TUNDU LISSU AMFUATA MNYIKA TUME YA MAADILI...

Mbunge wa Singida Mashariki na Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Katiba na Sheria, Tindu Lissu (CHADEMA), ameshindwa kutoa ushahidi kuthibitisha kwamba Rais Jakaya Kikwete anateua majaji wa Mahakama Kuu bila kushauriwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Kutokana na hali hiyo, Mweyekiti wa Bunge, Jenister Mhagama alilazimika kutumia Kanuni ya 2 ya Bunge, kuamuru suala hilo kupelekwa kwenye Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
Uamuzi huo ulichukuliwa juzi usiku kabla ya kuahirishwa kwa shughuli za Bunge, ikiwa ni siku moja tangu Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) kufikishwa katika kamati hiyo, baada ya kushindwa kuwasilisha ushahidi kwamba Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM), alihusika na wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Lissu alitoa madai hayo dhidi ya majaji bungeni juzi wakati akitoa maoni ya Kambi hiyo ya Upinzani kuhusu Hotuba ya Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe.
Katika maoni hayo ya Upinzani, Lissu alisema madhara ya ukiukwaji huo wa Katiba katika uteuzi wa majaji wa Mahakama Kuu ni makubwa na yameanza kujitokeza wazi.
Madhara hayo kwa mujibu wa madai ya Lissu, ni uwepo wa majaji ambao kwa sababu ya kutofanyiwa usaili na Tume ya Utumishi wa Mahakama, hawana uwezo wa kuandika mwenendo wa mashauri na hukumu zinazosomeka kutokana na ama kutokuwa na uwezo na ujuzi wa sheria au kutokuwa na weledi wa lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo lugha rasmi.
"Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo taarifa kwamba wapo majaji ambao kwa sababu hizo za kutofanyiwa usaili juu ya uwezo na ujuzi wao na mamlaka husika ya kikatiba, wameshindwa kabisa kuandika hukumu za kesi walizozisikiliza
na hivyo kusababisha mlundikano wa kesi mahakamani usiokuwa na sababu yoyote," alidai Lissu.
Kutokana na kutoa maneno hayo makali dhidi ya majaji, Naibu Spika Job Ndugai aliyekuwa akiongoza kikao cha Bunge, alimuagiza Lissu katika kikao cha juzi jioni awasilishe waraka maalumu ili kuomba kufuta maneno hayo baada ya Mbunge wa Karagwe, Godfrey Blandes (CCM) kuomba mwongozo wa Spika kuhusu maneno hayo ya Lissu.
Pamoja na kupewa agizo hilo, kilipowadia kipindi cha jioni cha Bunge, Lissu hakuwasilisha waraka wowote kwenye meza ya Katibu wa Bunge ili kuthibitisha au kufuta maneno hayo hatua iliyomlazimu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, kuomba mwongozo wa Spika.
Katika Mwongozo huo, Jaji Werema alisema maneno ya Lissu yalikiuka kanuni ya 64 (1) (a) ya Bunge inayozuia wabunge kumshambulia mtu ambaye hayuko bungeni.
Mbali ya kukiuka kanuni hiyo, Jaji Werema alisema
Lissu pia alikuwa amekiuka kanuni ya 64 (1) (e) inayosema Mbunge yoyote hataruhusiwa kumshutumu Spika, Naibu Spika, Rais na majaji kutokana na utendaji wao na kuongeza kuwa kauli ya Lissu ilikuwa imeingilia mwenendo wa utendaji wa Tume ya Utumishi ya Mahakama.
Naye Waziri Chikawe aliposimama, alisisitiza kwamba uteuzi wa majaji wa Mahakama Kuu, unafanywa kwa kuzingatia kanuni zilizopo ikiwa ni pamoja na majaji hao kufanyiwa usaili na kumtaka Lissu kutoa ushahidi wa walau jina la Jaji mmoja ambaye aliteuliwa na Rais Kikwete bila kufanyiwa usaili lakini Lissu hakumtaja.
Akitoa mwongozo wa Spika, Mhagama aliyekuwa akiongoza kikao cha Bunge kwa wakati huo, alimtaka Lissu kutekeleza agizo la Naibu Spika la kuondoa maneno hayo kutokana na kukiuka kanuni za Bunge lakini pia kutokana na kukiuka Ibara ya 89 (1) ya Katiba ambayo inazuia mhimili mmoja wa dola kuingilia utendaji wa mhimili mwingine isipokuwa kama kuna hoja mahususi ya kuacha kufanya hivyo.
Hata hivyo aliposimama Lissu alisema pamoja na kuelewa umuhimu wa majaji, lakini hawezi kuondoa maneno yaliyopo kwenye hotuba yake kwa vile taratibu na mwenendo mzima uliotumiwa na Kiti cha Spika, hazikufuatwa hatua iliyomfanya Mhagama kuamuru suala hilo kupelekwa kwenye Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
Muhagama alisema katika kamati hiyo, kitendo cha Lissu kuvunja kanuni za Bunge na mwenendo mzima uliotumiwa na Kiti cha Spika katika kushughulikia suala hilo vitapitiwa.

No comments: