WAIBA LITA MILIONI TATU ZA DIZELI RUKWA...

Mkandarasi anayejenga barabara ya Laela mpaka Sumbawanga mkoani Rukwa ya umbali wa kilometa 95.31 kwa kiwango cha lami, ameibiwa zaidi ya lita milioni tatu za mafuta ya dizeli ya kuendeshea mitambo ya ujenzi.
Meneja wa Ujenzi wa barabara hiyo, James Aikman akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, alidai dizeli iliyoibwa ina thamani ya zaidi ya Sh bilioni saba na imechangia kudhoofisha maendeleo ya mradi huo.
Kutokana na changamoto hiyo, Aikman alisema wamelazimika kuajiri walinzi kutoka Ulaya, washirikiane na Polisi nchini katika kudhibiti wizi huo.
Barabara hiyo inajengwa na kampuni ya Aersleff – BAM International ya Denmark na Uholanzi kwa ufadhili wa Serikali ya Marekani kupitia mradi wa Changamoto za Milenia (MCC) kwa gharama ya zaidi ya dola milioni 97 za Marekani sawa na zaidi ya Sh bilioni 155.
Wizi ulivyoanza
Aikman alisema wizi huo ulianza tangu kuanza kwa mradi huo mwaka juzi ambapo baada ya kupiga mahesabu, wakagundua kuwa mpaka sasa zaidi ya lita milioni tatu za dizeli zikiwa na thamani ya zaidi ya Sh bilioni saba, zimeibwa.
Pamoja na kukiri kuwa mradi huo umeathirika na wizi huo wa mafuta ya dizeli, Meneja huyo alilithibitishia gazeti hili kuwa mradi huo wa ujenzi wa barabara utakamilika kwa muda waliokubaliana, yaani Mei mwakani. Mkataba huo ulisainiwa Aprili 29, mwaka juzi na Aikman anasema kazi ya ujenzi imekamilika kwa asilimia 35.
Baadhi ya vijana waliokiri kujihusisha na uhalifu huo kwa masharti ya majina yao kutoandikiwa gazetini, walidai kwamba wizi wa dizeli ni rahisi kuliko wizi wa vifaa vingine vya ujenzi vikiwamo saruji, mabati na nondo ambavyo upatikanaji wake ni mgumu na ni vigumu kuvihifadhi.
Walidai kuwa wateja wao wakubwa ni baadhi ya wamiliki wa magari ya mizigo, magari ya abiria, magari madogo na pikipiki ambao huwafuata vijijini na kuuziwa nishati hiyo kwa bei nafuu.
Kwa mujibu wa madai ya mtoa habari huyo, lita 20 za dizeli ya wizi huuzwa kwa Sh 25,000 hivyo lita moja ni Sh 1,250 wakati mjini lita moja inauzwa kwa Sh 2,500.
Kutokana na biashara hiyo, mtoa habari huyo alidai wanapata faida ya zaidi ya Sh 200,000 kwa siku ikiwa ni faida baada ya kutoa matumizi yote huku madereva wakipata zaidi ya Sh 400,000 kwa siku.
"Hata ufanye kufuru ya matumizi, dereva wa magari makubwa lazima atalala na faida ya zaidi ya Sh 400,000 huku sisi vijana hata tutumieje lazima unaamka na faida ya zaidi ya Sh 200,000," alikiri mtoa habari huyo.
Walinzi kazi ngumu
Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Aikman alidai wamelazimika kuajiri walinzi kutoka Ulaya ingawa hakutaka kutaja idadi yao na nchi wanakotoka.
Alidai kuwa walinzi hao kwa kushirikiana na Polisi wilayani Sumbawanga, wamefanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa kadhaa wakiwa na kiasi kikubwa cha dizeli, ingawa pia hakuwa tayari kuweka wazi dizeli waliyokoa akidai kitendo hicho kinaweza kuvuruga uchunguzi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda amekiri kupata taarifa kutoka uongozi wa kampuni hiyo kuhusu wizi huo wa mafuta ya dizeli na kwamba kwa kushirikiana na walinzi hao wa kigeni wameweka mkakati wa kukabiliana na wizi huo.
Kamanda Mwaruanda alidai kuwa walinzi wa kigeni walioajiriwa na kampuni hiyo walizidiwa mbinu na madereva wa magari makubwa, kwani wakati wao wakilinda visima vya mafuta, ndani ya kambi yao katika Kijiji cha Ikunda, madereva walikuwa huru maeneo ya mradi vijijini na kuwa vigumu kubainika.
Baadhi ya vijana wanaoishi katika vijiji mradi huo unakopita, kwa masharti ya majina yao kutotajwa gazetini, walidai kushuhudia mradi huo ukihujumiwa, lakini wamekiri kuwa wanaogopa kutoa taarifa katika vyombo vya Dola kwa kuwa vijana wenzao ambao sasa wana uwezo mkubwa wa kifedha, wanatishia kuwadhuru kama watatoa siri hiyo.

No comments: