VIONGOZI WATOROSHA NJE SHILINGI TRILIONI 16...

Viongozi na wafanyabiashara nchini, wameelezwa kutorosha na kuhifadhi fedha nje ya nchi kiasi cha Sh trilioni 16.6 fedha ambazo zinazidi bajeti ya Serikali kwa mwaka 2012/13.
Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM) alisema hayo bungeni jana wakati akichangia hotuba ya Makadirio ya Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Tume ya Mipango kwa mwaka 2012/13 na kuituhumu Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuwa inajua fedha zote zilizofichwa na Watanzania nje ya nchi.
Mpina mbali na kuituhumu BoT kufahamu fedha hizo zilipo, alisema Benki Kuu ya Uswisi imekiri sehemu ya fedha hizo kuhifadhiwa katika benki za nchi hiyo na Watanzania sita.
"Taasisi ya Global Financial ilibainisha kuwa Sh trilioni 16.6 zimefichwa nje ya nchi na viongozi na wafanyabiashara wa nchini na Benki Kuu ya Uswisi imesema  Sh bilioni 315 ziko nchini mwao zimefichwa na watu sita.
"Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inajua fedha za Watanzania zilizo nje ya nchi, lakini hadi leo hawajatwambia ni za nani, ziliibwa lini na zitarejeshwa lini! Pia Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) inatakiwa itaifishe fedha hizo zirudi nchini na Hosea (Edward) yuko hapa atujibu," alisema Mpina.
Mbali na kufichwa kwa fedha hizo, Mpina alisema pia kwamba Tanzania inapoteza Sh bilioni 478 kila mwaka, zaidi ya nusu ya Bajeti ya Zanzibar kutokana na fedha hizo kufichwa katika benki za nje ya nchi.
Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage (CCM), akichangia hotuba hiyo, alishauri uundwe Mfuko wa Dharura wa kulipa madai ya watumishi ikiwamo malimbikizo ya mishahara yao ili kuepusha migogoro ya mara kwa mara.
Mbunge huyo ambaye alitolea mfano wa mkewe kutopandishwa daraja licha ya kusoma mara mbili, alitaka watumishi waliohusika katika kuidhinisha mishahara hewa serikalini ambazo ni Sh bilioni tisa, watajwe.
Mbunge wa Lushoto, Henry Shekifu (CCM), aliitaka Serikali itangaze nyongeza ya mshahara mapema kama ilivyokuwa zamani ili watumishi wajipange na si kama inavyofanya sasa kuwa siri.
Mbunge wa Korogwe Mjini, Yusuf Nassir (CCM) alisema katika leseni 28 zilizotolewa na Serikali za utafutaji gesi, hakuna Mtanzania anayefanya kazi hata katika ngazi za chini na taarifa ya mwekezaji ndiyo inapewa Serikali kitendo ambacho si sahihi.
Bunge juzi na jana liligeuka mdahalo kutokana na miongozo na taarifa za mara kwa mara zilizosababisha mabishano kwa siku mbili mfululizo wakati wa uchangiaji wa Bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Tume ya Mipango.
Mabishano hayo yalisababisha pia kutolewa maneno ya udhalilishaji kwa baadhi ya wabunge wakiwamo Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) aliyeambiwa na Mwenyekiti wa Bunge, Sylivester Mabumba kuwa ‘anawashwawashwa’.
Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi) aliambiwa na Mabumba kuwa anapenda kudandia hoja ili  kupata umaarufu na akatolewa nje ya Bunge baada ya kukaidi kukaa chini alipotaka kutoa taarifa.
Mbunge mwingine aliyekumbwa na maneno ya udhalilishaji ambayo baadaye yalifutwa ni wa Viti Maalumu Sabrina Sungura (Chadema), aliyeambiwa na Mbunge wa Iramba Mashariki, Mwigulu Nchemba (CCM) kuwa arudi darasa la kwanza akajifunze kusoma huku chama cha upinzani kikiambiwa kinaongozwa na mchezesha disko.
Juzi jioni wakati wa uchangiaji wa hotuba hiyo, alipokuwa akizungumza Mbunge wa Viti Maalumu, Stella Manyanya alieleza kuwa waliomteka kiongozi wa mgomo wa madaktari, Dk Steven Ulimboka walikuwa na magwanda yanayothibitisha ni ya Chadema na kusababisha Mnyika kusimama kuomba nafasi ili atoe taarifa.
Mnyika kabla ya kuruhusiwa, alisimama na kusema waliomteka Dk Ulimboka ni askari kwa mujibu wa alivyohojiwa na vyombo vya habari, ndipo Mabumba aliposimama na kusema "subiri Mnyika kaa chini kwanza, mbona unawashwawashwa?"
Wakati Mabumba anatoa kauli hiyo, Machali alisimama kutoa taarifa ya kumsaidia Mnyika ndipo naye akaambiwa akae chini kwani anapenda kudandia hoja kwa kutaka umaarufu.
Jana baada ya kipindi cha maswali na majibu, Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi) alisimama kuomba Bunge lijadili mgomo wa madaktari, ndipo akasimama Mnyika kuomba mwongozo.
Alipopewa nafasi alieleza jinsi Mabumba alivyomwita anawashwa na kwamba Machali ana kimbelembele, kuwa anadandia hoja.
Mwenyekiti Jenista Mhagama alieleza  kuwa Mkosamali alivunja kanuni kwa sababu suala hilo lilishatolewa uamuzi na Spika Anne Makinda kuwa limefungwa na halitajadiliwa bungeni.
"Nashangaa wabunge wanaendelea kujadili hili la mgomo wa madaktari, asiyeridhishwa atumie njia nyingine za kikanuni na si kuleta kauli zisizojenga heshima ya Bunge na hili la Mnyika nitalitolea uamuzi baadaye au siku yoyote nitakayoona inafaa, majibu yote niliyoyatoa ni kwa mujibu wa kanuni," alisema.
Alipopewa nafasi ya kuchangia, Mbunge wa Kisarawe, Selemani Jafu (CCM) akataka Serikali ifanyie uchunguzi suala la Dk Ulimboka, kwa kuwa kuna watu wana maslahi binafsi katika mgomo huo wa madaktari ili kuipaka matope Serikali.
Baada ya mchangiaji huyo, alifuata Mbunge wa Chake Chake, Musa Haji Kombo (CUF) aliyepongeza madaktari kurudi kazini, lakini Mnyika akasimama tena kuomba taarifa na kusema: "nasikitika kauli ya mbunge kwani vyombo vya habari vimesema madaktari bingwa wamegoma na Rais (Kikwete) amepotoshwa."
Mhagama alimwuliza Kombo kama anakubali taarifa hizo, akazikataa na kutoa sababu kuwa wao walikataa kufanya kampeni madaktari waache mgomo, lakini baada ya kuacha na kurudi kazini wanakataa uamuzi huo wakitaka waendelee kugoma.
Kombo wakati akichangia alisema; "wenzetu (bila kutaja chama) wawe wastaarabu kama CUF inayoongozwa na msomi Profesa Lipumba na si wao wanaoongozwa na disco joker(mchezesha disko).
Kauli hiyo ilimfanya Mhagama kuingilia kati akimtaka Kombo afute kauli yake ambaye alitii na kumfanya Mhagama kumsifu kwa kuonesha nidhamu ya Bunge kwa kufuta kauli baada ya kukosea.

No comments: