WANANCHI WA UNGUJA WATAKA MUUNGANO UDUMU MILELE...

Wananchi waliojitokeza kutoka maoni kuhusu Katiba mpya kwa Tume ya Kukusanya Maoni ya Mabadiliko ya Katiba katika Mkoa wa Kusini Unguja, wametaka Muungano uendelee huku ufumbuzi wa kero zilizopo ukitafutwa.
Wengi waliotoa maoni hayo jana, walizungumzia suala la Serikali mbili au tatu mbele ya wajumbe wa Tume wakiongozwa na Mohamed Yussuf.
Khatib Mwadini Ngondo mkazi wa Mzuri Makunduchi, Kusini Unguja alitaka kuendelea kwa Muungano.
Alisema Muungano umekuwa na tija kubwa kwa pande mbili, lakini alitaka kuona hadhi ya Rais wa Zanzibar inatambuliwa katika Jamhuri ya Muungano tofauti na muundo wa sasa.
Abeid Razak alitaka muundo wa sasa wa Muungano uimarishwe ili uwe na tija na faida kwa pande mbili kwani Zanzibar kwa sasa inaonekana kutofaidika na Muungano.
Hassan Ali Hassan alisema ni vema kuwa na Muungano wa Serikali mbili kama ilivyo sasa, lakini kero za Muungano zipatiwe ufumbuzi wa haraka ili kuondosha manung’uniko ya wananchi kiasi ya kusababisha baadhi kuuchukia.
Mjumbe wa Tume hiyo, Richard Rimo alisema Dola yoyote duniani, haiwezi kupata ufanisi bila kuwa na ushirikiano mzuri miongoni mwa jamii husika.
Aliwataka wakazi wa shehia ya Kibuteni kutoa maoni yao kwa uwazi zaidi ili kufikia lengo sambamba na kuwahakikishia kuwa watayafanyia kazi kadri itakavyowezekana.
Mkazi wa shehia hiyo, Rajab Haji akitoa maoni aliiambia Tume hiyo kuwa Katiba itakayoundwa izingatie haja ya kuwa na wagombea binafsi wa ubunge, udiwani na uwakilishi na kuondokana na utaratibu wa sasa wa kutoa fursa kwa wagombea wenye vyama vya siasa tu.
Alishauri Katiba ijayo izingatie kuwapo kwa Mamlaka ya Watu wa Zanzibar na ya Tanganyika Huru, pamoja na kutaka mgawanyo wa misaada kutoka nje itolewe sawa bila kuangalia ukubwa wa Tanzania Bara.
Pandu Haji ( 48 ), alishauri Katiba mpya izingatie kuwa Tanzania kuna Muungano wa nchi mbili hivyo ni vema suala la ukusanyaji wa kodi liundiwe utaratibu mpya kwa TRA kufanya kazi zake Tanzania Bara pekee na si Zanzibar.
Alisema hiyo itaipa mamlaka Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) kufanya kazi ya kukusanya mapato kwa uhuru ili yainufaishe Serikali ya Zanzibar na kuinua uchumi wake.
Wilayani Kahama, Shinyanga, wanawake walishauri Serikali kutenga siku maalumu ya kutembelea waume zao waliofungwa katika magereza nchini na kutengewa chumba maalumu kwa ajili ya mapumziko ya muda mfupi.
Mmoja wa wanawake hao, Mkora Athumani alisema kwa sasa wanawake wengi ambao waume zao wako vifungoni hawana watu wa kuwaenzi katika familia zao, na kwamba wakipata fursa hiyo itakuwa muhimu kwani ni haki yao ya msingi.
Wajumbe wa Tume wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Mary Kashonda wapo katika Mkoa wa Shinyanga tangu juzi huku Wilaya ya Kahama ikiwa ni ya kwanza katika uchangiaji wa maoni hayo kwa muda wa siku 10.

No comments: