KESI DHIDI YA DK. MWIGULU YAMKALIA VIBAYA MNYIKA...

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) amepelekwa mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kwa kushindwa kutoa ushahidi wa madai yake bungeni kuwa Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM) anahusika na kashfa ya wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA)  katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema jana kuwa amechukua uamuzi huo baada ya Mnyika kuwasilisha maelezo ya awali badala ya ushahidi wa kauli yake ndani ya siku saba alizopewa na Mwenyekiti wa Bunge, Jenister Mhagama Julai 3.
Kabla ya Ndugai kutoa msimamo huo wa Bunge, Nchemba aliomba Mwongozo wa Spika akitaka kujua kama Mnyika alikuwa tayari amewasilisha kwenye Kiti cha Spika ushahidi  wa kauli yake kwamba anahusika na wizi wa fedha za EPA.
Pamoja na kusema Mnyika ameshindwa kuwasilisha ushahidi huo, Ndugai alisema Mbunge huyo amekuwa akidanganya wananchi kupitia mitandao ya  kijamii, kwamba amewasilisha ushahidi wake kwa Spika jambo alilosema si la kistaarabu.
Alisema Mbunge anaposimama bungeni anapaswa kusema jambo alilokuwa na ushahidi nalo na endapo atakuwa na shaka yoyote ni vizuri akafuta kauli yake anapotakiwa kufanya hivyo, ili kuepuka kubanwa awasilishe ushahidi.
Ndugai alisema tangu wabunge waliposimama bungeni na kudai kuwa na taarifa kuhusu masuala mbalimbali, hadi sasa hakuna hata mmoja ambaye amewahi kuwasilisha ushahidi huo mbele ya Spika, suala linaloonesha wazi kwamba hawana uhakika na kauli zao.
"Kutokana na Mnyika kushindwa kuleta ushahidi wake kwamba Mwigulu (Nchemba) alihusika na wizi wa fedha za EPA wakati ambao alikuwa akisoma Chuo Kikuu, sasa nalifikisha suala hili kwa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili ichukue hatua kwa mujibu wa taratibu," alisema Ndugai.
Akizungumza baada ya Bunge kuahirishwa mchana jana, Mnyika alisema hakubaliani na hatua hiyo ya Ndugai ya kumfikisha mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa vile alishawasilisha maelezo ya kina kuhusu suala hilo na kusema atamfikisha Ndugai na Mwenyekiti wa Bunge,  Mhagama mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kanuni.
"Hili suala linafanyiwa propaganda kwa nia ya kunivunjia heshima kwa jamii na wapiga kura wangu. Ukiangalia mwenendo mzima wa suala hili ndani ya Bunge, hakuna mahali ambapo nilisema Nchemba anahusika na wizi wa EPA, nilichosema mimi ni kwamba ana tuhuma, lakini Mwenyekiti wa Bunge hakunipa nafasi nizitaje tuhuma zake," alisema Mnyika.

No comments: