SUALA LA DK. SLAA KUTAKA KUFUNGA NDOA LATINGA MAHAKAMANI...

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilibrod Slaa, amewasilisha hoja za awali dhidi ya utaratibu wa ufunguaji wa kesi ya kupinga ndoa aliyopanga kufunga na mchumba wake wa siku nyingi, Josephine Mushumbusi.
Dk Slaa na Josephine wamepanga kufunga ndoa Julai 21 wilayani Karatu mkoani Arusha lakini juzi ilipingwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania na mkewe, Rose Kamili.
Hoja ya Dk Slaa iliwasilishwa jana katika Mahakama Kuu ya Tanzania na wakili wake, Mutakyamirwa Philemon.
Dk Slaa katika hoja hiyo, anadai kuwa suala la ndoa halikupaswa kuwasilishwa mahakamani kama la madai, bali kwa kutumia hati ya kuitwa mahakamani ikiambatanishwa na kiapo cha mdai.
Kama Kamili anayewakilishwa na wakili Joseph Tadayo atakuwa na hoja yoyote dhidi ya hoja ya Dk Slaa, atapaswa kuiwasilisha mahakamani hapo Agosti 7.
Jaji Lawrence Kaduri wa Mahakama Kuu ya Tanzania aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 14 itakapokuja kusikilizwa.
Kamili katika kesi aliyofungua dhidi ya Dk Slaa anapinga kufungwa kwa ndoa hiyo, na pia anadai fidia ya Sh milioni 550 kwa gharama ya malezi ya familia na usumbufu aliopata kwa kutelekezwa na mumewe.
Kesi hiyo ilifunguliwa na Tadayo na kusajiliwa kwa namba 5 ya mwaka huu. Kwa mujibu wa hati ya madai iliyowasilishwa mahakamani, mdaiwa wa kwanza ni Dk. Slaa na wa pili ni Josephine.
Kamili anadai kuwa yeye na Dk Slaa ni wanandoa na Josephine ndiye alisababisha Dk. Slaa atelekeze familia.
Kamili anadai yeye na Dk Slaa walifunga ndoa mwaka 1985 na Juni 18, 1987 wakajaaliwa mtoto wa kwanza wa kike Emiliana na wa pili Septemba 23, 1988 Linus na kwamba maisha yao awali yalikuwa ya upendo.
Anadai kuwa kabla ya hapo, Dk Slaa alikuwa padri lakini kwa ridhaa yake aliacha kazi hiyo ili aishi na familia yake na kutimiza majukumu yake katika ndoa hiyo.
Anaendelea kudai kuwa kuanzia hapo yeye na mdaiwa waliishi nyumba moja baada ya Dk Slaa kuacha utumishi wa Mungu kama mke na mume na walitambuliwa kuwa wanandoa, kwa sababu taratibu zote za ndoa zilifuatwa na familia zote mbili ambazo zinatambua hilo.
Alitaja kuwa katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na nyaraka kama hati za kusafiria zinawatambulisha kama mke na mume halali.
"Mdai na mdaiwa wa kwanza (Dk Slaa) waliishi maisha ya ndoa kwa amani, furaha na kuunganisha nguvu zao kwa ajili ya manufaa ya familia yao hapo baadaye na walichuma mali zikiwamo nyumba ya Sinza, Dar es Salaam katika kiwanja namba 609 Block E.
"Pia nyumba iliyoko Karatu katika kijiji cha Gongali ambayo ilijengwa mwaka 2005 pamoja na samani mbalimbali za nyumbani," sehemu ya hati hiyo ilisema.
Aidha, anadai mambo yalibadilika mwaka 2009 baada ya Dk Slaa kuanza uhusiano na Josephine, na hivyo kutotimiza majukuu yake kama mume na kulala nje ya nyumba akitumia mali za familia kutimiza maisha ya anasa na Josephine.
"Tangu mwaka 2009 mdai amekuwa akitunza familia peke yake bila msaada akijitunza mwenyewe na watoto hao wawili kwa kila kitu, ikiwa ni pamoja na ada za elimu ya juu za mtoto wa kwanza Emiliana akiwa Chuo Kikuu cha Ardhi mwaka wa mwisho akichukua Shahada ya Usimamizi wa Ardhi na Linus ambaye hivi karibuni amemaliza mafunzo ya Stashahada ya Tehama katika Chuo cha Tehama cha Learn cha Dar es Salaam," ilidai hati hiyo.
Anaiomba Mahakama itamke kuwa ndoa inayotakiwa kufungwa Karatu au kokote na tarehe yoyote ni batili hivyo imwamuru Dk Slaa alipe Sh milioni 50 kama gharama ya kutunza familia kwa kipindi chote hicho na Josephine alipe Sh milioni 500 kwa uzinzi uliosababisha mumewe atelekeze familia.

No comments: