RAIS KIKWETE AZUNGUMZIA MGOMO WA MADAKTARI...

Rais Jakaya Kikwete jana amesema katika hotuba yake ya kila mwisho wa mwezi kwa Taifa kwamba kama kuna daktari anaona kuwa hawezi kufanya kazi serikalini bila ya kulipwa mshahara Sh milioni 7.7 awe huru kuacha kazi na kwenda kwa muajiri anayeweza kumlipa kiasi hicho.
Rais Kikwete aliweka bayana kuwa Serikali haina uwezo wa kulipa mshahara na posho hiyo kwa daktari anayeanza kazi kutoka shuleni na zaidi ya hapo kwa madaktari wengine.
Kutokana na ukweli huo, aliwatakia kila la heri wasioweza kufanya kazi serikalini, lakini akaongeza kuwa “hana sababu ya kugoma ili ashinikize kulipwa mshahara huo. Asisumbuke, hatalipwa mshahara huo.” 
 “Isitoshe, hana sababu ya kuendelea kuwa na mgogoro na mwajiri ambaye hana uwezo wa kumlipa anachokitaka. Huna sababu ya kumpa usumbufu mwajiri wa kukuandikia barua ya kujieleza au kukuachisha kazi. Kwa nini upate usumbufu wa kupata barua hizo na kuzijibu. Kwa nini upate usumbufu wa kuachishwa kazi na kutakiwa kuondoka kwenye nyumba ya Serikali ndani ya saa 24,” alihoji. 
Rais Kikwete pia aliwaonya madaktari hao kwa kuingia katika mgogoro na Mahakama ambayo iliwapa amri kurudi kazini wakaikataa na mgogoro mwingine na waajiri wao isivyostahili.  
 “Wagonjwa wanateseka na wengine kupoteza maisha kwa mgomo huu usiokuwa halali kisheria ambao pia haustahili kuwepo hata kwa mujibu wa maadili ya udaktari. Viongozi wa MAT na wenzao wanawaingiza madaktari katika mgogoro na Mahakama na waajiri wao isivyostahili. 
 “Ni vyema viongozi wa madaktari na madaktari wakatambua kuwa wanashiriki katika mgomo usiokuwa halali ambao pia kiongozi wao mkuu amekana Mahakamani kuwa hahusiki nao. Madaktari lazima watambue pia kwamba ajira zao wanaziweka hatarini.  
 “Ni vyema watambue kuwa wanashiriki katika mgomo usiokuwa halali ...mfanyakazi ana kinga ya kutofukuzwa kazi na mwajiri kwa kushiriki mgomo unaokubalika kisheria. Huu siyo.  
 “Watapoteza ajira, hawana pa kukimbilia, hawana cha kuwalinda. Kwa madaktari walio mafunzoni, wanahatarisha maisha yao kwani hawatapata cheti cha kudumu wakishiriki mgomo usiokuwa halali.   Lazima watafakari sana kwa hayo wafanyayo,” alihadharisha Rais Kikwete.  
Tofauti na madai ya madaktari yaliyochapishwa katika mabango waliyoyabeba jana kuwa wanagoma kwa kuwa katika hospitali za Serikali hakuna vitendea kazi, Rais Kikwete aliweka wazi kuwa kiini ni maslahi makubwa wanayoyadai ambayo Serikali haina uwezo wa kuwapa. 
Alibainisha kuwa madaktari hao wanataka walipwe mshahara wa Sh milioni 3.5 kwa mwezi kwa daktari anayeanza kazi kutoka chuoni. Pia wanataka posho za kila mwezi ikiwamo asilimia 10 ya mshahara huo iwe posho ya kuitwa kazini ambayo ni Sh 350,000, asilimia 30 ya mshahara huo iwe posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi ambayo ni Sh 1,050,000. 
Posho nyingine wanazodai katika mlolongo huo wa maslahi ni kupatiwa nyumba grade A au asilimia 30 ya mshahara iwe posho ya makazi ambayo ni Sh 1,050,000 na posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu ambayo ni asilimia 40 ya mshahara huo sawa na Sh milioni 1.4. 
Madaktari hao pia wanataka posho ya usafiri asilimia 10 ya mshahara sawa na Sh 350,000 ambapo vikijumlishwa vyote, kima cha chini cha mshahara na posho kwa daktari anayeanza kazi leo, itakuwa Sh milioni 7.7. 
Madai mengine ambayo hawakuyaweka katika kiwango cha fedha ni pamoja na kupatiwa kadi ya kijani ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa watendaji wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii. 
Mengine ni viongozi wa kisiasa kulazimisha kupewa rufaa nje ya nchi, madaktari waliofukuzwa warudishwe kazini, huduma za afya ziboreshwe nchini na kuongeza posho ya uchunguzi wa maiti ambayo nayo hawakueleza ni kwa kiasi gani. 
Rais aliweka wazi mambo waliyofikia muafaka na madaktari hao kuwa ni pamoja na usafiri wa kwenda na kurudi kazini ambapo Serikali ilitaka madaktari watumie fursa ya utaratibu uliopo ili wakopeshwe magari, pikipiki, samani na matengenezo ya magari.  
Pia ilikubalika na utekelezaji ukaanza kuwapatia madaktari kadi ya kijani ya NHIF na katika hatua za kinidhamu dhidi ya watendaji wakuu wa Wizara, uongozi wa juu wa wizara ulibadilishwa na sasa kuna uongozi mpya.  
Hata hivyo, pamoja na Serikali kubadilisha uongozi huo, Rais Kikwete alisema Waziri mpya wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Husein Mwinyi alipowataka madaktari hao waonane kuzungumzia hoja zao, walikataa kumuona kwa madai kuwa hawaoni sababu kwa vile wamezungumza na Kamati yake kwa miezi mitatu bila mafanikio. 
 “Muafaka haukufikiwa baina ya Serikali na madaktari kuhusu mshahara wa kuanzia kazi wa daktari.  Madaktari wanataka uwe Sh milioni 3.5 wakati Serikali inasema kiasi hicho hatukiwezi... Madaktari wamekataa katakata na wameng’ang’ania Sh milioni 3.5,” alisema Rais Kikwete. 
Suala lingine walilotofautiana ni posho ya kuitwa kazini ambapo Serikali iliongeza tangu Februari 2012  kutoka Sh 10,000 hadi Sh 25,000 kwa daktari bingwa, Sh 20,000 kwa dakari mwenye usajili wa kudumu  na Sh 15,000 kwa madaktari walio katika mafunzo. 
 “Madaktari kwa upande wao hawakukubali uamuzi huo wa Serikali na kusisitiza walipwe asilimia 10 ya mshahara. Ugumu wa kukubali pendekezo la madaktari ni kuwa sharti la malipo haya ni mtu kuitwa kazini.  
“Ukitaka ilipwe kiwango cha mshahara ina maana kuwa hata kama daktari hakupangwa kuitwa au alipangwa na hakutokea aendelee kulipwa. Hili haliwezi kuwa sahihi, linaweza kuwafanya baadhi ya madaktari kutotimiza wajibu wao kwa vile wana hakika mwisho wa mwezi malipo yako pale pale,” alisema Rais Kikwete. 
Rais Kikwete aliahidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha mishahara na maslahi ya wafanyakazi na kuongeza kuwa nia hiyo Serikali imeitekeleza kwa vitendo. 
Alikiri kuwa mishahara haitoshi, lakini akasema lazima uwezo wa kufanya hivyo uwepo na kuonesha alipoingia madarakani mwaka 2004/2005, mshahara wa kuanzia wa daktari ulikuwa Sh 178,700. 
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, mwaka uliofuata 2005/ 2006, ulipanda na kufikia Sh 403,120 na ukaendelea kupandishwa mwaka hadi mwaka mpaka kufikia Sh  957,700 kwa sasa kiasi ambacho ni mara mbili ya mishahara ya watumishi wa taaluma nyingine wenye shahada ya kwanza wanaoanza kazi na Sh 446,100. 
“Hata hizo huduma za afya tunazosema ni duni tuziboreshe, hatutaweza kuziboresha kama tutatumia sehemu kubwa ya pesa za Serikali kuwalipa mishahara wafanyakazi. Hivi sasa matumizi ya mishahara ni asilimia 48 ya Bajeti ya Serikali. Kiwango hicho ni kikubwa mno,” alisema Rais Kikwete na kuongeza: 
“Uwiano mzuri ni kuwa na matumizi ya mishahara yasiyozidi asilimia 35 ya bajeti na asilimia 65 zitumike kugharimia huduma na shughuli nyingine za maendeleo ya wananchi na taifa.  Sisi tumezidi kwa asilimia 13.  Hivyo, hatuna budi tukubali kujinyima kwa manufaa ya walio wengi.”  
Aidha, Rais Kikwete alieleza masikitiko yake makubwa na kuhuzunishwa na kitendo cha kinyama alichofanyiwa Dk Steven Ulimboka, akisema ni kinyume kabisa na mila na desturi zetu. 
“Nimeelekeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli ujulikane.  Nimesema kuwa ningependa ukweli huo ujulikane mapema ili tuondoe wingu baya la kutiliana shaka na kulaumiana kunakoendelea hivi sasa,” alisema na kuongeza.” 
“Natambua kuwa Serikali nayo inatajwa katika orodha ya wanaotiliwa shaka. Mimi nimeshangazwa sana na hisia hizo kwani siioni sababu ya Serikali kufanya hivyo. Kwa nini Serikali imdhuru Dk Ulimboka? Na, kuhusu mgomo, Mahakama Kuu imekwishatoa amri ya kusitisha mgomo. Anayekaidi amri ya Mahakama ananunua ugomvi na mhimili huo wa dola ambao wenyewe una mamlaka ya kumtia adabu mtu huyo. 
“Hivi baada ya kufika hapo Serikali iwe na ugomvi na Dk Steven Ulimboka kwa sababu ipi na jambo lipi hata iamue kumdhuru? Kama kuna mtu wa Serikali kafanya, itakuwa kwa sababu zake binafsi na siyo za Serikali au kwa kutumwa na Serikali.” 

1 comment:

Anonymous said...

You finally found the best spot to compare and purchase Invicta Grand Diver [url=http://invicta-grand-diver.pkak.com/] Invicta Grand DiverWatches.[/url]
In our site you can compare the prices from high quality shops.
You can find full details and description of our Invicta Grand Diver Watches.
Here you'll be able to buy the right [url=http://invicta-grand-diver.pkak.com/] Invicta Grand Diver watches[/url] that fits your needs and budget, and most important, those you wish to have.