BODI YAMSIMAMISHA KAZI MKURUGENZI MKUU WA TANESCO...

Mhandishi William Mhando.
Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), imemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, William Mhando kutokana na tuhumu za ubadhilifu na matumizi mabaya ya madaraka.
Hatua hiyo imefikiwa katika kikao cha dharura cha bodi hiyo kilichokaa juzi na kumalizika jana ambacho kilijadili masuala mbalimbali ikiwemo tuhuma zinazoelekezwa kwa menejimenti ya shirika hilo.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa bodi hiyo, Robert Mboma na kusainiwa na Makamu Mwenyekiti wa bodi hiyo, Victor Mwambalaswa ambaye pia ni Mbunge wa Lupa (CCM), uamuzi huo unalenga kupisha uchunguzi huru na wa kina ambao umeanza mara moja.
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa baada ya vikao hivyo vya dharura na majadiliano, bodi hiyo iliona kuwa tuhuma hizo ni nzito, hivyo ni vyema Mhando akae pembeni ili kupisha uchunguzi.
Sambamba na Mhando wengine waliosimamishwa kazi katika shirika hilo ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Huduma za Tanesco, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi, Ununuzi, Harun Mattambo.
"Pamoja na hatua hizi bodi imechukua hatua stahiki za kuhakikisha kwamba shughuli za kiutendaji na uendeshaji wa Tanesco zinaendelea kama kawaida," ilieleza taarifa hiyo.
Hata hivyo bodi hiyo haikuwa tayari kuzungumza na waandishi wa habari walioitwa katika ofisi za Wizara ya Nishati na Madini kulikofanyika kikao hicho.
Badala yake ofisa mmoja wa wizara hiyo aliyekuwa akigawa taarifa hizo ambaye hakutaja jina alidai bodi imeamua kutoa taarifa hiyo kwa maandishi.
Taarifa hiyo pia haikufafanua kwa kina tuhuma hizo zaidi ya kueleza kwamba zinahusu ubadhilifu na matumizi mabaya ya madaraka.

No comments: