BAJETI YA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI KWA MWAKA 2012 - 2013...


HOTUBA YA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI MHESHIMIWA DKT. EMMANUEL JOHN  NCHIMBI   (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI KWA MWAKA 2012/2013
I. UTANGULIZI

1. Mheshimiwa Spika, baada ya kuzingatia taarifa iliyowasilishwa mbele ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba kutumia  fursa hii kutoa rambirambi zangu kwa familia na wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kutokana na mvua kubwa iliyonyesha mwishoni mwa  mwezi Desemba, 2011 ambayo ilisababisha mafuriko na hivyo kuleta adha kubwa kwa wananchi vikiwemo vifo na uharibifu wa mali na miundombinu. Aidha, nawapa pole ndugu na jamaa wa marehemu waliopoteza maisha yao kutokana na tukio hilo. Namwomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi. Amina.
3. Mheshimiwa Spika, napenda kuishukuru kwa dhati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama chini ya Mwenyekiti wake, Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa, Mbunge wa Monduli kwa kuyachambua Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.  Naishukuru pia Kamati hiyo kwa ushauri wao wenye tija katika kuboresha  utendaji  kazi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
4. Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii pia kuwapongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na Waziri wa Fedha kwa hotuba zao walizozitoa mapema katika mkutano huu wa Bunge ambazo  zimetoa mwelekeo wa bajeti ya Serikali  na hali ya uchumi kwa jumla kwa mwaka wa fedha 2012/2013.
5. Mheshimiwa Spika,  majukumu ya msingi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ni kulinda usalama wa raia na mali zao, kuhifadhi na kuwarekebisha wafungwa, kutekeleza Programu ya Huduma  kwa Jamii, kudhibiti uingiaji na utokaji nchini wa raia na wageni, kutoa huduma za zimamoto na uokoaji, kuwahudumia wakimbizi waliopo nchini, na kutoa vitambulisho vya Taifa. Majukumu haya yanatekelezwa kupitia Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Idara ya Huduma kwa Jamii, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Idara ya Wakimbizi na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa.

II.  HALI YA USALAMA NCHINI 

6. Mheshimiwa Spika, amani, utulivu na usalama  wa wananchi ni mihimili mikuu ya maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Kuongezeka kwa matishio ya uhalifu na kupungua kwa hali ya usalama wa raia husababisha kuathirika kwa mfumo mzima wa ustawi wa  nchi katika nyanja mbalimbali na kwa ujumla hudhoofisha nguvu na jitihada za wananchi katika kujiletea maendeleo.
7. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2011 makosa ya jinai makubwa na madogo 564,716 yaliripotiwa katika vituo vya Polisi ikilinganishwa na makosa  543,358  yaliyoripotiwa katika kipindi kama hiki mwaka 2010. Idadi ya makosa imeongezeka kwa asilimia 3.9. Kutendeka kwa makosa haya kwa kiwango kikubwa kunachangiwa na mmomonyoko wa maadili, tamaa ya utajiri wa haraka haraka, imani za kishirikina, tamaa ya maisha na umaskini. Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wadau limeendelea kubuni na kutekeleza mikakati ya aina mbalimbali ya kukabiliana na uhalifu nchini ukiwemo mkakati wa Ulinzi Shirikishi.
8. Mheshimiwa Spika, yapo baadhi ya maeneo hapa nchini ambayo kutokana na sababu zikiwemo za kijamii, kiuchumi na kisiasa yalikithiri kwa vitendo vya uhalifu vilivyosababisha uvunjifu wa amani na kuleta hofu miongoni mwa wananchi. Hali ya aina hii ilipojitokeza, Jeshi la Polisi lililazimika kuongeza nguvu na kuendesha operesheni kwenye maeneo husika. Katika mwaka 2011/2012, operesheni maalum ziliendeshwa katika Bahari ya Hindi kutokana na tishio la uharamia, kwenye majimbo ya Arumeru Mashariki na Igunga yaliyokuwa na uchaguzi mdogo wa nafasi ya ubunge, Mbeya kutokana na vurugu za wafanyabiashara wadogo wadogo, Rufiji kutokana na vurugu za wakulima na wafugaji, Tandahimba kufuatia vurugu za wananchi kudai malipo ya korosho awamu ya pili, Zanzibar kufuatia vurugu za wafuasi wa kundi la UAMSHO, Songea kutokana na vurugu zilizosababishwa na uvumi wa kuuawa kwa waendesha pikipiki kwa imani za kishirikina na katika maeneo mengine.
9. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Jeshi la Polisi litaendelea kujiimarisha katika kufanya kazi za operesheni kwa mtindo wa Vikosi  Shirikishi ili kukabiliana na matishio ya uhalifu yanayoikabili nchi yetu hususan ugaidi, uharamia, uhalifu unaovuka mipaka kama vile biashara ya dawa za kulevya, biashara haramu ya kusafirisha binadamu, uhamiaji haramu, wizi kwa kutumia mitandao ya TEHAMA, bidhaa bandia, biashara haramu ya silaha, uchafuzi wa mazingira na ongezeko la vifo na majeruhi kutokana na ajali za barabarani.
10. Mheshimiwa Spika, kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma ya usalama wa raia na mali zao katika maeneo ya uwekezaji, mwezi Mei, 2012 Jeshi la Polisi ngazi ya Makao Makuu limeanzisha vitengo maalum vya kuratibu usalama katika migodi, ulinzi wa mazingira na usalama wa watalii. Kabla ya kuanzishwa kwa vitengo hivi huduma ya usalama katika migodi, maeneo ya utalii na ulinzi wa mazingira ilikuwa ikitolewa kwa kutumia vikosi vya Jeshi la Polisi vilivyopo katika ngazi ya Mkoa na Wilaya. Kazi ya awali iliyofanywa  na vitengo hivi ni kuandaa muundo wa vikosi vitakavyoanzishwa na mikakati ya kuimarisha usalama wa maeneo hayo kwa kushirikiana na wadau wa sekta husika.  Aidha, makubaliano maalum ya kutoa huduma ya ulinzi katika benki za biashara na katika migodi  ikiwemo inayomilikiwa na Kampuni ya Barrick Gold na Williamson Diamond yaliendelea kutekelezwa. Katika mwaka 2012/2013, Jeshi la Polisi litaendelea kuimarisha uwezo wake wa utendaji kwa kuongeza weledi wa watendaji na vitendea kazi hususan pikipiki kwa ajili ya kuongeza wigo wa doria za Jeshi la Polisi hadi ngazi ya Kata/Shehia.

11. Mheshimiwa Spika, vyanzo vikubwa vya ajali za barabarani hapa nchini ni pamoja na:-
i) Uzembe wa madereva, ukiwemo uendeshaji wa kasi usiozingatia sheria na alama za barabarani
ii) Ubovu wa magari
iii) Ubovu na ufinyu wa barabara zilizopo
iv) Usimamizi usioridhisha wa usalama barabarani
v) Ukosefu wa alama za barabarani na
vi) Ongezeko la vyombo vya usafiri na usafirishaji

12. Mheshimiwa Spika, ajali za barabarani bado zinaendelea kuwaangamiza wananchi. Ajali hizi zimeendelea kupoteza maisha na kusababisha ulemavu wa kudumu na upotevu wa mali za wananchi. Takwimu zinaonyesha kuwa katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2011 ajali za barabarani 24,078 ziliripotiwa katika vituo vya Polisi ambapo watu 4,013 walipoteza maisha na wengine 20,917 kujeruhiwa ikilinganishwa na ajali 24,926 zilizoripotiwa katika kipindi cha Januari hadi  Desemba, 2010 ambapo watu 3,687 walifariki na wengine 22,064 kujeruhiwa. Idadi ya ajali ilipungua kwa asilimia 3.4. Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wadau wengine kama SUMATRA, TBS, TANROADS na Shule za Udereva limeendelea kuchukua  hatua zifuatazo ili kudhibiti ajali za barabarani:-
i) Kutoa elimu ya kuzingatia sheria za usalama barabarani kwa watumiaji wa barabara
ii) Kuhuisha viwango vya  adhabu kwa makosa ya usalama barabarani
iii) Kushirikisha wadau wa usalama barabarani katika kuhuisha mikakati ya kupunguza ajali za barabarani
iv) Kuendeleza doria za masafa mafupi na marefu katika kusimamia sheria za usalama barabarani
v) Kufanya ukaguzi wa magari
vi) Kutumia kamera za kutambua madereva wanaotumia mwendo kasi bila kuzingatia alama za usalama barabarani
vii) Kusimamia zoezi la utoaji wa leseni mpya
viii) Kushirikisha jamii ili kupata taarifa za madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani
ix) Wamiliki wa Mabasi kutakiwa kubandika kwenye Mabasi yao namba za simu za viongozi wa Polisi Usalama Barabarani

III. TAARIFA YA UTEKELEZAJI  WA MALENGO YA ILANI YA UCHAGUZI YA CCM YA MWAKA 2010 KATIKA KIPINDI CHA 2011/2012

13. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ina malengo 10 ya kutekeleza yanayotokana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010. Taarifa ya utekelezaji wa malengo hayo kwa mwaka 2011/2012 ni kama ifuatavyo:-
14. Mheshimiwa Spika, lengo la kwanza ni kuendeleza mapambano dhidi ya biashara ya dawa za kulevya. Katika kipindi cha Julai 2011  hadi Aprili, 2012 Jeshi la Polisi liliwahamasisha na  kushirikiana na wananchi katika Ulinzi Shirikishi ili kudhibiti uhalifu ukiwemo uingizaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya katika maeneo yao. Ushirikiano wa wananchi na vyombo vingine vya dola uliliwezesha Jeshi la Polisi kukamata watuhumiwa 10,384 wakiwa na jumla ya kilo 397.984 za dawa za kulevya za viwandani aina ya Cocaine kilo 140.547, Heroine kilo 257.437, Mandrax gramu 5 na kilo 63,480.738 za dawa za kulevya za mashambani. Dawa za kulevya za mashambani zilizokamatwa ni bhangi kilo 50,548.41 na mirungi kilo 12,932.328. Aidha, ekari 235 za mashamba ya bhangi ziliteketezwa katika Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya.
15. Mheshimiwa Spika, maeneo yaliyotambuliwa kuingiza nchini dawa za kulevya ni vituo vya mipakani na nchi jirani, Viwanja vya Ndege, bandarini na vituo vya Mabasi yaingiayo na kutoka nchini. Maeneo ya usambazaji na utumiaji ni yale ambayo yana mkusanyiko wa watu wasiokuwa na ajira maalum maarufu kama 
“ vijiwe”. Jeshi la Polisi litaendelea kubaini mtandao wa wahalifu wa ndani na nje ya nchi unaojihusisha na uingizaji na usambazaji wa dawa za kulevya nchini, kushirikiana na Shirika la Polisi la Kimataifa (INTERPOL) kupata taarifa za kiintelijensia kuhusu wasafirishaji wa dawa za kulevya na kukiimarisha Kikosi Kazi cha Kitaifa cha Vyombo vya Ulinzi na Usalama cha kupambana na biashara ya dawa za kulevya kwa kukiongezea rasilimali watu pamoja na vitendea kazi.
16. Mheshimiwa Spika, lengo la pili ni kupunguza msongamano wa wafungwa na mahabusu katika Magereza. Tatizo la msongamano wa wafungwa na mahabusu bado ni kubwa licha ya hatua mbalimbali zinazochukuliwa katika kukabiliana nalo. Tarehe 1 Aprili, 2012 idadi ya wafungwa na mahabusu waliokuwepo Magerezani ilifikia 37,676. Wafungwa walikuwa 18,068 na mahabusu 19,608.
17. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2011 hadi Aprili, 2012 wafungwa  142 waliachiliwa huru kwa utaratibu wa Parole. Jumla ya wafungwa 693 walikuwa wanatumikia kifungo cha nje kwa kutumia kanuni za kifungo cha nje za mwaka 1968. Vile vile wafungwa 1,080 waliachiliwa na Mahakama ili kutumikia kifungo cha nje chini ya Sheria ya Huduma kwa Jamii na  wafungwa 3,803 walifaidika na msamaha wa Rais uliotolewa tarehe 9 Desemba, 2011 wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru na wafungwa 2,973  waliachiliwa  tarehe 26 Aprili, 2012 wakati wa sherehe za kuadhimisha  miaka 48 ya Muungano.  
18. Mheshimiwa Spika, hatua zingine zinazochukuliwa ili kupunguza msongamano ni kutoa elimu kwa jamii kuhusu haki ya dhamana kwa watuhumiwa, Wakuu wa Magereza wa Mikoa kuwasilisha kwenye Kamati za Kusukuma Mashauri orodha ya mahabusu ambao kesi zao zimechukua muda mrefu kabla ya kukamilika, Jeshi la Magereza kuifahamisha Mahakama Kuu kila mwezi idadi ya mahabusu waliokaa gerezani zaidi ya siku 60, upanuzi, ukarabati na ujenzi wa mabweni ya wafungwa na kuundwa kwa  Kikosi Kazi chini ya uenyekiti wa Mkurugenzi wa Mashtaka ambapo wajumbe wengine ni Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza na Mahakama ili kushughulikia tatizo la msongamano Magerezani na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa.
19. Mheshimiwa Spika, lengo la tatu ni kuimarisha na kuboresha mfumo wa upelelezi wa makosa ya jinai ili kurahisisha uendelezaji wa kesi mahakamani.  Kati ya Julai, 2011 hadi Aprili, 2012 Jeshi la Polisi limetoa mafunzo ya Intelijensia na mbinu za kisasa za upelelezi kwa wapelelezi 511 na limepata vifaa vya kisasa kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kisayansi (forensic) katika Maabara iliyopo Makao Makuu ya Polisi. Aidha, mchakato wa kuikabidhi Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kazi za kuendesha mashtaka Mahakamani umekamilika katika Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya katika  Mikoa 22 ya Tanzania Bara na Mikoa mitano ya Zanzibar. Waendesha Mashtaka wa Polisi 120 waliokuwa wanafanya kazi za kuendesha mashtaka Mahakamani wamehamishwa na wamepangiwa kufanya kazi za upelelezi katika Mikoa mbalimbali nchini.
20. Mheshimiwa Spika, lengo la nne ni kuanzisha mpango wa kuwapatia askari nyumba bora za kuishi. Tathmini iliyofanywa na Jeshi la Polisi inaonyesha kwamba ili askari wote waweze kuishi kambini, zinahitajika kujengwa nyumba mpya zipatazo 32,114 katika Mikoa ya Kipolisi 33 ikiwemo Mikoa mipya ya Katavi, Njombe, Geita na Simiyu. Katika mwaka 2011/2012, Jeshi la Polisi lilikamilisha ujenzi wa nyumba 30 za ghorofa katika Kambi ya Polisi Barabara ya Kilwa na kukamilisha ujenzi wa nyumba nane eneo la Uwanja wa Ndege Mkoani Arusha ambapo jumla ya askari 128 pamoja na familia zao walipata makazi katika nyumba hizo. Aidha, ujenzi uliendelea wa nyumba sita za ghorofa Mkoani Mwanza, nyumba sita za ghorofa Mkoani Mara,  nyumba tatu za ghorofa Mkoani Kagera na nyumba nane Wilaya ya Ludewa. Ujenzi wa nyumba hizi utakapokamilika jumla ya askari 74 na familia zao watapatiwa makazi.  Kwa upande wa Jeshi la Magereza ujenzi wa nyumba tatu umekamilika Gereza Singida na ujenzi wa nyumba mbili uliendelea  Gereza Chato, nyumba moja Gereza Ngara na nyumba moja Gereza Magu. Aidha, Idara ya Uhamiaji ilikamilisha ujenzi wa nyumba moja katika Kituo cha Rusumo na kukamilisha ukarabati wa nyumba nne Kibaha na nyumba nne Sirari. Ujenzi na ukarabati wa nyumba unafanyika kwa kadri uwezo wa fedha unavyoruhusu.
21. Mheshimiwa Spika, lengo la tano ni kujenga vituo vya Polisi katika kila Tarafa nchini.  Hivi sasa Jeshi la Polisi lina jumla ya vituo 417 vya daraja A, B na C  nchi nzima. Kwa kutumia  vigezo vya Amri za Kudumu za Jeshi la Polisi, vituo vya Wilaya ambavyo ni daraja “A” vilivyopo ni 162, vituo vya Tarafa ambavyo ni daraja “B” vipo 91 na vituo vya Kata daraja “C” vipo 164. Ni azma ya Serikali kujenga vituo katika Tarafa 526 za Tanzania Bara na Majimbo 50 ya Zanzibar na hatimaye kufikisha vituo katika Kata 3,876 zilizopo nchini.  Kutokana na ufinyu wa bajeti, badala ya kujenga vituo vipya katika Tarafa Jeshi la Polisi limewapanga Wakaguzi 526 kuwa Wasaidizi wa Wakuu wa Polisi wa Wilaya wanaoshirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika kuzuia uhalifu katika Tarafa hizo.
22. Mheshimiwa Spika, lengo la sita ni kuwapatia wananchi mafunzo ya Ulinzi Shirikishi ili wawe tayari kujilinda katika maeneo yao. Lengo la Ulinzi Shirikishi ni kuiwezesha jamii kuishi maisha ya amani na utulivu katika maeneo yake. Serikali inazingatia ukweli kwamba kila raia anawajibika kwa ulinzi wake binafsi, familia yake, jirani yake na jamii kwa ujumla tofauti na fikra potofu za baadhi ya watu kwamba usalama wa raia na mali zao ni jukumu la Jeshi la Polisi na viongozi wa Serikali pekee. 
23. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Jeshi la Polisi liliendelea kutoa mafunzo ya Ulinzi Shirikishi na kuanzisha mradi mpya wa Utii wa Sheria Bila Shuruti. Aidha, kupitia mikutano ya hadhara na vyombo vya habari, Jeshi la Polisi liliendelea kutoa mafunzo na kuhamasisha utekelezaji wa miradi ya Ulinzi Jirani, Usalama Wetu Kwanza, Ukamataji Salama, Michezo na Vijana na Miji Salama. Wizara inaipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa uamuzi wake wa kuanza kufundisha somo la Usalama Wetu Kwanza kwa kuanzia katika shule 10 za msingi za majaribio.  Uamuzi huu ni wa kizalendo na utawawezesha watoto kujenga  uzalendo wa kuilinda nchi yao dhidi ya maadui na hata kuzuia uhalifu kutendeka kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu katika vituo vya Polisi. Hadi sasa jumla ya vikundi 3,876 vya Ulinzi Shirikishi vimeanzishwa na Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Wakuu wa Polisi wa Wilaya wanaendelea kuwapanga askari katika Kata na Shehia kwa lengo la kushirikiana kwa  karibu zaidi na wananchi katika kutatua kero za uhalifu na wahalifu katika maeneo yao.
24. Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio yaliyopatikana kutokana na wananchi kuhamasika na  Ulinzi Shirikishi, Jeshi la Polisi litaendelea kujenga uelewa wa wananchi kuhusu ushiriki wao katika kutekeleza kwa vitendo falsafa ya Polisi Jamii, kuimarisha uwezo wa wananchi katika kuzuia na kutanzua uhalifu, kujenga uwezo wa askari Polisi kushirikiana na jamii katika kazi ya kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu pamoja na kuongeza hatua za kukamilisha Sera ya Usalama wa Raia itakayorasimisha Polisi Jamii kuwa mkakati wa kitaifa wa kupambana na uhalifu.
25. Mheshimiwa Spika, lengo la saba ni kuimarisha mafunzo ya askari wa vyombo vya ulinzi na usalama. Katika kipindi cha Julai 2011 hadi Aprili 2012 askari 15,728 kutoka Polisi, Magereza, Zimamoto na Uokoaji na Uhamiaji wamepatiwa mafunzo katika fani mbalimbali ambapo Polisi ni 13,389, Magereza 1,764, Zimamoto na Uokoaji 60 na Uhamiaji 515. Mwaka 2012/2013, mafunzo yatatolewa kwa jumla ya askari 23,713 ambapo Polisi ni 20,000, Magereza 500, Uhamiaji 600 na Zimamoto na Uokoaji 2,613.
26. Mheshimiwa Spika, lengo  la nane ni kuimarisha uzalishaji wa mbegu bora za kilimo katika maeneo ya Magereza. Katika mwaka 2011/2012, Jeshi la Magereza limelima hekta 1,047.20 za mashamba ya mbegu bora za kilimo  kwa kushirikiana na Wakala wa Mbegu za Kilimo nchini katika Mikoa ya Arusha, Dodoma, Manyara, Lindi, Iringa, Mbeya, Kilimanjaro na Morogoro kwa matarajio ya kuvuna tani 1,500 za mbegu bora. Aidha,  Jeshi la Magereza kwa kushirikiana na  Kampuni ya Highland Seed Growers Ltd na TANSEED limelima hekta 990.2 za mashamba ya mbegu bora za kilimo katika Mikoa ya Rukwa, Ruvuma na Kigoma na  matarajio ni kuvuna tani 1,500 za mbegu bora. Lengo la mwaka wa fedha 2012/2013 ni kulima hekta 1,094 za mazao mbalimbali kwa matarajio ya kuvuna tani 4,923.
27. Mheshimiwa Spika, lengo la tisa ni kutoa vitambulisho vya Taifa. Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa imekamilisha utengenezaji wa kituo cha muda cha kuingizia kumbukumbu na kituo cha muda cha utunzaji na utengenezaji wa mfumo wa utambuzi na usajili  wa watu na hatimaye kutoa vitambulisho. Aidha, michoro kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za utambuzi na usajili wa watu za Wilaya Tanzania Bara na Zanzibar imekamilika ikiwa ni pamoja na michoro ya kituo kikuu cha kudumu cha utunzaji wa taarifa na uchapishaji. Hatua inayofuata ni ujenzi wa ofisi katika Wilaya 40 katika awamu ya kwanza.
28. Mheshimiwa Spika, zoezi la majaribio hatua ya kwanza ambalo limehusisha watumishi wa Serikali Mkoa wa Dar es Salaam na Zanzibar wapatao 290,000 na wananchi wa Wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro wapatao 220,000 limekamilika. Zoezi hili limehusisha ujazaji wa fomu, uhakiki wa taarifa na uingizaji wa taarifa katika mfumo wa kompyuta. Hatua itakayofuata ni uchukuaji wa alama za vidole, picha na saini kwa lengo la kuingiza katika mfumo na hatimaye kutoa vitambulisho.
29. Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa iliyo mbele yetu ni upatikanaji wa rasilimali fedha, vifaa na watu ili zoezi hili likamilike katika kipindi cha miaka miwili kwa lengo la kusaidia vitambulisho kutumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Mfumo wa utambuzi na usajli wa watu utakapokamilika utasaidia katika kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato, kupunguza gharama za uendeshaji wa mifumo mingine mikubwa ya Serikali na hivyo kuipunguzia mzigo Serikali. Aidha, wananchi watapata fursa ya kutambulika na kufaidika na fursa mbalimbali za kijamii mathalani mikopo na huduma nyinginezo. Mfumo huu vile vile utasaidia kudhibiti uhalifu na hivyo kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi hasa baada ya kuridhia makubaliano ya kuondoa vizuizi vya mipaka katika ukanda wa Afrika Mashariki.
30. Mheshimiwa Spika, lengo la kumi ni kuimarisha vikosi vya Zimamoto na Uokoaji vyenye wataalam na zana za kisasa ili kukabiliana na majanga ya moto.  Hatua mahsusi zimechukuliwa za kuwaunganisha  askari wa  Zimamoto na Uokoaji  kutoka katika Halmashauri na  Viwanja vya Ndege kwa upande wa Tanzania Bara kuwajibika chini ya komandi moja kuanzia mwezi Julai 2012.  Askari 60 wamepatiwa mafunzo ya uongozi katika Chuo cha Magereza Ukonga Dar es Salaam.
31. Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine, jumla ya magari makubwa manne ya kuzimia moto yamepatikana kwa ajili ya Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Viwanja vya Ndege. Magari hayo yatatumika katika Viwanja vya Ndege vya Dar es Salaam, Mwanza na Arusha.  Ili kusogeza huduma ya zimamoto na uokoaji karibu zaidi na wananchi, katika mwaka 2012/2013 Jeshi la Zimamoto na Uokoaji  linatarajia kufungua vituo vipya vya Zimamoto na Uokoaji katika Jiji la Dar es Salaam katika maeneo ya Tegeta, Mwenge, Kigamboni, Mbagala, Tabata, Mbezi Luisi na Gongo la Mboto. 

IV. MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2011/2012 NA MALENGO YA MWAKA 2012/2013

32. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ilipangiwa kukusanya mapato ya shilingi 72,751,137,075. Hadi tarehe 30 Aprili, 2012 Wizara ilikuwa imekusanya shilingi 70,775,666,564 sawa na asilimia 97.3 ya lengo la mwaka. Katika mwaka 2012/2013 Wizara ina lengo la kukusanya mapato ya shilingi 96,652,212,000. Nguvu zaidi zitaelekezwa katika kuziba mianya ya uvujaji wa mapato hususan katika kuimarisha na kuboresha matumizi ya benki kwa ajili ya kufanya malipo ya huduma zitolewazo na taasisi za Wizara.
33. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/2012, Wizara iliidhinishiwa kutumia shilingi 482,394,883,000 kwa ajili ya bajeti ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo. Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Aprili 2012, jumla ya shilingi 382,944,359,941 zilikuwa zimetumika sawa na asilimia  79.4 ya bajeti. Jumla ya shilingi 211,906,987,554 zimetumika kulipia mishahara, Matumizi Mengineyo shilingi 159,577,911,122 na fedha za maendeleo ni shilingi 11,459,461,265. Katika mwaka 2012/2013, Wizara imetengewa shilingi 555,540,268,000  kwa ajili ya bajeti ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo.

JESHI LA POLISI

34. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Jeshi la Polisi liliendelea kutekeleza jukumu lake la msingi la kuhakikisha nchi inakuwa na usalama, amani na utulivu. Jeshi la Polisi  limefanikiwa  kwa kiasi kikubwa katika kuwalinda wananchi na mali zao, kusimamia utii wa sheria za nchi, kuzuia makosa, kupeleleza makosa ya jinai yaliyoripotiwa katika vituo vya Polisi, kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani watuhumiwa wa makosa ya jinai na makosa ya usalama barabarani.
35. Mheshimiwa Spika, kwa kutumia rasilimali watu, fedha na vitendea kazi vilivyopo, Jeshi la Polisi limeendelea kuhuisha mifumo ya kuzuia uhalifu na kupeleleza makosa ya jinai, kuongeza matumizi ya TEHAMA katika kazi za Polisi, kuimarisha mifumo ya menejimenti na maslahi ya askari, kupunguza tatizo la uhaba na uchakavu wa kambi na vituo vya Polisi, kupunguza tatizo la uhaba na uchakavu wa vitendea kazi hususan magari na pikipiki, kuhamasisha wananchi na wadau mbalimbali kuhusu Ulinzi Shirikishi na kuimarisha ukaguzi, usimamizi na tathmini ya malengo, shahaba na kazi zinazotakiwa kufanywa na Jeshi la Polisi kwa mujibu wa sheria.

Udhibiti wa Silaha za Kiraia
36.  Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi liliendelea kuweka alama maalum katika silaha zinazomilikiwa na taasisi za Serikali, makampuni na raia ambapo katika kipindi cha Julai, 2011 hadi Aprili, 2012, jumla ya silaha 15,883 zimewekewa alama hiyo. Hivyo kufanya jumla ya silaha 37,604 zilizowekewa alama hiyo tangu zoezi hili lilipoanza mwaka 2009. Zoezi hili limefanyika katika Mikoa ya Dodoma, Tanga, Dar es Salaam, Morogoro, Tabora,  Manyara, Singida, Mwanza, Shinyanga, Kagera na Mara. Zoezi la kuweka silaha alama maalum litaendelea katika mwaka 2012/2013 na kuanza mchakato wa kutunga sheria mpya ya kusimamia umiliki wa silaha. 
37. Mheshimiwa Spika, kuzagaa kwa silaha ndogondogo ni tishio kwa usalama wa raia na mali zao. Jeshi la Polisi limeendelea kukabiliana na tatizo la kuzagaa kwa silaha hizo ambapo katika misako na operesheni maalum zilizofanyika katika mwaka 2011/2012, jumla ya silaha ndogondogo 503 zilikamatwa zikiwa zinamilikiwa kinyume cha sheria. Aidha, katika kutekeleza agizo lililotolewa na Inspekta Jenerali wa Polisi mwezi Agosti, 2011 la kusalimisha silaha kwa hiari, jumla ya silaha  59 zilisalimishwa. 

Jukwaa la Haki Jinai
38. Mheshimiwa Spika, ushirikiano wa kiutendaji kati ya Jeshi la Polisi na taasisi nyingine kuu zinazounda Jukwaa la Haki Jinai ambazo ni Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Jeshi la Magereza na Mahakama umeendelea kuimarika ambapo Jeshi la Polisi limejikita katika eneo  la kuongeza ufanisi katika upelelezi wa makosa ya jinai. Ili kuendeleza azma hiyo, katika mwaka 2012/2013 Jeshi la Polisi litatumia vyuo vyake vya Dar es Salaam na Kidatu kutoa mafunzo ya ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa za kiintelijensia na mbinu za kisasa za upelelezi kwa Maafisa, Wakaguzi na askari wapatao 1,000.

Ushughulikiaji  wa Malalamiko
39. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi limeendelea kushughulikia malalamiko ya wananchi dhidi ya watendaji wake wanaojihusisha na vitendo vya kuomba na kupokea rushwa.  Katika mwaka 2011/2012, jumla ya malalamiko 625 ya wananchi dhidi ya kero ya rushwa yalishughulikiwa. Askari 68 walifukuzwa kazi, 9 kesi zao zinaendelea katika Mahakama za jinai na wengine 15 uchunguzi unaendelea. Aidha, Jeshi la Polisi limeanzisha utaratibu wa kuwazawadia askari wanaokataa kupokea rushwa katika utendaji wao wa kazi. 

Ushirikiano wa Polisi Kikanda na Kimataifa
40. Mheshimiwa Spika,  Jeshi la Polisi liliendelea kushirikiana na Mashirika ya Polisi ya kikanda na kimataifa katika kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu hapa nchini, ukanda wa Afrika Mashariki, Kusini mwa Afrika, Barani Afrika na dunia kwa ujumla. Mashirika hayo ni pamoja na Shirikisho la Polisi la Kimataifa – Interpol, Shirikisho la Polisi la nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika – EAPCCO na Shirikisho la Polisi la nchi za Kusini mwa Afrika – SARPCCO. Ushirikiano uliopo umejielekeza katika ubadilishanaji wa taarifa za uhalifu na wahalifu, mafunzo, operesheni za pamoja na mikutano ya pamoja ya Wakuu wa Majeshi ya Polisi na Wakuu wa Upelelezi wa nchi wanachama.

41. Mheshimiwa Spika, mwezi Oktoba 2011 ilifanyika operesheni maalum iliyojulikana kama Operesheni Kwacha. Operesheni hii ililenga katika kuwasaka na kuwakamata wahalifu wa baadhi ya makosa yanayopewa kipaumbele katika kudhibitiwa na Shirikisho la Majeshi ya Polisi Kimataifa na Kikanda ambayo ni wizi wa magari, usafirishaji wa dawa za kulevya, usafirishaji haramu wa silaha, usafirishaji haramu wa binadamu na wahamiaji haramu. Katika operesheni hiyo jumla ya kilo 9,789 za dawa za kulevya za mashambani na viwandani na magari 19 yaliyoibwa kutoka Japan, Uingereza, Malaysia na Afrika Kusini yalikamatwa. Katika kuendeleza ushirikiano huu mwaka 2012/2013, Jeshi la Polisi litashiriki katika mafunzo, ubadilishanaji wa taarifa za kiintelijensia, operesheni za kikanda na litakuwa mwenyeji wa mkutano Mkuu wa Shirikisho la Wakuu wa Polisi wa  nchi za Kusini mwa Afrika kwa kuwa hivi sasa Inspekta Jenerali wa Polisi  Tanzania ndiye Mwenyekiti mteule wa Shirikisho hilo.
Maslahi ya Askari
42. Mheshimiwa Spika, hatua mbalimbali zimechukuliwa ili kuboresha maslahi ya askari. Hatua hizo ni pamoja na kuanza  kutumika kwa kanuni za fidia kwa askari wanaoumia au kuuawa wakiwa kazini. Katika mwaka 2011/2012, jumla ya askari 62 waliumia na 16 waliuawa wakiwa kazini. Askari hao au wategemezi wao wanastahili  kulipwa fidia kati ya shilingi milioni moja na shilingi milioni 15 kwa walioumia na wategemezi wao kulipwa shilingi milioni 15 kwa askari aliyeuawa wakati akiwa kazini. Pia katika kuongeza morali wa askari na kumpunguzia askari ukali wa maisha, Serikali imeongeza posho ya chakula  ya askari kutoka shilingi 100,000 kwa mwezi hadi shilingi 150,000. Kiwango hiki kitatumika  pia kwa Jeshi la Magereza, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Idara ya Uhamiaji.

Ajira
43. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Jeshi la Polisi limeajiri askari wapya 3,264. Katika mwaka 2012/2013, Jeshi la Polisi linatarajia kuajiri askari wapya 3,000. Sehemu ya waajiriwa itapatikana  kutoka katika mashule na vyuo vya elimu ya juu na idadi nyingine kutoka vijana wa JKT. Utaratibu huu unalenga kuwa na askari wenye sifa stahiki na waaminifu kwa kazi ya Polisi.

Ujenzi wa Ofisi na Vituo vya Polisi
44. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, hatua mbalimbali za ujenzi zimefikiwa katika ujenzi wa  Ofisi za Makamanda wa Polisi wa Mikoa kama ifuatavyo:- Kusini Pemba (asilimia 100), Mara  na Manyara ujenzi upo hatua ya msingi na vituo vya Polisi vya daraja “B” vya Ludewa ( asilimia 60), na Kwimba 
( asilimia 98) na vituo vya daraja “C” vya Horohoro ( asilimia 100) na Mtambaswala ( asilimia 85). 

Mapambano Dhidi ya UKIMWI
45. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, uhamasishaji  wa askari Polisi wote kutekeleza Sera ya Ukimwi mahali pa kazi ulifanyika nchi nzima kwa lengo la kupunguza maambukizi mapya ya VVU na ukimwi. Matokeo yake ni kwamba maambukizi ndani ya Jeshi la Polisi yamepungua kutoka asilimia 5 mwaka 2010/2011 hadi asilimia 4.8 mwaka 2011/2012.

JESHI LA MAGEREZA

Usafirishaji wa Mahabusu Kwenda Mahakamani na Kurudi Magerezani
46. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza linatekeleza jukumu la kuwasindikiza mahabusu kwenda Mahakamani na kurudi Gerezani katika Mkoa wa Dar es Salaam na Wilaya mbili za Mkoa wa Pwani za Kisarawe na Mkuranga.  Jukumu hili kwa kiasi kikubwa lilikuwa linapata fedha kutoka Programu ya Maboresho ya Sekta ya Sheria ambapo vitendea kazi kama vile magari ya kubebea mahabusu yalinunuliwa kupitia fedha za kapu la programu hiyo.  Hivi sasa, ufadhili wa programu hii umeshuka kwa kiwango kikubwa na kubaki na eneo lenye fedha kidogo la mafunzo. Kutokana na hali hiyo, jukumu hili imeshindikana kutekelezwa katika Wilaya zilizobakia za Mkoa wa Pwani na kuanza katika Mkoa wa Arusha kama ilivyokuwa imetarajiwa. 

Programu za Urekebishaji wa Wafungwa
47. Mheshimiwa Spika, hivi sasa mradi wa uendeshaji wa shughuli za wafungwa kwa kutumia mtandao wa kompyuta unafanya kazi katika Magereza ya Mkoa wa Dar es Salaam. Katika mwaka 2012/2013, Jeshi la Magereza linatarajia kuanza awamu ya pili ya utekelezaji katika Magereza ya Mkoa wa Dodoma, Mwanza na Tabora kwa kusimika mtandao wa mawasiliano ya kompyuta.

Ajira
48. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, jumla ya askari 684 waliajiriwa na  katika mwaka 2012/2013, Jeshi la Magereza linatarajia kuajiri askari 1,800.

Uimarishaji wa Magereza Yenye Ulinzi Mkali 
49. Mheshimiwa Spika, ukarabati wa majengo na miundombinu ya Magereza umefanyika na unaendelea katika Magereza ya Maweni – Tanga, Karanga – Moshi na Isanga – Dodoma. Katika mwaka wa fedha wa 2012/2013, ukarabati wa majengo na miundombinu utaendelea katika Gereza la Butimba – Mwanza.

Upanuzi, Ukamilishaji, Ukarabati na Ujenzi wa Mabweni ya Wafungwa
50. Mheshimiwa Spika, kazi ya upanuzi na ukarabati wa mabweni ya wafungwa iliendelea katika Gereza la Masasi. Aidha, kazi ya ujenzi iliendelea katika Magereza ya Chato, Utete na Masasi. Katika mwaka wa fedha wa 2012/2013, lengo ni kuendelea kukamilisha ukarabati wa kuta katika Gereza la Kilwa na Ilagala- Kigoma. Pia ukarabati wa mabweni ya wafungwa katika Magereza ya Korogwe na Bukoba utaanza.
Ujenzi wa Ofisi za Wakuu wa Magereza wa Mikoa
51. Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Ofisi za Wakuu wa Magereza katika Mikoa ya Dar es Salaam na Singida umeendelea. Ujenzi wa Ofisi ya Magereza Singida upo katika hatua za mwisho za ukamilishaji.  Katika mwaka wa fedha wa 2012/2013, Jeshi la Magereza litakamilisha ujenzi wa Ofisi ya Singida na kuendelea na ujenzi wa Ofisi ya Dar es Salaam. 

Matumizi ya Nishati Mbadala Magerezani
 52. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana  na changamoto zinazotokana na matumizi  makubwa ya kuni Magerezani na hivyo kuweko na tishio la uharibifu wa mazingira na kuongeza athari za tabianchi, Jeshi la Magereza limeendelea kuchukua hatua za kuanza kutumia gesi asilia, nishati itokanayo na tungamotaka  na makaa ya mawe kama nishati mbadala ya  kupikia chakula cha wafungwa Magerezani. Mfumo wa usambazaji wa gesi asilia na ufungaji wa vyungu husika umekamilika katika Gereza la Keko na matumizi yameshaanza. Matumizi ya nishati itokanayo na tungamotaka katika Gereza la Ukonga, ujenzi wa mfumo umekamilika na kuanza kutumika. Hivi sasa mtambo wake unazalisha asilimia 77 ya mahitaji yote ya nishati inayohitajika katika Gereza hilo. Upo uwezekano wa kuboresha mtambo huu ili uweze kuzalisha gesi zaidi kwa kuongeza malighafi ya kuzalishia gesi hiyo. Makaa ya  mawe yanaendelea kutumika katika Magereza ya Mkoa wa Mbeya.

Ujenzi na Ukarabati wa Nyumba za Askari
53. Mheshimiwa Spika, ujenzi wa nyumba tatu za makazi ya askari umekamilika Gereza la Singida na ujenzi wa jengo la ghorofa uliendelea Mkoani Iringa na pia ujenzi wa nyumba moja Chato, moja Ngara na moja Magu uliendelea. Katika mwaka wa fedha wa 2012/2013, Jeshi la Magereza litaendelea na ujenzi wa jengo la ghorofa la kuishi askari Mkoani Iringa. 
Uimarishaji wa Mifumo ya Majisafi na Majitaka
54. Mheshimiwa Spika, ukarabati wa miundombinu ya majitaka ulifanyika katika Magereza ya Kasungamile, Ngudu, Isanga na Chuo cha Ukonga. Vile vile mfumo wa majisafi umeboreshwa katika Magereza ya Keko, Ukonga, Maweni, Mbigiri, Handeni na Shinyanga. Katika mwaka wa fedha wa 2012/2013, ukarabati wa mfumo wa majisafi utafanyika Gereza Isupilo- Iringa pamoja na ukarabati wa mfumo wa majitaka katika Gereza Mkwaya – Mbinga.
Shirika la Magereza
55. Mheshimiwa Spika, Shirika la Magereza limeongeza eneo lililolimwa mazao mbalimbali ya chakula  kutoka ekari 5,435.5 msimu   wa 2010/2011 hadi ekari 6,343 msimu wa 2011/2012  kwa matarajio ya kuvuna tani 8,563 za mazao mbalimbali. Ongezeko hili la eneo lililolimwa linatarajiwa kutoa ziada ya tani 1,224 ya mazao mbalimbali ikilinganishwa na msimu uliopita wa 2010/2011. Aidha, Shirika  limeongeza ubora wa mifugo kwa kutumia uzalishaji wa ndama kwa njia ya uhamilishaji (AI)  na pia limeweza kutengeneza samani bora zikiwemo za watu binafsi, mashirika, idara na taasisi za Serikali. Matarajio ya Shirika ni kutumia ipasavyo soko la ndani la samani za ofisi, bidhaa za ngozi na shughuli za ujenzi ambalo linaendelea kupanuka.

Kilimo cha Umwagiliaji
56. Mheshimiwa Spika, ujenzi wa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji katika Magereza ya Idete – Morogoro na Kitengule – Kagera upo katika hatua mbalimbali za kufanya tathmini ya mazingira na usanifu wa michoro. Jeshi la Magereza litaendelea na miradi hiyo katika mwaka wa fedha wa 2012/2013.

HUDUMA KWA JAMII
57. Mheshimiwa Spika, Programu ya Huduma kwa Jamii ilianza rasmi mwaka 2005 kama njia mojawapo ya adhabu mbadala ya kifungo gerezani.  Programu hii inatekelezwa katika Mikoa 12 ya Tanzania Bara ambayo ni Dar es Salaam, Mwanza, Mtwara, Dodoma, Mbeya, Kilimanjaro, Tanga, Arusha, Iringa, Kagera, Mara na Shinyanga. Katika kipindi cha Julai, 2011 hadi Aprili, 2012 jumla ya wafungwa 1,080 wamefaidika na programu hii ambapo wanaume ni 908 na wanawake 172. Wafungwa hao hutumikia vifungo vyao nje ya magereza kwa kufanya kazi bila ya malipo katika taasisi za umma. Changamoto kubwa ya programu hii ni ufinyu wa bajeti unaokwamisha Mikoa mingine kushindwa kunufaika na programu hii. 

IDARA YA UHAMIAJI
58. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2011 hadi Aprili, 2012  jumla ya wageni 794,934 waliingia nchini, ikilinganishwa na wageni 625,308 walioingia nchini katika kipindi kama hiki mwaka jana. Wageni 779,174 walitoka nje ya nchi ikilinganishwa na wageni 664,037 waliotoka nchini katika kipindi kama hiki mwaka  jana. Idadi ya wageni walioingia imeongezeka kwa watu 169,086 sawa na asilimia 27. Kuongezeka kwa idadi hii kunaweza kuelezwa pamoja  na mambo mengine ni kutokana na kuimarika kwa  mazingira ya uwekezaji na hali ya usalama nchini.  
Wageni Waliopatiwa Hati za Ukaazi
59. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2011 hadi Aprili, 2012 wageni 14,781 walipewa hati za ukaazi nchini ikilinganishwa na wageni 12,563 waliopewa hati hizo katika kipindi kama hiki mwaka jana. Idadi ya hati zilizotolewa imeongezeka kwa hati 2,218 sawa na asilimia 17.7. Hali hii ni matokeo ya kuanza kuimarika kwa uchumi duniani na  hatua zinazochukuliwa na Serikali za kuboresha mazingira ya uwekezaji.

Wageni Waliopatiwa Uraia wa Tanzania
60. Mheshimiwa Spika, wageni 18 walipatiwa uraia. Wageni waliopata uraia ni wa kutoka  India (7), Kenya (2), Pakistani (2) na  Somalia (7). Wageni wawili kutoka Pakistani ni wanawake ambao wameolewa na Watanzania na kutoka Somalia ni watoto saba wa Kisomali ambao wazazi wao tayari ni raia wa Tanzania. Aidha, maombi ya wageni 43  kutoka India ( 20), Kenya (6), Rwanda (3), Uingereza (5), Pakistani (2) na Somalia (7) yalikataliwa. Hivi sasa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inaendelea kuandaa Sera ya Uhamiaji na Uraia ili kuweza kudhibiti kiwango cha wageni wanaopewa uraia wa Tanzania.

Watanzania Waliopatiwa Uraia wa Mataifa Mengine
61.  Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2011/2012, Watanzania 34 walipata uraia wa mataifa mengine ya Namibia (3), Uingereza (4), Ujerumani (6), Norway (3), Kenya (5), Botswana (4), Denmark (4), Korea ya Kusini (1), Marekani (1), Afrika Kusini (2) na Cuba (1) hivyo kupoteza haki ya kuwa raia wa Tanzania kwa  mujibu wa Sheria ya Uraia Na. 6 ya mwaka 1995. 
Hati za Kusafiria  Zilizotolewa
62. Mheshimiwa Spika, jumla ya hati za kusafiria 39,586 zimetolewa katika kipindi cha 2011/2012. Kati ya hizo 38,422 ni za kawaida, 895  za Afrika Mashariki, 209 za kibalozi na 60 za kiutumishi, ikilinganishwa na hati za kusafiria  36,818, ambapo 35,546 za kawaida, 813 za Afrika Mashariki, 360 za kibalozi na 99 za kiutumishi zilizotolewa mwaka 2010/2011.  

Misako na Doria
63. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2011 hadi Aprili, 2012 misako na doria iliwezesha kukamatwa kwa  wageni haramu 5,603 ambao walichukuliwa  hatua kwa mujibu wa sheria ikilinganishwa na wageni haramu  3,339 waliokamatwa katika kipindi kama hiki mwaka 2010/2011. Miongoni mwa idadi hiyo wageni haramu 1,376 ni wa kutoka nchi za Somalia na Ethiopia.

Ujenzi na Ukarabati wa Ofisi na Nyumba
64. Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Shinyanga upo katika hatua za mwisho na ujenzi wa Ofisi za Uhamiaji katika Mikoa ya Ruvuma, Morogoro na Manyara unaendelea. Aidha, upanuzi wa Afisi Kuu ya Uhamiaji Zanzibar na ujenzi wa nyumba moja katika Kituo cha Rusumo na ukarabati wa nyumba 4 katika Kituo cha Sirari na 4 Kibaha umekamilika. Wakandarasi wa kukarabati nyumba za watumishi katika Vituo vya Horohoro – Tanga, Igoma – Mwanza na Chuo cha Uhamiaji Kikanda, Moshi wamepatikana na taratibu za mikataba zinakamilishwa. 

65. Mheshimiwa Spika, lengo la mwaka 2012/2013, ni kuendeleza ujenzi  wa Ofisi za Uhamiaji katika Mikoa ya Morogoro, Manyara na Ruvuma,  kuanza ujenzi  wa Ofisi za Uhamiaji katika Mikoa ya Pwani na Singida na  kufanya ukarabati wa nyumba za watumishi Mkoani Dodoma na katika Vituo vya Uhamiaji vya Borogonja na Tunduma.

Ajira na Mafunzo
66. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, askari 52 wameajiriwa ambao watapatiwa mafunzo katika mwaka wa fedha 2012/2013 na watumishi 515 wamepatiwa mafunzo katika fani mbalimbali. Katika mwaka 2012/2013, mafunzo yatatolewa pia kwa watumishi 600.

Ununuzi wa Vyombo vya Usafiri
67. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, jumla ya magari tisa na pikipiki tano zimenunuliwa ili kuimarisha misako na doria. Katika mwaka 2012/2013 Idara itanunua magari 34, pikipiki 100 na boti tatu.

Mapambano Dhidi ya UKIMWI
68. Mheshimiwa Spika, katika suala la kupambana na maambukizi mapya ya UKIMWI mahali pa kazi Idara imeendelea kuwahudumia waathirika na kutoa elimu kwa askari na familia zao katika Mikoa ya Kagera, Mwanza na Mtwara sambamba na zoezi la kupima afya ambapo watumishi 450 pamoja na familia zao walijitokeza kupima virusi vya ukimwi kwa hiari. Aidha, vipeperushi vimesambazwa katika vituo vya kuingilia nchini kwa lengo la kutoa elimu juu ya janga la ukimwi kwa wasafiri wanaoingia na kutoka nchini. 
JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI
69. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012 Vikosi vya Zimamoto na Uokoaji  vimeendelea kutoa huduma za kuzima moto na uokoaji katika sehemu mbalimbali. Huduma hii inatolewa kwa mujibu wa Sheria ya Zimamoto na Uokoaji  Na. 14 ya mwaka 2007.  Aidha, katika kuboresha  utoaji wa huduma  hii, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limezingatia utoaji wa  elimu juu ya kinga na tahadhari ya moto. Jumla ya maeneo 41,774 yamefanyiwa ukaguzi ikiwa ni majengo 23,570 na vyombo vya usafiri na usafirishaji 18,204.  
70. Mheshimiwa Spika,  vile vile Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, limeajiri askari wapya 124 na kutoa mafunzo maalum ya uongozi na ukaguzi wa majengo  pamoja na vyombo vya usafiri na usafirishaji kwa askari 60 ili kuboresha uendeshaji wa zoezi zima la ukaguzi. Mafunzo hayo yalitolewa katika Chuo cha Magereza Ukonga – Dar es Salaam. Katika mwaka 2012/2013, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji litaendelea na zoezi la ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto, kuendeleza ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, kununua magari matano na kuajiri askari wapya 2,613 na kuwapatia mafunzo.
IDARA YA WAKIMBIZI
71. Mheshimiwa Spika, tarehe 30 Aprili, 2012 Tanzania ilikuwa na jumla ya wakimbizi 112,645  wakiwemo Warundi  48,195, Wakongo 62,632, Wasomali 1,548 na  270 wakimbizi wa mataifa mbalimbali. Katika kipindi cha Julai, 2011 hadi Aprili, 2012 jumla ya wakimbizi  189 walirejea kwao ambapo Warundi ni 155 na Wakongo 34. 
72. Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu ya mwaka 2011/2012 nilieleza kwamba wakimbizi 38,800 walioko katika kambi ya Mtabila, wangerejeshwa kwao na kambi hiyo kufungwa. Hata hivyo, katika mwaka 2011/2012, idadi ya wakimbizi wa Burundi kutoka kambi hiyo waliorejea kwao ni 155 tu, hali iliyosababisha kambi hiyo kutofungwa. Mkakati mpya wa kufunga kambi hiyo ni kwamba limefanyika zoezi la mahojiano ya kina na wakimbizi hao kwa lengo la kubaini kama wapo wakimbizi wenye sababu za msingi za kuendelea kuwepo nchini kama wakimbizi. Zoezi hilo lilifanyika mwezi Septemba hadi Desemba, 2011. Matokeo ya zoezi hilo yanaonyesha kuwa wapo wakimbizi 33,705 ambao hawana sababu za msingi za kuendelea kuwa wakimbizi na wengine 2,045 walionekana kuwa na sababu za msingi za kuwa wakimbizi.

73. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia matokeo ya zoezi hilo, kikao cha Pande Tatu (Tanzania, Burundi na UNHCR) kilifanyika Bujumbura - Burundi tarehe 22 Februari, 2012 na kukubaliana kwa pamoja kuifunga kambi ya Mtabila ifikapo tarehe 31 Desemba, 2012. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imekwishawasiliana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili iandaliwe Hati ya Ukomo wa Ukimbizi  (Cessation clause), kwa mujibu wa Sheria za Kimataifa. Mara hati hiyo itakapokuwa tayari litatolewa tamko la ukomo wa ukimbizi kwa wakimbizi hao walioko katika Kambi ya Mtabila. Baada ya tamko hilo, wakimbizi hao wataendelea kusaidiwa kurejea Burundi mpaka kambi itakapofungwa hapo tarehe 31 Desemba, 2012. Watakaokuwa wamegoma kurejea mpaka kufikia wakati kambi inafungwa, watachukuliwa kuwa ni wahamiaji haramu na hivyo kushughulikiwa kwa mujibu wa Sheria za Uhamiaji. Kwa upande wa wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya usalama nchini humo.

MAMLAKA YA VITAMBULISHO VYA TAIFA
74. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012 Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa imeajiri watumishi 105 na imenunua magari 12. Katika mwaka 2012/2013 Mamlaka itaajiri watumishi 110, itanunua magari 15  kwa ajili ya zoezi la utambuzi na usajili wa watu, kuanza ujenzi wa ofisi za utambuzi wa watu na usajili katika Wilaya 40, kupanua jengo la Makao  Makuu Dar es Salaam na kuendelea na zoezi la utambuzi na usajili wa watu katika Mikoa.

V. TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA AHADI ZA SERIKALI BUNGENI 2011/2012
75. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na Serikali Bungeni katika mwaka 2011/2012, umezingatiwa katika eneo la III na la IV katika hotuba hii katika maeneo ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi pamoja na mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2011/2012. 

VI. SENSA YA WATU NA MAKAZI
76. Mheshimiwa Spika, Mkutano wa Bunge la Bajeti la mwaka 2012/2013 unafanyika miezi michache kabla ya kufanyika kwa zoezi muhimu la sensa ya watu na makazi. Kabla ya kuwasilisha maombi ya fedha, naomba nieleze machache kuhusiana na umuhimu wa wananchi kushiriki kwenye sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika tarehe 26 Agosti, 2012 yenye kauli mbiu ya  “ Sensa kwa Maendeleo Jiandae Kuhesabiwa”.

77. Mheshimiwa Spika, maendeleo ya nchi yanawezeshwa na kuwepo kwa hali ya amani na utulivu. Hali ya amani na utulivu ni kipimo kinachoashiria  kuwepo kwa usalama wa raia na mali zao. Zoezi la sensa ya watu na makazi ni muhimu katika suala zima la usalama wa raia na mali zao. Kwa kuzingatia  umuhimu  wa zoezi lenyewe, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi itaweza kupata takwimu ya idadi kamili ya watu na makazi na hivyo kuiwezesha Wizara kupanga mipango na mikakati sahihi na endelevu ya kukabiliana na changamoto katika kulinda usalama wa raia na mali zao. Hivyo, ninawaomba kila mmoja wetu ashiriki katika sensa hii na awe ni balozi wa kuhamasisha umma kujitokeza na kushiriki kikamilifu katika zoezi zima la sensa ya watu na makazi kwa maendeleo na ustawi wa Taifa letu.

VII. SHUKRANI
78. Mheshimiwa Spika, natoa shukrani zangu za dhati kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa, Mbunge wa Monduli kwa kuyapitia na kuyachambua Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2012/2013. Ushauri wa Kamati hiyo utaisaidia Wizara yangu kuimarisha utendaji wa majukumu yake.
79. Mheshimiwa Spika, shukrani za pekee nazitoa kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Pereira Ame Silima, Mbunge wa Chumbuni, Katibu Mkuu Ndugu Mbarak Abdulwakil, Naibu Katibu Mkuu Ndugu Mwamini Malemi, Inspekta Jenerali wa Polisi Ndugu Saidi Mwema, Kamishna Mkuu wa Uhamiaji Ndugu Magnus Ulungi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa Ndugu Dickson Maimu, Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Ndugu Fidelis Mboya, Kaimu Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji Ndugu Pius Nyambacha na Wakuu wote wa Idara na Vitengo, Makamanda, askari pamoja na wafanyakazi wote wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambao wamefanikisha maandalizi ya hotuba hii. 
80. Mheshimiwa Spika, nachukua pia fursa hii kuwashukuru nchi wahisani ikiwemo Japan, China, Marekani, Misri na Saudi Arabia, taasisi za INTERPOL, IOM, EU, UNHCR, DfID, UNICEF, WFP, Pharm Access na Marie Stopes pamoja na wadau wengine wote kwa misaada yao ambayo imeongeza uwezo wa kiutendaji katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
81. Mheshimiwa Spika, mwisho ingawa sio mwisho kwa umuhimu ninamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa maelekezo yake mbalimbali na  Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda (Mb), Waziri Mkuu kwa kuhimiza utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

VIII. MAOMBI YA FEDHA KWA MWAKA 2012/2013
82. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naliomba Bunge lako Tukufu lipitishe Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2012/2013 ya shilingi 555,540,268,000 kwa ajili ya bajeti ya Matumizi ya Kawaida na miradi ya maendeleo. Kati ya maombi hayo shilingi 540,002,518,000 ni za Matumizi ya Kawaida ambapo shilingi 242,894,300,000 ni Matumizi Mengineyo na Mishahara shilingi 297,108,218,000. Maombi ya shilingi 15,537,750,000 ni kwa ajili ya  mipango ya maendeleo kwa mchanganuo ufuatao:-

Fungu 14: Jeshi la Zimamoto na Uokoaji
Matumizi Mengineyo shilingi         8,306,262,000
Mishahara shilingi                      8,661,572,000
Maendeleo shilingi                                      0.00
Jumla shilingi                   16,967,834,000

Fungu 28: Jeshi la Polisi
Matumizi Mengineyo shilingi      133,329,019,000
Mishahara shilingi                       198,944,297,000
Maendeleo shilingi                          3,332,250,000
Jumla shilingi              335,605,566,000

Fungu 29: Jeshi la Magereza
Matumizi Mengineyo shilingi      51,449,403,000
Mishahara shilingi                    62,908,822,000
Maendeleo shilingi                           1,555,500,000
Jumla shilingi                   115,913,725,000

Fungu 51: Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Matumizi Mengineyo shilingi           2,107,467,000
Mishahara shilingi                            2,902,343,000
Maendeleo shilingi                             650,000,000
Jumla shilingi                      5,659,810,000
Fungu 93: Idara ya Uhamiaji
Matumizi Mengineyo shilingi        47,702,149,000
Mishahara shilingi                       23,691,184,000
Maendeleo shilingi                       10,000,000,000
Jumla shilingi                        81,393,333,000
83. Mheshimiwa Spika, nakushukuru wewe pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza.
84. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

No comments: