MAHAKAMA YA RUFAA YAOMBA JALADA LA KESI YA MSANII LULU...

Mahakama ya Rufaa imeandika barua kuomba jalada la kesi ya Muigizaji wa filamu, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu anayetuhumiwa kumuua muigizaji mwenzake Steven Kanumba.
Jaji Dk Fauzi Twaib alisema hayo jana Katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam, wakati ombi la uchunguzi wa umri wa Lulu lilipotajwa.
Jaji Twaib aliutaka Upande wa Mashitaka kufuatilia na kuhakikisha jalada la kesi hiyo iliyofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu linapelekwa katika Mahakama hiyo.
Juni 11 mwaka huu, Mahakama Kuu ilitoa uamuzi kuwa imechukua jukumu la kufanya uchunguzi wa umri wa Lulu na kuwa Mahakama ya Kisutu ilikosea kukataa kuchunguza umri wa mshitakiwa huyo.
Mahakama ilitoa uamuzi huo kutokana na maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na jopo la mawakili wanaomtetea mshitakiwa huyo likiongozwa na Wakili Kennedy Fungamtama.

Mawakili wa mshitakiwa huyo walidai kuwa Lulu bado ni mtoto kwa kuwa ana umri wa miaka 17 na si 18 kama hati ya mashitaka inavyosomeka na hivyo anatakiwa kushitakiwa katika Mahakama ya Watoto (Juvenile Court).
Hata hivyo upande wa Mashitaka haukuridhika na uamuzi huo na kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa ili uamuzi wa Mahakama Kuu kuchunguza umri wa Lulu kama upo sahihi.
Juni 25 mwaka huu, Mahakama Kuu ilitarajia kuanza kusikiliza ushahidi na kupitia vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo na pande zote mbili lakini ilishindwa kutokana na Upande wa Mashitaka kukata rufaa.
Upande wa Utetezi uliwasilisha vielelezo kwa  njia ya maandishi  kupitia kiapo, ambapo katika ushahidi wa baba mzazi wa Lulu, ameapa kwamba binti yake  hadi anatuhumiwa  kufanya mauaji umri wake ni miaka 17, mama Mzazi wa Lulu anadai kuwa alimzaa mtoto huyo miaka 17 iliyopita  katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Jijini Dar es Salaam.
Vielelezo vilivyowasilishwa na Upande wa Mashitaka ni pamoja na CD iliyorekodi  mahojiano  kati ya mshitakiwa na Mtangazaji, Maelezo ya kuomba hati ya kusafiria,  na leseni ya udereva, maelezo ya Polisi na maombi ya hati kusafiria  ambapo mshtakiwa  ameeleza  kwamba ana umri zaidi ya  miaka 18.
Inadaiwa kuwa Aprili 7, mwaka huu katika eneo la Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam,Lulu alimuua Kanumba. hata hivyo upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kesi itatajwa tena Julai 23 mwaka huu.

No comments: