WABUNGE WA CHADEMA WAHUSISHWA NA MAUAJI

Baadhi ya wabunge wa Chadema, wamehusishwa na mauaji ya Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wa Kata ya Ndago wilayani Iramba mkoani Singida, Yohana Mpinga (30).
Akizungumza bungeni jana, Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba alisema kabla ya mauaji hayo anayoona yalipangwa, alitishiwa kuuawa kwa kutumiwa ujumbe mfupi wa simu na wabunge hao kutokana na mijadala yake bungeni. 
Nchemba alitoa madai hayo alipoomba Mwongozo wa Spika akitumia Kanuni ya Bunge ya 47 inayohusu kusitishwa kwa shughuli za Bunge ili kujadili jambo la dharura la Taifa.
Sehemu ya ujumbe huo ambao Spika wa Bunge, Anne Makinda alimzuia kuusoma, unamtaka Mwigulu asijifanye anajua, kwani mwenzake Chacha Wangwe (Marehemu Mbunge wa Tarime) alijifanya anajua na "sasa yuko wapi?" Ujumbe mwingine ulimwambia kuwa skafu ya Bendera ya Taifa anayovaa shingoni, itageuka sanda yake.
Akiomba Mwongozo huo, Nchemba alisema kutokana na tukio la kinyama lililotokea jimboni mwake juzi la kuuawa kwa Mpinga na watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chadema, aliomba Bunge liahirishwe ili suala hilo lijadiliwe kwa kina.
"Naomba tuahirishe Bunge tujadili suala hili, kwa kuwa inaonesha kilichotokea kilipangwa, nilipokea SMS (ujumbe mfupi) katika simu yangu za kunitishia kuuawa kutokana na mijadala ninayochangia bungeni na namba za walionitumia SMS zimebainika kuwa ni za wabunge wa Chadema," alisema Mwigulu.
Alisema namba za simu zilizokuwa zikitumika kumtumia ujumbe huo mfupi alizipeleka Polisi na tayari wabunge hao waliomtishia maisha wamebainika majina yao na hatua zaidi zitachukuliwa.
Pamoja na kukataa kutaja majina ya wabunge hao, Nchemba nje ya Bunge alionesha ujumbe mfupi aliotumiwa ambao unasema: "Hivi wewe unajiamini nini? Kwa nini unatusonga hivyo? Unadhani nchi hii ni ya CCM milele?
"Utajutia kimbelembele chako. Unadhani ni wewe tu unayejua sana? Ukabila kwenye chama chetu unakuhusu nini, hata kama ni kweli, kwa nini kututia aibu?" 
Ujumbe huo uliendelea: "Hata ufanyeje, 2015 tunaingia Ikulu na mjengoni tutajaa, Wangwe alijifanya kujua kama wewe leo yuko wapi?"
Ujumbe mwingine ulisema: "Bendera unayovaa kila siku shingoni itageuka sanda yako. Kila mtu ana haki ya kuvutia kwake, lakini wewe umezidi. Hatuwezi kuitema keki tuliyokwishaionja". Ujumbe mwingine ulisema: "Fahari yako leo, itageuka kilio kwako. Utatutambua."
Hata hivyo, Spika Anne Makinda alimkatisha Nchemba asiwataje kwa majina wabunge hao waliomtumia ujumbe mfupi wa kutishia kumwua na kumtaka aiachie Polisi ishughulike na jambo hilo, ambapo pia aliukataa Mwongozo wa kuahirisha kikao. 
"Kanuni hizi kweli zipo, lakini pia katika kifungu kinachoendelea kimetoa masharti yanayosema, Bunge litaahirishwa iwapo tu suala litakalojadili utatuzi wake utakuwa mikononi mwake, lakini suala hili la kuuawa kwa Katibu wa CCM hata tukijadili sisi kama wabunge, tutafika wapi?" Alihoji Makinda. 
Alisema taarifa alizonazo tayari Polisi wameanza kulifanyia kazi suala hilo, ambapo aliwataka kufanya uchunguzi wa kina na watakaobainika kuhusika na mauaji hayo wachukuliwe hatua.
Kuhusu kutishiwa maisha kwa Nchemba, Makinda alitaka wabunge kuacha tabia mbaya na ya kigaidi ya kuchukua masuala yanayojadiliwa ndani ya Bunge na kutokanayo nje kwa ajili ya kulipiza visasi.
"Wabunge tumeanzisha tabia mbaya na ya kigaidi, kinachojadiliwa hapa kinaachwa hapa, lakini sasa wabunge wanafikia hatua ya kutishia mtu kumwua, ni kweli habari za Nchemba ninazo na watu hao waliomwandikia ujumbe wa kutishia kumwua nawajua,
majina yao yamepelekwa Polisi, tuwe na heshima jamani," alilalamika. 
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Steven Zelothe alikataa kuthibitisha kufikishiwa suala hilo, ingawa alisema amelisikia likizungumzwa bungeni. 
"Kwa sasa naomba sisi tusiseme kitu, tuachieni kwanza tuangalie hali halisi inavyokwenda na tukipata taarifa kamili tutazungumza hatua zetu, ila sasa naomba nisilisemee chochote suala hili," alisema Zelothe.
Akiwa nje ya Bunge, Nchemba alimwomba Msajili wa Vyama vya Siasa kufuatilia kwa karibu zaidi mikutano au mienendo ya Chadema hasa Operesheni Sangara, ambao mara kwa mara wamekuwa wakienda kwenye majimbo ya wabunge na kutoa maneno ya uchochezi.
"Huu si utaratibu mzuri, tulipochukua vyama vingi tulimaanisha kuvumiliana na kufanya siasa za kistaarabu, leo nakwenda kumzika ndugu yangu, lakini nikirudi tutaangalia ni kwa namna gani tutaweza kulishughulikia suala hili," alisema Nchemba.
Mwishoni mwa wiki iliyopita katika mkutano wa Chadema uliohutubiwa na Mbunge wa Ubungo John Mnyika, kuliibuka vurugu zilizohusisha wafuasi wa Chadema na CCM na
kusababisha Katibu huyo kuuawa na mtu mwingine mmoja kujeruhiwa.

No comments: