PPRA YAZIFUNGIA KAMPUNI MAISHA KUSHIRIKI ZABUNI...

Ofisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Dk. Ramadhan Mlinga.
Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imefungia kampuni 358 ikiwamo moja ya kizalendo, kushiriki zabuni zinazoitishwa na taasisi za umma nchini, huku baadhi zikifungiwa maisha kutokana na sababu mbalimbali za ukiukaji maadili ya zabuni ikiwamo rushwa.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Dk. Ramadhan Mlinga alibainisha hayo jana Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua hizo baada ya kampuni hizo kufungiwa na Benki ya Dunia na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi ya Uganda.
Kwa mujibu wa Mlinga, miongoni wa kampuni hizo, tatu zinafanya shughuli zao nchini ikiwamo moja ya kizalendo ya Oxford University Press Tanzania Limited.
Nyingine mbili za kigeni ambazo zimesajiliwa nchini, zikijishughulisha na masuala ya ujenzi ambazo ni China Communications Construction na China Geo-Engineering.
Kampuni za Oxford na China Geo Engineering zimefungiwa kwa miaka saba kila moja wakati China Communications Construction imefungiwa miaka 10 kushiriki zabuni kwa sababu za udanganyifu, rushwa na nyingine.
Katika mlolongo huo, kampuni 246 zimefungiwa kati ya mwaka mmoja na miaka 10, kampuni 18 zimefungiwa kati ya miaka 10 na zaidi wakati kampuni 94 zimefungiwa maisha kushiriki zabuni, adhabu ambazo zilitolewa na Benki ya Dunia katika nyakati tofauti mwaka huu.
Mlinga pia alibainisha kuwa kufungiwa kwa kampuni hizo, kunahusu pia wakurugenzi na kampuni tanzu za kampuni zilizokumbwa na adhabu hiyo ya kufungiwa na lengo ni kuzuia uwezekano wa viongozi hao kusajili kampuni kwa jina lingine ili kuendelea kushiriki zabuni.
"Tunashauri taasisi zote za umma kufanya tathmini kwa kina kwa zabuni zote zinazowasilishwa na kampuni ili kuhakikisha kuwa hazitoi zabuni kwa kampuni zinazomilikiwa na wakurugenzi waliofungiwa au kampuni tanzu za kampuni zilizofungiwa," alisema.
Akitoa ufafanuzi kuhusu hatua hiyo ya kufungiwa kampuni hizo, Mlinga alisema endapo zilikuwa zimepata zabuni kabla ya kupewa adhabu hizo, zinatakiwa kukamilisha kazi walizopewa lakini kuanzia sasa haziruhusiwi kupata zabuni mpya hadi zitakapokamilisha adhabu husika.
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PPRA, Jaji mstaafu Thomas Mihayo alitoa mwito kwa wananchi wote kuhakikisha kampuni zilizofungiwa ambazo orodha yao inapatikana kwenye tovuti ya www.ppra.go.tz hazipewi zabuni popote endapo zitajipenyeza kuingia nchini hasa zinazotoka nchi jirani.

No comments: