YA DK. ULIMBOKA SASA YAMKUTA MWANASHERIA BARAZA LA MAZINGIRA...

Sakata la ubomoaji majumba ya kifahari yaliyojengwa katika fukwe za Dar es Salaam limechukua sura mpya baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, Dk Terezya Huvisa kufichua siri ya uhalifu.
Waziri amesema mbali na yeye kutishwa kuuawa, pia Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Heche Manchare ametekwa na watu wasiojulikana wakiwa wameficha nyuso zao kwa vitambaa na kumpiga kisha kumtelekeza eneo ambalo hakulitaja.
Dk Huvisa alisema hayo bungeni mjini hapa jana, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu sakata hilo ambapo pia alisema waliobomolewa watapelekewa gharama zilizotumiwa na Serikali katika kubomoa nyumba zao ili wazilipe.
Alisema baada ya bomoabomoa hiyo, alipokea vitisho kupitia ujumbe mfupi wa simu ya mkononi mara mbili zikimtishia kumwua kutokana na hatua yake ya kusimamia mkakati huo na kwamba akijaribu kupiga namba  hizo hazipatikani.
Alisema kutokana na simu hizo kutopatikana alipuuza vitisho hivyo akiamini kwamba vinatolewa na watu wasiojiamini, lakini siku chache mbele Mwanasheria  huyo wa NEMC alivamiwa na watu wasiojulikana waliokuwa wamejifunga vitambaa usoni ili kuficha sura zao.
"Suala hili lipo Polisi linafanyiwa kazi, lakini hali ya vitisho imekuwa kubwa, napenda kuwaeleza wazi wananchi kwamba bomoabomoa hiyo itaendelea nchi nzima," alisema Dk Huvisa.
Akizungumzia bomoabomoa hiyo, Waziri huyo alisema Serikali ilifanya kazi hiyo ya kubomoa nyumba katika fukwe za Mbezi na Kawe kutokana na kujengwa kwa kukiuka sheria zinazolinda maeneo oevu na fukwe za bahari, maziwa, mito na sheria za ardhi.
Alisema kazi hiyo iliigharimu Serikali Sh milioni 50 iliwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi.
"Si nia ya Serikali kulenga kuvunja nyumba za watu  lakini wahusika hawa walipewa kila aina ya maelekezo tangu walipokuwa wanajenga kwamba hawaruhusiwi kujenga katika maeneo hayo  na NEMC tangu mwaka 2008, lakini walikuwa wanapuuza maagizo hayo.
"Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 ipo wazi kabisa inapinga ujenzi  wa nyumba meta 60 kutoka fukwe za bahari na maziwa na meta 30 kutoka fukwe za mito. Tutabomoa nyumba zote zilizojengwa katika maeneo hayo nchi nzima bila kuangalia nani anahusika," alisema Waziri huyo.
Alisema katika zoezi hilo la jijini Dar es Salaam nyumba 17 na fensi nane zilibomolewa kutokana na kujengwa katika maeneo oevu ya fukwe za bahari hatua ambayo pamoja na kukiuka sheria ya mazingira lakini pia inakiuka sheria ya ardhi.
"Kutokana na utekelezaji wa hatua hiyo kitakachofuata sasa ni kwa Serikali kutathmini ili kujua kila mmoja anatakiwa kulipa kwa Serikali kiasi gani cha fedha kama gharama za kubomoa nyumba yake, tukishajua nani anatakiwa alipe nini, tutawapelekea wahusika gharama hizo," alisema.
Alisema Serikali pia pamoja na kutobomoa nyumba namba 2019/20 iliyojengwa kwenye fukwe ya bahari kutokana na mmiliki wake kukimbilia mahakamani kuweka pingamizi, lakini Serikali inapinga ujenzi huo kwa vile kiwanja hicho ni cha kubuni na kwamba mhusika alichepusha mkondo wa mto na baadaye kujaza kifusi katika kiwanja hicho kabla ya kujenga.
"Hapa tunasubiri kesi iliyo Mahakama Kuu ya Tanzania kitengo cha Ardhi isikilizwe na baadaye tutaendelea na utekelezaji wa kazi yetu. Tunapenda kuonya mara moja watu wanaotisha watumishi wa Serikali wanaotekeleza bomoabomoa, kwamba Serikali haitawavumilia," alisema.

No comments: