Tayari NDC imepata fedha kutoka Regional Spatial Development Initiative Programume (RSDIP) kupitia Benki ya Maendeleo ya Afrika ya Kusini (DBSA) kwa ajili ya kuajiri mtaalamu atakayeshirikiana na wananchi kuandaa Mpango Shirikishi kunufaisha wananchi wa Halmashauri ya Ludewa.
Mheshimiwa Spika,  Wizara kupitia NDC imekamilisha tafiti za kisayansi kuhusu Kemia, Haidrolojia, Ekolojia na Hydrodyanamics za Ziwa Natron ili kuepusha athari katika mazingira wakati wa utekelezaji wa mradi wa kuzalisha magadi (soda ash). Mradi wa Magadi (Soda Ash) unatarajiwa kuzalisha tani 500,000 za Magadi kwa mwaka kwa kuanzia. Aidha, NDC wamefanya uchorongaji katika eneo la Engaruka lililoko kilometa 50 kutoka Ziwa Natron ambalo lina mashapo yenye magadi mengi. Hata hivyo, utekelezaji wa mradi huo unategemea uboreshaji wa miundombinu ya reli kati ya Tanga na Arusha, ujenzi wa reli mpya kati ya Arusha na Ziwa Natron na upanuzi wa Bandari ya Tanga.

Kuimarisha Uzalishaji Mali Viwandani kwa Kuvifufua na Kuviendeleza kwa Teknolojia ya Kisasa Viwanda Vyote ambavyo Viliuzwa huko Nyuma kisha Kutelekezwa
Mheshimiwa Spika, mwaka 2008, Wizara ilifanya uperembaji katika viwanda vilivyobinafsishwa chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara. Ripoti ya uperembaji huo ilibainisha kuwa kati ya viwanda 74 vilivyobinafsishwa, viwanda 42 utendaji wake ni mzuri na wa kuridhisha na vimewekeza zaidi ya ahadi za mikataba ya mauzo. Viwanda 15 vinalegalega na vimewekeza pungufu ya mkataba wa mauzo, na viwanda 17 vimesimamisha uzalishaji na kufungwa. Viwanda 45 viliuzwa mali moja moja (asset stripping) na hivyo kuondolewa katika orodha ya viwanda. Mwezi Juni, 2011, Wizara ya Viwanda Biashara kwa kushirikiana na Consolidated Holdings Corporation (CHC) na wadau wengine ilifanya uchambuzi wa kina wa viwanda na mashirika yaliyobainishwa kuwa yamefungwa au yanakabiliwa na matatizo makubwa. Kwa sasa, CHC kwa kushirikiana na wadau husika ikiwemo Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya Fedha wameanza majadiliano na wawekezaji ambao hawakuzingatia mikataba ya mauzo ili kukubaliana hatua za kuchukua na kuhakikisha viwanda vinafufuliwa na kuanza uzalishaji ili kuchangia katika uchumi. 

Kuboresha Vivutio kwa Ajili ya Uwekezaji Kwenye Viwanda Vitakavyotumia Malighafi Mbalimbali Zilizopo Nchini Vikiwemo Viwanda vya Nguo, Ngozi, Usindikaji Matunda, Mbogamboga na Usanifu wa Madini na Vito.

Mheshimiwa Spika, mazingira ya utoaji huduma katika maeneo maalum ya uwekezaji yameboreshwa. EPZA kwa sasa inaweza kutoa leseni kwa mwekezaji kwa muda wa siku mbili endapo vigezo vingine vyote vimezingatiwa. Aidha, Wizara kwa kushirikisha wadau wa sekta ilifanya uchambuzi wa changamoto zinazoikabili Sekta ya Nguo na Mavazi na kuandaa mapendekezo Serikalini kwa lengo la kupata maamuzi. Moja ya mapendekezo hayo ni kuondoa VAT katika bidhaa za nguo na mavazi zinazozalishwa hapa nchini ambapo maamuzi yametolewa ya kupunguza VAT katika nguo zinazozalishwa kwa kutumia pamba inayozalishwa hapa nchini kuanzia Julai, 2012. Vile vile Wizara imekamilisha maandalizi ya mkakati wa sekta ndogo ya nguo na mavazi ambao utekelezaji wake utaanza mwezi Agosti, 2012 kwa Wizara kuunda kitengo (Textile Development Unit) cha kusimamia utekelezaji wa Mkakati wake. Vilevile, Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Ngozi na Bidhaa za Ngozi unaendelea kutekelezwa.

Kuendelea Kuhamasisha Uzalishaji na Uimarishaji wa Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa Mauzo Nje (EPZ) na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (SEZ)

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa ajili ya Kuuza Bidhaa Nje (EPZA) imehamasisha na kutoa mafunzo ya uwekezaji kitaifa na kimataifa kuvutia wawekezaji nchini. Kutokana na uhamasishaji huo, jumla ya wawekezaji 59 wameanzisha viwanda vya kuzalisha bidhaa kwa soko la nje. Jumla ya mtaji wa Dola ya Marekani milioni 792.2 umewekezwa ambapo mauzo nje ni jumla ya Dola ya Marekani milioni 440.2. Ajira za moja kwa moja zilizotokana na uwekezaji huo ni 16,105. Aidha, katika eneo la Kamal EPZ lililoko Bagamoyo, viwanda viwili tayari vimeanza kazi. Viwanda hivyo ni kiwanda cha kusindika mazao ya kilimo (Kamal Agro Ltd) na cha kutengeneza gesi ya viwandani ya Acetylene. Ujenzi wa Kiwanda cha kuzalisha chuma pamoja na kiwanda cha kusafisha mafuta machafu cha Kamal Refinery Ltd uko kwenye hatua za mwisho. Viwanda vilivyopo chini ya EPZA zimebainishwa katika kitabu cha Mafanikio ya Sekta ya Viwanda.

Kuendelea Kutekeleza Mkakati Unganishi wa Kufufua na Kuendeleza Viwanda vya Ngozi
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Wizara imeendelea kutekeleza Mkakati unganishi wa Kufufua na Kuendeleza Viwanda vya Ngozi. Kwa ujumla kuna viwanda 13 vya kusindika ngozi nchini vikiwa na uwezo wa kusindika futi za mraba 73,977,000 kwa mwaka. Kati ya hivyo, viwanda vitano vya Himo Tanneries - Kilimanjaro, Moshi leather Industries - Kilimanjaro, Afro Leather Industries - DSM, Lake Trading Co. Ltd – Pwani na ACE Leather Industry – Morogoro ndivyo vinafanya kazi. Pia viwanda vipya vitano (5) vimejengwa lakini havijaanza kufanya kazi kutokana na kushindwa kupata ngozi za kutosha kunakosababishwa na ushindani usio haki katika biashara ya ngozi ghafi. Viwanda hivyo ni Open Enterprises (Footwear Manufacturing, Dar es Salaam; Morogoro Super Leather Ltd (Leather Product Manufacturing), Morogoro; Leather Products Manufacturing Mbagala, Dar es Salaam; Petrocity Tannery (Leather Processing), Mwanza na Morogoro Leather Community (Leather Products Manufacturing), Morogoro. Aidha, miradi sita (6) mipya ya viwanda vya kusindika ngozi na bidhaa za ngozi ambavyo viko katika hatua mbalimbali za utekelezaji ni pamoja na Tanmbuzi Co. (leather Processing), Kilimanjaro; Arusha City Complex Co. Ltd. (Leather processing), Arusha; Bhat Bangla Agritech (T) Ltd. (Leather products Manufacturing), Dodoma; Bhat Bangla Agritech (T) Ltd (leather processing), Dodoma; JAET Tannery Co. Ltd. (Mwanza) na Zhung FU International Co. Ltd. (Leather Production and Plastic Footwear, Mkuranga. 
Mheshimiwa Spika, kutokana na ukosefu wa ngozi za kutosha na ushindani usio wa haki kati ya wafanyabiashara wanaouza ngozi ghafi nje na wenye viwanda, Wizara kwa kushirikiana na wadau wa sekta iliwasilisha mapendekezo Serikalini ya kuzuia uuzaji wa ngozi ghafi nje ya nchi au kuongeza ushuru unaotozwa. Lengo ni kuhakikisha upatikanaji wa ngozi za kutosha kwa viwanda vya kusindika ngozi nchini ili kuuza ngozi zilizosindikwa na bidhaa za ngozi badala ya ngozi ghafi. Makubaliano yamefikiwa na Wizara ya Fedha kuanzia Julai, 2012, ngozi ghafi zitakazouzwa nje ya nchi zitozwe ushuru wa asilimia 90 au Shilingi 900 kwa kilo kutegemea thamani iliyo juu ikilinganishwa na asilimia 40 au Shilingi 400 kwa kilo iliyokuwa inatozwa.
Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea na utekelezaji wa Programu ya Uanzishwaji na Uendelezaji wa Vijiji vya viwanda kupitia mipango mitatu. Mpango wa kwanza ni wa kuanzisha na kuendeleza vijiji vya viwanda kama maeneo maalum ya kuhamasisha na kuchochea uwekezaji wa viwanda vya usindikaji na utengenezaji wa bidhaa za ngozi nchini. Katika kutekeleza mpango huo, Wizara imeanza na Kanda ya Kati inayojumuisha mikoa ya Morogoro, Dodoma na Singida; na Kanda ya Mashariki inayojumuisha mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ambapo maeneo husika yamekwishabainishwa na kutengwa na Halmashauri husika. Hatua inayofuata ni ya kutekeleza taratibu za kuyatwaa maeneo hayo na kuanza kuweka miundombinu ya msingi kwa shughuli za viwanda.
Mheshimiwa Spika, mpango wa pili ni wa kuwezesha wadau wa Sekta Binafsi kuyafikia na kuyakuza masoko ya ndani na nje ya nchi kwa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini. Katika mpango wa kuwawezesha wajasiriamali wa sekta ya ngozi kutangaza bidhaa zao na kuyafikia masoko, Wizara iligharamia ushiriki wa wajasiriamali 40 katika Maonesho ya Kimataifa DITF, 25 katika NaneNane na 32 katika Maadhimisho ya Miaka Hamsini ya Uhuru. Vilevile, chini ya Mpango wa Kujengea Wajasiriamali wa Sekta ya Ngozi Uwezo wa Kitaalamu na Kiushindani katika Vijiji, Wizara kwa kushirikiana na LAT, SIDO, TBS na TIRDO wameendelea kutoa mafunzo ya usindikaji kwa njia ya asili na utengenezaji wa bidhaa za ngozi kwa wajasiriamali 120.

Kuandaa Taarifa Kuhusu Fursa za Uwekezaji katika Miradi ya Maendeleo ya Viwanda Nchini
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mkakati Unganishi wa Maendeleo ya Viwanda unaolenga Sekta Ndogo za Viwanda umekuwa unaendelea kwa kuainisha sekta za kipaumbele ili kuwezesha utekelezaji. Sekta ndogo za kipaumbele ambazo uhamasishaji unafanyika ili kupata wawekezaji ni nguo na mavazi, ngozi na bidhaa za ngozi, usindikaji mazao ya kilimo, mbolea na makaa ya mawe ya kuzalisha umeme. Aidha, rasimu ya Mpango Kabambe wa kutekeleza Mkakati Unganishi wa Maendeleo ya Viwanda iliandaliwa na kujadiliwa na kikao cha wadau kilichofanyika tarehe 19 Aprili, 2012 ili kupata maoni ya wadau. Mpango huo ukikamilika utakuwa dira nzuri ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya viwanda kwa muda mfupi, wa kati na mrefu.

SEKTA YA VIWANDA VIDOGO NA BIASHARA NDOGO
Kuendeleza Programu ya Muunganisho wa Ujasiriamali Vijijini (MUVI) kwa Kutoa Ushauri, Mafunzo, Mitaji na Huduma za Kiufundi kwa Wajasiriamali
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea na zoezi la kuperemba na kutathmini shughuli za  utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo kulingana na malengo iliyojiwekea. Katika mwaka 2011/2012, tathmini imefanyika katika mradi wa Muunganisho Ujasiriamali Vijijini (MUVI) ulioanza kutekelezwa mwaka 2007 wenye lengo la kuchangia katika kupunguza umasikini vijijini kwa kuhamasisha wadau kujikita katika kuongeza thamani ya mazao na kupatikana kwa soko la uhakika kwa ajili ya mazao hayo. Walengwa wa mradi ni wakulima na wananchi walio vijijini ambao hupata mafunzo ya kilimo cha kisasa, masoko, teknolojia rahisi na umuhimu wa kuongeza thamani na kuwaunganisha na taasisi za fedha kwa ajili ya kupata mikopo yenye masharti nafuu. 

Mheshimiwa Spika, mradi unatekelezwa kwa kuzingatia uboreshaji wa mawasiliano kwa ajili ya kubadilishana taarifa za masoko na kujenga uwezo wa taasisi zinazohusika katika baadhi ya mikoa nchini. Mikoa hiyo ni Ruvuma (Namtumbo, Mbinga na Songea Vijijini), Mwanza (Sengerema, Ukerewe na Kwimba), Tanga (Muheza na Handeni), Iringa (Kilolo na Iringa Vijijini) Manyara (Simanjiro, Hanang na Babati), Pwani (Rufiji, Mkurunga na Bagamoyo) na Njombe. Mradi umewezesha kuundwa jumla ya vikundi 319 vyenye wanachama 15,482. Mfumo wa usambazaji mbegu bora umeimarishwa kupitia kampuni 20 zilizopatikana kiushindani na wakulima 117 wa mazao mchanganyiko wamepata mafunzo kupitia mashamba darasa ya matumizi ya mbegu bora. Utaratibu huo umeweza kutoa mkulima bora kutoka Wilaya ya Handeni na kuzawadiwa trekta la power tiller.
Kuongeza mchango wa Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo (SMEs) katika Pato la Taifa kutoka asilimia 33 hivi sasa kufikia asilimia 40 mwaka 2015

Mheshimiwa Spika, kwa miaka mingi, Wizara haikuwa na takwimu za uhakika za ukubwa na mchango wa Sekta ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo katika Pato la Taifa na ajira. Kufuatia kukamilika kwa utafiti (baseline Survey) wa Sekta hiyo, imebainika kuwa mchango halisi wa sekta katika Pato la Taifa kwa sasa ni asilimia 27.9 na inachangia asilimia 23.4 katika ajira ya Taifa. Taarifa hizo zinabaini kuwepo zaidi ya jasiriamali milioni 3 ambazo zinaajiri zaidi ya Watanzania milioni 5. Takwimu hizo zitaiwezesha Wizara kupanga mipango makini ya kuendeleza sekta. Aidha, miradi na Programu mbalimbali zinatekelezwa vijijini ikiwepo Muunganisho wa Ujasiriamali Vijijini (MUVI) na Wilaya Moja Bidhaa Moja (ODOP) ili kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja,  Pato la Taifa na uchumi kwa ujumla. Wizara pia, iko katika hatua za awali za kuanzisha kongano za viwanda vidogo (Industrial Clusters) katika Mikoa ya Morogoro, Dodoma, Singida, Manyara na Kilimanjaro ili kuinua kipato cha wananchi kwa kukuza shughuli za wajasiriamali wadogo na kuwezesha wengi kuanzisha biashara.
Kuendeleza, Kuzalisha na Kusambaza Teknolojia za Kuongeza Thamani Mazao Kupitia Vituo ya Maendeleo ya Teknolojia vya SIDO vilivyopo Mbeya, Arusha, Kilimanjaro, Lindi, Iringa na Kigoma

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, jumla ya teknolojia mpya 174 zimetafutwa kutoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya matumizi ya miradi ya uzalishaji. Aidha, SIDO kupitia vituo vyake vya uendelezaji wa teknolojia vilivyopo Mbeya, Arusha, Kilimanjaro, Lindi, na Kigoma iliwezesha utengenezaji wa mashine mpya za aina mbalimbali 604 na vipuri 2,472 zikiwemo za kubangua korosho na karanga, kupukuchua na kukoboa mahindi na mpunga, na kusindika alizeti. Teknolojia hizo zimewezesha wajasiriamali kuongeza tija katika uongezaji thamani ya mazao ya kilimo.

Kutoa Elimu na Kuwajengea Uwezo Wakulima wa Kusindika Mazao Kabla ya Kuyauza kama vile Usindikaji wa Asali, Utengenezaji wa Mvinyo, Utengenezaji wa Juisi pamoja na Ufungashaji wa Bidhaa kwa Kutumia Teknolojia ya Kituo cha TBS
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, SIDO, imetoa mafunzo kwa Wajasiriamali ili kuwaimarisha katika kuendesha na kuendeleza shughuli za biashara na miradi ya uzalishaji. Mafunzo yaliyotolewa ni usindikaji wa nafaka na matunda kwa wajasiriamali 1,764, ujuzi maalum ya usindikaji wa mafuta ya alizeti, utengenezaji sabuni, mishumaa, chaki, utengenezaji wa mizinga ya kisasa na usindikaji wa asali ulitolewa kwa wajasiriamali 2,054 kupitia kozi 143 na wajasiriamali 63 wa usindikaji wa ngozi na bidhaa zake . Wasindikaji wa mazao 840 walipata vifungashio katika mikoa yote. Vilevile, jumla ya wajasiriamali 8,880 kupitia kozi 368 wamepata mafunzo ya maarifa na stadi za kuimarisha shughuli zao za uzalishaji mali. Mafunzo hayo yamewawezesha wajasiriamali kufanya kazi kwa kujiamini na kuweza kuzalisha bidhaa bora zenye kukubalika na soko la ndani na nje na hususan katika soko la Afrika Mashariki na SADC.

Kuwaunganisha Wajasiriamali Wadogo na Makampuni Makubwa yaliyo Tayari Kununua Bidhaa Zao
Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na SIDO imeweza kuwaunganisha Wajasiriamali wadogo na makampuni makubwa na ya kati ambapo jumla ya biashara za  wajasiriamali wadogo 228 ziliunganishwa na viwanda vya kuchambua na kukamua mafuta ya pamba, viwanda vya kusindika samaki. Pia, makampuni kama Katani ltd, Handeni mini refinery, SUMA JKT, Nyanza Mine, Tobacco Authority, Prume Timber Ltd, Kampala University, Intermec Engineering, Katapala Engineering, Safari Co. Ltd; Mohamed Enterprises, Lavena U-Tum Supermarkets na Kiwanda cha Bisikuti katika mikoa ya Tanga, Arusha, Dar es Salaam, Morogoro, Mwanza, Shinyanga, Rukwa na Tabora ikilinganishwa na wajasiliamali 58 waliounganishwa na makapuni hayo mwaka 2010/11. Wajasiriamali wamehamasishwa kuzalisha bidhaa zenye ubora na kupata masoko ya uhakika kwenye makampuni hayo.

Kujenga Uwezo wa SIDO na Kuwatafutia Vyanzo vya Fedha ili Kuwawezesha Kutoa Mafunzo ya Usindikaji kwa Wajasiriamali Wadogo. Aidha, Kuifanyia Mapitio Sheria Iliyoanzisha SIDO ili Iendane na Mahitaji ya Uchumi wa Sasa
Mheshimiwa Spika, Wizara imefanya jitihada mbalimbali katika kuijengea uwezo SIDO, licha ya ufinyu wa Bajeti ya Serikali. Kwa mfano SIDO ilipata fedha za maendeleo Shilingi milioni 860, mwaka 2009/2010, Shilingi milioni 542 mwaka 2010/2011 na Shilingi bilioni 1.8 mwaka 2011/2012. SIDO pia, imekuwa ikifanya kazi kwa kushirikiana na Sekta Binafsi pamoja na Washirika wa Maendeleo kama vile IFAD kupitia mradi wa MUVI, KOICA na EU katika kutoa mafunzo na upatikanaji wa vitendea kazi. Katika mwaka 2011/2012, Serikali imepeleka maofisa 11 wa SIDO katika mafunzo na semina mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kitaalamu wa kuwahudumia wajasiriamali wadogo kwa ufanisi zaidi. Katika mwaka 2012/2013 SIDO imetengewa Shilingi 3,645,000,000.00.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2011/2012, Serikali kupitia SIDO imeendelea kutoa huduma za kuendeleza ujasiriamali nchini ambapo jumla ya wajasiriamali 10,964 walipata mafunzo mbalimbali na wajasirimali 16,138 walipata huduma za ushauri na ugani. Aidha, wajasiriamali 1,518 waliwezeshwa kushiriki maonesho ya bidhaa za wajasiriamali na mikopo 4,387 yenye thamani ya Shilingi 4.18 bilioni ilitolewa kupitia Mfuko wa WafanyaBiashara Wananchi (National Enterpreneurship Development Fund (NEDF).

Kuendeleza Miundombinu ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuhamasisha Manispaa na Halmashauri za Miji na Vijiji  kutenga  maeneo kwa ajili ya shughuli za wajasiriamali wadogo. Vilevile, Wizara kupitia SIDO inaendelea na maandalizi ya awali ya kujenga miundombinu ya kuanzisha kongano ya wahunzi wilayani Kwimba na utaratibu wa umiliki unakamilishwa. Wizara inaendelea kushirikiana na wadau wengine wakiwemo Mamlaka ya Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Sekta Binafsi katika kutenga na kuendeleza maeneo kwa ajili ya wenye viwanda vidogo na biashara ndogo ambapo maeneo 23 tayari yametengwa. EPZA pia, inatenga maeneo ya wajasirimali wadogo katika maeneo ya uwekezaji yanayopatikana. 

SEKTA YA BIASHARA 
Kuhamasisha Matumizi ya Fursa za Masoko ya Ndani, Kikanda na Kimataifa zikiwemo Fursa za Masoko ya AGOA, EBA, China, Japan, Canada na India ili Kukuza Biashara ya Nje kwa Kiwango Kikubwa
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea na uhamasishaji wa fursa za masoko baina ya nchi na nchi, kikanda na kimataifa kwa kutoa mafunzo kwa Maafisa Biashara wa Wilaya, Manispaa na Miji kuhusu fursa za masoko ya nje ikiwa ni pamoja na Sheria na kanuni za kuingia masoko hayo, Wizara kwa kushirikiana na Taasisi ya Misaada ya Southern Africa Trade Hub-SATH imetoa mafunzo kwa wadau 100. Jitihada nyingine ni kuwawezesha wajasiriamali kushirikisha wadau katika fursa za masoko hayo ni pamoja na yale ya upendeleo maalum yanayotolewa chini ya mpango wa AGOA na EBA, China, Japan, Canada na India; na yale ya kikanda ya SADC na EAC. Vilevile, Wizara imekuwa ikihusisha wadau hususan jamii ya wafanyabiashara katika majadiliano ya kikanda na kimataifa, misafara na maonesho ya kibiashara ili kujenga ufahamu wa mahitaji na changamoto za masoko ya ndani na nje. Pamoja na uhamasishaji huo, bidhaa zinazolenga masoko hayo zimeboreshwa na hivyo, kuongeza mauzo katika masoko hayo kama ilivyofafanuliwa katika aya 18 - 20.

Kutoa Mafunzo ya Kuwajengea Uwezo Wajasiriamali Kuhusu Mbinu za Kuyafikia Masoko ya Nje
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Wizara imefanikiwa kuwahamasisha na kuwapa mafunzo wajasiriamali 60 Kanda ya Mashariki kuhusu  fursa za masoko yaliyopo katika mfumo baina ya nchi na nchi, kikanda na kimataifa na pia masoko yanayopatikana katika Jumuiya ya Ulaya. Wajasiriamali 215 wamepata  mafunzo kuhusu soko la AGOA na masharti yake. Wizara pia, kwa kushirikiana na Sekretariati ya SADC imetoa mafunzo kwa wajasiriamali wapatao 90 huko Morogoro na Zanzibar kuhusu namna ya kukabiliana na changamoto zinazotokana na masharti kwenye Kanuni za Afya za Binadamu, Mimea na Wanyama (SPS), Vigezo vya Uasili wa Bidhaa (Rules of Origin -RoO) na Vikwazo Visivyokuwa vya Kiushuru (Non Tarrif Barriers NTBs)
Kuendelea na Majadiliano ya Ubia wa Kiuchumi kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Ulaya (EU)

Mheshimiwa Spika, Tanzania na nchi wanachama wa EAC zinaendelea na majadiliano ya Mkataba wa Ubia wa Uchumi (Economic Partnership Agreement -EPA) kati yao na Jumuiya ya Ulaya (EU), yaliyolenga katika maeneo matatu; Fursa za Masoko, Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo na Ushirikiano katika masuala ya Uvuvi. Kutokana na majadadiliano hayo, Jumuiya ya Ulaya imefungua soko lake kwa bidhaa kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki kuuzwa bila kutozwa  ushuru na bila ukomo (Duty Free Quota Free) isipokuwa kwa bidhaa za sukari na mchele ambazo zitaendelea kupewa mgao (Quota) katika kipindi hiki cha mpito. Kwa upande wa Jumuiya ya Afrika Mashariki imekubaliwa kuwa nayo itafungua soko lake kwa awamu katika kipindi cha miaka 25 kwa kiwango cha asilimia 82.6 ili kuruhusu bidhaa kutoka Ulaya kuingia bila ushuru. Jumuiya ya Ulaya itazisaidia nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kifedha na kiufundi katika shughuli za uzalishaji, miundombinu na uvuvi. 

Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo ya awali, majadiliano ya EPA yanakabiliwa na changamoto mbalimbali katika maeneo ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo, fursa za masoko na kilimo. EU inashindwa kuonyesha nia dhahiri ya kuzisaidia nchi wanachama kifedha.  Hii ni pamoja  na kutaka kupewa upendeleo sawa pale nchi wanachama wa EAC zitakapotoa upendeleo zaidi kwa nchi nyingine duniani zinazoibukia kiuchumi kwa kuingia mkataba na nchi hizo mara baada ya kusainiwa kwa Mkataba wa EPA. Aidha, EU imeshikilia msimamo wa kuzitaka nchi za EAC kutotoza ushuru kwa bidhaa zinazouzwa katika soko lao na kutoondoa ruzuku kwa bidhaa za kilimo wanazozalisha ambazo EAC pia wanazalisha kwa ajili ya soko hilo. Majadiliano bado yanaendelea kwa pande zote mbili kwa lengo la kuondoa changamoto hizo kabla ya kuhitimishwa kwa majadiliano na kusainiwa kwa mkataba huo.








Kuendelea na uanzishwaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)  na Kuendelea Kutekeleza Itifaki ya Biashara ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC)
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Tanzania ikiwa nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliendelea kushiriki katika majadiliano ya kukamilisha baadhi ya vipengele katika Itifaki ya Soko la Pamoja ambayo ilisainiwa mwezi Novemba 2009 na kuanza kutumika rasmi mwezi Julai, 2010. Hata hivyo, changamoto tuliyonayo ni kutokuwa na Sera inayoruhusu uwekezaji nje ili kutuwezesha kufaidika na fursa za uwekezaji wa mitaji katika Soko la Pamoja. Aidha, Tanzania imeendelea kushiriki katika hatua ya tatu ya mtangamano ya kuanzishwa kwa Umoja wa Fedha  (Monetary Union) wenye lengo la kuwa na Sarafu ya Pamoja. Hatua hiyo ikikamilika itasaidia kupunguza gharama za kufanya biashara na kuwepo kwa uchumi endelevu kwa Jumuiya. 
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC, Tanzania imeendelea na utekelezaji wa Itifaki ya Biashara ya SADC kwa kuendelea kupunguza viwango vya ushuru hadi kufikia asilimia sifuri ilipofika mwezi Januari, 2012. Hii ina maana kuwa bidhaa ziingiazo nchi wanachama hazitozwi ushuru. Vilevile, Tanzania inashiriki katika majadiliano ya kuanzishwa kwa Umoja wa Forodha wa nchi za SADC. Aidha nchi wanachama ikiwemo Tanzania ziko katika hatua ya awali ya kuanza majadiliano ya kufunguliana milango katika Biashara ya Huduma (Trade in Services) kwa kuanza na sekta sita za kipaumbele ambazo ni: Mawasiliano; Fedha; Usafirishaji; Utalii; Nishati; na Ujenzi. Hatua hizo zikikamilika zitapanua wigo wa biashara kwa kujumuisha biashara ya huduma.
Kufanya Utafiti wa kina juu ya Gharama za Kufanya Biashara Nchini kwa Lengo la Kupunguza Gharama hizo na Kuchochea Ukuaji wa Biashara
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Wizara kwa kushirikiana na wadau imekamilisha mapitio ya tafiti mbalimbali kuhusiana na vikwazo vya biashara visivyo vya kiushuru vinavyowakabili wafanyabiashara katika biashara ya ndani na pia, wanaposafirisha bidhaa zao kwenda nje ya nchi kupitia vituo vya mipakani. Hatua za awali zilizochukuliwa kukabiliana na tatizo hili ni pamoja na kuanzishwa kwa Kamati Maalum za Kitaifa na Kikanda kwa kushirikiana na nchi wanachama wa EAC na SADC. Majukumu ya Kamati hizo ni pamoja na  kuainisha, kutoa taarifa na hatimaye kutafuta njia za kuondoa vikwazo vilivyoainishwa. Vilevile, nchi wanachama wa EAC na SADC zimeanzisha mfumo maalum wa kupeana taarifa  kwa njia ya mtandao (online) pale inapobainika kuwepo kwa vikwazo hivyo na hatimaye kuvitafutia ufumbuzi. Aidha, tumeanzisha Kamati Maalum za mipakani (Joint Boarder Committees) ambazo zinajumuisha taasisi na mamlaka zote zilizopo vituo vya mipakani ili kufuatilia kwa karibu na kuondoa vikwazo vyote visivyo vya kiushuru vinavyojitokeza. Hatua nyingine ni kuanzishwa kwa Vituo vya pamoja vya Mipakani (One Stop Boarder Posts) ambavyo vitasaidia kupunguza urasimu unaochangia ucheleweshwaji wa kuvusha bidhaa mipakani. Juhudi zinaendelea kuhakikisha kuwa vituo hivyo vinafanya kazi kila siku kwa saa ishirini na nne.

Kuratibu na Kuhamasisha Ushiriki wa Wajasiriamali wa Tanzania katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Ndani na Nje ya Nchi

Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na TanTrade imeendelea kuhamasisha wafanyabiashara na Taasisi za Serikali kushiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (35th DTIF) maarufu kama SabaSaba. Kwa mwaka 2011/2012, zilishiriki nchi 12, makampuni ya ndani 900 na 141 kutoka nje ya nchi. Wajasiriamali 46 wa Sekta za Nguo, Usindikaji, Ufungashaji, Uzalishaji, Ubunifu Mitambo na Zana mbalimbali pamoja na ngozi waliwezeshwa kushiriki katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yaliyoandaliwa na Kanda ya Kati mkoani Dodoma. Vilevile, makampuni yapatayo 9 yanaendelea kushiriki kwa awamu katika maonesho ya kimataifa ya EXPO Korea yaliyoanza mwezi Mei 2012 na yanatarajiwa kuhitimishwa mwezi Agosti, 2012. Ushiriki katika maonesho hayo umewezesha bidhaa za Tanzania kutangazwa na kupata masoko ya ndani na nje ya nchi na hivyo kuchochea uzalishaji na maendeleo ya viwanda nchini. 

Kufanya Utafiti wa Masoko na Bei ili Kupanua Wigo wa Mahitaji ya Masoko ya Bidhaa zetu
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Wizara ilifanya tafiti za kina zilizoainisha fursa za masoko na changamoto katika kutumia kikamilifu fursa za masoko zilizotolewa na nchi mbalimbali. Tafiti hizo zilihusu masoko ya upendeleo ya EAC na SADC, AGOA, EBA, na yale ya India, China, Japan, Korea na Mashariki ya Kati. Tafiti hizo zimesaidia wadau na hasa wafanyabiashara kwa ujumla kufahamu kwa kina fursa na changamoto zilizopo ambapo zitawasaidia katika kupanga mikakati endelevu ya kuzitumia fursa hizo. Changamoto hizo ni pamoja na ubora wa bidhaa, ufungashaji, Kanuni za Afya za Binadamu, Wanyama na Mimea (SPS), Vigezo vya Uasili wa Bidhaa (Rules of Origin -RoO) na Vikwazo Visivyokuwa vya Kiushuru (Non Tarrif Barriers - NTBs. )
Kuanzisha Programu ya kuwa na Utambulisho wa Kitaifa kwa Bidhaa
Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na wadau kutoka Sekta Binafsi imewezesha kuanzishwa kwa Programu ya utambuzi wa bidhaa na inaendelea kuhamasisha na kuwaelimisha wenye viwanda na Wajasiriamali kuhusu matumizi ya Nembo za Mistari (Bar Code). Wizara imekuwa ikitoa elimu kwa wajasiriamali na wenye viwanda vidogo juu ya umuhimu wa kutumia mfumo wa utambuzi wa bidhaa zao kwa kutumia nembo za mistari. Mpaka kufikia mwezi Aprili, 2012, jumla ya wazalishaji 151 wamejisajili kutumia huduma hiyo na bidhaa 3,000 ambazo ziko sokoni zina mfumo huu wa utambuzi. Baadhi ya viwanda kama vile Kagera Tea Company Ltd, Tanzania Breweries Ltd, Konyagi Tanzania Ltd, pamoja na wasanii wa muziki wameanza kutumia nembo hizo ambazo zinatolewa hapa nchini. Wizara inaendelea pia, kushirikiana na Wizara ya Habari na Maendeleo ya Vijana ili kuwashawishi wasanii kutumia huduma hiyo ya utambuzi wa bidhaa. Mfumo huo umeonyesha mafanikio makubwa ambapo bidhaa nyingi na hasa za wajasiriamali zimekubalika katika maduka makubwa (supermarkets). Vilevile, mfumo huo umewapunguzia gharama wazalishaji wetu ambao walikuwa wanafuata huduma hiyo nje ya nchi kwa mfano Kenya na Afrika ya Kusini.
SEKTA YA MASOKO 
Kukamilisha Mkakati wa Sera ya Masoko ya Mazao na Bidhaa za Kilimo
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Wizara ya mifugo na Uvuvi, Bodi za mazao ya pamba, kahawa, korosho, chai, tumbaku, sukari, katani na pareto, Agricultural Council of Tanzania (ACT) na Sekta Binafsi imekamilisha maandalizi ya Mkakati wa Masoko ya Mazao ya Kilimo na Bidhaa za Kilimo. Ufuatiliaji unaendelea ili kupata idhini ya Serikali kutekeleza Mkakati huo. Utekelezaji wa mkakati huo utawawezesha wakulima, pamoja na mambo mengine, kupata taarifa za bei za mazao na masoko ya ndani na nje ya nchi kwa wakati.

Kuendeleza Miundombinu ya Masoko ya Mikoa na kuanzisha Masoko Katika Vituo vya Mipakani ili Kukuza Biashara ya Ndani na Kikanda
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Wizara imeendelea kuhamasisha na kuibua miradi ya ujenzi wa miundombinu ya Masoko ya mazao katika Halmashauri zote nchini. Uhamasishaji huo hufanyika kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP). Miradi ya kuendeleza miundombinu ya masoko huibuliwa Wilayani na kuingizwa  katika Mipango ya Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya (District Agricultural Development Plans -DADPs). Uendelezaji wa miundombinu ya masoko hufanyika kupitia miradi mingine inayotekelezwa chini ya ASDP kama vile Mradi wa District Agricultural Sector Investment Project (DASIP) unaotekelezwa katika mikoa ya Mwanza, Geita, Kagera, Shinyanga, Mara na Kigoma. Aidha, Wizara imefanya tathmini ya maghala 47 yaliyojengwa kupitia Mradi wa DASIP katika mikoa ya Shinyanga (43) na Mwanza (4) ili kuyawezesha maghala hayo kutumika katika mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani.
Mheshimiwa Spika, ili kukuza biashara ya kikanda, maandalizi ya kujenga masoko saba ya mipakani katika mikoa ya Kagera, Mara, Shinyanga na Kigoma kupitia mradi wa DASIP yanaendelea vizuri. Masoko hayo yatajengwa katika mipaka ya Mtukula, Murongo, Mkwenda, Kabanga, Manyovu, Sirari na Isaka (bandari kavu). Mradi wa DASIP unakamilisha mpango wa kumpata Mshauri Mwelekezi wa usanifu na usimamizi wa ujenzi wa masoko hayo. Vilevile, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri za wilaya za Kasulu, Nanyumbu na Songea zinakamilisha maandalizi ya kufanikisha ujenzi wa masoko katika mipaka ya Kilelema (mpaka Kigoma/Burundi). Mtambaswala (mpaka Mtwara/Msumbiji) na Daraja la Mkenda (Songea/Msumbiji). Tayari timu ya wataalam ya Wizara imetembelea Mikoa hiyo.
Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kushirikiana na Halmashauri husika kufanikisha ujenzi wa masoko ya mipakani. Aidha, Wizara imekagua masoko yaliyoko kando kando mwa barabara kuu kati ya Dar es Salaam na Dodoma ili kuandaa mpango wa kuendeleza masoko hayo kwa kushirikiana na Halmashauri husika.

Kutekeleza Mkakati wa Kukuza Mauzo Nje na Mpango Unganishi wa Biashara 
Mheshimiwa Spika, ili kukuza mauzo nje Wizara kwa kushirikiana na Wizara za Kilimo, Chakula na Ushirika na Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Sekta Binafsi, TRA, TBS, WMA, Uhamiaji na Halmashauri husika, imeanzisha Kamati za Kufanya Kazi kwa Pamoja Mipakani (Joint Border Committee - JBC). Lengo ni kufanikisha ukaguzi na upitishaji wa mizigo na watu mipakani ili kupunguza muda wa kupitisha mizigo na watu wanapovuka mipaka kwenda nchi jirani. Kamati hizo zimeundwa katika mipaka ya Rusumo, Kabanga, Mtukula, Namanga, Kasumulu na Tunduma. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na USAID COMPETE imeandaa Mwongozo wa kupitisha bidhaa mipakani (Clearance Manual) na Mkakati wa Kufanya Kazi kwa pamoja katika vituo hivyo.
Mheshimiwa Spika, Wizara pia imeendelea kutangaza bidhaa za Tanzania kupitia maonesho mbalimbali. Katika kutekeleza mkakati huo, Wizara kwa kushirikiana na Taasisi zake imeshiriki kikamilifu katika maonesho ya NaneNane, Maonesho ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) na Maonesho ya Miaka 50 ya Uhuru kutangaza bidhaa zinazozalishwa na viwanda vyetu. Tathmini ya maendeleo ya Sekta za Viwanda, Biashara, Masoko na Viwanda Vidogo na Baishara Ndogo kwa miaka 50 imeonesha kuimarika kwa bidhaa zilizosindikwa na ubora wake, matumizi ya teknolojia za kisasa na kukua kwa biashara. Uzalishaji wa bidhaa za viwandani umeongezeka kukidhi mahitaji ya wananchi ikiwa ni pamoja na kupanuka kwa wigo wa bidhaa zinazozalishwa nchini. Wajasiriamali pamoja na taasisi nyingine binafsi ziliwezeshwa kushiriki katika maonesho ya Wakulima – NaneNane katika eneo la Wizara. Vilevile, Wizara kwa kushirikiana na Taasisi zake za Wakala wa Vipimo, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TanTrade), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) zilishiriki maonesho ya Wajasiliamali Wanawake yaliyofanyika Mnazi Mmoja ili kutangaza bidhaa wanazozalisha, kujenga mtandao wa kibiashara kuwezesha kujua fursa za masoko, mikopo n.k. Ushiriki wa Wizara ulilenga kutoa mafunzo ya ujasiriamali, ufungashaji, udhibiti ubora, matumizi ya vipimo na kuwapatia usajili wa majina ya biashara wajasiriamali hao na hivyo kuwajengea wajasiriamali hao uwezo wa kuzalisha bidhaa zenye ubora wa kimataifa. Kimataifa, Wizara kwa kushirikiana na TanTrade, imefanikisha maandalizi ya ushiriki wa Expo 2012 nchini Korea ambayo yameanza mwezi Mei, 2012 na yatamalizika Agosti, 2012. Pamoja na kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini, jumla ya makampuni tisa (9) yameshiriki katika maonesho hayo na kuonyesha na kuuza bidhaa mbalimbali za Tanzania. 
Mheshimiwa Spika, Wizara pia imeendelea kuwawezesha Wajasiriamali Kutumia Fursa za Soko la AGOA kwa kutoa elimu kwa wadau kuhusu fursa za soko hilo pamoja na masharti yake. Katika mwaka 2011/2012, Wizara imetoa elimu kwa wajasiriamali 30 kutoka sekta ya bidhaa za mikono, asali na vinyago. Aidha, mauzo ya Tanzania kupitia mpango wa AGOA yameongezeka kutoka Dola ya Marekani milioni 2.1 kwa mwaka 2010/2011, hadi kufikia Dola ya Marekani milioni 5.7 2011/2012, sawa na ongezeko la asilimia 171. Wizara imeshiriki katika mkutano wa kumi na moja wa AGOA ili kuhakikisha mpango wa AGOA unakuwa endelevu na wenye masharti nafuu. Ujumbe wa Tanzania uliitaka Serikali ya Marekani kuuangalia upya mpango huo na pia, tumeiomba Serikali ya Marekani kuongeza muda wa kuruhusu nchi za Afrika ikiwemo Tanzania kuagiza majora ya vitambaa nje ya nchi zilizopo katika mpango wa AGOA kwa ajili ya wajasiriamali kutengeneza nguo na kuuza Marekani bila ushauri.
Mheshimiwa Spika, Wizara pia, imeendeleza mikakati ya kutumia fursa za masoko kupitia Vituo vya Biashara vya Tanzania vilivyopo London na Dubai  kwa  kutoa taarifa za masoko kwa wadau kuhusu fursa za masoko zinazopatikana kupitia vituo hivyo. Taarifa za kuwepo kwa masoko ya uhakika kwa mazao mbalimbali eneo la Mashariki ya Kati imepatikana na mkakati unaandaliwa ili kuyatumia masoko hayo. Bidhaa zenye soko kubwa ni pamoja na viungo vya chakula (spices). 
Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha Mfumo wa Taarifa za Masoko, Wizara imeendelea kukusanya, kuchambua, kuhifadhi na kusambaza kwa wadau taarifa za masoko ya mazao makuu ya chakula mara tatu kwa wiki na zile za rejareja mara mbili kwa kila mwezi. Aidha, taarifa za bei ya mifugo hukusanywa na kusambazwa mara moja kila juma. Wizara pia, imeandaa Mfumo Mpana na Unganishi wa Taarifa za Masoko kwa kushirikiana na Benki ya Dunia. Mfumo huo wa taarifa utawezesha kupatikana kwa taarifa zitakazounganisha biashara ya ndani na nje ya nchi. Wizara inajiandaa kufanya majaribio ya utekelezaji wa mfumo huu wa taarifa na majadiliano yanafanyika na Wahisani wa Maendeleo ili kupata fedha za kuufanyia majaribio ya utekelezaji wa mfumo huo nchi nzima .

Kuendeleza Biashara ya Ndani ikiwa ni Pamoja na Kujenga Dhana ya Kutumia Bidhaa Zilizozalishwa Tanzania (NUNUA BIDHAA ZA TANZANIA)

Mheshimiwa Spika, katika juhudi za Serikali kuhamasisha matumizi ya  bidhaa za ndani kwa kupitia kauli mbiu ya ‘NUNUA BIDHAA ZA TANZANIA JENGA TANZANIA’, Wizara imeendelea kuwajengea uwezo wajasiriamali ili kuzalisha bidhaa zenye ubora na matumizi ya vifungashio bora kwa kuzingatia matakwa ya soko. Ili kutimiza azma hiyo, Wizara kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) imeendelea kutoa mafunzo ya ubora wa bidhaa na ufungashaji bora kwa wajasiriamali wadogo na wa kati. Hadi kufikia mwezi Machi, 2012, jumla Wajasiriamali (SMEs) 248 kutoka mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya walipatiwa mafunzo hayo.

Kuboresha na Kupanua Wigo wa Biashara Mtandao Katika Ngazi ya Wilaya, Mkoa hadi Taifa

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia BRELA, imekamilisha zoezi la kubadilisha taarifa za Makampuni na Majina ya Biashara kutoka katika Mfumo wa makabrasha na kuwa katika mfumo wa digitali (digital). Kukamilika kwa mfumo huo kutasaidia kupatikana kwa taarifa za makampuni na majina ya biashara kwa urahisi zaidi mara zinapohitajika na hivyo kupunguza muda wa kusajili majina ya biashara na makampuni hadi wastani wa siku mbili au tatu ikilinganishwa na siku zaidi ya saba hapo awali.
Mheshimiwa Spika, katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na taratibu za utoaji wa leseni za biashara, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) wameandaa mwongozo wa kurahisisha maandalizi ya nyaraka (MEMART) za usajili wa kampuni inayopatikana katika mtandao. Serikali pia, imepunguza urasimu wa kupata leseni za biashara kwa kuondoa masharti ya kupitisha maombi ya leseni za biashara katika Ofisi za Mipango Miji na hivyo kuwezesha leseni hutolewa kwa siku moja endapo masharti muhimu yamekamilika; na Sheria mbalimbali za Biashara zimefanyiwa marekebisho ili zikidhi mahitaji ya sasa ya kufanya biashara. 

Kupanua Matumizi ya Simu za Viganjani Katika Kutoa Taarifa za Bei ya Mazao na Masoko kwa Wakati. Aidha, Kuangalia Uwezekano wa Kuanzisha Mbao za Matangazo Katika Ngazi ya Wilaya na Mkoa ili Kutoa Taarifa Mbalimbali Ikiwemo Bei na Masoko kwa Wakati Muafaka
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2011/2012, Wizara imeendelea kuboresha mfumo wa kukusanya na kusambaza taarifa za masoko kwa kushirikiana na Sekta Binafsi ili kuweza kutumia simu za viganjani katika kukusanya na kusambaza bei ya mazao kwa wakati. Wizara imesaini Mkataba wa Maelewano na Sekta Binafsi na tayari majaribio ya kukusanya na kusambaza taarifa za bei za mazao na huduma za ugani katika mikoa ya Dar es salaam, Morogoro, Iringa na Dodoma yameanza. Lengo ni kupanua matumizi ya teknolojia hiyo ili iweze kutumika nchi nzima katika ukusanyaji na usambazaji wa taarifa za bei za mazao na huduma za ugani kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kuwa taarifa hizo zinawafikia wananchi wengi zaidi, hasa wale waliopo vijijini, Wizara kwa kushirikisha Sekta Binafsi imeanza kusambaza taarifa za masoko kupitia redio za jamii (community radios) ambazo zipo katika wilaya nyingi nchini pamoja na mbao za matangazo katika ngazi ya wilaya na kata.
Kuendeleza Mchakato wa Kuanzisha Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara
Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) ilizinduliwa rasmi mnamo tarehe 01 Julai, 2011, na Mhe. Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika mwaka 2011/12, TanTrade imeanza kutekeleza majukumu yake mapya ya kuendeleza biashara ya nje na ya ndani. Ili kufanikisha hilo,  marekebisho madogo ya Sheria ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania Na. 4 ya 2009 yamefanyika kwa lengo la kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini. Marekebisho hayo yalipitishwa na Bunge tarehe 12 Aprili, 2012. 

Kuendeleza Utekelezaji wa Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani 
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12 Wizara kupitia Bodi ya Leseni za Maghala Tanzania imetoa mafunzo kuwezesha kuanzishwa kwa mfumo wa Stakabadhi kwa zao la kahawa mkoani Kagera. Aidha, uhakiki wa maghala yanayofaa kwa kazi hiyo umefanyika na kwa kuanzia utekelezaji wa mfumo utafanyika kwa majaribio katika Wilaya ya Ngara. Vile vile, timu ya Maafisa wa Wizara kwa kushirikiana na maafisa wa Bodi ya Leseni za Maghala walikagua maghala yaliyojengwa kupitia Mradi wa DASIP katika mikoa ya Shinyanga na Mwanza ili kubaini yale yanayofaa kwa ajili ya matumizi ya Mfumo wa stakabadhi za Maghala. Uhakiki huo ulilenga kuwezesha matumizi ya mfumo wa stakabadhi kwa mazao ya mpunga na pamba. Bodi ya Leseni za Maghala imeanza kutoa elimu ya mfumo katika mikoa hiyo ili kuwezesha uanzishaji wa matumizi ya mfumo wa stakabadhi kwa zao la mpunga ambalo linazalishwa kwa wingi katika eneo hilo. Mfumo wa stakabadhi kwa hivi sasa unatekelezwa katika mazao ya korosho, kahawa, ufuta, alizeti, mahindi na mpunga. Ikumbukwe kuwa, mfumo huo utakuwa nguzo kuu ya uanzishwaji wa Soko la Bidhaa (Commodity Exchange) kwa kuwa unawezesha upatikanaji wa mazao katika maghala kwa kuzingatia viwango vya ubora na wingi.

Kuendeleza Miundombinu ya Masoko ya Mikoa na Kuanzisha Masoko Mpakani kama vile Karagwe, Kigoma, Holili, Horohoro, Namanga, Sumbawanga, Taveta na Tarakea

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, ujenzi wa miundombinu ya masoko ya mazao kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP) inayopangwa katika Mipango ya Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya (District Agricultural Development Plans - DADPs) na miradi kama vile DASIP unaendelea katika Wilaya za Tarime (Sirari), Misenyi (Mtukula), Karagwe (Murongo na Mkwenda), Ngara (Kabanga), Kigoma (Manyovu) na Kahama (Isaka – Bandari kavu). Miundombinu kama masoko, maghala, machinjio na barabara za vijijini imejengwa. Wizara inaendelea na uhamasishaji wa kuibua miradi ya kuimarisha na kujenga masoko ya mazao katika Halmashauri  zote nchini. 
Mheshimiwa Spika, vile vile, kazi ya kuandaa Mpango Kabambe (Master Plan) wa ujenzi wa masoko katika miji ya Segera na Makambako iliyofanywa na Chuo Kikuu cha Ardhi imekamilika. Maeneo ya ujenzi wa masoko haya yamepimwa na kuwekewa alama za mipaka kwa kushirikiana na Halmashauri husika ili kuzuia uvamizi maeneo hayo. Wizara imeanzisha majadiliano na Benki ya Rasilimali (TIB) ili kufanikisha ujenzi wa masoko haya muhimu. Aidha, maandalizi  ya kujenga masoko saba ya mipakani katika mikoa ya Kagera, Mara, Shinyanga na Kigoma kupitia mradi wa DASIP yanaendelea vizuri. Masoko haya yatajengwa katika mipaka ya Mtukula, Murongo, Mkwenda, Kabanga, Manyovu, Sirari na Isaka (bandari kavu). Mradi wa DASIP unakamilisha mpango wa kumpata Mshauri Mwelekezi wa usanifu na usimamizi wa ujenzi wa masoko hayo. 
Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kufanya tafiti za masoko ya mipakani na kuzishauri Halmashauri za Wilaya husika ili kufanikisha ujenzi wa masoko hayo. Timu ya Wizara imetembelea Mkoa wa Kigoma, Wilaya ya Kasulu kubainisha maeneo yanayofaa kuendelezwa kimasoko ili kukuza biashara kati ya nchi yetu na nchi jirani ya Burundi. Wizara itaendelea kushirikiana na Halmashauri husika kufanikisha ujenzi wa masoko ya mipakani. Aidha, Wizara imekagua masoko yaliyoko kando kando mwa barabara kuu kati ya Dar es Salaam na Dodoma ili kuandaa mpango wa kuendeleza masoko kando kando ya barabara hiyo. Wizara itashirikiana na Halmashauri husika ili kufanikisha ujenzi wa masoko hayo.

Kushirikiana na Sekta Binafsi Katika Kubuni na Kutekeleza Mikakati ya Masoko ya Ndani, Kikanda na Kitaifa
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kushirikiana na Sekta Binafsi kupitia Jukwaa la Wadau wa Masoko ya Mazao ya Kilimo (Agricultural Marketing Forum) ambalo huwakutanisha wadau ili kujadiliana maendeleo ya masoko ya mazao ya kilimo na mifugo. Kupitia jukwaa hilo Wizara imeweza kushirikiana na Taasisi zifuatazo: Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA), Tanzania Horticultural Association (TAHA), Horticultural Development Council of Tanzania (HODECT), Agricultural Council of Tanzania (ACT), Rural Livelihood Development Company (RLDC), Tanzania Agricultural Market Development Trust (TAGMARK), Bodi za Mazao na Vyama vya Ushirika.  Mafanikio ya ushirikiano huo ni pamoja na kuandaliwa kwa Andiko la Kuanzisha Soko la Bidhaa (commodity exchange); Mkakati wa Masoko ya Mazao na bidhaa za Kilimo, Mkakati wa Leseni za Udhibiti, mapendekezo ya kuboresha mazingira ya biashara, kufanya mapitio ya utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo kwa pamoja.
Kuwalinda Wajasiriamali wa Ndani kwa Kutoingiza Bidhaa Mbalimbali Kutoka Nje ambazo Zinaua Soko la Ndani la Bidhaa
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha udhibiti wa bidhaa duni (substandard) kutoka nje ya nchi, Wizara kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) tangu tarehe 01 Februari, 2012 imeanza kutekeleza utaratibu wa kupima ubora wa bidhaa zote mahali zinakotoka kabla ya kuingiza nchini (Preshipment Verification of Conformity to Standards – PVoC). Katika kuwalinda wajasiriamali, Wizara kupitia Tume ya Ushindani imeendelea kufanya ukaguzi wa bidhaa bandia katika bandari Kuu ya Dar es Salaam na bandari kavu (Inland Container Depots). Vilevile, Tume imeendelea kufanya ukaguzi katika maghala na maduka ya wafanyabiashara. 

2.3 MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MWAKA 2011/12 

SEKTA YA VIWANDA,
Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza utoaji wa mafunzo ya kuongeza tija, ufanisi na ubora wa bidhaa za viwanda ikiwa ni pamoja na uzalishaji unaozingatia hifadhi na kulinda mazingira, Wizara inaendelea kupata ushirikiano mzuri kutoka Serikali ya Japan, kupitia Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) ambapo imeendelea kupata wataalam wa kusaidia katika kuendeleza viwanda. Hii inajumuisha msaada wa kuanzisha Programu ya Kaizen itakayotoa mafunzo ya kuongeza tija, ufanisi, usimamizi wa shughuli za viwanda na kuongeza ubora wa bidhaa. Mradi huo unatekelezwa kufuatia mafanikio ya majaribio (pilot project) ya mwaka 2010/2011 yaliyohusisha wajasiriamali 113 wenye viwanda vidogo vya nguo na mavazi katika mkoa wa Dar es Salaam. Aidha, makampuni kutoka Japan yenye nia ya kuwekeza nchini katika sekta ya viwanda yameendelea kujitokeza kutokana na kuimarika kwa ushirkiano na kuboreshwa kwa mazingira ya biashara. Makampuni hayo ni pamoja na NITORI HOLDINGS Ltd linalotaka kuwekeza katika pamba na bidhaa za pamba na SUMITOMO katika uzalishaji wa mbolea.
Mheshimiwa spika, Wizara imeendelea kushiriki katika majadiliano ya kukamilisha Sera na Mkakati wa Maendeleo ya Viwanda ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), ikizingatia maslahi ya nchi na mapendekezo ya Sekta Binafsi. Vilevile, Wizara iliendelea kushirikiana na Sekta Binafsi kwa kuandaa vikao vya kisekta kujadili maendeleo na changamoto na kutoa mapendekezo husika Serikalini. Sekta hizo ni pamoja na nguo na mavazi; ngozi na bidhaa za ngozi; chuma na uhandisi; kemikali; chakula na vinywaji; karatasi na vifungashio; mafuta ya kula na sabuni. Wizara ilishiriki katika mikutano ya UNIDO LDC na UNIDO General Conference iliyojadili maendeleo na changamoto za Sekta ya Viwanda na iliwezesha majadiliano kati ya viongozi wa Wizara na UNIDO na kukubaliana juu ya miradi ya kutekelezwa kwa ushirikiano. Miradi hiyo ambayo imeanza kutekelezwa ni pamoja na Industrial Policy Analysis, Industrial Upgraging and Mordernisation na Africa Agribusiness and Agroprocessing Development Initiative (3ADI).
Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na National Bureau of Statistics (NBS), CTI na UNIDO imekuwa ikifanya Tathmini ya Maendeleo ya Viwanda (Industrial Survey) nchini ambapo tathmini ya mwaka 2010 inakamilishwa. Aidha, kwa kuzingatia kuwa sensa ya viwanda ilifanyika mara ya mwisho mwaka 1989, Wizara kwa kushirikiana na NBS, Sekta Binafsi na wadau wa maendeleo itaendelea na majadiliano ya kuona namna ya kutekeleza kazi hii ifikapo mwaka 2013. Wizara tayari imeandaa andiko la kufanya sensa hiyo ambalo litagharimu takribani jumla ya Shilingi bilioni 8. Mazungumzo na UNIDO na NBS yanaendelea ili kupata wahisani wa kufadhili zoezi hilo. Kufanyika kwa sensa inayokusudiwa itawezesha kupata taarifa na takwimu sahihi zikiwemo idadi ya viwanda vilivyopo, bidhaa zinazozalishwa, ajira, mchango wa sekta katika Pato la Taifa, matumizi na mahitaji halisi ya umeme, maji na huduma nyinginezo. Aidha, taarifa hizo zitaiwezesha Serikali na wadau wengine kuweka mipango ya sekta kwa usahihi zaidi. 
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mradi wa Kasi Mpya unaendelea vizuri. Kampuni ya Maganga Matitu Resources  Development Limited (MMRDL) ambayo ni kampuni ya ubia kati ya NDC na MM Steel Resources Company Ltd imekamilisha kazi ya uchorongaji ili kuhakiki wingi na ubora wa mashapo ya chuma cha Maganga Matitu. Mashimo 58 yenye urefu wa jumla ya mita 11,298 yalichimbwa kwa ajili hiyo. Aidha, uchorongaji katika eneo la makaa ya mawe ya Katewaka umekamilika na jumla ya mashimo 28 yenye urefu wa mita 4,547 yamechimbwa. Ujenzi wa migodi ya chuma na makaa ya mawe na kiwanda cha kuzalisha chuma ghafi unatarajiwa kuanza mwaka 2013. Uzalishaji wa chuma ghafi unatarajiwa kuanza mwaka 2014. 
Mheshimiwa Spika, Mradi wa Ngaka Kusini wa kuzalisha umeme kutokana na makaa ya mawe unatekelezwa na Kampuni ya TANCOAL ENERGY Ltd ambayo ni kampuni ya ubia kati ya NDC na kampuni ya Intra Energy Ltd. Mradi huo tayari umeanza uchimbaji wa makaa ya mawe kwa ajili ya matumizi viwandani na unatarajiwa kuzalisha umeme wa MW 400 hadi MW 600 kwa ajili ya kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa. Shirika la NDC linamiliki asilimia 30 ya hisa na Intra Energy asilimia 70. Upembuzi yakinifu wa kuanzisha mgodi wa makaa ya mawe wa Ngaka Kusini umekamilika na kuthibitisha kuwepo kwa mashapo kiasi cha tani milioni 251. Ujenzi wa mgodi wa makaa ya mawe ulianza Agosti 2011. Kampuni ya TANCOAL imeanza uzalishaji wa makaa ya mawe na kiasi cha tani 85,000 kimechimbwa na kuuzwa kwa viwanda vya saruji vya Mbeya, Tanga na kiasi kimeuzwa nchini Malawi na kuingiza jumla ya Dola ya Marekani milioni 3. TANCOAL ina mpango wa kujenga kituo cha kuzalisha umeme wa MW 200 kwa kuanzia ifikapo mwezi Desemba 2015 hadi MW 400 mwaka 2017/2018 na kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa. Sambamba na ujenzi huo, TANCOAL imepanga kujenga njia ya msongo mkubwa wa umeme (Kilovoti 220 hadi 400) kati ya Ngaka na Songea (Kilometa 100) kwa ajili ya kupitishia umeme utakaozalishwa. Hivi sasa, TANCOAL inafanya mazungumzo na TANESCO kuhusu mkataba wa mauzo ya umeme (Power Purchase Agreement-PPA) utakaozalishwa na kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa.
Mheshimiwa Spika, Mradi wa Umeme wa Upepo unaotekelezwa na Kampuni ya ubia kati ya NDC, TANESCO na Kampuni ya Power Pool East Africa Limited (PPEAL) iitwayo Geo Wind Power Tanzania Ltd. unategemewa kuzalisha umeme wa Megawati 50  kwa kuanzia na kufikia MW 300 ifikapo 2018/2019 kwa kutumia upepo huko Singida. Aidha, mkataba wa ujenzi (EPC Contract) umesainiwa kati ya NDC na Kampuni ya China Dalian International Economic & Technical Cooperation Group Co. Ltd (CDIG). Vilevile, maombi ya awali ya mkopo nafuu (Concession Loan) wa Dola ya Marekani milioni 136 yamewasilishwa Benki ya Exim ya China. Mazungumuzo yanaendelea kati ya Kampuni ya ubia na TANESCO ili kupata mkataba wa kuuza umeme (PPA) wakati uzalishaji utakapoanza. Ujenzi wa mradi unategemewa kuanza mwezi Agosti, 2012 na kukamilika mwezi Septemba 2013.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza viuadudu (biolarvicides) wa kibaiolojia wa kuua viluwiluwi vya mbu wanaoeneza malaria katika eneo la TAMCO-Kibaha, unaendelea vizuri. Wizara kupitia NDC inasimamia na kugharimia ujenzi wa kiwanda hicho ambacho ujenzi unafanywa kwa kutumia teknolojia na utaalam wa kiufundi kutoka nchi ya Cuba. Kiwanda kitakapoanza kazi kitakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 6 za viuadudu kwa mwaka. Gharama za ujenzi wa kiwanda hadi kukamilika ni Dola ya Marekani 22,307,688.00. Asilimia 75 ya fedha hizo imekwishalipwa hadi sasa. Aidha, NDC inatafuta wadau kutoka kwenye mashirika na Sekta Binafsi ili kugharimia asilimia 25 iliyobakia ambayo ni sawa na Dola ya Marekani5,576,922. Ujenzi wa kiwanda unatarajiwa kukamilika  Desemba 2012.. NDC inaendelea na mazungumzo na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuhusu kuingia mkataba wa ununuzi wa viuadudu hivyo pindi uzalishaji utakapoanza, mwanzoni mwa mwaka 2013. 
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia NDC imejipanga kutekeleza miradi ya usindikaji wa mazao ya kilimo ya mpira, michikichi na nyama kwa njia ya ubia kati yake, na wawekezaji, na kushirikisha wakulima wadogo. Juhudi za uongezaji thamani nyama zimeendelea ambapo NDC  imebainisha eneo la Themi Arusha kuwa ni muafaka  kujenga kiwanda hicho. Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi inayomiliki eneo hilo imekubali NDC kulitumia. Aidha, NDC imefanikiwa kumpata mwekezaji, Kampuni ya Kichina ya China Dalian International Economic & Technical Cooperation Group Co. Ltd (CDIG) na makubaliano ya awali (Memorandum of Understanding-MOU) yalisainiwa mwezi Julai 2011. Majadiliano yenye nia ya kusaini Mkataba wa Ubia yanaendelea. 
Mheshimiwa Spika, Vilevile, upembuzi yakinifu wa mazao ya muhogo, mtama mtamu na mchikichi (palm) ulifanyika na kuchagua mafuta ya mawese kama kipaumbele kati ya mazao hayo matatu. Juhudi za NDC kupata ardhi ya kuanzisha kilimo cha michikichi wilaya ya Kisarawe na Kibaha zinaendelea. Mwekezaji, Kampuni ya Nava Bharat African Resources PVT Ltd ya India kwa kushirikiana na NDC katika kilimo cha michikichi amepatikana. 
Mheshimiwa Spika, uendelezaji wa zao la mpira kwa mashamba ya Kalunga, Kilombero na Kihuhwi, Muheza yanaendelea vizuri na uzalishaji umeongezeka kutoka tani 120 mwaka 2010 hadi tani 202 mwaka 2011. Upanuzi wa shamba la Kalunga umeanza katika eneo ambalo lilikuwa halijaendelezwa. Kwa upande wa shamba la Kihuhwi bado upandaji miche haujaanza katika eneo ambalo halijaendelezwa kutokana na uvamizi uliojitokeza. Juhudi za kupata ufumbuzi kwa kushirikiana na Wilaya ya Muheza zinaendelea. Pia, juhudi za kupata ardhi zaidi kwa ajili ya mashamba mapya ya mpira katika Wilaya ya Kilindi zinaendelea.
Mheshimiwa Spika, uandaaji wa kanuni za kusimamia mfumo wa SEZ ili usajili wa wawekezaji uanze kutumika umeanza na rasimu ya kanuni za SEZ tayari  imeandaliwa na utaratibu wa kutangaza kanuni hizo katika Gazeti la Serikali uko katika hatua za mwisho. Vilevile, uandaaji wa Mpango Kabambe (Master Plan) wa eneo la kipaumbele la Bagamoyo SEZ unaendelea. Tayari maandalizi ya upembuzi yakinifu, uthaminishaji mali na kulitangaza eneo la mradi katika Gazeti la Serikali yamekamilika. Ujenzi wa miundombinu ya msingi kwa kushirikiana na Sekta Binafsi utaanza mara Mpango Kabambe wa Bagamoyo SEZ utakapokamilika. Makampuni 16 yameshawasilisha maombi ya kuendeleza miundombinu na kujenga viwanda katika eneo hilo. Aidha, taratibu za uendelezaji wa maeneo ya bandari huru na SEZ katika eneo la uwekezaji Mtwara na Kigoma zimeendelea. 
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Wizara kupitia EPZA imeendelea kuhamasisha wawekezaji kujenga miundombinu na  viwanda vya kuzalisha bidhaa katika maeneo maalum ya uwekezaji. Makampuni 19 yamepewa leseni kama yalivyobainishwa katika kitabu cha Mafanikio ya Sekta ya Viwanda na kuanzisha viwanda katika maneneo maalum na kufanya makampuni yanayozalisha kupitia mfumo huo kufikia 59. Aidha, mtaji katika maeneo ya EPZ umeongezeka kutoka Dola ya Marekani650 milioni na kufikia 792.2 milioni na ajira za moja kwa moja zimeongezeka kutoka 12,500 mpaka 16,105.
Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na UNIDO inatekeleza Mradi wa Kuboresha utendaji ili kuongeza ufanisi wa viwanda (Industrial Upgrading and Modernisation) hasa viwanda vidogo na vya kati. Mradi huu unalenga zaidi kutoa ushauri katika kuboresha maeneo ya menejimenti/utawala, matumizi mazuri ya rasilimali (wastes reduction), matumizi sahihi ya nishati, mpangilio wa mitambo ya uzalishaji (plant layout), ubunifu (innovation), matumizi ya teknolojia sahihi na kushauri juu ya ukarabati unaohitajika na hatimaye kuunganisha viwanda husika na masoko hasa ya nje. Kitengo cha kutekeleza mradi huo kimeanzishwa na UNIDO imekwishatoa mtaalamu atakayetoa mafunzo kwa Watanzania watakaotoa mafunzo na ushauri viwandani (trainer of trainers). Kwa kuanzia viwanda 15 vitanufaika.
Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na UNIDO inatekeleza Mradi wa Kujenga uwezo wa Wizara na wadau wa kuchambua Sera ya Maendeleo ya Viwanda. Aidha, chini ya mradi huo, ripoti (Industrial Competitiveness Report) imeandaliwa ili kuwezesha Serikali kutoa maamuzi sahihi. Mafunzo ya awali yalifanyika mwezi Machi 2012 na kuhusisha Wizara ya Viwanda na Biashara, Ofisi ya Rais - Mipango,  Wizara ya Fedha, Vyuo Vikuu (UDSM na Mzumbe), Sekta Binafsi na Asasi Zisizo za Kiraia. Ripoti hiyo inatarajiwa kuzinduliwa mwezi Agosti 2012. 
Mheshimiwa Spika, kupitia sera za uwekezaji ikiwa ni pamoja na sera ya PPP, Tanzania imeendelea kuvutia wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali duniani. Baadhi ya wawekezaji ambao wameonesha nia ya kuwekeza hapa Tanzania hivi karibuni ni Kampuni ya NITORI HOLDINGS Ltd. ya Japan. Nia yao ni kuwekeza katika kilimo cha pamba, viwanda vya nguo na mavazi, kauri (ceramics), bidhaa za vioo (glass) na ngozi na bidhaa za ngozi. Tayari Kampuni hiyo imefanya tafiti za awali kwa ajili ya kubainisha malighafi zilizopo nchini na kiasi kinachoweza kupatikana kwa ajili ya matumizi ya viwanda husika. 
SEKTA YA VIWANDA VIDOGO NA BIASHARA NDOGO

Mheshimiwa Spika, katika kujenga uwezo wa kutoa huduma za ugani kwa wajasiriamali hasa vijijini, Wizara imeendelea kuimarisha uwezo wa SIDO kwa kuongeza idadi ya wafanyakazi wenye ujuzi, kuwapa mafunzo watumishi wake ndani na nje ya nchi na kuwapatia vitendea kazi. Kutokana na juhudi hizo, SIDO imeweza kutoa huduma za ugani kwa wajasiriamali 16,138 katika mikoa yote ya Tanzania Bara. Serikali imezingatia umuhimu wa kuhakikisha kuwa teknolojia zinazofaa zinatafutiwa utaratibu wa kuzizalisha kwa wingi (commercialization of proven technologies), na kuzisambaza kwa watumiaji. Utekelezaji umefanywa hatua kwa hatua kwa kutumia vituo vya kuzalisha na kuendeleza teknolojia vya SIDO na vya wajasiriamali wadogo. Katika kipindi cha mwaka 2011/12, teknolojia 142 zilitafutwa kwa ajili ya matumizi ya wajasiriamali pia, wajasiriamali wabunifu waliweza kutengeneza teknolojia mpya 76. Aidha, kwa kutumia baadhi ya teknolojia hizo, jumla ya mashine 396 zilizalishwa na kusambazwa kwa watumiaji mbalimbali hasa katika usindikaji wa mazao ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea  kuhamasisha Manispaa na Halmashauri za Miji na Vijiji  kutenga maeneo kwa ajili ya kujenga viwanda vidogo ambavyo vitasaidia kuongeza thamani mazao. Aidha, Wizara imeanzisha mpango wa kuhamasisha ujenzi wa kongano (industrial clusters) katika mikoa kwa lengo la kusindika mazao na kuongeza thamani. Katika mkoa wa Singida, eneo la ekari 20 limetengwa katika Wilaya ya Singida Vijijini  kwa ajili ya kujenga kongano la kusindika na kuongeza thamani ya zao la alizeti. Ramani na michoro katika kijiji cha Mtinko, Singida Vijijini imekamilishwa. Eneo hilo ni mojawapo kati ya maeneo ambayo Shirika la Ushirikiano la Japan (JICA) limeonyesha nia ya kusaidia ujenzi wa makongano ya usindikaji wa zao la alizeti katika mikoa ya Dodoma, Manyara na Singida. Aidha, kwa mikoa ya Kilimanjaro na Morogoro yataanzishwa makongano ya shughuli za chuma (metal works). Usindikaji  na uongezaji thamani wa mazao unaongeza tija kwa mjasiriamali na bidhaa zinazozalishwa zitapata soko na kutoa ushindani katika soko la ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, ili kujenga misingi na kusaidia uzalishaji wa bidhaa mpya kutokana na ubunifu wa wajasiriamali binafsi, utaratibu wa kulea wabunifu (incubator Programu) unaosimamiwa na Wizara na kutekelezwa na SIDO, umeendelea kuwawezesha wajasiriamali kuendeleza ubunifu. Aidha,  ukarabati umefanyika kwa majengo 6 ili kukidhi haja ya ubunifu na wabunifu wapya 32 wamewezeshwa kwa kupewa sehemu ya kufanyia shughuli zao katika majengo hayo. Vilevile, jengo la kudumu kwa ajili ya kutoa huduma za ushauri, teknolojia na mawasiliano (ICT) katika mikoa ya Shinyanga, Mbeya, Arusha, Dar es Salaam, Tanga, Kigoma na Kagera limekamilishwa.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Wizara kwa kushirikiana na SIDO imetoa elimu ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara kwa wajasiriamali 8,880 katika mikoa yote ya Tanzania Bara. Maarifa na ujuzi waliopata washiriki umewasaidia kuongeza uelewa na ufanisi wa kuendesha miradi ya uzalishaji na biashara. Vile vile, wazalishaji wadogo wamewezeshwa kupata masoko ya bidhaa na huduma zao kwa kutengeneza miundombinu ya kupokea na kusambazia habari za kibiashara na kutengeneza sehemu za kuoneshea bidhaa za wazalishaji wadogo. Katika kufanikisha lengo hilo, Wizara kwa kushirikiana na SIDO, imetoa fursa kwa wajasiriamali kutangaza bidhaa zao na kupata habari za masoko, kupitia maonesho matatu ya kanda za Mashariki, Kusini na Nyanda za Juu Kusini ya bidhaa za wajasiriamali yaliyofanyika na kutoa fursa kwa wajasiriamali 649 kutangaza na kuuza bidhaa zao ambapo mauzo ya Shilingi milioni 316. 5 yalifanyika.
Mheshimiwa Spika, katika kutoa huduma za kifedha ikiwa ni pamoja na ushauri na mikopo pale itakapojidhihirisha kuhitajika, hadi kufikia Machi 2012, Serikali imeipa SIDO kiasi cha Shilingi milioni 300 kwa ajili ya kuongeza fedha za  mfuko wa NEDF na kufanya kiasi kilichotolewa na Serikali kwa ajili ya Wajasiriamali kufikia Shilingi bilioni 5.326 toka mfuko huo ulipoanzishwa mwaka 1994. Katika kipindi cha Julai 2011 hadi Machi 2012, jumla ya mikopo 4,387 yenye thamani ya Shilingi bilioni 4.181 ilitolewa kwa wajasiriamali.  Jumla ya ajira 8,719 zilitengenezwa kutokana na mikopo hiyo na asilimia 51.6 ya ajira hizo ilienda kwa wanawake. Aidha, ili kuhakikisha kuwa wajasiriamali wadogo wanatumia mikopo waliyopewa inavyotakiwa, Wizara kupitia SIDO imetoa mafunzo na ushauri wa mikopo kwa wajasiriamali 14,688 katika mikoa yote ya Tanzania Bara.
Mheshimiwa Spika, katika kujenga uwezo wa uzalishaji wa zana za kilimo, Wizara kwa kushirikiana na SIDO kupitia vituo vyake vya uendelezaji wa teknolojia vilivyopo Mbeya, Arusha, Iringa, Kilimanjaro, Lindi, Shinyanga na Kigoma, iliwezesha utengenezaji wa zana mpya za aina tofauti 604. Zana hizo ni pamoja na  jembe la kukokotwa na wanyama kazi, mashine ya kupandia, pampu za maji, mashine ya kuvunia, mashine ya kupura mtama na mashine za kupukuchua nafaka.  Zana hizo zimerahisisha kazi ya kilimo na hatua za awali za usindikaji wa mazao ya shamba kwa ajili ya mahitaji mahsusi kwa uzalishaji mali. Aidha, vipuri 2,472 vilizalishwa na kusambazwa kwa watumiaji ili kuhakikisha kuwa shughuli za uzalishaji haziathiriki kwa kukosa vifaa hivyo muhimu.
SEKTA YA BIASHARA
Mheshimiwa Spika, katika kuendelea kusimamia na kutekeleza Mikataba na Itifaki mbalimbali ambazo Tanzania imeridhia, Tanzania inatekeleza makubaliano ya kibiashara na uwekezaji baina yake na nchi mbalimbali zikiwemo Vietnam, Comoro, Uturuki, India, China, Canada na Marekani. Aidha, Tanzania inatekeleza Itifaki za biashara ya kikanda kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika; na mikataba ya kibiashara chini ya Shirika la Biashara la Dunia. 
Mheshimiwa Spika, katika kutoa mafunzo kwa Maafisa Biashara wa Wilaya, Manispaa na Miji kuhusu fursa za masoko ya nje ikiwa ni pamoja na Sheria na kanuni za kuingia masoko hayo, Wizara kwa kushirikiana na Taasisi ya Misaada ya Southern Africa Trade Hub-SATH imetoa mafunzo kwa wadau 100. Fursa za masoko hayo ni pamoja na yale ya upendeleo maalum yanayotolewa chini ya mpango wa AGOA na EBA, China, Japan, Canada na India; na yale ya kikanda ya SADC na EAC.
Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2011/2012, Wizara iliunda Kamati za Kitaifa za Wataalamu kwa ajili ya kujadili na kuishauri serikali kuhusu masuala ya biashara ya kimataifa. Kamati hizo ni pamoja na National Monitoring Committee on NTBs (NMC – NTBs), National SPS Committee, Technical Barriers to Trade (TBTs) na Trade Facilitation Committee. Kamati hizo zinajumuisha wadau kutoka Serikali na Sekta Binafsi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar. Kamati hizo zimekuwa zikifuatilia kwa ukaribu majadiliano yanayoendelea ya Duru la Doha kwa maeneo husika na kuishauri Serikali. Aidha, Wizara imeendelea kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) katika kuboresha mazingira ya biashara kama njia mojawapo ya kuleta maendeleo endelevu.
Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na wadau imefanya mapitio ya sheria ya Anti Dumping and Countervailling Measures. Rasimu ya mapitio hayo ipo katika hatua za mwisho kwa ajili ya kuwasilishwa ngazi za juu kwa ajili ya kupitishwa.  Sheria hiyo itakapoanza kutumika itatusadia kukabiliana na changamoto za uingizaji wa bidhaa kutoka nje zinazouzwa kwa bei ya chini kuliko gharama zake za uzalishaji ambapo itatuwezesha kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa makubaliano ya Shirika la Biashara la Dunia (WTO) ili kuleta ushindani wa haki katika biashara.  Aidha, Wizara kwa kushirikiana na WTO chini ya mwavuli wa EAC, inafanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Biashara kwa lengo la kuhakikisha kwamba inatangamana na matakwa ya WTO na hasa katika suala la uwazi na urahisishaji biashara. 
Mheshimiwa Spika, katika kuendelea kuimarisha mahusiano kati ya Nchi na Nchi, Kikanda na yale ya Kimataifa kwa lengo la kuendelea kukuza fursa za masoko kwa bidhaa zetu na kuvutia wawekezaji, Tanzania ilisaini Mkataba wa kulinda na kuendeleza uwekezaji baina yake na Uturuki. Aidha, Wizara iko katika majadiliano na Serikali  ya China kwa lengo la kuanzisha Kituo cha Biashara (Logistics Center) jijini Dar es Salaam. Kituo hicho kitawezesha wajasiriamali wa Tanzania hususan wanawake kupata maeneo ya kufanyia biashara. Kituo hicho kitawezesha upatikanaji wa teknolojia ya kisasa katika uongezaji thamani wa bidhaa  za Tanzania
Mheshimiwa Spika, Wizara pia inaendelea kushiriki katika majadiliano yatakayowezesha Jumuiya za COMESA, EAC na SADC kuanzisha Eneo Huru la Biashara (Tripartite Free Trade Area). Majadiliano hayo yanalenga kupanua fursa za masoko ya bidhaa za Tanzania na kurahisisha biashara kwa kuondoleana vikwazo visivyo vya kiushuru, kuimarisha miundombinu, kuvutia wawekezaji na kuleta maendeleo ya Viwanda. Wizara inaendelea kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Biashara ya mwaka 2003  ili iweze kuendana na mfumo wa utandawazi na mabadiliko yanayojitokeza katika nyanja ya biashara duniani.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuviimarisha Vituo vya Biashara vya Tanzania vilivyopo London na Dubai kwa kuviongezea uwezo kifedha ili kutekeleza majumu yake kikamilifu. Vituo hivyo vimekuwa vikitangaza vivutio mbalimbali vilivyoko Tanzania kwa lengo la kuvutia wawekezaji na vile vile kutoa taarifa za fursa za masoko ya bidhaa za Tanzania. Kituo kwa ushirikiano na Bodi ya Utalii na Kamisheni ya Utalii ya Zanzibar zinazoratibu Maonesho ya Kimataifa ya London huwezesha makampuni zaidi 60 kushiriki ili kupata masoko ya bidhaa zao na wabia.  

SEKTA YA MASOKO 
Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Benki ya Dunia imeandaa Mfumo Mpana na Unganishi wa Taarifa za Masoko. Mfumo huo utaunganishwa na mifumo ya wadau wengine katika kutoa taarifa za masoko ya ndani na nje. Hadi sasa Mfumo wa majaribio umekamilika kama ilivyoelezwa katika aya ya 73. Katika kuwajengea uwezo wazalishaji na wafanyabiashara kuzalisha zaidi na kuuza katika masoko yenye bei shindani, Wizara imeendelea kukusanya, kuhifadhi, kuchambua na kusambaza taarifa za masoko kwa wadau kupitia ujumbe wa simu za kiganjani, mtandao wa kompyuta na vyombo vya habari. Taarifa hizo hukusanywa mara tatu kwa wiki kwa mazao makuu ya chakula na mara moja kwa mifugo.
Mheshimiwa Spika, katika kuleta ufanisi wa biashara mipakani, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha inakamilisha taratibu za ujenzi wa Vituo vya Pamoja vya Ukaguzi Mipakani (OSBP) katika Vituo vya Tunduma/Nakonde na Kabanga/Kobero. Makubaliano ya ujenzi wa vituo hivyo kati ya Tanzania na nchi za Zambia na Burundi kuhusu ujenzi wa Vituo hivyo yamesainiwa. Kwa upande wa Kituo cha Tunduma/Nakonde, maandalizi ya awali ya ujenzi wa kituo hicho yamekamilika ikiwa ni pamoja na utafiti wa mahitaji na michoro, chini ya uratibu wa Wizara ya Fedha na ufadhili wa Taasisi ya Trade Mark East Africa.
Mheshimiwa Spika, ili kuendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini, Wizara imefanya mapitio ya Sheria ya Usajili wa Shughuli za Biashara (BARA 2007), ambayo ilihitaji marekebisho zaidi ya yale yaliyofanywa kupitia Sheria ya Fedha Na. 5 ya Mwaka 2011. Lengo ni kuwezesha utekelezaji wa sheria hiyo hususan kuruhusu utozaji wa ada za leseni. Wizara kwa kushirikiana na wadau imeandaa mapendekezo ya marekebisho husika kwa hatua zaidi. 
Mheshimiwa Spika, ili kusogeza huduma ya usajili wa majina ya Biashara na Makampuni karibu na Jamii ya wafanyabiashara, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni, (BRELA) wameendelea kuwasiliana na Chama cha Wafanya Biashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) ili ofisi zao zitumike kutoa huduma ya usajili wa majina. Aidha, BRELA wametembelea ofisi za TCCIA za Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Arusha, Kilimanjaro na Manyara ili kuona uwezekano wa kutoa huduma hiyo.Wafanyabishara wadogo 70 mkoa wa Tanga na 35 mkoa wa Pwani na wadau wengine wameelimishwa kuhusu huduma za usajili wa majina ya biashara na makampuni zinazotolewa na BRELA. 
Mheshimiwa Spika, vile vile, matumizi ya TEHAMA katika usajili wa majina ya biashara na uandikishwaji wa makampuni imewezesha upatikanaji wa taarifa na utoaji wa huduma za usajili kwa urahisi. Taarifa zote zinazohusu BRELA zinapatikana kupitia tovuti HYPERLINK "http://www.brela-tz.org"www.brela-tz.org. Huduma zinazopatikana ni pamoja na fomu za maombi ya kuandikisha makampuni; fomu za usajili wa majina ya biashara; fomu za maombi ya usajili wa alama za biashara na huduma; fomu za kuomba hataza; na fomu za maombi ya leseni za viwanda. 
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia utoaji wa leseni za Biashara kwa mujibu wa Sheria ya Leseni za Biashara Na. 25 ya Mwaka 1972 na marekebisho yake. Jumla ya leseni za Biashara 1,612 zimetolewa kwa kipindi cha Julai, 2011 – Machi 2012. Pia, marekebisho ya baadhi ya Sheria za biashara zinazosimamiwa  na Wizara ya Viwanda na Biashara imefanyiwa marekebisho na kupitishwa na Bunge ili kuboresha mazingira ya biashara nchini. Sheria hizo ni Sheria ya Makampuni ya mwaka 2002 (CAP 212); Sheria ya Usajili wa Majina ya Biashara (CAP. 213); “Merchandise Act, R.E. 2002”; na Sheria ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade). Vilevile, mapendekezo ya kutungwa Sheria Mpya inayoruhusu kuanzisha Kampuni za Ubia (Limited Liability Partnership) yamekamilika. Aidha, Wizara imekamilisha maandalizi ya rasimu ya Sera ya Leseni za Udhibiti pamoja na mkakati wake.  Sera hiyo inatoa mwongozo wa utoaji wa leseni za uthibiti ambazo kwa hivi sasa hutolewa na taasisi mbalimbali za udhibiti na hivyo kuongeza gharama za kufanya biashara. 
Mheshimiwa Spika, ili kufanikisha lengo la kukuza matumizi ya mfumo wa utambuzi wa bidhaa kwa kutumia nembo za mistari (bar codes) unaoratibiwa na Shirika la Kimataifa la GSI lenye ofisi zake huko Brussels Ubelgiji, Wizara inaendelea kuhamasisha wenye viwanda juu ya matumizi ya mfumo wa utambuzi wa bidhaa kupitia vikao mbalimbali vya wadau wa sekta. Aidha, Wizara imekuwa ikisisitiza wajasiriamali na wenye viwanda wadogo juu ya umuhimu wa kutumia mfumo wa utambuzi wa bidhaa zao kwa kutumia nembo za mistari (Bar Codes). Tangu mwezi Agosti 2011, utaratibu huo ulipoanzishwa, jumla ya Makampuni 151 yamejisajili kutumia huduma hiyo na takriban bidhaa 3,000 zimepata alama ya GS1. Aidha, baadhi ya viwanda vikubwa kama vile Kampuni ya Chai ya Kagera, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Tanzania Distilleries Co. Ltd yameanza kutumia nembo ya Tanzania. Vilevile, baadhi ya wasanii wa muziki wameanza kutumia nembo hizo na Wizara inaendelea pia kushirikiana na Wizara ya Habari na Maendeleo ya Vijana ili kuwashawishi wasanii zaidi kutumia huduma hiyo.
Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Maghala, ufuatiliaji wa ununuzi wa zao la korosho kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani umefanyika katika mikoa yote inayozalisha zao hilo (Pwani, Mtwara, Lindi, Ruvuma na Tanga). Changamoto kubwa iliyojitokeza katika msimu huu wa ununuzi wa zao la korosho ni kushuka kwa bei ya zao kulikosababisha korosho nyingi kutouzwa kwa wakati. Hadi kufikia Juni, 2012, takriban tani 14,000 za korosho kutoka mkoa wa Pwani na wilaya ya Tunduru zilikuwa hazijapata mnunuzi. Hata hivyo, Serikali imekamilisha taratibu za kuhakikisha kuwa wakulima wote wanalipwa sio chini ya Shilingi 1,200 kwa kilo ya korosho za daraja la kwanza.
TAASISI CHINI YA WIZARA

MAMLAKA YA MAENDELEO YA BIASHARA TANZANIA (TANTRADE)
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia TanTrade iliendelea na utafiti wa mifumo ya masoko na bidhaa zinazozalishwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga. Utafiti huo ni muendelezo wa utafiti uliofanyika mwaka 2010/2011, katika mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera, Shinyanga, Kigoma, Tabora na Singida unaokusudia kuweka mfumo wa mnyororo wa thamani (value chain) kwa kuanzia na bidhaa za asali, ngozi na bidhaa za utamaduni. Wizara inategemea kukamilisha zoezi hilo mwaka ujao wa fedha kutegemeana na upatikanaji wa fedha. 

KUIMARISHA OFISI YA ZANZIBAR ILI IWEZE KUSAIDIA JUHUDI ZA KUKUZA SEKTA YA BIASHARA VISIWANI
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia TanTrade iliendelea kuimarisha ofisi ya Zanzibar kwa kuweka vitendea kazi na mtumishi mmoja kwa lengo la kukuza uzalishaji na Biashara visiwani Zanzibar.

UTAFITI, MAFUNZO NA MAENDELEO YA TEKNOLOJIA

Kituo cha Zana za Kilimo na Ufundi Vijijini (CAMARTEC)

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza lengo la kuendeleza uboreshaji, uundaji na uanzishwaji wa uzalishaji kibiashara wa matrekta madogo aina ya CFT 221 na zana zake; kuendesha mafunzo kwa mafundi, waendesha matrekta na wasimamizi wao, Wizara kupitia CAMARTEC imekwishatengeneza matrekta 8 yaliyobuniwa ambayo yana matumizi mbalimbali (multipurpose). Kati ya matrekta hayo, matatu (3) yalitumika katika majaribio mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Pwani. Upungufu uliojitokeza kaika zoezi la majaribio ulifanyiwa marekebisho. Aidha, matrekta mengine 6 yapo katika hatua za matengenezo na yanatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Augosti 2012. Uzalishaji huo unatumia fedha za mkopo za utafiti chini ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia ambazo zitakiwezesha Kituo kutengeneza matrekta 14 na zana zake. Zana zitakazotengenezwa ni plau, jembe la matuta (ridger), harrow na vifungasho (attachments) kama vile pampu za maji, mashine za kupukuchua, kukoboa na kusagisha nafaka. Mkopo fedha za utafiti kutoka Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia wa Shilingi milion 225 wa riba nafuu ya asilimia 0.25 kwa mwezi na utalipwa kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Juni 2012. Matrekta yatakayotengenezwa kwa kutumia mkopo huo yatakapokamilika, itakifanya Kituo kuwa kimetengeneza jumla ya matrekta 20. Matrekta yanayoendelea kutengenezwa na Kituo (pre-commercial stage) yanauzwa moja kwa moja kwa watumiaji.
Mheshimiwa Spika, Ili kuendeleza uzalishaji wa trekta la CFT 221 na zana zake kibiashara, CAMARTEC itaanzisha kampuni ya ubia ya kutekeleza jukumu hilo. Mazungumzo kati ya CAMARTEC na NDC yanaendelea kwa nia ya NDC kuipatia kampuni hiyo eneo la kufanyia uzalishaji katika eneo la Kilimanjaro Machine Tools Co. Ltd (KMTC), Moshi. Vilevile, CAMARTEC wameongea na Benki ya Rasilimani Tanzania (TIB) kwa ajili ya kuipatia mkopo kampuni hiyo na TIB imeonesha utayari wa kutoa mkopo kwa kampuni hiyo itakapokuwa tayari. Takribani kiasi cha Shilingi billion tatu kinahitajika kwa ajili ya kuanzisha uzalishaji kibiashara.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza lengo la kuendeleza utafiti wa ufuaji umeme jadidifu kwa kutumia teknolojia ya biogesi, Wizara kupitia CAMARTEC imeendelea na majaribio ya kufua umeme kwa kutumia nishati ya biogesi ambapo jenereta kwa ajili hiyo zinatarajiwa kufungwa Chalinze, mkoani Pwani (kwa wakulima wa Msoga) na Wilaya ya Masasi (Gereza la Namajani). Mradi huo unatekelezwa kwa kushirikiana na asasi ya Rural Energy Agency (REA). Maeneo mengine yatakayohusishwa katika mradi huo wa ushirikiano na REA ni pamoja na Mbinga (Mlale JKT), Bukombe (Seminari ya Queen of Apostles) na Kasulu (Shule ya Sekondari St. Bakanja).
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012 Wizara kupitia CAMARTEC  iliunda na kutengeneza mashine za kusindika mazao ya kilimo kama vile za kukamua nyanya kupata mbegu ambapo mashine tano zimeuzwa kwa wakulima wa eneo la Tengeru Arusha. Aidha, imeboresha mashine ya kupukuchua mahindi inayoendeshwa kwa trekta dogo lililoundwa na CAMARTEC na kubainika kufanya kazi vyema. Mashine ya kupukuchulia mahindi iitwayo Vicon yenye uwezo wa kupukuchua gunia 200 kwa saa iko katika hatua za mwisho za kuikamilisha na kuizalisha kibiashara kwa kushirikiana na Shirika la Mzinga. Pia, Kituo cha CAMARTEC kimeunda na kutengeneza mashine mpya ya kukatia malisho ya wanyama, kama ng’ombe, inayoweza kuendeshwa kwa injini ya HP5. Aidha, Wizara kupitia CARMATEC imebuni na kutengeneza mashine za kuvunia mpunga inayoendeshwa na trekta dogo aina ya power-tiller. Lengo la ubunifu ni kuwapunguzia wakulima wadogo wadogo suluba ya kuvuna mpunga na kuongeza tija katika kilimo cha mpunga nchini. Utafiti wa mashine hii umekamilika na kituo kinaandaa taratibu za kumpata mbia wa kuzalisha kibiashara.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza lengo la kuendeleza uhawilishaji wa teknolojia mbalimbali zilizobuniwa na taasisi za utafiti, sambamba na kutoa huduma katika viatamizi vilivyopo kwenye taasisi za utafiti; Wizara kupitia CAMARTEC imeeneza zaidi ya majiko 335 bunifu ya mkaa ya kutumia kwenye kaya; mashine 5 za kukamua nyanya kupata mbegu, mabomba 700 ya kutolea gesi kwenye mitambo ya biogesi (dome pipes), mabomba 300 ya kuingiza gesi kwenye majiko ya biogesi (burner pipes) na majiko 61 ya kutumika kwenye taasisi (majiko 25 ya lita 200, majiko 16 ya lita 100, majiko 10 ya lita 50 na 10 ya lita 25). 

SHIRIKA LA UHANDISI NA USANIFU WA MITAMBO (TEMDO)
Mheshimiwa Spika,  Wizara kupitia Shirika la Uhandisi na Usanifu wa Mitambo (TEMDO) imeendelea na uhawilishaji wa teknolojia ya kiteketezi cha taka ngumu za hospitali (bio-medical solid waste incinerator) pamoja na teknolojia ya kutengeneza briketi za mabaki ya mimea kwa kushirikiana na Shirika la Mzinga. Viteketezi vimefungwa katika hospitali za Kibong’oto, Bagamoyo na Nzega. Kwasasa ufungaji wa kiteketezi unaendelea katika hospitali za Mount Meru. Uhawilishaji wa mashine za kutengeneza bidhaa za ngozi (mashine ya kukata mikanda, kuweka urembo na kukata pateni) umefanyika kupitia SIDO kwa ajili ya kuzitengeneza kibiashara. Vilevile, TEMDO imehawilisha teknolojia za kusindika matunda na asali kupitia Shirika la Kuendeleza Viwanda Vidogo (SIDO). Aidha, TEMDO iliendelea kuboresha mashine na vifaa vya kusindika mazao ya kilimo ikiwa ni pamoja na: mashine za kusindika maziwa (cheese press, cup seal, pasteuriser); kahawa (kumenya, kukaanga, kusaga); karanga (kukaanga, kumenya, kutoa siagi ya karanga); matunda na vifaa vya kusindika asali (centrifugal honey extractor, honey strainer, honey press). Baadhi ya teknolojia (mashine na vifaa) hizi zimehawilishwa kupitia Shirika la SIDO kwa lengo la kuzitengeneza na kuzisambaza kibiashara.
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia shirika hilo, katika kutekeleza lengo la kutoa mafunzo na kuhamasisha wajasiriamali kwa kutumia  viatamizi vya teknolojia mbalimbali, wajasiriamali 12 katika nyanja za usindikaji wa vyakula na utengenezaji wa briketi za mkaa waliendelea kupatiwa huduma kupitia Kiatamizi cha Teknolojia na Biashara na TEMDO. Vilevile, TEMDO imeendelea kubuni na kuendeleza teknolojia mpya zikiwemo mashine na vifaa kwa ajili ya machinjio ya kuku (slaughtering cones, hot water scalder, chicken plucker); uendelezaji wa teknolojia za kuongeza thamani ya bidhaa zitokanazo na mabaki ya mifugo.
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia TEMDO iliendelea kutoa huduma za kihandisi katika viwanda mbalimbali nchini hususan viwanda vya kusindika vinywaji (bia na mvinyo), kiwanda cha kutengeneza bidhaa za umeme na sukari. Mafunzo juu ya kutambua vihatarishi, ukadiriaji wa hatari, uchunguzi wa ajali na matukio hatarishi pamoja na kutunza na kuweka mfumo wa utawala wa mazingira kwa wajumbe wa Kamati za Usalama na Afya Sehemu ya Kazi yalifanyika kwa viwanda vya kutengeneza sukari TPC Ltd., Moshi na kiwanda cha kutengeneza mvinyo cha Banana Investment Arusha.

SHIRIKA LA UTAFITI NA MAENDELEO YA VIWANDA TANZANIA (TIRDO) 
Mheshimiwa Spika, Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda (TIRDO) likishirikiana na TEMDO na kampuni binafsi liko katika hatua za awali za kuhaulisha teknolojia ya kurejeleza plastiki. Moja ya juhudi hizo ni kugawana majukumu ya usanifu wa mitambo. Hii itafanya mitambo ya kurejeleza plastiki kuzalishwa hapa nchini na inategemewa kusambaza teknolojia hii sehemu nyingi na kupunguza kero za taka za plastiki nchini.
Mheshimiwa Spika, Shirika la TIRDO limeendeleza ujenzi wa majengo ya viatamizi vya TEHAMA na usindikaji wa mazao ya kilimo kwa ajili ya kuendeleza viwanda na wajasiriamali. Vilevile, TIRDO imetengeneza makaushio sita yanayotumia nishati ya jua na kuyasambaza kwenye vitongoji vitatu Wilayani Mkuranga. Wajasiriamali wapatao 116 walipata mafunzo ya jinsi ya kutumia makaushio hayo kukausha mboga na matunda ili zisiharibike na kuwawezesha kuuza katika masoko ya ndani. Shirika la TIRDO lilipata fedha za utafiti chini ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia za kuendeleza utafiti wa kaushio la jua. Aidha, Shirika linafanya majaribio ya kuboresha kaushio hilo kufikia viwango vya kanda ya Afrika. Lengo kuu la mradi huo ni kutengeneza kaushio linaloweza kutumiwa na wafanyabiashara hasa katika kukausha muhogo.
Mheshimiwa Spika, Shirika la TIRDO limeendelea kutoa huduma za upimaji wa uharibifu wa mazingira unaotokana na uzalishaji wa viwandani na kutoa ushauri wa utunzaji na uhifadhi wa mazingira katika uzalishaji wa viwandani kwenye sekta ndogo ya chuma, tumbaku, plastiki na ngozi katika mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Tanga na Iringa. Viwanda vilivyopata huduma hiyo, kwa sasa uchafuzi wa mazingira uko katika viwango vinavyokubalika kimataifa. Vilevile, Shirika la TIRDO linaendelea kuhakiki ubora wa vifaa vya kihandisi kama panton na matanki ya mafuta.  Katika, kutoa huduma hiyo vifaa vya kisasa kama X-ray machines, ultrasonic testing machines hutumika. Vilevile, wataalamu wamepata mafunzo ya utaalam huo huko Afrika Kusini.
Mheshimiwa Spika, Shirika la TIRDO kwa kushirikiana na Benki ya Rasilimali (TIB), pia limeweza kufanya ukaguzi wa kitaalamu (technical assessment) katika viwanda vitano (5) vya kusindika mazao ya kahawa, maziwa, matunda, nyama na maji vilivyopo Rombo, Bukoba, Sumbawanga, Arusha na Dar es Salaam ili kutoa ripoti ya kitaalamu itakayowezesha viwanda hivyo kupata mkopo toka Benki hiyo. TIRDO pia limetumiwa na NDC kuwa mshauri mwelekezi katika kufanya upembuzi yakinifu na kutathmini mitambo iliyopo katika kiwanda cha Kilimanjaro Machine Tools Company Ltd (KMTC) na kisha kutoa ushauri juu ya hatua zinazoweza kuchukuliwa ili kufufua uzalishaji katika kiwanda hicho.
Mheshimiwa Spika, Shirika la TIRDO limetengeneza mashine zinazotumika kusindika vyakula na matunda (Hammer mill, Juice extractor), mashine ambazo zimetumia malighafi zisizo na madhara kwa walaji na zinazokubalika kimataifa kama vile chuma cha pua (stainless steel) au manganese steel. Bei za mashine hizo ni mara mbili hadi nne za mashine zinazotumika sasa lakini hudumu zaidi ya miaka nane na kukidhi viwango vya Kimataifa, ukilinganisha na mashine za kawaida huchakaa ndani ya mwaka mmoja na kuzalisha bidhaa duni.
Mheshimiwa Spika, katika kuendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia ya kisasa ili viwanda vya ngozi nchini vipunguze uharibifu wa mazingira, Wizara kupitia Shirika la TIRDO, linatekeleza mradi wa kurejeleza taka za ngozi viwandani na kuzalisha bidhaa kama Leather board katika juhudi za kuimarisha sekta ya ngozi.  Kwa kuanzia, mradi utaangalia takwimu za uchafuzi wa mazingira unaotokana na viwanda vya ngozi katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Arusha, Kilimanjaro na Mwanza.  Aidha, TIRDO iko katika hatua ya kununua vifaa vya maabara baada ya kupata fedha za utafiti.
Mheshimiwa Spika, katika kukamilisha mchakato wa kuhakiki na kuboresha maabara ya mazingira na ya vifaa vya kihandisi ili iweze kufikia viwango vya kimataifa na kuweza kutoa huduma bora kwa wazalishaji viwandani, Shirika la TIRDO limeendelea na shughuli zitakazoiwezesha maabara ya mazingira kupata uhakiki ikiwa ni pamoja na kujenga uwezo wa maabara kwa kuagiza vifaa vifuatavyo, dragger pump with its detectors testing tubes, Multi probe system and Dust sample. Vilevile, shirika limewapeleka mafunzoni watafiti wawili wa ndani wa maabara ya mazingira kwenye mafunzo ya Method Validation and Measurement of Uncertainty kutoka kwa mtaalamu aliyetoka Afrika ya Kusini. Mafunzo hayo yaliandaliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).  Vilevile, maabara imeweza kujiandikisha katika mfumo wa kuhakiki matokeo ya upimaji kwa ustadi (Proficiency Testing) wa hewa ili kuweza kutoa matokeo yenye uhakika zaidi yanayozingatia kiwango cha kimataifa cha ISO/IEC 17025. Maabara nyingine ziko katika hatua mbalimbali za uhakiki na kwa sasa taasisi kupitia Wizara inatafuta fedha za kuendeleza uhakiki huo. Shirika linategemea baada ya kuhakiki maabara zake litapata wateja zaidi na matokeo ya majaribio hayo kukubalika ulimwenguni kote.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa mazao ya kilimo yanaingia katika masoko ya kimataifa, TIRDO imekuwa inatekeleza mfumo wa ufuatiliaji wa mazao (traceability).  Mfumo huu ulifanyika kwa mazao ya chai, kahawa, korosho na samaki wa maji baridi kwa ufuatiliaji wa kujaza taarifa kwenye karatasi (paper based tracebility system) katika viwanda vya usindikaji wa mazao hayo. Majaribio (Mock recall) yalionesha mafanikio kwa kiwango kikubwa kwani kumbukumbuku zote ziliweza kupatikana na kuhifadhiwa kwa uhakika. Hata hivyo, tatizo la upatikanaji wa fedha lilifanya mfumo huu wa ufuatiliaji kushindwa kuwekwa kwenye mfumo wa kikompyuta (computerised traceability system) ili kuboresha zaidi mfumo huo.
Mheshimiwa Spika, katika kutoa huduma viwandani zinazolenga matumizi ya teknohama, Shirika la TIRDO limeendelea na utekelezaji wa Mradi wa Kusaidia Wajasiriamali Wasindikaji (Agro-processors) katika kupata masoko ya bidhaa zao zinazotokana na usindikaji wa mazao ya kilimo. Shirika pia limeendelea kutoa ushauri wa kiufundi kwa wajasiriamali na wadau wengine kuhusu manufaa ya matumizi ya mifumo ya utambuzi wa bidhaa kwa kutumia nembo za mistari. Kutokana na juhudi hizo, makampuni 151 yamesajiliwa katika matumizi ya nembo za mistari na bidhaa 3,000 zimepata nembo za mstari. Aidha, Shirika limeweza kuunda tovuti 77 za wajasiriamali katika mikoa ya Pwani, Tanga, Dar es Salaam, Mtwara na Lindi na kutoa mafunzo juu ya matumizi ya tovuti hizo kwa lengo la kujitangaza. Jitihada hizo zimewezesha jumla ya wajasiriamali 14 kupata nembo za ubora za TBS, TFDA na nembo za mistari. 

CHUO CHA ELIMU YA BIASHARA (CBE)
Mheshimiwa Spika, katika kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wajasiriamali wadogo ili kuwasaidia kufanya biashara zao kisasa zaidi, Chuo cha Elimu ya Biashara, kimeendesha kozi tatu za muda mfupi kwa jumla ya wajasiriamali 163. Mafunzo hayo yalikuwa katika maeneo yafuatayo: Namna ya kubuni na kusimamia miradi, Usimamizi wa fedha na rasilimali nyingine kama watu (HRM), Njia bora za utunzaji wa kumbukumbu za biashara na mbinu za kuimarisha ubora wa bidhaa na huduma zitolewazo na wafanyabiashara wadogo.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza lengo la kuandaa mitaala ya kozi ya ujasiriamali katika ngazi ya Astashahada, Stashahada na Shahada, Chuo kimeanza kutekeleza mpango wa kuandaa mafunzo ya ujasiriamali kupitia mradi wa ‘Netherlands Initiatives for Capacity Building of Higher Education’. Katika mradi huo Chuo kitaandaa mitaala ya ujasiriamali katika ngazi za astashahada, stashahada na shahada. Mitaala hiyo itapitiwa na kupata kibali kutoka kwa Baraza la Ithibati (NACTE) kabla ya utekelezaji. Mradi huo kwa sasa uko katika hatua zake za awali (Inception Stage). Chuo kimefanikiwa kwa kiwango kikubwa kubadilisha matumizi ya eneo la Nzuguni kutoka kuwa bustani ya wanyama (Capital Zoo) kwa mujibu wa taratibu na kuwa eneo la Ujenzi wa taasisi ya Elimu. Chuo kimeweza pia kufuatilia na kufanikiwa kupata hati miliki ya eneo la Nzuguni.  Kwa upande wa eneo la Kiseke Mwanza, Chuo kimefanikiwa kulipia gharama za fidia zilizokuwa zikidaiwa. Kati ya Shilingi milioni 243 zilizokuwa zikihitajika, Chuo tayari kimelipa Shilingi milioni 203, kati ya hizo Shilingi milioni 103 zikiwa zimelipwa katika kipindi cha mwaka 2011/2012.
UDHIBITI WA USHINDANI, UBORA WA BIDHAA NA HUDUMA
SHIRIKA LA VIWANGO TANZANIA
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) imeendelea na juhudi za kuziwezesha maabara zake kufikia viwango vya upimaji vya kimataifa (Laboratory Accreditation). Lengo ni kuziwezesha maabara hizo kupima sampuli na kutoa taarifa za upimaji (Test reports) zinazotambuliwa duniani kote. Maabara hizo ni za Uhandisi Umeme, Uhandisi Mitambo na Uhandisi Ujenzi ambazo miongozo yao ya ubora imekamilishwa kulingana na kiwango cha kimataifa ISO 17025. Hatua inayofuata ni kufanyiwa tathmini na Shirika la SANAS la Afrika ya Kusini ili kuthibitishwa umahiri wa upimaji katika nyanja za nyaya za umeme, nondo na saruji. 
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS), imekamilisha utaratibu wa upimaji wa ubora wa bidhaa kabla ya kusafirishwa kuja Tanzania (Pre-shipment Verification of Conformity to Standards - PVoC). Utekelezaji ulianza rasmi tarehe 01 Februari, 2012 na makampuni matatu (3) yamepatikana kwa njia ya ushindani wa Kimataifa. Makampuni yaliyofanikiwa kupata zabuni ya kufanya kazi hiyo ni M/S Intertek International Ltd ya Uingereza; M/S Bureau Veritas Inspection, Valuation and Control (BIVAC) ya Ufaransa; na M/S SGS Societe Generale De Surveillance S.A. ya Uswisi. Baada ya utaratibu huo kuanza, bidhaa zenye ubora hafifu ikiwa ni pamoja na zile za bandia zimeanza kupungua katika soko la Tanzania. 
Mheshimiwa Spika, katika kuongeza ufanisi na kuimarisha ukaguzi wa ubora wa bidhaa yakiwemo magari yaliyotumika, Wizara imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha uongozi wa shirika, kuyafungia makampuni ya ukaguzi ya WTM Utility Services ya Uingereza, na Jaffar Mohamed Garage ya Dubai, ambayo yamekuwa yakikiuka taratibu za ukaguzi wa magari kwa kutokuwa na vifaa na utaalam unaohitajika na kuchelewesha malipo ya ukaguzi. Shirika pia limeendelea kuimarisha utaratibu wa kukusanya mapato yatokanayo na shughuli za ukaguzi wa ubora toka kwa mawakala kwa kuzishirikisha Idara za Uthibiti Ubora, Huduma za Shirika na Kitengo cha Fedha (Uhasibu) na kufanya kazi kwa karibu na Mamlaka ya Mapato nchini, Tume ya Ushindani, Jeshi la Polisi na Mamlaka za Miji na Majiji husika. Kwa upande wa ukaguzi wa bidhaa kupitia PVoC, mapendekezo ya wadau yatawezesha pia kuangalia uwezekano wa kutenganisha bidhaa zinazohitaji kukaguliwa ndani na nje ya nchi kwa kuzingatia makundi tofauti ya wafanyabiashara wa Tanzania (wakubwa, wa kati na wadogo) bila kuathiri ubora wa bidhaa zinazoingizwa nchini. 
Mheshimiwa Spika, kutokana na ushauri uliotolewa na Kamati za bunge, Wizara imeunda Kikosi Kazi kinachowajumuisha wajumbe kutoka Taasisi za Umma na Sekta Binafsi ili kuishauri Serikali kuhusu utaratibu mzuri zaidi wa kukagua bidhaa nje ya nchi ikiwa ni pamoja na magari. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba nimepokea taarifa ya Kikosi Kazi tarehe 20 Julai 2012. Taarifa hiyo ina mapendekezo kwa ajili ya kuishauri Serikali kuhusu utaratibu zaidi wa kukagua bidhaa nje ya nchi ikiwa ni pamoja na magari. Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kuwa, Wizara itayafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na Kikosi Kazi. Baadhi ya mapendekezo ya Kikosi Kazi ni pamoja na: Kuishauri Serikali kutangaza upya mchakato wa kuwapata mawakala wa ukaguzi wa magari nje ya nchi kwa kufuata Sheria ya Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2004; Kupata maoni ya wadau kuhusiana na mahitaji ya maboresho ya Sheria ya Viwango ya mwaka 2009 ili kuangalia uwezekano wa ukaguzi wa magari kufanyika ndani au nje ya nchi au yote kwa pamoja. Tayari baadhi ya Taasisi za Serikali zikiwemo Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na VETA zimeonesha nia ya kufanya ukaguzi wa magari ndani ya nchi; na kuangalia upya muundo wa TBS hususan Idara ya Ubora na Udhibiti na vilevile, kuwa na ratiba ya mzunguko kwa watendaji baada ya muda maalum.
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) hadi kufikia mwezi Machi, 2012 imetoa jumla ya leseni 90 za ubora wa bidhaa mbalimbali kwa wazalishaji wa hapa nchini ambao walitimiza masharti ya ubora wa bidhaa zikiwemo zile zinazogusa afya na usalama wa walaji, mazingira na uchumi wa Taifa.  Idadi hii ni sawa na asilimia 75 ya lengo zima la kutoa leseni 120 kwa mwaka 2011/2012. Leseni za ubora zitawezesha bidhaa husika kushindana kikamilifu katika masoko ya ndani na nje ya nchi. 
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Shirika la Viwango Tanzania iliendelea na utoaji wa mafunzo ya ufungashaji bora kwa wajasiriamali wadogo na kati (SMEs) wapatao 248 hadi kufikia mwezi Machi 2012 katika mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya. Mafunzo hayo hutolewa kuwasaidia wajasirimali wadogo ili waweze kupata nembo ya ubora ya TBS kwa lengo la kuongeza uwezo wa kushindana katika soko. Aidha, Wizara inaendelea na juhudi za kutafuta fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kupimia vifungashio mbali mbali. Vilevile, katika kudhibiti bidhaa duni kutoka nje ya nchi, hadi kufikia mwezi Machi 2012 Shirika la Viwango lilitoa vyeti vya ubora wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje vipatavyo 1,945 sawa na asilimia 69.5 ya lengo la vyeti 2,800 kwa mwaka 2011/2012. 
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Shirika la Viwango Tanzania iliendelea na upimaji wa sampuli za bidhaa kutoka viwanda mbalimbali nchini na nchi za nje vikiwemo vya wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs). Hadi kufikia mwezi Machi, 2012 lilikuwa limepima jumla ya sampuli 6,019 katika maabara mbalimbali za Shirika, idadi hii ni sawa na aslimia 65 ya lengo la mwaka la kupima sampuli 9,300.

 BARAZA LA USHINDANI (FAIR COMPETITION TRIBUNAL – FCT)
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Baraza la Ushindani katika mwaka 2011/2012 ilikuwa na kesi kumi na tatu zilizokuwa zinaendelea kusikilizwa ambazo zilisajiliwa mwaka 2010/2011. Aidha, Baraza lilisajili kesi mpya kumi na hivyo kufanya idadi ya kesi za kusikilizwa katika kipindi cha 2011/2012 kuwa ishirini na tatu Hadi kufikia mwezi Aprili 2012 kesi tisa zilikuwa zimesikilizwa na kutolewa maamuzi na kumi na nne zilikuwa katika hatua mbalimbali za mchakato wa usikilizwaji. Lengo la Baraza ni kesi kusikilizwa na kutolewa maamuzi katika miezi isiyozidi sita tangu tarehe ya kusajiliwa.
Mheshimiwa Spika, katika kujenga uwezo zaidi wa Baraza katika kushughulikia kesi hizo, Baraza limeweza kutekeleza malengo yake ya kujenga uwezo zaidi wa Baraza katika kushughulikia kesi kwa kupata mafunzo mbalimbali. Katika kutoa elimu kwa umma juu ya kazi za Baraza katika Uchumi; Baraza limeweza kuendelea  kutoa elimu kwa umma kupitia warsha, semina na vyombo vya habari juu ya kazi zake ili kujenga uelewa na ufahamu wa wadau. Katika mwaka 2012/2013, Tume itaendelea kutoa elimu kwa wadau kikanda. Wizara kupitia Baraza la Ushindani iliweza kuchambua Sheria ya Ushindani ya mwaka 2003 na kubainisha upungufu unaosababisha Baraza lisifanye kazi kwa ufanisi uliokusudiwa. Aidha, Baraza limefanikiwa kutoa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria hiyo ambayo yamewasilishwa Serikalini pamoja na mapendekezo yaliyopendekezwa na Tume ya Ushindani ili yaweze kufikishwa Bungeni. 
WAKALA WA VIPIMO
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Wizara kupitia Wakala wa Vipimo (WMA) iliendelea na majukumu ya kukagua, kuhakiki na kusimamia usahihi wa Vipimo vinavyotumika katika biashara ili kumlinda mlaji. Jumla ya vipimo 545,506 vinavyotumika katika biashara vilikaguliwa na wafanyabiashara 5,503 walipatikana na makosa ya kukiuka Sheria ya Vipimo. Katika kuhakiki vipimo vya mita za umeme, mita za maji na mitungi ya gesi ya kupikia, Wakala imekamilisha taratibu za ununuzi wa vifaa vya kukagua mita za maji. Aidha, Kitengo cha Wakala wa Vipimo bandarini kimeanza ufuatiliaji wa mfumo wa upimaji, ujazaji na ufungashaji kwenye mitungi ya Gesi inayotoka nje na Gesi Asilia inayozalishwa hapa nchini. Lengo ni kuhakiki usahihi wa vipimo vinavyotumika katika uuzaji wa Gesi bila kumpunja mtumiaji.
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha huduma za Kitengo cha Vipimo Bandarini, Wakala wa Vipimo imewezesha watumishi saba kupata mafunzo ya usimamizi wa biashara ya mafuta na vipimo nchini Marekani. Aidha, vitendea kazi  kama standard densitometer, kipimajoto kwenye matenki ya mafuta melini na offshore vimenunuliwa. Katika kutimiza lengo la kuendelea kukagua usahihi wa bidhaa zilizofungashwa (quantities in pre-packed goods) zinazozalishwa na viwanda vya hapa nchini na pia kutoka nje ya nchi, kitengo cha ukaguzi bandarini kwa bidhaa zilizofungashwa (pre-packed goods) kimeanzishwa na maandalizi ya hatua za utekelezaji wa majukumu yake unaendelea.
Mheshimiwa Spika, Wakala wa Vipimo imekamilisha ununuzi wa kiwanja eneo la misugusugu, Pwani. Kiwanja hiki kitatumika kwa ujenzi wa kituo cha kisasa cha kupimia ujazo wa matenki (Calibration Bay) ya malori ya kusafirisha mafuta ya nishati hapa nchini na nchi jirani. Hati ya kiwanja hicho imekabidhiwa kwa Wakala na kazi ya ujenzi wa uzio imekamilika. Aidha, Wakala wa Vipimo inaendelea kuimarisha ofisi zake mikoani kwa kuanza kununua viwanja (plots) kumi na tano ili hatimaye yajengwe majengo kwa ajili ya ofisi zake mikoani. Hatua hiyo itaiwezesha Wakala kuwa na ofisi zinazokidhi mahitaji ya kitaalamu na pia kupunguza gharama za pango kwani ofisi nyingi za Wakala hivi sasa zipo katika majengo ya kupanga. 
Mheshimiwa Spika, Wizara imeandaa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Vipimo CAP 240 RE 2002 yanayolenga kupanua wigo wa matumizi ya vipimo rasmi kutoka sekta ya biashara na kuhusisha pia sekta za afya na mazingira. Aidha, marekebisho yanazingatia maridhiano yaliyofikiwa na nchi kikanda na kimataifa kuhusu masuala ya vipimo.
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Wakala wa Vipimo inaendelea na kuelimisha umma juu ya masuala ya vipimo sahihi kupitia televisheni, redio, magazeti, vipeperushi, kalenda pamoja na kushiriki maonesho mbalimbali hapa nchini. Jumla ya vipindi 20 vya televisheni viliandaliwa na kurushwa hewani. Aidha, jumla ya vipindi 10 vya redio, taarifa 37 za magazeti ziliandaliwa. Vile vile, Wakala ilishiriki jumla ya maonesho 5 ya Kitaifa ambayo ni; Sabasaba, Nanenane, SIDO na Maonesho ya Mwanamke Mjasiriamali – Month of Women Enterpreneurs (MOWE). 
Mheshimiwa Spika, kuhusu matumizi ya mizani ya rula (steel yard) katika ununuzi wa zao la pamba, Wizara yangu kama nilivyoahidi katika Kikao cha Bunge la Bajeti la mwaka 2011/12, ilikamilisha taratibu za kisheria za kuondoa matumizi ya mizani ya rula  na kutangazwa kupitia GN No. 47 ya mwaka 2012. Hata hivyo, hadi kufikia mwezi Juni 2012, ni kiasi cha mizani 2,460 tu ambazo zilikuwa zimeingizwa nchini ikilinganishwa na mahitaji ya mizani zaidi 9,000.  Kutokana na kutokamilika kwa ununuzi wa mizani za digitali ambazo ndizo zilizopendekezwa na wadau, Serikali baada ya majadiliano na wadau wa zao kupitia vyama vyao vya Tanzania Cotton Association (TCA) na Tanzania Cotton Growers Association (TACOGA) imeruhusu matumizi ya mizani za rula sanjari na mizani za digitali kwa msimu huu ili kutoathiri ununuzi wa pamba ambao umeanza tarehe 2 Julai 2012. Chama cha Wakulima wa pamba (Tanzania Cotton Growers Association) kwa kushirikiana na Chama cha Wanunuzi  wa Zao la Pamba (Tanzania Cotton Association) wameandaa mpango wa kuondoa matumizi ya mizani ya rula hatua kwa hatua kadiri upatikanaji wa mizani za digitali utakavyokuwa unapatikana. Wizara kupitia Wakala wa Vipimo imekamilisha uhakiki wa mizani hizo za aina mbili. Aidha, Wizara kupitia Wakala wa Vipimo, inaendelea kuelimisha umma juu ya masuala ya vipimo kupitia televisheni, redio, magazeti, vipeperushi, kalenda pamoja na kushiriki maonesho mbalimbali hapa nchini. 
WAKALA WA USAJILI WA BIASHARA NA LESENI (BRELA)
Mheshimiwa Spika, BRELA imekamilisha kazi ya kuingiza taarifa zake zote za Makampuni na Majina ya Biashara yaliyosajiliwa katika mfumo wa kielektroniki na wanaendelea kuunganisha mfumo huo na Mfumo wa Usajili (Registry Management System-RIMS). Mifumo hiyo imeanza kutumika kusajili makampuni (siku tatu) na majina ya biashara kwa muda mfupi zaidi siku moja iwapo nyaraka zote muhimu zimekamilika. Aidha, utaratibu huo umerahisisha ulipaji kwa kutumia mabenki kupokea ada mbalimbali. Vilevile, BRELA na TRA inakamilisha utaratibu wa kutoa Hati ya Kumtambulisha Mlipa Kodi (TIN) mara tu anaposajili kampuni au jina la biashara. Hatua hiyo inatarajia kuwaondolea adha wateja wa BRELA na TRA ya kulazimika kwenda TRA, baada ya kusajili Makampuni au Majina ya biashara zao.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua upungufu ya uwezo wa matumizi ya mitandao kwa watanzania wengi hasa wanaojihusisha na biashara ndogo ndogo mijini na hasa vijijini  kutokana na changamoto mbali mbali, BRELA imekubaliana na Chama cha Wafanya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), kusaidiana na wadau wengine wakiwemo, Mawakili, Wahasibu binafsi ambao hutoa huduma ya matumizi ya mtandao huko huko wilayani ambako hadi sasa TCCIA ina mtandao katika wilaya tisini na tano. Aidha, BRELA ikishirikiana na TCCIA imetoa mafunzo ya kutoa huduma hiyo kwa wadau tajwa. Ushirikiano huo utapunguza gharama za kufanya biashara  na kupanua wigo na wateja.
Mheshimiwa Spika, BRELA imeendelea kusajili Majina ya Biashara papo kwa papo katika maonyesho mbali mbali yanayofanyika kitaifa. Hadi sasa majina ya biashara 1,408 yamesajiliwa kwa njia hiyo ambayo imeonekana kuwa na manufaa sana kwa wajasiriamali wadogo wadogo waliotapakaa nchi nzima na kuwaondolea gharama isiyo ya lazima. 
Mheshimiwa Spika, katika eneo la Miliki Ubunifu BRELA kwa kushirikiana na Miliki la Dunia (WIPO) inaendelea na mpango wake wa kuhifadhi takwimu kutoka kwenye majalada na kuziweka katika mfumo wa kielektroniki (Automated Intellectual Property System (IPAS). Mfumo huo unakusudia utahusisha pia suala la utoaji wa Hataza, hatua ambayo ipo katika ngazi za mwisho. Aidha, BRELA imeendelea kutoa elimu juu ya umuhimu wa wazalishaji bidhaa na watoaji huduma kutumia Alama za Biashara katika bidhaa wanazotengeneza na za Huduma wanazozitoa, ili kuzitofautisha bidhaa zao na au huduma zao na bidhaa na au huduma zinazofanana za washindani wengine. Njia hiyo imekwishaonesha mafanikio ya kuongezeka kwa thamani ya bidhaa na huduma za wafanyabiashara wanazingatia kwa usahihi wa utaratibu huo.
Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kupitia BRELA, imefanya mapitio ya Sheria za Makampuni ya mwaka 2002, Majina ya Biashara sura 213 ambayo ilijumuishwa katika mswada wa kurekebisha sheria mbali mbali za biashara uliopitishwa na Bunge hili katika kikao chake cha mwezi April 2012. Marekebisho hayo ni pamoja na kuwezesha mtu mmoja kumiliki hisa zote kwenye kampuni (Single Shareholder)na pia itaruhusu matumizi ya mwongozo wa kurahisisha maandalizi ya nyaraka za usajili wa kampuni na fomu inayopatikana katika mtandao. Marekebisho hayo yanaruhusu matumizi ya fomu kwa lugha ya Kiswahili, kupanua wigo wa mawasiliano na wateja kwa kuongeza mawasiliano kwa njia ya nukushi, mtandao wa kompyuta na simu za viganjani. 
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Leseni za Viwanda sura 46 inafanyiwa mapitio ili kuangalia kama inakidhi matakwa ya sasa ya Uwekezaji. Lengo la sheria hiyo ni pamoja na kuratibu uanzishwaji wa viwanda na kukusanya takwimu zinazohusiana na viwanda. Hamasa zinaendelea ikiwa ni pamoja na ukaguzi elekezi usiolenga udhibiti tu. Nia ni kuhamasisha wazalishaji kwa hiari yao waone umuhimu wa kupata leseni za viwanda na kuvisajili kwani kwa kufanya hivyo, wamiliki wa viwanda hivyo huweza kupata punguzo la ushuru wakati wa kuingiza nyenzo na zana za kuzalishia ikiwa ni pamoja na mali ghafi za uzalishaji zinazotoka nje. Aidha, imebainika kuwa utaratibu wa awali haukuwa na mvuto mkubwa hasa kwa wajasiriamali wadogo kutokana na ada kubwa ya kupata huduma hiyo. 
Mheshimiwa Spika, BRELA imefanikiwa kupata kiwanja eneo la Ada Estate katika Manispaa ya Kinondoni – Dar es Salaam ambako inatarajia kujenga ofisi zake na taratibu za kuanza ujenzi zinaendelea. Jitihada za Kazi ya usanifu wa majengo umekwishafanyika na tathmini na mapendekezo yamewasilishwa kwenye Bodi ya Zabuni. Pia, kutokana na utendaji mahiri, BRELA, ilitunukiwa tuzo ya “International Arch of Europe Quality Award 2012, Gold Category  na Business Initiative Directions B.I.D katika Mkutano wa 38 uliofanyika Frankfurt, Ujerumani, mwezi Aprili, 2012.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza huduma za usajili na utoaji wa leseni za viwanda, Wakala imesajili makampuni 7,058 ikiwa ni ongezeko la Makampuni 1,780 ukilinganisha na makampuni 5,278 yaliyosajiliwa 2009/10, Majina ya Biashara 14,866 yalisajiliwa mwaka 2010/11 yakilinganishwa na Majina ya Biashara 11,127 yaliyosajili mwaka 2009/2010 ikiwa ni ongezeko la asilimia 34. Kwa upande wa alama za biashara na huduma maombi yaliongezeka kutoka 1,259 kwa mwaka 2009/2010 hadi 2,502 kwa mwaka 2010/2011 hili ni ongezeko la asilimia 99. Hali kadhalika, kwa upande wa leseni za Viwanda, BRELA ilitoa leseni 105 kwa mwaka 2010/2011 ukilinganishwa na leseni 99 zilizotolewa kwa mwaka 2009/2010.

TUME YA USHINDANI (FAIR COMPETITION COMMISSION – FCC)
Mheshimiwa Spika, katika kufanikisha lengo ililojiwekea la kutangaza shughuli za Tume kwa umma ili kuongeza utekelezaji wa sheria (compliance), Wizara kupitia Tume ya Ushindani, imefanya semina katika mikoa mitano kwa lengo la kuelemisha umma juu ya kazi na majukumu yake kama yalivyoanishwa katika Sheria ya Ushindani No. 8 ya 2003 katika Mikoa ya Mara, Mwanza, Dodoma, Morogoro na Singida. Tume inatarajia pia kuandaa semina katika mikoa ya Mbeya na Iringa kufuatana na uwezo wa kifedha. Kutokana na semina hizo, Tume imeweka kwa wadau wa masuala ya ushindani na kujua changamoto za ushindani na pia wafanyabiashara kupata hamasa ili kuchangamkia fursa zinazoletwa na ushindani na imeweza kuibua masuala yanayofifisha ushindani, kwa mfano katika semina ziliyofanyika Tume iliweza kuibua masuala ya ushindani kwa sekta mbali mbali, na muungano wa makampuni ambayo hayakutoa taarifa na masuala mengine ambayo Tume inaendelea kuyachambua.
Mheshimiwa Spika, ili kumuelimisha na kumlinda mlaji, Wizara kupitia FCC imetoa elimu kwa mlaji kwa kushiriki katika maonesho ya SabaSaba na NaneNane. Pia, Wizara kupitia Tume imetoa elimu kwa mlaji na wafanyabiashara kupitia  mpango wa  semina kwa wafanyabiashara wakubwa,  wa kati na wadogo  unaoendeshwa  na Mamlaka ya  Mapato Tanzania (TRA) katika Manispaa za Ilala Karikoo tarehe 19 Aprili, 2012, Segerea tarehe 25 Aprili, 2012; na Temeke Kigamboni tarehe 15 Machi, 2012. Lengo la mafunzo hayo ni kuwa na waelimishaji ambao sambamba na majukumu yao ya kila siku watakuwa tayari kusambaza elimu ya mlaji katika maeneo mbali mbali nchini. Pia, Tume imefanya tathmini ya mafunzo yaliyotolewa awali kwa waelimishaji wa masuala ya kumlinda mlaji katika mikoa ya Dodoma na Mtwara. Lengo la tathmini hiyo ni kupima mafanikio na changamoto katika utoaji wa elimu ya mlaji katika maeneo yao. Mapendekezo ya waelimishaji hao yatasaidia katika kubuni mikakati itakayoboresha utoaji wa elimu kwa mlaji katika maeneo mbali mbali nchini. Vilevile, Wizara kupitia Tume imeweza kufanya mchakato wa Tenda ya kutafuta Mshauri Mwelekezi katika masuala ya matangazo ya biashara katika Radio na Televisheni, tenda hiyo imetangazwa na kufunguliwa.  Tenda inasubiri kibali cha Tenda Bodi ya Tume kumthibitisha mzabuni aliyeshinda. Lengo la utafiti huu ni kufahamu jinsi gani matangazo ya biashara yanaweza kuchochea (kwa njia ya upotoshaji) utashi wa mlaji juu ya ununuzi wa bidhaa na huduma pia kufahamu ukubwa wa tatizo hili katika jamii.
Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza lengo la kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari kama radio, luninga na magazeti kuhusiana na bidhaa bandia na madhara yake kwa binadamu na mali zake, Wizara kupitia Tume ya Ushindani, imerusha hewani matangazo madogo yapatayo 32 kati ya mwezi wa saba 2011 na mwezi wa tatu 2012. Aidha, Tume ilishiriki katika maonesho ya wiki ya utumishi wa Umma Dar es salaam. Maonesho ya 35 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam, Julai 2011, maonesho ya Wakulima (NaneNane) na maonesho ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru, Desemba 2011. Katika maonesho hayo, Tume ilitoa mafunzo kwa vitendo kuhusu namna ya kutambua bidhaa bandia. Vile vile, Tume imefanya semina kwa wadau mbali mbali katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Mara, Mwanza, Dodoma na Morogoro kati ya Julai na Desemba 2011. Wadau zaidi ya 600 walifikiwa katika mikoa hiyo kutoka katika jumuiya za wafanyabiashara (TCCIA, CTI na wafanya biashara mmoja mmoja), Wazalishaji viwandani, Wanasheria, Maafisa biashara, Maofisa wa mamlaka ya Mapato (TRA), Polisi na Watumishi wa Manispaa.
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Tume, pia inashiriki katika shughuli na mikutano inayoratibiwa na Jukwaa la Mlaji Tanzania (Tanzania Consumer Forum) ambayo inaandaa Jarida la Sauti ya Mtumiaji na Sera ya Utetezi wa Mlaji Tanzania. Vile vile, Wizara kupitia Tume imeshiriki katika mikutano ya kimataifa kwa njia ya simu (Monthly Teleconferencing) kujadili masuala mbali mbali ya utetezi wa mlaji; maandalizi na maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mlaji  “World Consumer Rights Day” inayoadhimishwa tarehe 15 Machi kila mwaka ambayo mwaka huu 2012 yalifanyika Jijini Mwanza, hivyo kwa mara ya kwanza, yamefanyika nje ya Dar es Salaam.  Maadhimisho hayo yalijumuisha shughuli mbali mbali zilizolenga kutoa elimu kwa mlaji hususan  mkutano na vyombo vya habari (Press Conference), vipindi na mijadala katika Radio mbali mbali ambazo ni “Radio Free Africa”,” Kiss Live. Kongamano na Wanafunzi wa Vyuo vya Biashara (CBE) na St. Augustine, shule za sekondari na maonesho ya siku nne katika viwanja vya  Makongoro-jijini Mwanza.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2011/2012, Wizara kupitia Tume imefanya kazi ya Mapitio ya Mikataba baina ya Mlaji na Muuzaji (review of standard form contracts). Rasimu ya Kanuni za “Standard Form Contract” imeandaliwa. Aidha, Tume imeweza kuandaa kanuni za kumlinda mlaji Tanzania (consumer protection regulations). Zabuni ya kutafuta Mshauri Mwelekezi (Consultant) imetangazwa ambapo jumla ya maombi manne yamewasilishwa na kuchambuliwa. Kutokana na elimu iliyotolewa katika semina mbalimbali, Wizara kupitia Tume imepokea jumla ya malalamiko 30 kutoka kwa walaji kuhusu bidhaa na huduma mbali mbali ambazo hazijakidhi matarajio au matumizi yaliyokusudiwa (unmerchatable goods and services). Tume hutoa ushauri wa kisheria ikiwa ni sehemu ya elimu kuhusu Sheria ya Ushindani hususan vifungu vinavyomlinda mlaji, kwa pande zote mbili (muuzaji na mlaji) za mgogoro  na kufanya pande zote mbili kuweza kuafikiana kumaliza mgogoro kwa njia ya amani. Endapo suluhu haijafikiwa, upande usioridhika huwa na haki ya kisheria kufungua kesi ya madai mahakamani.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, bidhaa zilizolalamikiwa kwa kiwango kikubwa ni bidhaa za elektroniki na vifaa vya umeme, simu za viganjani, komputa (Laptops), luninga, feni, betri za magari na za simu na jenereta. Katika malalamiko yote 30 malalamiko 14 yalitatuliwa kwa makubaliano kati ya mlalamikaji na mlalamikiwa (mlaji na muuzaji) chini ya usimamizi wa Kitengo cha Kumlinda Mlaji, malalamiko yapatayo 12 ya walalamikaji hawakuleta vielelezo na malalamiko yapatayo manne yanaendelea kufuatiliwa.
Mheshimiwa Spika, ili kupambana na kudhibiti makampuni yanayokula njama kwa pamoja kupanga bei, na kwa kudhibiti kiasi cha bidhaa inayopelekwa kwenye soko (output restrictions between competitors), Wizara kupitia Tume ya Ushindani inashughulikia lalamiko moja linalohusu kampuni za mafuta kuthibiti bidhaa za mafuta kuingia sokoni na kusababisha uhaba. Lalamiko hili ambalo lilifikishwa mbele ya Tume liko katika hatua za mwisho za uchunguzi.
Mheshimiwa Spika, ili kufanikisha lengo la kufanya uchunguzi wa masoko na kusikiliza kesi za ushindani, katika mwaka 2011/2012, Tume ya Ushindani imefanya uchunguzi wa masoko na kesi nane ziko mbele ya Tume. Kesi hizo zinahusu masoko ya bidhaa za maziwa, sabuni, gesi, Umeme, tumbaku, sukari, vinywaji baridi na saruji. Tume inaendelea kusikiliza kesi tatu ikiwa ni sehemu ya utekelezwaji wa sheria ya ushindani (enforcement). Kesi hizo zimefikia hatua mbalimbali za usikilizwaji. Pia, Tume ya Ushindani inakabiliwa na kesi moja ambayo ipo Mahakama Kuu na rufaa moja ambayo ipo Baraza la Ushindani.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2011/2012, Wizara kupitia Tume ya Ushindani, imepokea na kupitia jumla ya maombi 21 ya muungano wa makampuni. Kati ya maombi hayo 18 yalipitishwa bila masharti. Maombi yaliyobaki bado yanashughulikiwa na yapo katika hatua mbalimbali za ukamilishwaji. Maombi yaliyopokelewa yanahusu sekta za fedha, kilimo, huduma, madini, mafuta, mawasiliano, majengo, nguo na uzalishaji. 
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Tume ya Ushindani iliwezesha watumishi wa Tume kupata mafunzo ya awali ya jinsi ya kutumia mfumo wa ASYCUDA++ ambayo yaliendeshwa na maofisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA). Aidha, Wizara kupitia Tume ya Ushindani imeunda Kikosi Kazi (Task Force) ili kuboresha mahusiano na Taasisi nyingine za Serikali zikiwemo TRA, TFDA, POLISI, TBS na Ofisi ya Mawanasheria Mkuu wa Serikali (AG’s Chamber) kwa mujibu wa Kanuni ya Alama za Bidhaa ya mwaka 2008. Uteuzi wa wajumbe wa Kikosi Kazi umekamilika na kuwasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua ya kuchapishwa katika Gazeti la Serikali.

BARAZA LA TAIFA LA UTETEZI WA MLAJI 
Mheshimiwa Spika, katika kusimamia maslahi ya Mlaji kwa kupeleka maoni yake kwenye tume ya ushindani na mamlaka za udhibiti na serikali kwa ujumla, Baraza la Taifa la Utetezi wa Mlaji limeendelea kutoa elimu na uhamasishaji kwa mlaji/walaji kuhusu haki na wajibu wao, kama inavyoainishwa katika sheria za mlaji. Katika kutekeleza majukumu hayo, Baraza la Taifa la Utetezi wa Mlaji limewahamasisha vijana na hasa wanafunzi wa vyuo mbalimbali ili wawe chachu ya mageuzi katika kutambua haki ya mlaji. Aidha, Baraza limetoa semina na vipeperushi kwa wadau mbalimbali kuhusu haki na wajibu wa mlaji.
Mheshimiwa Spika, Baraza la Taifa la Utetezi wa Mlaji liliendelea kutoa elimu kwa wananchi kwa kushirikiana na mabaraza ya utetezi wa mlaji/ mtumiaji. Baraza pia kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Fair Competition Commission, EWURA, SUMATRA, TCAA, FTC na TCRA tumefanikiwa kuchapisha jarida la utetezi wa mlaji na mtumiaji Tanzania ambalo lengo lake kuu ni kuwaelimisha Watanzania kuhusu haki na wajibu wao. Majarida hayo yamesambazwa katika taasisi mbali mbali vikiwemo vyuo, shule na katika vituo vya mabasi.  Pia, Baraza lilitoa matangazo ya moja kwa moja kupitia vyombo vya habari. 
Mheshimiwa Spika, Baraza limefanikiwa kuanzisha Kamati mbali mbali za utetezi wa mlaji, katika Kanda ya Ziwa (Mwanza), Kaskazini (Arusha), Kanda ya Kati (Singida), Kanda ya Mashariki (Morogoro), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Iringa), na Kanda ya Kusini (Mtwara). Vilevile, Baraza limepokea na kushughulikia malalamiko ya Walaji waliouziwa vifaa bandia na kuwashauri kuwasilisha malalamiko yao katika vyombo vya udhibiti kama vile FCC, EWURA na TCRA. Baraza pia limewaelimisha wadau kuhusu haki na wajibu wao pale wanapokuwa wameuziwa bidhaa bandia. 

BODI YA LESENI ZA MAGHALA 
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Bodi ya Leseni za Maghala, iliendelea kusimamia utekelezaji wa Mfumo wa Stakabadhi Ghalani ili kuhakikisha mkulima analipwa bei inayolingana na ubora wa mazao aliyoleta ghalani. Kutokana na matumizi ya mfumo huo, wanunuzi wengi wameonesha kuridhishwa na ubora wa mazao yaliyohifadhiwa ghalani kutokana na uthibiti wa ubora katika maghala hayo. Katika msimu wa 2011/2012, Bodi iliratibu matumizi ya mfumo katika mazao ya korosho, kahawa, alizeti, mpunga, pamba na mahindi. 
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2011/2012, Bodi ya Leseni za Maghala imetoa jumla ya leseni 52 za Maghala na leseni 28 za Waendesha Maghala. Aidha, tani zipatazo 158,587 za korosho, 2,800 za alizeti na zaidi ya tani 15,000 za kahawa zilikusanywa na kuuzwa kwa kutumia mfumo huo (Jedwali Na. 10 na Kielelezo Na. 1). Kutokana na usimamizi thabiti wa Bodi, bei za mazao zilizidi kuimarika na pia ubora wa mazao uliongezeka. Kwa mfano, bei ya kahawa isiyokobolewa iliongezeka na kufikia Shilingi 5,000 kwa kilo wakati bei ya korosho iliongezeka kutoka Shilingi 800 mwaka 2010/2011 hadi Shilingi 1,200 msimu wa mwaka 2011/2012 sawa na ongezeko la asilimia 50 (Jedwali Na. 11).
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Wizara kupitia Bodi ya Leseni ya Maghala, imefanikiwa kutoa elimu katika mikoa ya Kagera na Mwanza kuhusu Mfumo wa Stakabadhi za Maghala kwa wakulima na wadau wengine kupitia mikutano, warsha na vyombo vya habari vikiwemo radio na luninga. Kutokana na uhamasishaji huo, wilaya za Misungwi, Kwimba na Magu walitumia Mfumo wa Stakabadhi ghalani kwa zao la mpunga msimu wa 2011/2012. 
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Bodi ya Leseni za Maghala iliendelea kuwahamasisha Halmashauri za Wilaya na Sekta Binafsi na hivyo kufanikisha ujenzi wa maghala ya Mang’ula – Morogoro, Gendi - Manyara na Malula - Arusha. Vilevile, Benki ya NMB imekubali kutoa mikopo kwa vyama vya msingi kwa ajili ya ujenzi wa maghala katika mikoa ya Singida na Pwani. Katika msimu wa mwaka 2011/2012, kiasi cha Shilingi bilioni 33.3 kilitolewa na NMB kwa ajili ya malipo ya awali ya wakulima ukilinganisha na Shilingi bilioni 42.9 za msimu 2010/2011. Benki ya CRDB walitoa jumla ya Shilingi bilioni 26.4 katika msimu wa 2011/2012, ikilinganishwa na Shilingi bilioni 66.47 za msimu 2010/2011, na KCB Shilingi bilioni 3.8 msimu 2011/2012 ukilinganisha na Shilingi bilioni 12.23 za 2010/2011 (Jedwali Na. 12). Aidha, Bodi inaendelea kukusanya taarifa za wadau wa Mfumo kwa ajili ya kuanza kutengeneza kitabu cha kumbukumbu za wadau.


CHAMA CHA HAKIMILIKI TANZANIA (COSOTA)
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia COSOTA, imeendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ya mwaka 1999 na imeandaa marekebisho ya sheria hiyo na kuwasilishwa Baraza la Mawaziri kwa maamuzi. Aidha, katika kulinda maslahi ya wasanii, makubaliano yamefanyika kati ya Wizara yangu na Wizara ya Fedha, Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo ili TRA ianze kutoa stika za kudhibiti uzalishaji na usambazaji wa kazi za muziki na filamu kuanzia mwezi Julai, 2012. Vilevile, kampeni ya uhamasishaji wa masuala ya hakimiliki kupitia vyombo vya habari, kama vile luninga na redio umefanyika. Sambamba na zoezi hilo, COSOTA imetoa elimu kwa wauzaji wa kanda na wanunuzi kuhusu CD na mikanda bandia kwa Maafisa Ugani na Maafisa Leseni kuhusu Hakimiliki na Hakishiriki. 
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia COSOTA imesajili jumla ya Makampuni 106 yakiwemo makampuni 38 ya uzalishaji na usambazaji wa kazi za muziki; 19 ya uzalishaji na usambazaji wa kazi za filamu; na 49 ya uzalishaji, usambazaji wa kazi za uchapishaji na maandishi. Aidha, Wizara kupitia COSOTA imeendelea kusuluhisha migogoro na kufungua kesi dhidi ya wakiukaji wa Sheria na wasiotoa ushirikiano kulipia mirabaha kwa kupatia ufumbuzi migogoro 18 kati ya migogoro 24 iliyopokelewa. Jumla ya Kesi kumi zilifunguliwa dhidi ya ukiukaji wa Hakimiliki, tatu katika Mahakama zilizopo mkoani Dar es salaam na saba katika mkoa wa Singida. Kati ya hizo, Jamhuri imeshinda kesi sita kati ya saba mkoani Singida na tatu za mkoani Dar es Salaam zinaendelea. Pia, katika mwaka 2011/12, COSOTA imetayarisha Kanuni za Utoaji Leseni ya Maonesho kwa Umma na Utangazaji ili iweze kuanza kutumika.

MAENDELEO YA RASILIMALI WATU
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa 2011/2012, Wizara imepata kibali cha kuajiri watumishi wapya 42 kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma kati ya nafasi 80 zilizoombwa. Hadi kufikia Aprili, 2012 watumishi 10 wameripoti kazini na Sekretariati ya Ajira inaendelea kuajiri watumishi 38 waliobaki. Vile vile, Wizara imewathibitisha kazini watumishi watano na kuwapandisha vyeo watumishi 65 wa kada mbalimbali ikilinganishwa na malengo ya watumishi 67 kwa kutumia Mfumo wa Wazi wa Upimaji Utendaji Kazi (MWATUKA/OPRAS). Aidha, watumishi 20 waliwezeshwa kupata mafunzo katika ngazi ya Shahada, Shahada ya Uzamili na Shahada ya Uzamivu na watumishi 25 walihudhuria mafunzo ya muda mfupi ndani na nje ya nchi.

MASUALA MTAMBUKA

KUDHIBITI RUSHWA
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2011/2012, Wizara na taasisi imeendelea kutoa elimu kwa watumishi na umma kupitia mikutano ya ndani na maonesho ya biashara katika kupambana na kudhibiti rushwa na kubaini mianya ya rushwa kwa lengo la kuiziba. Vilevile, Wizara imeshirikiana na Menejimenti ya Utumishi kuendesha mafunzo ya maadili na utawala bora kwa wafanyakazi wote wa Wizara mwezi Aprili 2012. Aidha, Wizara imeanza kupitia Mkataba wa Huduma kwa Mteja ili kuboresha taratibu za utoaji huduma kwa umma na kuainisha haki na wajibu wa mteja na wa mtoa huduma.


JANGA LA UKIMWI
Mheshimiwa Spika, Wizara katika kutekeleza maelekezo ya Serikali kupitia Waraka Na. 2 wa mwaka 2006, imeendelea kutoa mafunzo kwa njia ya vipeperushi, maonesho na mikutano mbalimbali juu ya kujikinga na maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI na kuhamasisha upimaji wa afya za wafanyakazi kwa hiari. Aidha, imeendelea kuwawezesha wafanyakazi waishio na virusi vya UKIMWI kupata huduma ya virutubisho (food suplements), lishe na usafiri.

MAZINGIRA
Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Baraza la Mazingira -NEMC ilifanya tathmini ya hali ya uzingatiaji wa masuala ya mazingira (Enviromental Impact Assessment - EIA) kwa miradi mipya inayoanzishwa. Wizara, pia imefanya ukaguzi wa mazingira (enviromental audit) kwa mitambo ya viwanda vilivyopo ili kushauri wawekezaji na wenye viwanda kuzingatia utunzaji na uhifadhi wa mazingira katika uzalishaji Viwandani.
3.0 CHANGAMOTO ZA SEKTA NA HATUA ZILIZOCHUKULIWA
Mheshimiwa Spika, Wizara katika kutekeleza majukumu yake imekabiliwa na changamoto kadhaa zikiwa ni pamoja na uhaba wa umeme na maji, ushindani usio haki, miundombinu duni, uhaba wa mitaji na fedha, upatikanaji wa masoko, ukosefu wa wataalam na teknolojia duni. Katika kukabiliana na changamoto za kisekta, Wizara imechukua hatua kadhaa ikiwemo kuzingatia ushauri wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara wa kuweka vipaumbele vichache katika kutekeleza majukumu yake ya kisekta. Kwa mfano, katika kukabiliana na changamoto za uhaba wa mitaji na fedha, Wizara imetayarisha maandiko mbalimbali yatakayosaidia sekta hiyo kunufaika na mikopo ya kibenki pamoja na Mpango wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi – Public Private Partnership (PPP). Aidha, Wizara imeshirikiana na Taasisi za Serikali kama Commission for Science and Technology (COSTECH)  na hivyo kuziwezesha Taasisi zifuatazo kufaidika na fedha za Sayansi na Teknolijia: TIRDO – kwa ajili ya accreditation ya maabara, solar dryier na ngozi; CAMARTEC – kwa ajili ya uendelezaji wa trekta dogo; na TEMDO kwa ajili ya kiteketezi cha taka za hospitali (Bio-medical incinerator); na kuwawezesha kuendeleza ubunifu wao.
Mheshimiwa Spika, vile vile, jitihada zimefanyika za kuwa na majadiliano (Setor Dialogue) na Washirika wa Maendeleo hasa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Benki ya Dunia (WB), Denmark, Jumuiya ya Ulaya (EU), International Fund for Agricultural Development (IFAD), Japan, Switzerland, UNDP, UNIDO pamoja na Washirika Wapya wa Maendeleo hasa Korea Kusini, India na China ili kushirikiana katika kuandaa na kutekeleza mikakati na Programu za kuendeleza sekta hii ambayo ni moja ya vipaumbele vya Taifa. 
Mheshimiwa Spika, kuhusu uboreshaji wa mazingira ya biashara na urasimishaji wa biashara zisizo rasmi, Wizara kwa kushirikiana na sekta nyingine, iliendelea kuboresha mazingira ya biashara na kusaidia kupunguza gharama za kufanya biashara. Kwa mfano, utaratibu wa kupitisha maombi ya leseni za biashara katika ofisi za mipango miji na afya kama sharti la utoaji leseni ya biashara umeondolewa. Aidha, BRELA imerahisisha taratibu za usajili wa Makampuni kwa kuweka fomu zote za maombi ya usajili kwenye tovuti yake (www.brela-tz.org), kufupisha muda wa kusajili kutoka siku tano hadi kufikia siku tatu. Wizara kupitia SIDO inahamasisha ujasiriamali na kuelimisha umma kuhusu kufanya shughuli rasmi na kuunda vikundi ili kuwezesha upatikanaji wa mitaji na fedha. 
Mheshimiwa Spika, kuhusu changamoto ya elimu ya biashara na ushindani usio wa haki, Wizara kupitia CBE, COSOTA, FCC, NCAC, SIDO, TBS, TWLB, TanTrade na WMA, imetoa elimu na mbinu  za kufanya biashara kiushindani, kumlinda mlaji dhidi ya bidhaa bandia na pia kusimamia matumizi sahihi ya vipimo na viwango katika biashara. 
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia NDC inaendelea kukabiliana na uhaba wa upatikanaji wa umeme wakati huo huo inaendelea na utekelezaji wa miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe na upepo ambayo ipo katika hatua za awali. Hii ni pamoja na utekelezaji wa mradi wa mawe wa Ngaka Kusini na Mchuchuma na mradi wa umeme wa upepo Singida.
Mheshimiwa Spika, msisitizo na mwelekeo wa bajeti ya mwaka 2012/2013, ni kutatua changamoto zinazoikabili Sekta ya Viwanda, Biashara, Masoko na Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo; kuongeza ubunifu katika utendaji; kuimarisha ushirikiano na Sekta Binafsi kupitia mfumo wa PPP; kutafuta mitaji na fedha zaidi ili itoe mchango zaidi katika Pato la Taifa kama ilivyoanishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.

4.0 MALENGO YA MWAKA 2012/13
SEKTA YA VIWANDA
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Wizara itaendelea na utekelezaji wa Mkakati Unganishi wa Uendelezaji Viwanda nchini unaohusisha sekta ndogo ya nguo na mavazi, ngozi na bidhaa za ngozi, korosho, na nyama kwa kuhamasisha uwekezaji zaidi ili kupanua wigo wa soko la mazao hayo ndani na nje ya nchi. Hatua hiyo itaboresha bei ya mazao ambayo ni changamoto inayojitokeza mara kwa mara. Pia utekelezaji wake utaenda sambamba na utekelezaji wa Programu za Africa Agribusiness and Agroprocessing Development Initiative (3AD), Industrial Upgrading and Modernisation na Programu ya Mafunzo ya Kuongeza Tija, Ufanisi na Ubora wa Bidhaa (Kaizen Programume). Vilevile, Wizara itaendelea kufuatilia ujenzi wa Kiwanda cha Kuzalisha Viuadudu vya Mazalia ya Mbu waenezao malaria kinachojengwa katika eneo la TAMCO-mkoani Pwani. Matokeo ya mradi huo ni pamoja na kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa wa malaria na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni kuagiza dawa za kutibu malaria. 
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Wizara itafuatilia utekelezaji wa miradi ya Mchuchuma na Liganga unaoendeshwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania kupitia NDC na Kampuni ya Sichuan Hongda ya nchini China. Aidha, Wizara itafuatilia miradi ya TANCOAL, Kasi mpya na Umeme wa Upepo (Mkoani Singida) inayoendeshwa kwa ubia kati ya Serikali kupitia NDC na Sekta Binafsi. Lengo ni kuhakikisha kuwa miradi hii inatekelezwa kwa wakati ili kuhakikisha uzalishaji wa umeme na uchimbaji wa chuma unakamilika ili kuongeza uzalishaji viwandani na kupunguza utegemezi wa chuma chakavu unaochangia uharibifu wa miundombinu. 
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia EPZ itaendelea kuhamasisha uwekezaji,  ujenzi wa miundombinu katika maeneo ya EPZ/SEZ na kutoa fidia kwa maeneo ya EPZ/SEZ nchini likiwemo la ujenzi wa kituo cha biashara - Tanzania – China Logistic Centre, ili kuwezesha hatua za awali za ujenzi kuanza. Ujenzi wa maeneo ya EPZ/SEZ pamoja na Tanzania – China Logistic Centre yataongeza ajira, soko la malighafi nchini pamoja na kuvutia uwekezaji na biashara. Aidha, Tanzania – China Logistic Centre itakuwa kitovu (hub) cha biashara cha kutangaza fursa ya bidhaa za Tanzania kwa soko la ndani na nje. 
Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kukamilisha hatua zilizokwishaanza za kushughulikia viwanda vyenye changamoto maalum ikiwa ni pamoja na viwanda vilivyobinafsishwa, Viwanda vya General Tyre na Urafiki, biashara ya vyuma chakavu na biashara ya ngozi ghafi nchini. Lengo ni kuhakikisha ufufuaji na uendelezaji wa viwanda nchini, kuimarisha uzalishaji na upatikanaji wa bidhaa, kuongeza ajira na mapato yatokanayo na mchango wa sekta.

SEKTA YA VIWANDA VIDOGO NA BIASHARA NDOGO
Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kujenga na kuhamasisha Halmashauri kutenga maeneo ya kufanyia kazi wajasiriamali wadogo. Katika kufanikisha hilo, Wizara itaandaa mwongozo utakaosaidia Halmashauri kutenga maeneo yanayohamasisha sekta kupanuka. Hii itasaidia wajasiriamali kukua na kurasimisha biashara zao ili kuwawezesha kukopesheka. Wizara kupitia SIDO na Halmashauri  itaratibu uanzishwaji wa kongano (cluster) za uzalishaji na teknolojia katika Mikoa ya Dodoma, Kilimanjaro, Manyara, Morogoro na Singida. Kongano hizo zitachochea uzalishaji na ubora wa bidhaa na hivyo kuongeza kipato kwa wananchi. 
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia SIDO na wadau wengine itaendelea kutoa elimu ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara na huduma za ugani kwa wajasiriamali hasa vijijini. Aidha itawezesha  upatikanaji, uzalishaji na usambazaji wa teknolojia hasa za usindikaji ili kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na mifugo na hivyo kuongeza tija katika uzalishaji. Hii itasaidia bidhaa za wajasiriamali kushindana katika soko la ndani na la Afrika Mashariki na hivyo kuongeza ajira, pato la mjasiriamali na Taifa kwa ujumla. 
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia SIDO na taasisi nyingine, itaendelea kubuni mbinu mbalimbali za kuwezesha wajasiriamali wadogo kupata mitaji na fedha za kuendeshea shughuli zao. Aidha, Wizara itaendelea kuratibu utoaji wa mikopo kupitia Mfuko wa NEDF. Upatikanaji wa mitaji na fedha utaongeza ajira na ukuaji wa wajasirimali wadogo na hivyo kupanua wigo wa kodi. Wizara itaendelea na juhudi za kutafuta na kuwaunganisha wajasiriamali na masoko ya ndani na nje ya nchi kwa bidhaa na huduma zinazozalishwa na sekta. Hii ni pamoja na kuwawezesha wajasiriamali  kushiriki katika maonesho ya ndani na nje ya nchi ambapo watapata fursa ya kutangaza bidhaa, kupata miadi ya biashara na kujifunza kutoka kwa wenzao.

SEKTA YA BIASHARA
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Wizara itaendelea na majadiliano baina ya nchi na nchi (bilateral), ya kikanda (Regional) na yale ya kimataifa (Multilateral) kwa lengo la kupanua fursa za masoko kwa bidhaa na huduma na hivyo kuvutia wawekezaji. Majadiliano hayo yatazingatia maslahi ya nchi yetu na kutetea masuala yanayohusu vikwazo visivyo vya kiushuru (NTBs) na Uasili wa Bidhaa (Rules of Origin). Majadiliano hayo yanazingatia kulinda viwanda vyetu, kupata fursa za masoko kwa masharti nafuu (mfano China na India), masoko ya upendeleo (mfano Marekani - AGOA, EU –EBA, Japan na Canada) na kuleta ushindani wa haki. Katika fursa hizo tunalenga kuongeza uuzaji bidhaa na mazao yaliyoongezwa thamani katika masoko hayo hususan katika zao la korosho, pamba, tumbaku, bidhaa za ngozi,  maua, matunda na mboga (horticultural produce)  na nyinginezo. 
Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea na majadiliano ya kuanzishwa kwa Eneo Huru la Biashara la Utatu (Tripartite Free Trade Area - FTA) linalojumuisha Kanda za COMESA- EAC- SADC ikiwa ni utekelezaji wa Mpango wa Lagos Plan of Action wa mwaka 1980 wenye lengo la kukuza mtangamano wa kiuchumi na biashara katika nchi 26 za Afrika. Pia majadiliano ya Eneo Huru la Utatu yanalenga kurazinisha sera zinazokinzana kutokana na baadhi ya nchi ikiwemo Tanzania kuwa na uanachama wa zaidi ya kanda moja. Katika majadiliano yanayoendelea kuhusu Ubia wa Uchumi kati ya EAC na EU, Wizara itaendelea na majadiliano ili kuhakikisha maslahi ya Tanzania na ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yanazingatiwa.
Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kuimarisha vituo vya biashara vilivyopo London na Dubai ili kuendelea kukuza masoko ya bidhaa za Tanzania na kuvutia wawekezaji na watalii nchini. Aidha, vituo hivyo vitaendelea kuratibu ushiriki wa makampuni ya Tanzania katika maonesho ya kimataifa yakiwemo maonesho ya bidhaa za chakula yatakayofanyika mwezi Machi 2013 London, Uingereza.  Vituo vitaendelea kufanya utafiti wa soko (market intelligence) kwa bidhaa za Tanzania na kuunganisha wazalishaji na wanunuzi. Ili kuongeza upanuzi wa masoko katika nchi zinazoibukia kiuchumi (emerging economies) zikiwemo Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini (BRICs), Wizara inakusudia kuanzisha vituo vya biashara kwa kuanzia nchini China na Afrika Kusini. Vilevile, Wizara inakusudia kupeleka Waambata wa Biashara nchini Marekani na Ubelgiji.

SEKTA YA MASOKO
Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuendeleza miundombinu ya masoko nchini hususan masoko na maghala ya kuhifadhia mazao. Masoko ya kipaumbele ni yale ya mipakani ambayo ni: Sirari, Mtukula, Murongo, Mkwenda, Kabanga, Manyovu na Isaka (bandari kavu). Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri za Kasulu, Nanyumbu na Songea imelenga kuendeleza masoko katika mipaka ya Kilelema, Mtambaswala, Daraja la Mkenda, mtawalia. Kwa masoko ya Segera na Makambako, Wizara itahimiza kufikia makubaliano kati ya TIB na Halmashauri za mikoa husika ili kuanza ujenzi wa masoko hayo mapema. Masoko hayo yatawahakikishia wakulima soko la uhakika ikiwa ni hatua muhimu ya kutekeleza mkakati wa kukuza biashara ya ndani na nje na kurasimisha biashara nchini. Vilevile, Wizara itaendelea kushirikiana na wadau wengine kufanikisha uendelezaji wa Vituo vya Ukaguzi wa Pamoja Mipakani (One Stop Border Post - OSBP) na kuanzisha Kamati za Kufanya Kazi Pamoja Mipakani (Joint Border Committees – JBCs) ili kuboresha mazingira ya kufanya biashara (Doing Business)
Mheshimiwa Spika, Wizara pia imeweka lengo la kufanya mapitio ya sheria ili kuweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa masoko ya mazao na mifugo na kuendeleza soko la ndani. Sheria zilipangwa kufanyiwa marekebisho ni pamoja na Sheria ya The Export Control Act, Control of Movement of Agricultural Product Act, Sheria ya Usajili wa Shughuli za Biashara, The Limited Liability Partnership Act, The Warehouse Receipt Act 2005, na The Weight and Measure Act Cap 340 RE 2002. Aidha mabadiliko ya sheria ya Warehouse Receipt Act (2005) inalenga kuwezesha uanzishwaji wa Soko la Bidhaa (Commodity Exchange) ambalo litatumia Mfumo wa WRS. Mfumo huo utawezesha kuanzishwa kwa Tanzania Commodity Exchange (TCX), kupanua wigo wa biashara na kutoa bei shindani kwa wakulima. Wizara imefanya maandalizi ya kuanzisha Soko la Bidhaa  (Commodity Exchange) ili kuwahakikishia wakulima soko la uhakika. Maandalizi yaliyofanyika ni pamoja na kuunda Kikosi Kazi cha kuratibu uanzishaji wa Soko la Bidhaa.  Kikosi hicho kilipata fursa ya kujifunza Ethiopia, China na India ili kupata uzoefu.  Aidha, andiko la mpango (concept note), Mpango wa utekelezaji (road map ) vimeandaliwa na Waraka wa Baraza la Mawaziri umewasilishwa ili kupata maamuzi ya kuanzishwa kwa soko hilo.
Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kushirikiana na Bodi ya Stakabadhi za Maghala, Uongozi wa Mkoa wa Kagera na Vyama vya Ushirika ili kuanzisha matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi kwa zao la kahawa kwa msimu wa ununuzi wa 2013/2014. Wizara kwa kushirikiana na wadau wengine itaendelea kutoa elimu na kufuatilia utekelezaji wa Mfumo huo katika maeneo ambayo yanautumia ili kuendeleza manufaa yake. 
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha Mfumo wa Taarifa za Masoko, Wizara itaendelea kukusanya, kuchambua na kusambaza taarifa za masoko kwa kushirikiana  na Sekta Binafsi. Aidha, Wizara itaendelea kuhamasisha matumizi ya simu ya kiganjani na mtandao wa kompyuta ili kupata taarifa za masoko hususan taarifa za bei kwa wakati muafaka ambazo zitaunganishwa na mifumo ya taarifa za masoko ya mipakani. Wizara itaanza kwa majaribio (piloting) kutekeleza Mfumo Mpana na Unganishi wa Masoko kutegemeana na upatikanaji wa rasiliamali fedha. Hii ni moja ya hatua muhimu katika kukuza masoko ya kikanda na kimataifa.

UDHIBITI WA USHINDANI, UBORA WA BIDHAA NA HUDUMA
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu ina jukumu la kusimamia, ubora wa bidhaa na huduma, ushindani wa haki na matumizi ya vipimo rasmi ili kulinda maslahi ya walaji. Usimamizi huo hufanywa kupitia mashirika ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Tume ya Ushindani (FCC), Baraza la Ushindani (FCT), Wakala wa Vipimo (WMA), Baraza la Utetezi wa Haki ya Mlaji (NCAC) na Chama cha Hakimili Tanzania (COSOTA). 
Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto zilizojitokeza kuhusu ukaguzi na udhibiti wa ubora wa bidhaa kutoka nje ikiwa ni pamoja na magari kwa mwaka 2011/2012, Wizara kupitia Shirika la Viwango Tanzania katika mwaka 2012/2013, itafanyia kazi changamoto zote na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara; Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC). Vilevile, Wizara itaendeleza jitihada za kuijengea uwezo TBS kwa kuwezesha ajira za wataalam wa kutosha na kuwapa vitendea kazi ili kuboresha utendaji.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, TBS itaendelea kuimarisha utaratibu wa kukagua ubora wa bidhaa ukiwemo ukaguzi wa magari kabla ya kuingia nchini. Hii ni pamoja na kuwashirikisha wadau mbalimbali ili kupata maoni yao yatakayowezesha kufanywa marekebisho ya Sheria ya Viwango ya mwaka 2009, kwa lengo la kuangalia uwezekano wa kufanya ukaguzi wa magari ndani ya nchi. Kwa upande wa ukaguzi wa bidhaa kupitia PVoC, mapendekezo ya wadau yatawezesha pia kuangalia uwezekano wa kutenganisha bidhaa zinazohitaji kukaguliwa ndani na nje ya nchi kwa kuzingatia makundi tofauti ya wafanyabiashara wa Tanzania (wakubwa, wa kati na wadogo) bila kuathiri ubora wa bidhaa zinazoingizwa nchini. 
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Wizara pia itahakikisha kuwa TBS inashirikiana kwa ukaribu na vyombo vingine vya serikali kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Mkemia Mkuu wa Serikali, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Tume ya Ushindani Halali (FCC), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) ili kuhakikisha kuwa bidhaa zinazoingia nchini ni zenye ubora unaokubalika.  Wizara pia itaendeleza juhudi za kutoa elimu na kuhakikisha kwamba maabara zote za Shirika zinapata vyeti vya umahiri (laboratory accreditation) ili kuwezesha kukubalika kwa bidhaa nyingi zaidi za Tanzania katika soko la ndani na nje. 
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Baraza la Ushindani (FCT) litasikiliza kesi za rufaa zinazotokana na mchakato wa Udhibiti na Ushindani wa Biashara kwenye Soko; kujenga uwezo zaidi wa Baraza katika kushughulikia kesi hizo kwa kuimarisha rasilimali watu na Wajumbe wa Baraza; kutoa elimu kwa umma juu ya kazi za Baraza na umuhimu wake katika Uchumi; na kukamilisha maandalizi ya Mpango Mkakati (Strategic Plan-SP) wa Baraza wa miaka mitano. Aidha, Tume ya Ushindani itadhibiti na kupambana na uingizaji na uzalishaji wa bidhaa bandia; uchunguzi wa usikilizaji wa kesi za ushindani; utafiti wa masoko ili kubaini matatizo ya masoko husika na kama hatua za kurekebisha; na kumlinda na kumwelimisha mlaji. Vile vile, Baraza la Taifa la Utetezi wa Mlaji litasimamia maslahi ya mlaji kwa kupeleka maoni yake kwenye Tume ya Ushindani, Mamlaka za Udhibiti na Serikali kwa ujumla; kuendelea kupokea na kusambaza habari na maoni yenye maslahi kwa mlaji; kuanzisha Kamati za Mlaji za Mikoa na Sekta na kushauriana na kamati hizo; wenye viwanda, Serikali na jumuiya nyingine za walaji katika mambo yenye maslahi kwa mlaji.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Wakala wa Vipimo itaendelea kuimarisha kaguzi za matumizi ya vipimo nchini kwa kutoa elimu ya matumizi ya vipimo na ufungashaji wa bidhaa kwa wananchi sambamba na kuongeza weledi kwa watumishi wa Wakala na kuwaongezea vitendea kazi. Aidha, itaimarisha Kitengo cha Vipimo Bandarini (WMA Ports Unit) na kuhakiki usahihi wa vipimo vitumikavyo katika biashara ya gesi na mafuta ili kulinda mapato ya Serikali na haki ya mlaji. Wakala itakamilisha kazi ya upembuzi yakinifu kwa mradi wa ujenzi mpya na wa kisasa (eneo la kupimia magari yanayo safirisha mafuta) katika eneo la Misugusugu, Pwani; na kukamilisha taratibu za utungaji wa Sheria mpya ya Vipimo (Legal Metrology Act) ili kukidhi matakwa ya sasa ya biashara na pia kuzingatia maridhiano yaliyofikiwa na nchi kikanda na kimataifa kuhusu masuala ya vipimo. 
Mheshimiwa Spika, katika kulinda haki za wasanii dhidi ya uharamia wa kazi zao, Wizara kwa kupitia COSOTA katika mwaka 2012/2013, inatarajia kukamilisha marejeo ya Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ya mwaka 1999. Hatua hii itawezesha sheria hiyo kuendana na Standard Act ya Afrika iliyozingatia makubaliano ya mikataba iliyofanyika baada ya mwaka 1999. Makubaliano hayo yanatenganisha shughuli za udhibiti wa Hakimiliki na zile za Vyama vya Usimamizi wa Pamoja wa Hatimiliki. Aidha, COSOTA itaendelea kupanua wigo wa  utendaji kwa kufungua ofisi mjini Arusha na Dodoma; kukusanya mirabaha kutoka kwenye mashirika ya utangazaji; na kuhamasisha wanunuzi wa CD, kanda za miziki na filamu kununua kanda  na CD zenye Hakigram.
MAZINGIRA WEZESHI YA KUFANYA BIASHARA
Mheshimiwa Spika, Wizara ina jukumu la kukuza na kuweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara kupitia Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA); Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TanTrade); na Bodi ya Leseni ya Maghala (TWLB). Katika mwaka 2012/2013; Wizara kupitia BRELA itaboresha usajili wa makampuni na majina ya biashara kwa kutumia mfumo na mashine za kisasa zijulikanazo kama ‘special machine readable certificates’ ili kuondoa wimbi la kughushi vyeti na kuleta uthibiti.  Aidha, BRELA itaendeleza jitihada za kupunguza muda unaotumika kusajili kampuni na majina ya biashara kwa kutumia mifumo Programu ya kompyuta inayowezesha kufanya usajili kwa mtandao (On line registration systems), kuboresha Masijala za kisheria zinazosimamiwa na Wakala ili kuendana na mifumo ya kitekinolojia na hivyo kurahisisha utoaji huduma; kufanya marekebisho ya sheria zinazosimamiwa na Wakala ili ziweze kwenda na wakati; na kutoa elimu kwa umma kuhusu taratibu za usajili wa makampuni na majina ya biashara kwa kuzingatia taratibu za sheria na kanuni zilizopo. Pia Wizara itatoa msukumo wa kuanza ujenzi wa ofisi za BRELA.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Mamlaka ya Biashara Tanzania (TanTrade) itaendelea kuboresha biashara ya ndani na nje kwa kuongeza wigo wa masoko ya kikanda na kimataifa. Wizara kupitia TanTrade itaboresha maonesho ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) na kuhamasisha ushiriki wa wajasiriamali kwenye maonesho ndani na nje ya nchi kwa lengo kutangaza bidhaa za Tanzania na kutumia fursa za masoko mbalimbali. Aidha, Wizara kupitia TanTrade itaimarisha Kituo cha Zanzibar na kutoa huduma ya taarifa za biashara kwa wadau. 
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha upatikanaji wa masoko ya mazao na bei shindani kwa wakulima, katika mwaka 2012/2013 Bodi ya leseni ya Maghala itasimamia uanzishwaji wa utekelezaji wa Mfumo wa Stakabadhi za Maghala katika zao la kahawa mkoani Kagera na kupanua matumizi ya mfumo katika mazao mengine na kufanya maandalizi ya kuwezesha mfumo huo kutumika katika Soko la Bidhaa (Commodity Exchange). Aidha, Bodi itasimamia utekelezaji wa mfumo huo katika maeneo yote yanayotekeleza mfumo hapa nchini; kuboresha mfumo wa ukaguzi wa maghala; na kutoa elimu ya mfumo kwa wadau.

MAMLAKA YA MAENEO MAALUM YA KUZALISHA BIDHAA ZA KUUZA NJE (EXPORT PROCESING ZONES AUTHORITY –EPZA)
Mheshimiwa Spika, malengo ya EPZA kwa mwaka 2012/2013 ni kulipa fidia na kuanza uendelezaji wa eneo la kipaumbele la Bagamoyo SEZ utakaohusisha ujenzi wa miundombinu ya msingi katika eneo la awamu ya kwanza (phase one). Aidha, kufanya uthamini na ulipaji fidia katika eneo la mradi wa Tanzania - China Logistics Center, Kurasini, Dar es salaam na kuanza utekelezaji; kulipa fidia kwa maeneo  ya EPZ  na SEZ  ya Mara, Ruvuma, Tanga na Kigoma ambayo yameshathaminiwa na kuthibitishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali. Vile vile,  kwa kushirikiana na uongozi wa mikoa mipya ya Geita, Njombe, Katavi na Simiyu; itakamilisha zoezi la ubainishaji wa maeneo ya EPZ na SEZ katika mikoa hiyo.  Aidha, EPZA itaendelea kuhamasisha wawekezaji wa kujenga miundombinu na wale wa kujenga viwanda vya kuzalisha bidhaa katika maeneo ya EPZ na SEZ ikiwemo kujenga mfumo wa maji taka katika eneo la Benjamin William Mkapa SEZ;  kufanya detailed design ya ujenzi wa miundombinu ya msingi katika maeneo ya Kigoma SEZ na Mtwara Freeport Zone. Vilevile itafanya upembuzi yakinifu (feasibility study) na kuandaa mpango mpana (Master plan) kwa ajili ya uendelezaji wa Mtwara SEZ, Tanga SEZ,  Ruvuma SEZ  na Mara SEZ; na kuandaa mpango mkakati mpya wa miaka mitano wa EPZA  (Five Years Strategic Plan  2013-2018) 

SHIRIKA LA TAIFA LA MAENDELEO (NDC) 
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013,  Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) litaendelea na utekelezaji wa miradi ya makaa ya mawe ya Mchuchuma  na  Chuma cha Liganga; kuendeleza utekelezaji wa miradi ya makaa ya mawe iliyoko Katewaka na mradi wa Chuma ulioko Maganga Matitu  kuzalisha chuma ghafi (Mradi wa Kasi Mpya); kujenga kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe (Ngaka Kusini, Songea); kujenga Kituo cha kuzalisha umeme wa upepo (Singida)  na ; kukamilisha ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha Viuadudu (biolarvicides) kwa ajili ya kuua viluwiluwi kwenye mazalia ya mbu wa malaria (TAMCO, Kibaha). Vilevile, NDC itaendelea na ukarabati wa Kiwanda cha General Tyre, Arusha ili  kukifufua na kuanza uzalishaji wa matairi; kujenga maeneo ya viwanda (Industrial parks) sehemu za TAMCO, KMTC (Moshi) na Kange (Tanga); kuanzisha viwanda vya kusindika nyama, mpira na mazao mengine ya Kilimo; Kukamilisha tafiti na kuanzisha kiwanda cha kuzalisha magadi (soda ash) katika Ziwa Natron na Engaruka, Arusha; kuratibu uendelezaji wa kanda za maendeleo za Mtwara, Tanga, Kati na Uhuru; na kuwajengea uwezo wananchi wa maeneo ya miradi kufaidika na  fursa zinazotokana na miradi  hiyo inayotekelezwa na NDC.

KUKUZA VIWANDA VIDOGO NA KUKUZA UJASIRIMALI
Mheshimiwa Spika, Wizara ina jukumu la kusimamia maendeleo ya ujasirimali ambalo linatekelezwa na SIDO. Katika mwaka 2012/2013, SIDO imepanga kuimarisha uwezo wa kuzalisha na kusambaza mashine ndogo za kuongeza thamani mazao na kuwezesha usambazaji wa teknolojia vijijini kupitia Programu ya Wilaya Moja bidhaa Moja (ODOP). Vilevile, SIDO itasaidia uanzishaji wa kongano za viwanda vidogo vya kusindika alizeti; kuchochea ubunifu na utengenezaji wa bidhaa mpya kupitia Programu ya kiatamizi na kutoa elimu ya ujasiriamali, na uongozi wa biashara. Pia SIDO itakamilisha ujenzi wa Ofisi ya SIDO Mkoa wa Manyara na kuwezesha vyuo vya mafunzo na uzalishaji vya SIDO kufanya kazi; kupanua wigo wa masoko ya wajasirimali wadogo, kutafuta na kusambaza taarifa za kuboresha biashara; na kutoa huduma za kifedha ikiwa ni pamoja na ushauri. Malengo hayo yataongeza idadi ya wajasirimali, ajira na kipato na hivyo kuchangia katika kupunguza umasikini.

UTAFITI, MAFUNZO NA MAENDELEO YA TEKNOLOJIA
Mheshimiwa Spika, Wizara ina majukumu ya kufanya utafiti, kutoa mafunzo mbalimbali ya kisekta na kuendeleza teknolojia mbalimbali kwa kushirikisha Taasisi za TIRDO, TEMDO, CAMARTEC na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) ili kuongeza ubora na ufanisi wa bidhaa zinazozalishwa na viwanda mbalimbali na kujipatia teknolojia rahisi na yenye tija. 
Mheshimiwa Spika, TEMDO katika mwaka 2012/2013 itaboresha miundombinu ya kiatamizi cha teknolojia/biashara (Technology/Business Incubator) na kuwezesha wajasiriamali watano (5) wanaosindika vyakula na kutengeneza mashine na vifaa kwa matumizi ya viwanda vya kati kwa kuwapatia teknolojia na mafunzo.  Aidha, TEMDO itaendeleza utoaji huduma na ushauri wa kihandisi pamoja na mafunzo kwa viwanda kumi kwa lengo la kuongeza tija, uzalishaji, kulinda afya na usalama pamoja na kuhifadhi mazingira sehemu za kazi. Vilevile, TEMDO itaendelea kubuni, kuendeleza na kuhamasisha utengenezaji wa chasili (prototypes) za  vifaa vya hospitali (hospital equipment and devices) kama vile mashine za kufua nguo, majokofu ya kuhifadhi dawa au maiti (hospital refrigerators or mortuary facilities), vitanda na viti maalum ili kupunguza uagizaji wa vifaa hivyo kutoka nje ya nchi kwa kutumia fedha nyingi za kigeni. 
Mheshimiwa Spika, TEMDO, itabuni na kuendeleza chasili za teknolojia za kutumia upya au kurejesha (re-use or re-cycle) taka za mijini na kutengeneza umeme, kutengeneza vifaa vya plastiki na karatasi (Municipal Solid Waste recycling technologies. Halikadhalika, TEMDO itafanya majaribio ya chasili za machinjio ya kisasa yenye gharama nafuu pamoja na teknolojia  za kuongeza thamani ya bidhaa zitokanazo na mabaki ya mifugo na kuendelea na maboresho pamoja na uhawilishaji wa teknolojia mbalimbali zilizothibitishwa ikiwa ni pamoja na teknolojia ya kuteketeza taka za hospitali (bio-medical waste incineration).
Mheshimiwa Spika, TIRDO katika mwaka 2012/2013 itatekeleza mradi wa kurejeresha taka za ngozi ili kutengeneza bidhaa kama leather boards kwa lengo la kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na viwanda vya kusindika ngozi  na kuimarisha uzalishaji katika viwanda vya kusindika ngozi na viwanda vya bidhaa za ngozi. Aidha, itashughulikia umahiri (accreditation) wa maabara ya mazingira na ya vifaa vya kihandisi ili iweze kufikia viwango vya kimataifa na kuweza kutoa huduma bora kwa wazalishaji viwandani; TIRDO pia, itatekeleza mfumo wa ufuatiliaji wa mazao (traceability) kwa kutumia kompyuta na pia kutoa ushauri wa kiufundi kwa viwanda vikubwa na vidogo katika sekta ya uzalishaji bidhaa zitokanazo na mazao ya kilino (agro-processing industries) kupitia benki ya rasilimali (TIB) na; kujenga tovuti ili kusaidia wazalishaji wadogo na kati kutangaza bidhaa zao ili wapate masoko ya ndani na nje ya nchi. 
Mheshimiwa Spika, CAMARTEC katika mwaka 2012/2013 itaendeleza uzalishaji wa trekta ndogo lililobuniwa na CAMARTEC na kuharakisha uzalishaji wake kibiashara (commercialisation) kupitia Sekta Binafsi; itabuni na kutengeneza, vipandio vya mbegu za mahindi na jamii ya mikunde vinavyoendeshwa kwa trekta; mashine ya kufyatua matofali ya udongo saruji inayoendeshwa kwa injini; teknolojia za nishati jadidifu; mitambo ya kuchemsha maji kwa kutumia nishati ya mionzi ya jua na ; mashine za kukatakata majani ya kulishia wanyama zinazoendeshwa kwa injini. Teknolojia hizi zitapunguza suluba na kurahisisha utendaji kazi kwa wananchi vijijini na hivyo kuongeza uzalishaji na tija. Vile vile CAMARTEC itanunua na kusimika mashine na vifaa kwa ajili ya maabara ya kisasa (kupima tabia za udongo, majaribio ya mashine na teknolojia za nishati ya mionzi ya jua na biogas), kuendesha mafunzo ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu. Aidha, itakarabati na kuboresha majengo ya ofisi na karakana ya Tawi la CAMARTEC lililoko Nzega; na kukamilisha ujenzi wa ukuta kuzunguka eneo la Kituo huko Themi (Arusha) kwa ajili ya usalama wa mali za Kituo.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Chuo Cha Elimu ya Biashara kitaimarisha mafunzo yenye mwelekeo wa kiutendaji katika nyanja za biashara yaani: Menejimenti ya Ununuzi na Ugavi, Utawala na Uongozi wa Biashara, Uhasibu, Menejimenti ya Masoko, Taaluma ya Mizani na Vipimo, Taaluma ya Habari na Mawasiliano na Taaluma nyingine zinazohusiana na hizo katika ngazi za astashahada, stashahada, shahada na stashahada ya uzamili. Aidha, Chuo kitaandaa mitaala mipya ya shahada ya kwanza katika Ujasiriamali, Menejimenti ya Rasilimali Watu na Elimu ya Biashara. Vile vile Chuo kitaandaa mitaala ya shahada ya uzamili; kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wajasiriamali wadogo wadogo na wakati ili kuwasadia wafanye biashara zao kwa ustawi mkubwa zaidi. Pia Chuo kitaandaa mpango kabambe wa Chuo (Master Plan) katika Kampusi zake  tatu yaani: Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza kwa ajili ya upanuzi wa chuo; kukarabati majengo ya Chuo na kupeleka watumishi katika mafunzo ya muda mrefu katika ngazi ya Shahada za Uzamivu (PhD) na shahada ya uzamili.

MAENDELEO YA RASILIMALI WATU
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Wizara inatarajia kuajiri watumishi wapya 53 wa kada mbalimbali ili kuziwezesha idara na vitengo kupata rasilimali watu wa kutosha ili  kutoa huduma nzuri na kwa ukamilifu. Pia, Wizara inatarajia kuwathibitisha kazini watumishi 42 na kuwapandisha vyeo Watumishi 28. Pia Wizara inatarajia kuwapeleka watumishi 15 mafunzo ya muda mrefu katika vyuo mbalimbali nchini na watumishi 20 kwenye mafunzo ya muda mfupi ili kuboresha utendaji wao wa kazi.
MASUALA MTAMBUKA 
KUDHIBITI RUSHWA
Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha mwaka 2012/2013, Wizara itaendelea  na jitihada za kupambana na kudhibiti rushwa kwa  watumishi wake kwa kutoa mafunzo ya Sheria mbalimbali za kazi, Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sheria ya Fedha ili kuwawezesha kufanya kazi na kutoa maamuzi kwa kuzingatia matakwa ya sheria tajwa.  Ili kuweza kutoa huduma bora zinazokidhi viwango vilivyoainishwa katika Mkataba wa Huduma kwa Mteja, Wizara itaendesha mafunzo ya elimu ya huduma kwa mteja kwa watumishi 50 ili kuwapatia mbinu mbalimbali za kuhudumia wateja.  Vilevile wizara inatarajia kuimarisha dawati la kushughulikia malamiko ya Sekta ya Viwanda, Biashara, Masoko na Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo ili kuweza kutatua kero mbalimbali za wananchi. 
JANGA LA UKIMWI
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Wizara itaendelea na jitihada za kuwawezesha watumishi waliojitokeza na watakaojitokeza wanaoishi na virusi vya UKIMWI kupata huduma ya virutubisho,  lishe na  usafiri. Pia Wizara itaendelea kutoa mafunzo ya kujikinga na maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI na kuhamasisha upimaji wa afya za wafanyakazi kwa hiari. Aidha, Waelimishaji rika watapewa mafunzo ili kuwawezesha kupata mbinu mpya ambazo zitawawezesha kuwaelimisha watumishi wenzao na familia zao. 

MAZINGIRA
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2012/2013, Wizara itaendelea kutekeleza mikakati inayohusu utunzaji wa mazingira pamoja na Programu ya utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi na Utunzaji wa Mazingira Viwandani na taasisi za Sekta za Viwanda na Biashara.

5.0  SHUKRANI
Mheshimiwa Spika, napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kutoa shukrani za dhati kwa nchi rafiki na Mashirika ya Kimataifa ambayo yamekuwa yakitoa na yanaendelea kutoa misaada mbalimbali kusaidia Wizara yangu. Misaada na michango hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa Wizara yangu kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na tija. Nchi rafiki ni pamoja na Austria, Canada, China, Denmark, Finland, India, Ireland, Japan, Korea ya Kusini, Marekani, Norway, Sweden, Uholanzi, Uingereza, Ujerumani na Uswisi. Mashirika ya Kimataifa ni pamoja na: Benki ya Dunia, DANIDA, CFC, ARIPO, DFID, EU, FAO, IFAD, JICA, Jumuiya ya Madola, KOICA, Sida, UNCTAD, UNDP, UNIDO, USAID, WTO na WIPO.

6.0 MAOMBI YA FEDHA KATIKA MWAKA 2012/2013
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Wizara na Taasisi zilizo chini yake inaomba kutengewa jumla ya Shilingi 170,199,842,000 kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya kuendeleza Sekta ya Viwanda, Biashara, Masoko na Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo. Kati ya fedha hizo, Shilingi 38,819,055,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Shilingi 131,380,787,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

MAPATO YA SERIKALI 
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Wizara inatarajia kukusanya kiasi cha Shilingi 43,974,000 kutokana na faini zitokanazo na kukiuka sheria ya leseni, uuzaji wa nyaraka za tenda pamoja na makusanyo mengine.

(ii) MATUMIZI YA KAWAIDA
  Mheshimiwa Spika, kati ya Shilingi 38,819,055,000 zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, Shilingi 31,378,315,000 zimetengwa kwa ajili ya mishahara (PE) na Shilingi 7,440,740,000 zimetengwa kwa ajili ya matumizi mengine (OC). Aidha, kati ya fedha za mishahara (PE) Shilingi 2,443,590,000 zimetengwa kwa ajili ya mishahara ya Wizara na Shilingi 28,934,725,000 zimetengwa kwa ajili ya mishahara ya Taasisi. Vile vile, kati ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya matumizi mengine (OC), Shilingi 6,143,859,000 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya Wizara na Shilingi 1,296,881,000 zimetengwa kwa ajili ya Taasisi zilizo chini ya Wizara.

(iii) MATUMIZI YA MIRADI YA MAENDELEO
Mheshimiwa Spika, Kiasi cha Shilingi 123,713,139,000 kati ya Shilingi 131,380,787,000 zilizotengwa kwa shughuli za miradi ya maendeleo katika Wizara na Taasisi zake ni fedha za ndani, na Shilingi 7,667,648,000 ni fedha za nje zitakazotoka kwa Washirika wa Maendeleo. Shilingi 60,000,000,000 kati ya Shilingi 123,713,139,000 zilizotengwa kutokana na fedha za ndani, zitatumika katika uanzishaji wa Tanzania –China Logistic Centre na Shilingi 50,200,000,000 zitatumika katika kulipa fidia na kuendeleza maeneo huru kwa ajili ya uzalishaji bidhaa za mauzo nje na ndani ya nchi (Special Economic Zones – SEZ/EPZ). Shilingi 7,960,000,000 zitatumika kwa ajili ya kutekeleza shughuli za kuendeleza viwanda mama katika Shirika la NDC na Shilingi 5,553,139,000 zitatumika kwa ajili ya kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo katika Wizara na Mashirika mengine chini ya Wizara.
Mheshimiwa Spika, Napenda kukushukuru tena wewe na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza. Hotuba hii inapatikana kwenye tovuti ya Wizara  HYPERLINK "http://www.mit.go.tz" www.mit.go.tz
Mheshimiwa Spika, Naomba kutoa hoja.

1 comment:

Anonymous said...

We stumbled over here different web address and thought I may as well check
things out. I like what I see so now i'm following you. Look forward to going over your web page yet again.
Also visit my web blog ... Winning Trade System Scam